Ijue Parokia ya Oysterbay
Wanaojifunza ushonaji hapo hupewa cherehani mwisho wa mafunzo yao
PAROKIA ya Osterbay ni miongoni mwa Parokia za Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Dar Es Salaam ambayo imeonyesha juhudi zake za dhati katika kupambana na tatizo la ajira. Katika mazungumzo yaliyofanyika Parokiani hapo hivi karibuni, Paroko wa parokia hiyo Padre Valens Mruma anaeleza kwa ufupi juu ya Parokia hiyo kama alivyohojiwa na Mwandishi Wetu NEEMA DAWSON.
Swali; Padre Mruma unaweza kuwaelezea wasomaji wetu, Parokia ya Osterbay ilianzaanzaje kufikia mahali ambapo sasa inaonekana kuwa ni parokia kubwa inayojitegemea bila kuomba misaada katika parokia nyingine au hata Jimbo Kuu?
Jibu; Parokia ya Mtakatifu Petro iliyopo Oysterbay Wilayani Kinondoni ilianzishwa kama kigango miaka 43 iliyopita, yaani mwaka 1956 ikiwa chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.
Kigango hicho kilichojengwa katika eneo la Katani mpakani na kijiji cha wavuvi cha Msasani, eneo ambalo awali lilikuwa ni shamba la katani, mwanzoni kilijengwa kama kikanisa kidogo kwa ajili ya wafanyakazi wa mkonge na baadhi ya wenyeji wa Msasani pamoja na watumishi wa nyumbani.
Mwaka 1956 Jimbo Kuu la Dar es Salaam lilimteua Padri J.F Denis ambaye mwanzoni alikuwa kasisi wa dhehebu la Kianglikana na hatimaye alibadili dini akawa Mkatoliki.
Huyo ndiye aliyekuwa Paroko wa kwanza wa Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay na parokia hiyo hadi sasa imeongozwa na mapadre saba. Mnamo mwaka 1962 ulimalizika ujenzi wa kanisa kubwa na kuwekwa chini ya usimamizi wa Mtakatifu Petro. Ujenzi wa kanisa hilo kuwa uliowahusisha waumini na wakazi waliokuwa wanaishi maeneo ya jirani kwani walifanya hivyo baada ya kuona kuwa waunini wanazidi kuongezeka siku hadi siku.
Swali;Unaweza kuelezea ni shughuli gani manazozifanya hapa parokiani ambazo zinawasaidia katika maendeleo ya wanaparokia?
Jibu; Parokia imefanikiwa kuanzisha shule ya Chekechea iliyo na watoto 150, Shule ya ushonaji ambayo ni ya maendeleo ya akina mama na wasichana iliyo na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 25 na mwaka wa pili 25. Wanafunzi wa kike wanapomaliza masomo yao hapa parokiani kila mmoja hupewa cherehani moja ili aweze kuitumia na imsaidie kuyaendesha maisha yake
Tumeamua kufanya hivyo ili kuwasaidia wanafunzi hao kwani wengi wao wawapo majumbani kwao si rahisi kumudu kununua cherehani hizo kwa wakati unaotakiwa.
Swali; Maendeleo katika huduma yenu ya kuvisaidia vigango vilivyopo chini ya parokia yakoje?
Jibu;Tumekabidhiwa na Jimbo Kuu la Dar Es Salaam kazi ya kuisaidia Parokia ya Mlandizi katika majukumu waliyonayo kwani parokia hiyo bado ni changa.
Awali tulianza kuisaidia shilingi milioni moja kila mwaka lakini kwa sasa hivi tunamudu kuisaidia shilingi laki tano tu kwa kila mwaka .
Swali; Kwa nini awali mlikuwa mnamudu kuisaidia Parokia ya Mlandizi kiasi kikubwa cha fedha na sasa mmepunguza?
Jibu; Awali Parokia ya Osterbay ilikuwa inamudu kutoa shilingi milioni moja na kwa baadaye tulipunguza kiasi hicho cha pesa kutokana na parokia yenyewe kuwa na majukumu makubwa ambayo yaligharimu kiasi kikubwa sana cha pesa mojawapo likiwa ukarabati wa kanisa hilo ndani na nje.
Swali;Mliona ni bora zaidi kupunguza matatizo ya parokia yenu na kuipa wakati mgumu zaidi Parokia ya Mlandizi, sivyo?
Jibu; Kuna matatizo mengine ambayo mtu huwezi kuyavumilia kwani suala la kuvuja kwa kanisa ni tatizo ambalo linamgusa kila mtu na hilo ndilo lililokuwa likitukabili hapa parokiani. Hivyo tuliona ni bora kuikarabati nyumba hii ya kuabudia, lakini haimaanishi kuwa tulipuuza matatizo ya Mlandizi. kimsingi ni kwamba nao wamekuwa wakiendelea kukomaa hivyo msaada wa awali hauwezi kuendelea milele, tunapunguza kidogo kidogo kadri wanavyokua.
Swali Je hadi hivi sasa Parokia ya Oysterbay ina mipango gani ya kujiendeleza ?
Jibu:Parokia ya Osterbay kwa mtazamo wake inatarajia kwanza kabisa kuziimarisha zaidi jumuia zake 37 zilizopo kwa kuwatembelea wenye matatizo na kuwapa ushauri, pamoja na kuanza kujenga uzio kuzunguka kanisa hilo kwani kufanya hivyo ni kupunguza vurugu na kuliweka kanisa katika hali ya usalama.
Swali: Kwani usalama wa mahali ni lazima kuwe na uzio?
Jibu: Hapa kwetu ni muhimu kuwepo na uzio kwani Parokia ya Osterbay iko jirani kabisa na barabara mahali ambapo pana muingiliano mkubwa wa wapita njia, licha ya kwamba pia tunapakana na Shule ya Msingi Mbuyuni, na kama unavyojua baadhi ya watoto ni watundu na wanaweza kuleta usumbufu wasipodhibitiwa.
Swali: Ni kamati gani mlizo nazo katika parokia hii?
Parokia ya Osterbay ina kamati saba ambazo ni pamoja na Kamati ya Haki na Amani, Kamati ya Afya, Kamati ya Litrujia, Kamati ya Mipango Uchumi na Fedha, Kamati ya Elimu ya Dini, Kamati ya Mafundisho ya Kanisa na Teolojia pamoja na Kamati ya Malezi na Familia ambazo zote zimekuwa zikifanya kazi kwa ufanisi mkubwa.