Familia takatifu chimbuko la utakatifu (2)

 

w    Ndoa ni kazi ngumu, lakini muhimu

w    Kwanini wengine hawaoi au kuolewa ?

 

KATIKA Toleo lililopita, tuliliona Shirika la Kutetea Uhai (PRO-LIFE), Tawi la Tanzania likisema kuwa, Familia kama hifadhi takatifu ya uhai, haina budi kutambua kuwa, zawadi kubwa na yenye thamani katika ndoa ni WATOTO. Ndiyo maana ulimwengu umepewa zawadi ya ukombozi yaani, KUZALIWA KWA YESU KRISTO. Endelea :

 

Kristo, alipenda kuzaliwa na kukua katika Familia Takatifu ya Yosefu na Maria. Hivyo, Kanisa si kitu kingine, bali ni FAMILIA YA MUNGU. Na familia ni KANISA LA NYUMBANI.

Umuhimu wa familia ni mkubwa kiasi kwamba, nafasi yake katika kujenga utamaduni wa uhai, haiwezi kuchukuliwa na kitu kingine. Hivyo, jukumu la malezi si la mtu mmoja ni la wote, ni la jamii nzima.

Kama Kanisa la nyumbani, familia imeitwa kutangaza Injili ya Uhai. Kwa mantiki hiyo, familia isali ili kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai. Haki za familia zizingatiwe.

 

NDOA NA FAMILIA

 

“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba, Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia zaeni mkaongezeke…” (Mwa 1: 26-27)

 “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Mwa 2: 23-24)

Msingi  wa familia unatokana na katika Maandiko Matakatifu yanayoibua dhana zifuatazo, mwanaume na mwanamke wanaounganika na kuunda familia, wameumbwa kwa mfano wa Mungu

Binadamu ni kiumbe kilichobarikiwa na Mungu, uzao ambao ndio tunda la mwunganiko wa mume na mke umebarikiwa

Watoto, yaani uzao ni baraka itokayo kwa Mungu, ni baraka inayoendeleza tendo la uumbaji ambalo binadamu anashiriki pamoja na Mungu

“Kutozaa kwa makusudi, au kuzuia kuzaa bila sababu yoyote ni kuzuia tendo la uumbaji ambalo binadamu amepewa na kubarikiwa na Mungu na kama lingefanyika katika familia ya Maria na Yosefu, ulimwengu huu usingepata Mkombozi na badala yake, ungeamia,” linasema Shirika hilo la kutetea uhai, tawi la Tanzania kupitia Mwenyekiti wake, Bw. Emil Hagam.

Linasema, Mke na mume huunda muunganiko usioweza kugawanyika; kila mmoja ni mali ya mwezake, na kwa ajili ya mwenzake. Hawa, huunda familia ya pekee nje ya wazazi wao wakishiriki agano lisiloweza kuvunjwa

Sasa, katika dunia hii yenye mkanganyiko wa mawazo, dhana ya familia inaweza kuelezwa kwa namna mbalimbali kutegemeana na mwelekeo wa taaluma na lengo la mfasiri.

Mwanamume na mwanamke walioungana katika ndoa, pamoja na watoto wao ndio wanaounda familia. Familia kama taasisi ipo hata kabla mamlaka za kijamii hazijaitambua na ambazo zina wajibu wa kuitambua. Hii ndiyo tafsiri ambayo kwayo tafsiri nyingine zozote zihusizo familia zitarejea.

Kwa kuumba mwanamume na mwanamke, Mungu alikusudia kuunda familia ya binadamu na kuitengenezea mazingira maridhawa ya makubaliano. Wanafamilia ni wale wanaokaa na kushirikiana kijamii pamoja, lakini kila mmoja akiwa na hadhi yake.

 

Silika ya familia ya Kikristo

Agano la Kindoa

Wakati wote familia imetambulika kama msingi na namna ya kueleza tabia ya kijamii ya binadamu. Familia kwa hiyo ni muunganiko wa watu ambao namna yao ya kuishi na kukaa pamoja ni kwa njia ya “Komunioni”- - muunganiko wa watu.

Ndoa ni agano ambalo kwalo mwanaume na wanamke kila mmoja hujitoa kwa mwenzake na kila mmoja anamkubali mwenzake kama mwenzi na mshirika wake wa maisha.

