Ijue Parokia ya Kunduchi

lParokia ambayo inawatafutia ajira wahitimu wa ufundi

lIna nyumba ya kuwasaidia wazee wasiojiweza

Parokia ya Kunduchi ni moja ya Parokia za Jimbo Kuu la Dar es Salaam iliyopo chini ya Shirika la Damu Azizi ya Yesu ( Precious Blood) ambayo mbali na kutoa huduma za kiroho kwa waamini wake, pia ina shule za ufundi stadi (VETA PRIVATE) shule sita za chekechea, nyumba ya kuwasaidia wazee, pamoja na mafunzo ya kompyuta na na Ufundi Cherehani.Paroko wa Parokia hiyo Padri Dominic Alteri anaelezea kwa undani zaidi shughuli mbalimbali zinazofanyika Parokiani kwake kama alivyohojiwa na Mwandishi Wetu GETRUDER MADEMBWE.

SWALI:Nimesikia kwamba parokiani kwako kuna chuo cha ufundi ambacho huwatafutia ajira wanafunzi wake wanapomaliza mafunzo yao. Je, ni kweli? Na kama ndivyo, chuo chenu kinaitwaje?

JIBU: Chuo chetu kinajulikana kama St. Gasper Training Centre, na hilo la kuwatafutia ajira baadhi ya wanafunzi ni kweli kabisa.

Wengi wa wahitimu wetu tuliowatafutia ajira wapo katika mashirika mbalimbali na wamefanikiwa kiutendaji na wanafanya kazi vema katika mashirika na makampuni hayo.

SWALI: Sijui ni mashirika yapi ambayo mmewatafutia ajira hizo?

JIBU:Mashirika tuliyokwisha watafutia ajira ni mengi yakiwemo haya ya TANESCO, COCACOLA na pia kuna mashirika mengine ambayo tayari tumeshawasiliana nayo lakini hata hivyo baadhi ya wanafunzi huweza kujiajiri wenyewe.

SWALI:Hivi ina maana chuo chenu kina uhusiano wowote na kile chuo cha ufundi cha VETA kilichopo Chang’ombe?

JIBU: Chang’ombe ni chuo cha serikali na hiki ni chetu wenyewe yaani ni (private) na hata hivyo masomo yote tunayofundisha hapa ndiyo yale yale yanayofundishwa Chang’ombe.

SWALI:Unataka kusema kwamba hiki chuo kinatambulika serikalini?

JIBU: (akacheka kidogo) Chuo hiki kinatambulika serikalini na ndiyo maana mwanafunzi ambaye amesoma Chang’ombe cheti cha daraja la tatu au la pili anaweza kuja hapa na kumalizia la pili au la kwanza; akapata cheti ambacho kinatambulika serikalini.

SWALI:Mna walimu wangapi walioajiriwa kikamilifu hapa chuoni kwenu, au huwa mnawatumia walimu wa mikataba maalum, yaani part time?

JIBU: Baadhi ya walimu huwepo kila siku na wengine hutoka mjini kuja kufundisha tu na kuondoka.

SWALI: Kwa hiyo tuseme parokia yako huwalipia wanafunzi gharama za masomo au hakuna gharama zozote ambazo wanafunzi hutakiwa kugharamia ?

JIBU: (Anatingisha kichwa na kucheka) Ili kusaidia katika kukiendesha chuo, kuna gharama kidogo wanazotakiwa kuchangia; sh. 70,000/= kwa mwaka.

Swali: Mna huduma gani nyingine ya kielimu mnayoitoa hapa parokiani?

JIBU: Tuna shule sita za chekechea ambazo zipo parokiani hapa.

SWALI:Kuna habari pia kwamba parokiani kwako kuna nyumba ya kutunzia wazee; hilo ni la kweli?

Na kama ni kweli hivi sasa mnao wazee wangapi katika nyumba zenu mnaowasaidia?

JIBU: Ni kweli, parokia inao wazee sita inaowasaidia na hivi sasa wapo katika ile nyumba iliyopo Boko; tunawapa huduma zote bila malipo yoyote.

SWALI:Bila shaka wasomaji wa gazeti hili wangependa kujua ni wazee wa namna gani wanaosaidiwa na parokia yako?

JIBU: Wazee wanaosaidiwa ni wale ambao hawajiwezi na wale wasio na ndugu kabisa wa kuwasaidia na umuhimu wa kusaidiwa kwao unaonekana kwa kila mwanajamii.

SWALI: Paroko; unaweza kutueleza parokia ilianza na waamini wangapi na hivi sasa wamefika wangapi?

Jibu :Parokia ilianzishwa mwaka 1979. Idadi ya waamini wakati huo siikumbuki vizuri ila kwa sasa ina Wakristo wapatao 12,000.

Tuna vigango 13 ambavyo ni Wazo Hill, Kisauke, Boko, Bunju, Mabwepande, Mbweni, Tegeta pamoja na Mpigi Magoe.

Vingine ni Mtongani,Mbezi Beach, Salasala na Mtakatifu Dominic kwa Maranta.

Tunatarajia pia kuigawa parokia hii ili ziwe mbili ambazo ni Parokia ya Tegeta na Parokia ya Mtongani.

Parokia ya Tegeta itakuwa na vigango vya Wazo Hill, Kisauke, Boko, Bunju, Mabwepande pamoja na Mpigi Magoe wakati Parokia ya Mtongani itakuwa na vigango vitatu yaani Mbezi Beach,Salasala na kigango cha Mtakatifu Dominic kwa Marantana.

SWALI:Mkiwa na vigango vingi namna hiyo mnaendesha vipi misa zenu?

JIBU: Vigango vyote huwa na misa mbili kila Jumapili. Misa ya kwanza inaanza saa moja na misa ya pili inaanza saa nne.

SWALI:Nini matarajio yenu ya baadaye?

JIBU:Tunarajia kukamilisha ujenzi wa vigango hivi na mwezi Oktoba kigango cha Mtakatifu Dominic kinatarijiwa kukamilika na kitabarikiwa na Kardinali Pengo ambapo pia atatoa sakramenti ya kipaimara.

SWALI:Kwenye mafanikio hapakosekani matatizo; parokia yako hadi sasa ina mafanikio na matatizo gani?

Jibu: Parokia imefanikiwa kuongeza vigango vitatu ambavyo vipo katika ujenzi ambavyo ni Mtakatifu Dominic,Mwenyeheri Mathiasi na Yohane Merlini ambavyo vitagharimu zaidi ya Milioni140.

Parokia yetu ina waumini wengi lakini mapadri ni wachacha hali ambayo husababisha mara nyingine vigango vya Mabwepande na Mpigimagoe kukosa misa kila Jumapili.Aidha tunapata msaada wa mapadri kutoka sehemu mbalimbali.