Naweza kuitafutia Stars kocha - Kajumulo

Mfadhili na mdhamini wa michezo aliyeibuka hivi karibuni na kupata umaarufu mkubwa, Alex Kajumulo amesema kuwa anaweza kuitafutia timu ya soka ya taifa ya Tanzania "Taifa Stars" kocha mtaalamu wa kuifundisha iwapo ataombwa kufanya hivyo.

Kajumulo ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya kajumulo Sports World, alisema juzi wakati alipohojiwa juu ya ahadi yake ya kuwapeleka nje ya nchi wanasoka wawili Nteze John wa Tanzania Stars na Slavatory Edward wa Yanga kupata elimu zaidi ya mambo ya soka.

Kajumulo alisema kuwa soka ya Tanzania imejaa wanasoka wenye vipaji, lakini wasiokuwa na elimu ya mchezo huo wakiwemo waalimu wa kuifundisha timu ya taifa, hivyo ataangalia uwezekano wa kutafuta kocha wa kufundisha timu hiyo ya taifa pindi atakapoombwa kufanya hivyo.

Alisema kuwa Chama cha Soka nchini (FAT) kinapaswa kuliangalia kwa makini suala la kuwa na wataalamu wa soka wa kufundisha timu ya taifa, kwani msingi wa timu hiyo ambao ni vilabu sio mzuri kwa vile katika vilabu hivyo hakuna makocha wataalamu.

Kuhusu hilo alisema kuwa ufumbuzi wake ni kupata makocha walio na elimu ya kutosha ya mambo ya soka, ambao kwa sasa aliongeza kuwa wanapatikana nje ya nchi.

Alisema yeye akiwa ni mzalendo halisi yupo tayari kumtafuta mtaalamu ambaye ataifundisha timu ya taifa, lakini hawezi kuchukua hatua hiyo kienyeji kwa vile inahitaji kufuata taratibu ikiwemo makubaliano na vyombo vinavyohusika.

Mbali na kocha wa timu hiyo ya taifa pia Kajumulo ameonyesha nia ya kuvisaidia vilabu mbali mbali vya soka hapa nchini ili kuweza kuinua kiwango cha soka nchini.

Alisema klabu chochote hapa nchini ambacho kina uwezo wa kuweka mikataba ya kumlipa kocha kutoka nje ya nchi bila matatizo, yupo tayari kukitafutia kocha mtaalamu.

Hata hivyo alisisitiza kuwa msingi mzuri wa sasa ni kuanza kuwa na wataalamu wetu wa hapa nchini, na moja ya juhudi anazofanya ni hiyo ya kuwapeleka Marekani wachezaji Nteze na Salvatory kujinoa katika elimu ya soka.

Katika kipindi kifupi tangu aliporejea nchini kutoka Marekani , Kajumulo ameonyesha nia nzuri ya kuvisaidia vilabu vya hapa nchini zikiwemo timu za Simba, Yanga na Tanzania Stars.

 Timu yahaha kutafuta wafadhili

TIMU ya wasichana ya mpira wa mikono ya Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imesema inakwamishwa na tatizo la ukosefu wa wafadhili ili kuifanya ifanikiwe zaidi.

Akizungumza na gazeti la Kiongozi ofisini kwake hivi karibuni, mmoja wa walezi wa timu hiyo ambaye pia ni Afisa Utamaduni, Vijana na Michezo wilayani hapa Bw. Julius Kisamba alisema timu yake iko katika hali mbaya sana na akawataka wafadhili kujitokeza ili kuikwamua kwani imeanza kutia matumaini kutokana na michezo mbalimbali ambayo imekuwa ikifanya ili kujipima nguvu.

Alisema timu hiyo changa hivi inafanya juhudi kubwa ili kujiimarisha zaidi katika mazoezi na kujiweka tayari kushiriki katika maashindano (SHIMISEMITA) ambayo hufanyika nchini kila mwaka.

Kisamba alisema timu yake haina vifaa kama jezi na kwamba inatumia za kuazima katika vikundi mbalimbali.

Alisema mlezi mwingine ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bi. Maimuna Tarishi ameahidi kuinunulia timu hiyo jezi timu hiyo iliyotarajiwa kuwa na ziara ya mafunzo mkoani Dar Es Salaam kwa kutembelea timu ya Kiwalani Shooting Stars ili kufanya mazoezi ya kubadilishana uzoefu toka kwa timu mwenyeji wao na akasisitiza kuwa tayari uongozi wa timu ya Kiwalani ulikwisha kubali kuifundisha timu hiyo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Bi. Adasa Wilson na Mwenyekiti wake Bi. Mary Dule kwa nyakati tofauti waliwaomba popote walipo wanamichezo, wafadhili na wakereketwa kujitokeza ili kuilea timu hiyo ambayo ndiyo tegemeo la wilaya hii.

"Tunaomba wafadhili, wataalam na walezi zaidi wajitokeze ili tuikwamue timu yetu kwani tuna uhakika wa kufanya vizuri endapo timu itakuwa katika mazingira mazuri kuliko ilivyo sasa na hivyo kuweza kushiriki kikamilifu katika mashindano mbalimbali na kuiwakilisha wilaya yetu na ha hata kufikia ngazi ya taifa kwa ujumla."alisema Bi.Mary.