 

Muungano wa hiari wa mwanamume na mwanamke

Ni binadamu tu mwenye uwezo wa kuamua kwa hiari juu ya kuunganika pamoja kwa msingi wa uchaguzi wa hiari. Katika ndoa mwanamume na mwanamke wanaungana kiasi cha kuwa mwili mmoja (Mwa. 2:24). Japo ni binadamu wawili walio tofauti wanao uwezo wa kuishi pamoja katika ukweli na upendo.

 

Uzao wa binadamu 

Muunganiko unaotokana na ndoa huleta furaha na faraja ya uzao wa binadamu wapya. Kwa hiyo, kwa tendo hilo wazazi hushiriki na Mungu Muumbaji katika kuumba na kuzalisha kiumbe kipya. Mungu anashiriki katika ubaba wa mzazi wa kiume na umama wa mzazi wa kike katika kuleta uhai mpya.

Sifa za familia kwa kadiri ya barua ya Papa Yohane Paulo II:  Families of the World”

Familia halisi ni taasisi ya msingi ya jamii, inayojengwa katika uhalisi wa binadamu, na yenye kujikita katika muunganiko wa hiari wa mwanamme na mwanamke katika agano la maisha ya ndoa kwa ajili ya Kushibisha hamu za moyo wa binadamu za kutoa na kupokea upendo, Kuwapokea na kuwalea watoto katika maendeleo yao ya mwili na akili

 na Kushirikiana makazi ambayo huunda msingi wa maisha ya kijamii, kielimu, kiuchumi na kiroho.

Mengine ni Kujenga uhusiano na kupasisha kizazi kipya pamoja na Kutoa huduma kwa wahitaji mbalimbali.

 

Familia kama Fumbo la Kanisa

Familia ya Kikristo inajifunua wazi na kutambulika kama jumuiya na wanakanisa, na kwa msingi huu familia ni kanisa la (mwanzo) nyumbani. Hii ni jumuiya ya imani, matumaini na mapendo.

Familia hii ni muunganiko wa watu, ishara na mfano wa muunganiko wa Baba na Mwana katika Roho Mtakatifu. Katika uzazi wa watoto na kuwaelimisha tunarejeshwa kutambua uumbaji wa Mungu Baba. 

Kwa hiyo, familia inaalikwa kuishi maisha ya sala na ya sadaka ya Kristo. Sala za kila siku zinaimarisha upendo na hivyo kuwezesha kazi ya uinjilishaji na umisionari kufanyika.

Familia imepewa jukumu la kutoa huduma ya kujenga ufalme wa Mungu kama mshiriki katika maisha na umisionari wa kanisa. Katika familia matendo ya kikanisa ya uinjilishaji, ufundishaji na uelimishaji hufanyika.

Matendo hayo hufanyika mithili ya mama kanisa anavyowezesha kizazi kuendelea kufundisha na kujenga familia ya kikristu. Familia hutekeleza utume wake wa kikanisa ndani na nje ya kanisa.

Katika familia wanandoa wanaishi kisakramenti, na hivyo ndoa inayojenga msingi wa familia inaonekana kama sakramenti ya kutakatifuza na kama tendo la ibada au kuabudu.

Wajibu wa familia

Familia kama taasisi iliyo wazi na ya msingi ina wajibu mbalimbali miongoni kwa watu wanaoiunda.

Mwandishi wa Barua kwa Waefeso anatujulisha wajibu wa kila mmoja wa watu wanaounda familia, mume, mke na watoto.

Mwandishi anatukumbusha kuwa wajibu wa msingi ni ule wa uhusiano. “Kila mmoja amstahi wenzake kwa sababu ya kumcha Kristo”. (Efe. 5: 21). Huu ndio wajibu wa msingi kwani unatutambulisha na kutushirikisha maisha yetu na Kristo.

Baada ya kueleza wajibu huo wa msingi, mwandishi wa barua hiyo anafafanua wajibu wa mume, mke na watoto. Kimsingi wajibu zote zinaegemea tunu za upendo, utii na heshima.

Familia zinazojengeka katika misingi hiyo ndizo zinazodumu na kuwa imara. Wanafamilia katika familia za namna hiyo hukubaliana, huchukuana, hujengana, kila mmoja kwa manufaa ya mwenzake na kwa manufaa ya pamoja.

