FAT yaonya wateka nyara Yanga
CHAMA cha Soka nchini (FAT) kimeonya kundi lililodai kufaya mapinduzi ya kuung'oa madarakani uongozi halali wa klabu ya Yanga, na kisha kuiteka nyara timu nzima ya wachezaji wa klabu hiyo.
Katibu Mkuu wa FAT Isamil Aden Rage alisema jijini juzi kuwa hatua hiyo siyo ya kukubalika wala kuvumilika katika fani ya soka nchini, na amewataka wale wote waliofanya hivyo kufuata na kuheshimu katiba ya Yanga.
Rage alisema kuwa FAT haikubaliani na wala haifurahishwi na hatua hiyo iliyofanywa na wanachama 223 wa Yanga mapema wiki hii ya kujitwalia madaraka na halafu kuiteka timu nzima na kwenda kuiweka mafichoni.
Alisema kuwa mambo kama hayo yanayofanywa na shinikizo la watu wachache wenye uchu katika madaraka ndiyo ambayo yamekuwa yakichangia kuporomoka kwa soka nchini kwani vilabu vimekuwa vikitumia muda wao mwingi katika kuendeleza migogoro badala ya soka.
"Migogoro hutokana na mambo kama hayo ya kuwaengua kinyemela viongozi halali madarakani, ambapo matokeo yake mambo huamia mahakamani na hivyo kusababisha kupotezwa kwa muda mwingi huko mahakamani, huku timu husika ikidorora", alisema kiongozi huyo.
Aidha, kuhusu mapinduzi hayo ya kuwang'oa viongozi halali wa Yanga yaliyoongozwa na Abbas Tarimba na George Mpondela, Katibu Mkuu huyo wa FAT alisema kuwa chama chake hakiyatambui.
Rage alisema kuwa FAT bado inawatambua viongozi halali wa Yanga lkiwa Mwenyekiti ni Ngozoma Matunda na wenzake, na wala sio viongozi waliojitwalia madaraka na kuuunda kamati yao ya muda.
Alisema kuwa hadi sasa FAT haijapokea taarifa ya msajili wa vilabu vya michozo kuhusu mabadiliko hayo, hivyo chama chake kitaendelea kuwatambua viongozi walewale wa awali.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa FAT amweakumbusha wanachama na viongozi wa vilabu mbalimbali vya soka nchini kuheshimu na kufuata katiba za vilabu vyao pale wanapotaka kufanya jambo lolote wanaloona lina manufaa au maslahi katika klabu yao, na wala siyo kutimia nguvu kushinikiza maslahi hayo.
Uchaguzi Mkuu TABA kufanyika Mwanza
UCHAGUZI mkuu wa viongozi wa Chama cha Ngumi za Ridhaa nchini (TABA) umepangwa kufanyika Agosti 9 mjini Mwanza.
Kabibu Mkuu wa TABA, Nasis Tarimo aliiambia KIONGOZI jana kuwa uchaguzi huo utafanyika sambamba na mashindano ya Taifa y akumtafuta bingwa wa ngumi za ridhaa.
Tarimo alisema kuwa katika uchaguzi huo nafasi zitakazowaniwa na wagombea ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu.
Nafasi nyingine zitakazogombewa ni zile za Halmashauri Kuu ambazo zitakuwa nafasi sita, na Kamti ya Utendaji kutakuwa na nafasi mbili.
Alisema kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za maandalizi ya uchaguzi pamoja na mashindano hayo, ambapo alisema iwapo vyote vitakfanyika sambamba zitapunguza gharama hasa kwa wajumbe wa mkutano mkuu watakaohudhuria kutoka mikoani.
Bingwa wa mashndano hayo ya ngumi ya Taifa ataiwakilisha Tanzania katika michuano ijayo ya ngumi ya nchi za Africak Mashariki, Kati na Kusini.