Naye Bi. Adasa alisema timu yake imekwisha tuma maombi ya ufadhili katika Umoja wa Maendeleo Kisarawe (UMAKI) "Tunaamini Profesa Mlawa ambaye ni Mwenyekiti na Katibu wake Bw. Mlata watashirikiana nasi kwani ni watu wanaojua umuhimu wa michezo katika jamii."

Timu hiyo ambayo kwa mara ya mwisho Machi 20, mwaka huu iliichapa timu ya Sanze Seminari kwa magoli 10 kwa 2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika katika uwanja wa Bomani mjini hapa, inaundwa na kikosi cha wachezaji 29.

WAKATI HUOHUO: Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee iliyopo wilayani Temeke katika Mkoa wa Dar Es Salaam, Luteni Kanali Fabiani Massawe amesema wakuu wa shule za sekondari wanaokataa kuhudhuria vikao vya pamoja ndio wanaozorotesha mashindano ya UMISETA na akatoa wito kwa walimu hao kuachana na tabia hiyo na badala yake washiriki kikamilifu ili kuinua mashindano hayo muhimu katika kuinua kiwango cha michezo nchini.

Akiongea shuleni kwake wiki iliyopita, Massawe ambaye shule yake ndiyo ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo katika wilaya ya Temeke yanayoendelea shuleni hapo hivi sasa, amesema anaupongeza uamuzi wa Kikao cha Walimu hao kilichofanyika shule ya sekondari Forodhani Machi 21, na kuzisimamisha shule ambazo wakuu wake hawahudhurii vikao hivyo , shule zao kutokushiriki katika mashindano yote ya UMISETA ambayo yanahusisha pia "drama" na "debate". Hata hivyo alikataa kutaja shule zilzosimamishwa.

 Vilabu 15 vya ndondi kuwania medali ya dhahabu Dar

JUMLA ya vilabu 15 vinatarajiwa kushiriki katika mchezo wa ndondi kuwania medali za dhahabu, fedha,na shaba utakaofanyika katika ukumbi wa DDC Kariakoo jijini Dar Es Salaam Aprili 14, mwaka huu.

Akiongea na gazeti la Kiongozi ofisini kwake hivi karibuni,mjumbe wa kamati ya ufundi ya (DABA) Timoth Kingo alisema kwamba kati ya vilabu hivyo 15 vinne ni vipya.

Bw. Kingo alivitaja vilabu hivyo vipya kuwa ni Redgreem ya Sinza, PTW, Buguruni Boxing Club,na Ubungo Boxing Club.

Aidha alivitaja vilabu vingine ambavyo vimeleta barua ya kuthibitisha kushiriki michezo hiyo ni JWTZ, JKT, Polisi, Uhamiaji, Kata ya 14 Temeke, Chui-Kawe, Matumla Boxing , Maner Boxing .

Kwa mujibu wa mjumbe huyo vilabu vingine vitakavyoshiriki ni Msisili Boxing , Anatoglo Boxing pamoja na Keko Boxing.

Kingo alisema katika mashindano hayo ambayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar luteni Yusufu Makamba, jumla ya medali 12 za fedha ,12 za dhahabu na 24 za shaba zitashindaniwa .

 

Ubia wa Uwanja wa FAT na NSSF mashakani

lNSSF yahofia kanuni za FAT

Mipango ya chama cha soka nchini FAT ya kujenga uwanja mpya wa kisasa kwa kushirikiana na Shirika la Akiba ya Jamii (NSSF) huenda ikawa ndoto ya mchana kutokana na suala hilo linavyoshughulikiwa na pande zote mbili.

Habari zilizopatikana toka ndani ya vyanzo vyety vya habari katika shirika la NSSF, zimedai kuwa shirika hilo linataka liachiwe kazi yote ya kufanya tathmini na kuujenga uwanja huo bila kushirikiana na FAT na baada ya hapo liumiliki

Chanzo chetu hicho cha habari kimedai kuwa uongozi wa shirika umeishauandikia uongozi wa FAT kuhusu suala hilo na kinachosubiriwa ni majibu tu na kama FAT itakubaliana na masharti hayo ya kukubali uwanja ujengwe bila wao kutaka wawe na hisa ya kuumiliki basi ujenzi huenda ukaanza mwaka huu.

Habari hizo zimedai kuwa, shirika hilo limekataa kushirikiana na FAT katika kuujenga na kuumiliki uwanja kwa sababu mara nyingi chama hicho kimekuwa hakina kanuni maalum jambo linalotia shaka kama kinaweza kumiliki kwa ubia kitega uchumi kama hicho cha uwanja.

Aidha imedaiwa kuwa ikiwa FAT itang'ang'ania kuingia ubia wa kuujenga uwanja wa Karume uwe wa kisasa basi Shirika hilo litatafuta eneo lingine na kujenga uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu na michezo mingine kama vitega uchumi wa shirika..

Pia habari zaidi toka ndani ya shirika hilo zimedai kuwa, shirika hilo lina mikakati ya kujiingiza katika kudhaminimchezo kama yalivyo mashirika mengine ili kujitangaza zaidi ikiwemo na kuwafanya wanamichezo wajiunge.

Juhudiza kuwapata viongozi wa Fat ili waweze kueleza kama tayari walishaipata barua ya NSSF yenye masharti yaliyotajwa zilishindikana hadi tunakwenda mitamboni.