Wajibu wa familia kwa jamii unaelezwa vizuri kwa kutambua uhusiano asilia uliopo kati ya familia ambayo sehemu, na ndiyo inayouunda jamii kwa upande mmoja, na jamii ambayo hundwa na mkusanyiko wa familia moja moja kwa upande mwingine. Kwa hiyo bila familia hakuna jamii. Kwa upande mwingine familia inahitaji jamii kwa ajili ya ustawi wake.                                       

 

 

Haki za Binadamu ndani ya Utawala Bora Tanzania

TANZANIA ni moja ya nchi zinazojali suala la Haki za Binadamu na Utawala Bora. Katika kuhakikisha utekelezaji wake, tayari inayo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 129. Ungana na MWANDISHI WETU katika makala haya ujue mambo haya kwa undani zaidi.

Haki za binadamu ni haki na uhuru muhimu anaokuwa nao binadamu kwa sababu yeye ni binadamu.

Uhuru na Haki hizi mtu hapaswi kuwa nazo kutokana na kuainishwa katika mikataba ya kimataifa, Katiba au Sheria za nchi, bali ni haki na uhuru huo mtu anakuwa nao kwa sababu yeye ni binadamu na hakuna mtu anayeweza kumny’ang’anya au kumwondolea.

Hata hivyo, jukumu la kuulinda uhuru na haki hizo za binadamu, uko mikononi mwa dola ambayo ina vyombo vyake kama Mahakama na Polisi.

Haki za binadamu zimekuwa zikikua katika hatua zijulikanazo kama vizazi na katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na haki za kiraia na kisiasa, haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Katika utekelezaji wa haki za binadamu kwa upande wa sheria, inaweza kuwa na manufaa kwa jamii pale tu, inapoonesha muelekeo wa kutekelezeka.

Mkataba au sheria yoyote ile, itakuwa haina maana kama haiwezi kutekelezeka. Hivyo basi, ili mkataba au sheria iwe ya manufaa, lazima ieleze wazi taratibu za utekelezaji wake na zizingatiwe na kuheshimiwa.

Hata hivyo katika Tanzania yetu sasa, raia wengi wamekuwa hawazijui haki zao. Wengi wao wamekuwa wakifikiri kuwa, hata palipo na haki yao ya msingi, basi huhisi kuwa labda wanafanyiwa upendeleo wa aina fulani.

Hali inaonesha kuwa, bado serikali ina kazi ya kupeleka elimu hiyo kwa raia wake, na pia kuunga mkono juhudi za kuelimisha jamii kuhusu haki zao, kazi ambayo hivi sasa imekuwa ikifanywa na asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) na jumuiya za kidini, kwa asilimia kubwa.

Mtazamo wa utofautishaji wa uelewa wa haki za binadamu katika jamii unaonesha kuwa, utekelezaji wa haki hizo pia, umekuwa tatizo hata pale ambapo jamii imekuwa ikielewa haki zake za msingi.

Hali hiyo imekuwa ikichangiwa na mfumo uliopo wa utawala katika sehemu husika kutokana na kukithiri kwa rushwa na udhaifu wa watendaji.

Katika kulitafiti hilo, hali ya kuwa na utawala bora na wenye kujali sheria, haki na kanuni za msingi katika utawala bora na wenye demokrasia ya kweli, itamsaidia mwananchi wa kawaida kuelewa vizuri haki zake za msingi na namna ya kuzipata kwa njia ya amani.

Kitabu cha KWANINI TUJALI MANUFAA, USTAWI KWA WOTE kilichotolewa na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kinabainisha kuwa, Utawala bora una maana pana kuliko inavyodhaniwa na wengi.

Kinasema kuwa, wananchi wanayo nafasi ya kutambua kama utawala wao katika kipindi fulani ulikuwa ni utawala bora ama la.

Hata hivyo katika hili, Tanzania inaweza kujiuliza kama wananchi wake wana maoni gani juu ya hilo. Lakini, ni wazi kuwa raia hao wanazijua kasoro nyingi zilizo bayana katika utawala wa nchi yao. Hivyo, hawawezi kujidai kuwa wanao utawala bora.

Mara nyingi utawala bora ambao unajulikana ulimwenguni kote, ni ule ambao unajali na kufuata sheria na kanuni na unaojali na kuzingatia haki za binadamu daima.

