VIFUU: Takataka zinazogeuka kuwa pesa

WAKATI mwingine mazingira humfanya mtu akae bila kujua ana kipaji gani. Bi Janeth Kente (36) msanii anayetengeneza vifaa vya urembo kwa kutumia vifuu vya nazi anaelezea kilichomfanya agundue kipaji chake na umahiri wake katika sanaa katika mahojiano yake na mwandishi PETER DOMINIC.

"Nilikuwa mhudumu kibarua wa maktaba katika chuo cha maendeleo ya jamii Tengeru Arusha,nikipata pesa kidogo za kujikimu lakini niligundua baadae kuwa kipato changu hakinitoshelezi kulingana na hali ya maisha,"anaserma na kuongeza; hivyo, niliomba niajiriwe moja kwa moja lakini sikukubaliwa, nikaamua kuacha kazi".

Bi Janeth ambaye ana watoto watatu alianza kujihusisha na usanii mwaka 1994 kabla ya kuachana na kibarua chake.Hata hivyo, hakuweza kugundua mara moja kipaji alichokuwa nacho wakati ule na badala yake alikaa nyumbani kwa muda mrefu bila kuwa kazi yoyote rasmi.

Angali hajui afanye nini alikutana na kijana mmoja ambaye anamtaja kwa jina la Moses ambaye alikuwa msanii aliyekuwa akitengeneza picha na mapambo mbali mbali kwa kutumia majani ya migomba na vifuu.

Bi Janeth anasema kijana huyo alijitolea kumfundisha kutengeneza mapambo hayo ya makuti na majani ya mgomba, lakini baadaye aligundua kwamba kipaji chake kililala zaidi katika uundaji wa marembo yatokanayo na vifuu vya nazi.

Muda si mrefu alijikuta akiwa mahiri katika sanaa hiyo katika uundaji wa vitu kama hereni, mikufu na marembo mengine.

Wakati wote huo Janeth alikuwa akiishi Arusha na hakutilia maanani sana usanii wake kwa vile mumewe alikuwa na kazi nzuri iliyowahakikishia mlo wa kila siku bila matatizo.

Lakini mambo hayawi sawa kila siku; mumewe akapunguzwa kazi katika kampuni aliyokuwa akifanya kazi. Hali hiyo iliwalazimu wahamie jijini Dar es Salaam maeneo ya Mbagala ambapo walifanikiwa kujenga nyumba yao.

"Baada ya kuokota vifuu vya nazi na kuvikereza kwa kutumia tupa na msasa, nakata ramani ya kitu nilichokikusudia.

Baada ya hapo naweka maua na kisha napiga rangi ya kuving’arisha tayari kwa kutafuta soko. Ni kazi ndogo tu japo inahitaji uwe na kipaji"anasema Bibi Janeth.

Katika kufanikisha kazi yake Bi Janeth, anashirikiana na wenzake katika kufanikisha kazi hiyo ambao ni watoto wake na mume wake.

Wasanii wengi huwa wachoyo kwa maana ya kutotaka wengine wajifunze kazi wanazozifanya wao, lakini mambo ni tofauti kwa Janeth. Yeye tayari ametoa mafunzo kwa jirani zake ili kuhakikisha kikundi kinapanuka na kuboresha usanii wake na wakati huo huo nao wajipatie kipato cha kujikimu.

"Hapo mwanzo ilikuwa nikimaliza kukuna nazi natupa kifuu chake tofauti na sasa, kwani nimejua umuhimu wake. Kifuu ni mali kwa vile kinaweza kubadilishwa kutoka jina la kuitwa takataka hadi kuwa vitu virembo na muhimu kama bangili, kifaa cha kuweka majivu ya sigara,vifungo vya nguo,vibanio vya nywele ,hereni,vikombe na vifaa vingine vingi". ambavyo vinawapendeza akina mama.

Vifaa vinavyotengenezwa kwa vifuu huuzwa kati ya shilingi 150 hadi 700, na Bi Janeth anasema anamshukuru Mungu kwamba kwa kazi hiyo "mkono unaenda kinywani na watoto wanazunguka uani".

"Kazi hii ni nzuri kwa upande wetu akina mama, nimejifunza kwa muda mfupi na sasa nina uwezo wa kuchonga na kuweka urembo wowote" anasema mwanafunzi mmoja wa kikundi hicho aliyejitambulisha kwa jina la mama Inno..

Bi Janeth ambaye ana matarajio makubwa ya kukiendeleza kikundi chake ambacho bado ni kichanga ametoa wito kwa akinamama wasiwe wavivu katika kutafuta maendeleo na wasividharau vipaji vyao.

Tatizo pekee analokabiliana nalo Bi. Janeth na kikundi chake ni ukosefu wa vitendea kazi, lakini wanatumaini tatizo hilo litakwisha siku moja.