Utawala huo unapaswa ufanye juhudi za kukomesha vitendo vya rushwa na upendeleo wa aina yoyote ile. Watawala pia wanapaswa kutawala kwa kuzingatia na kuheshimu sheria na kanuni. Uwazi na uwajibikaji vinapaswa kuwapo, bila ya hivyo, ni rahisi kwa watawala kuvunja sheria bila ya kuwa na wasiwasi wowote.

Hata hivyo, kitabu cha KWANINI TUJALI MANUFAA, USTAWI KWA WOTE pia kinaeleza kuwa, “Utawala Bora ni ule unaozingatia Demokrasia.” Kinasema, palipo na utawala bora, sifa zote za demokrasia zinaonekana machoni pa umma.”

Kinaeleza kuwa, msingi muhimu katika hilo ni DEMOKRASIA ambayo ni sawa na utawala wa watu.

Katika kuzingatia misingi hiyo ya utawala bora, watawala wanapaswa kutoa uhuru na uhalali katika kuendesha mambo hususani ya UCHAGUZI, kwa kupokea na kuheshimu maoni ya watu.

Hali ya kuona na kuelewa mambo, itasaidia kutumia njia za kupunguza ulimbikizaji wa madaraka kwa wachache na pia, matumizi mabaya ya madaraka. Na kutatoa fursa kwa raia, kuwa na wawakilishi wanaotetea maslahi ya wanaowawakilisaha hasa maskini na wanyonge.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapanua maana ya Utawala Bora katika wajibu wa Kikatiba kwa viongozi katika Ibara ya 9 inayosema, “Viongozi wanapaswa kuendeleza utajiri wa Taifa, kuuhifadhi na kuutumia kwa manufaa ya wananchi wote.”

Itaendelea

 

Falsafa ya vita dhidi ya uhai

KATIKA Ukurasa wa kwanza wa Gazeti hili toleo lililopita, kulikuwa na habari toka Zanzibar ikimnukuu Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Mhashamu Augustino Shao, akilaumu uovu na hatari zilizopo sasa ikiwa ni pamoja na hatari ya kuhalalishwa kwa vituo vya kuangamiza uhai kwa visingizio mbalimbali huku vyombo vya dola na jamii kwa jumla, vikitazama na vingine kuhalalisha kwa kisingizio cha “uzazi wa majira”. Katika makala haya MWANDISHI WETU, anatuangalisha kwa undani juu ya  falsafa, kuanza na hata kuenea kwa utamaduni wa KIFO dhidi ya UHAI na hatimaye, tutaangalia mahitimisho ya jumla kuhusu makongamano juu ya idadi ya watu duniani. Fuatilia.

Nadharia na utekelezaji wa sera za udhibiti wa idadi ya watu zina msingi wake katika falsafa na mtazamo wa utamaduni wa kifo. Kimsingi, utamaduni wa kifo umeibuka kama upinzani  kati ya wema na ubaya. Wema na uhai ni mali ya Mungu; ubaya na kifo ni mali ya Shetani/Ibilisi. Kwa asili yake, Ibilisi ni MWONGO NA MWUAJI (Yoh. 8:44)

Utamaduni wa kifo ni matendo na maelekeo ya binadamu katika kuendeleza na kutetea hali zinazosababisha binadamu apoteze UHAI wake, audhuru mwili wake, adhalilishe utu wake na kuunfanya mwili wake kuwa bidhaa inayoweza kununuliwa  kuuzwa na kuchezewa.

Kwa hiyo, chochote kinachopingana na uhai, kama vile mauaji, utoaji mimba, kuua kwa huruma (yutanasia), chochote kinachodhoofisha afya ya binadamu, kama vile mazingira duni ya kuishi, hali mbaya za kazi, ubakaji, ulawiti, uporaji wa mali za watu walio hai au waliokufa vyote hivi, vinajenga msingi wa utamaduni wa kifo.

Sifa kuu katika utamaduni wa kifo ni kuwa, binadamu anakuwa amekufa kidhamiri na hivyo kukosa uwezo wa kutambua, kupenda na kutetea uhai na utu wa binadamu. Utamaduni wa kifo hufurahia matendo maovu na kuchukia matendo mema.

Katika utamaduni wa kifo, UONGO hutukuzwa na UKWELI huogopwa na kupigwa vita. Uongo katika utamaduni wa kifo huonekana katika kutoa takwimu za uongo na kuzitetea, katika kuficha kwa makusudi madhara ya matokeo ya matendo fulani na matumizi ya nguvu za kimabavu katika kutekeleza sera zake kwa kutumia nguvu za dola, miundo yake, vyombo vya habari na taasisi mbalimbali.

Utamaduni wa kifo huenea kwa kasi na kukubalika kwa sababu ya nguvu ya FEDHA. Mabilioni ya fedha hutumika katika kutangaza na kuhamasishwa matumizi ya nyenzo za umalaya na utasa, kama vile kondomu na vidhibiti mimba. Watetezi wa utamaduni wa kifo, hujenga chuki ya wazi na bayana dhidi ya watu/taasisi/mashirika yanayodiriki kufichua uovu unaofichika katika programu waziendeshazo.

IKUMBUKWE KUWA, Utamaduni wa kifo umeibuka kama ukinzano wa wema na ubaya (Mwa 2: 16-17; 3:1-5); Uongo na hila ndizo sifa kuu za Ibilisi. Hivyo, ndivyo anavyotunasa sisi wanadamu kwa mitego na lugha tamu. Matokeo yake ni kifo (Mwa 3:8-19).

Sote tutambue kuwa, tunaponaswa katika mitego ya Ibilisi, tunakoma (tunafuta) hali ya kimungu ndani mwetu na tunauvaa ubaya.

Wivu, chuki na hila hutokana na ubaya aliotupatia Ibilisi (Mwa. 4: 8-10). Ubaya huu husababisha kifo. Chuki na tamaa ndivyo vilivyomkumba Herode hata wakaua  watoto wachanga, akidhani kuwa katika kitendo hicho, atamwua  Yesu (Mt. 2:1-18)

Hii ndiyo chuki iliyopo sasa dhidi ya watoto wachanga wasiozaliwa. Baadhi ya watu wanawaua watoto hao wakidhani kuwa, wakizaliwa watapunguza pato la maendeleo ya jamii.  Hao, wanatumia vidhibiti mimba kuwazuia watoto kuzaliwa. Huu ni wivu usio na kifani, ni roho mbaya, ni ubaya wa ajabu sana (Ufu 12:1-7; Hek 2:23-24; Yak 1:13-15)

 

Mwanzo wa itikadi na falsafa ya udhibiti wa idadi ya watu

Itikadi kuwa ukuaji wa idadi ya watu huzuia maendeleo sio mpya. Mapema katika Karne ya Saba, Mshairi Myunani, Hesoid alilalamika vikali kuwa nchi yake, Ugiriki ilielekea kujaa watu na kwamba hali ya maisha ilikuwa ngumu kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo idadi ya watu ilikuwa ndogo.

Wakati Hesoid analalamika, ni wakati huo huo wahamiaji wa Kiyunani walikuwa wanajenga miji ya kibiashara kandokando ya Bahari ya Mediterranean. Karne mbili baadaye ustaarabu wa Ugiriki ulifikia kilele chake, ambapo uzalishaji  ulikuwa mkubwa, kazi za sanaa, uhandisi, fasihi, falsafa, hisabati na sayansi vilistawi sana.

Karne tano kabla ya kuzaliwa Yesu, Plato na Aristotle walipata wasiwasi kuwa idadi ya watu nchini Ugiriki ilikuwa kubwa wakiangalia kukua kwa idadi ya watu katika mji wa Athene. 

Huko China, Confucius na wanazuoni wenzake walihofu kuwa nchi yao ingekuwa na idadi kubwa mno ya watu wakati walipoona miji yao inaongezeka idadi ya watu.

Katika Biblia tunasoma kuwa, watawala wa Wamisri waliona kuwa Waisraeli walikuwa wakiongezeka kwa kasi  kiasi cha kutishia utawala wao. Watawala hao waliamua kuwa, busara itumike katika kuwapunguza Waisraeli hao. Na ndipo Mfalme wa Misri alipoongea na wakunga na kuwaamuru kuwaua watoto wa kiume wazaliwapo. (Kut 1:8-16).

Mwanakanisa Tertullan akiandika katika karne ya pili baada ya Kristo, alilalamika alipoona kuwa mjini Cathago, idadi ya watu ilikuwa inaongezeka kwa kasi na kufikiri kuwa hilo ni tatizo kwa dunia. Aliomba majanga, njaa, vita na matetemeko ya ardhi yaonekane kama ni matukio muhimu kama suluhisho la  kupunguza idadi ya watu.

Katika karne ya 4, Mtk. Hieronimo aliandika kuwa, dunia sasa tayari imejaa na idadi ya watu ni kubwa mno kwa ardhi iliyopo. Alipendekeza kuwa suluhisho la tatizo hili ni kwa vijana wengi kujiunga na utawa.

 

Kuimarika kwa itikadi za udhibiti wa idadi ya watu kimataifa

 

 Nadharia za Malthus (Malthusian Theses) – 1766-1834: alidai kuwa ongezeko la watu linakwenda kasi zaidi kuliko ongezeko la kiuchumi na mahitaji ya chakula. Nadharia hii bado inarudiwa leo hii ingawa bila uthibitisho wa kisayansi. Aliamini kuwa, watu maskini walikuwa mzigo kwa mali asili za dunia na hivyo hawapaswi kuishi.

Alipendekeza watu maskini wanyimwe misaada na  Kwamba, ziachwe nguvu asilia zifanye kazi yake ya mchujo na hivyo, watu wenye uwezo wataishi na wale  wasio na uwezo watakufa wenyewe.

Margaret Sanger (1883-1966) na Marie Stopes -1880-195]

Margaret Sanger alianzisha Shirika la “American National Birth Control League” mnamo 1914. Alipinga kuwapa watu maskini likizo ya uzazi. Alipendelea kufutilia mbali watu weusi na wale wasio na akili ambao aliona walikuwa wanaongezeka kwa kasi. Aliwaita watu hao “magugu”. Alipendekeza kuwatumia wachungaji weusi ili kuondoa kizazi cha watu weusi.

 Margaret Sanger na Marie Stopes walipendelea upatikanaji wa upeo wa raha kwa mtu binafsi. Kwa kadiri ya nadharia hii, mwenzi (partner) anakuwa muhimu tu kama analeta raha na faida. Kwa hiyo, watetezi hawa wanahubiri mapenzi huria (free love); matumizi ya vidhibiti mimba (contraception); watu kukanakana ndoa; wanapendelea ubaguzi (racism) na uwepo wa kizazi bora (eugenics).

Mnamo 1920 Margaret Sanger alimnukuu Aristotle kwa kukubaliana naye kuwa walemavu waachwe wafe. Alitaka iwe  sheria kuwa, kizazi kilicholaaniwa kisiachwe kuishi. Alisema kushindwa kwetu kuwatenga watu tahira wanaoendelea kuzaana na kuongezeka, kunathibitisha kushindwa kwetu kuona umuhimu wa jambo hilo.

Nadharia za Margaret Sanger ziliungwa mkono na watetezi wa nadharia za kizazi bora nchini Ujerumani. Adolf Hitler: kunako 1935 na kuendelea, alianza kutekeleza nadharia za uzao wa kizazi bora kwa nguvu sana. Mnamo Septemba 1939 alitoa waraka wa siri uliowataka watu wote wenye magonjwa yasiyotibika wauawe.

Kutokana  na waraka huo katika idadi ya Wajerumani milioni 80,  watu milioni 1.4 kati yao waliingia katika kundi hili. Mnamo Oktoba 1939 hadi Agosti 1941 kati ya watu 70,000 na 80,000 waliuawa katika programu iliyoitwa ‘T.4’.

Programu za kizazi bora za Hitler zililenga kuondoa duniani watu wa kizazi hafifu – walemavu, wagonjwa na matahira. Hitler aliendelea kuwaondoa watu hao kwa njia mbalimbali, zikiwemo za kuwaua katika kambi maalumu [concentration camps] na kuwafunga watu kizazi [sterilization]

 

Kutoka nadharia hadi utekelezaji

 MARIE STOPES

 

Mwaka 1921 Marie Stopes alianzisha kliniki ya uzazi wa mpango (kudhibiti kizazi) huko Uingereza katika eneo la watu maskini na baadaye shirika la kimataifa “Marie Stopes International” lilianzishwa kwa jina lake. Kwa sasa shirika hili linafanya kazi katika nchi 38 duniani, nyingi zikiwa nchi maskini, ikiwemo Tanzania. Shughuli za Shirika hili ni kutoa mimba, kufunga kizazi, kugawa/kuuza kondomu na uzazi wa mpango kwa kisingizio cha “afya ya mama na mtoto”.

 

 

Mjane wa Kiafrika anavyoteseka

l  Ni kweli wanahusika na vifo vya waume zao?

Wajane wengi wa Kiafrika wamekuwa wakipata matatizo sana wanapoondokewa na waume zao. Hii kwa kiasi kikubwa, inatokana na mila na desturi za Kiafrika zinazowafanya wanyanyaswe na ndugu wa mume. Ungana na makala haya ya THECKLA SHIJA, uone baadhi ya adha za mjane wa Kiafrika.

Nomvula Bhengu alikuwa mwanake mwenye mafanikio katika maisha hadi wakati mume wake anafariki. Alijiona wazi hahangaiki tena na majonzi aliyokuwa nayo, bali sasa anasumbuliwa na mila na desturi zilizowafanya wazidishe kibano kwake ili azifuate akiwa mwanamke wa Kiafrika baada ya kufiwa mume.

Anasema “Mume wangu alikutwa amefariki ghafla kwenye gari lake bila sababu yoyote inayoeleweka. Ilitokea kama mwaka mmoja uliopita. lakini ninaendelea bado kufanya uchunguzi kwani uchunguzi wa polisi umeishia tu kuwaweka baadhi ya watu ndani na hukumu bado haijatolewa.”

Anaendelea, “Nakumbuka vizuri usiku Gerald alipofariki. Ilikuwa kama saa tisa za usiku nilipoamka toka usingizini na kukuta watu wamejaa mlangoni kwangu. Kwa kawaida, Gerald alikuwa anarudi nyumbani usiku sana na wakati ule hakuwepo ndani, niliogopa sana.”

“Nilijua lazima kutakuwa na tatizo. Nikachanganyikiwa na kukimbilia chumbani kwangu huku nikilia. Mara, shangazi akafichua siri kwamba, Gerald amefariki.

Watoto wangu Thambo aliyekuwa na umri wa miaka 12 wakati huo na Phumzike miaka 7, walizipokea habari za kifo cha baba yao kwa msikitiko makubwa. Nilijaribu kujikaza kwa heshima yao lakini, mambo yalizidi kwenda vibaya tokea hapo.”

Nilikazana kuwa karibu na mama mkwe wangu aliyekuwa anaishi kati ya mji wa Johannesburg na Bizana.” Mwanamke huyo wa Afrika Kusini, alikaririwa na jarida la FEMINA.

Akaendelea, “Kwa kweli familia ya Gerald ilinitenga hata kabla mwanao hajazikwa kwani hata shangazi niliyemtuma akatoe taarifa za msiba badala yangu, alijibu kwa shida sana.

Nilikuwa mshukiwa wa kwanza katika familia ya marehemu ya kwamba ni mimi, niliyemuua Gerald kitu ambacho ni jambo la kawaida mjane kuhusishwa na kifo cha marehemu. Ulikuwa ni ushukiwa wenye maumivu makali sana.

Nilibaki kuwa mjane nisiye na haki wala upendeleo wakati awali, nilikuwa na maisha mazuri ya ndoa na nilikuwa mama mwema. Sikuwa na la kusema hata ilipofikia wakati wa kutoa mawazo kuhusu mazishi.”

Akizidi kusimulia kwa uchungu mintarafu matatizo yanayowakumba wajane wa Kiafrika, Bibi Bhengu anasema kuwa, uwezo aliokuwa nao ulikuwa wa kulipia shughuli zote za mazishi kwani familia ya Gerald ilisema, haiwezi kugharamia mazishi.

“Lakini bado mawazo yote ni wapi atazikwa walikuwa wanapanga viongozi wa familia yao. Zilikuwa ni mila za kizamani lakini, kwa upande wangu ilikuwa kama ukatili kuiga mila hizo,” anasema.

Anazidi kuelezea akisema, “Ilinibidi niandae mazishi jambo ambalo nilikuwa sijwahi kufanya maishani na katika kila hatua niliyokuwa nikiifanya, nilikuwa naongozwa na familia ya Gerald. Alisha kuwa amepanga ni wapi azikwe lakini, yote hayo yalikuwa yamezimwa na famlia yao na wakapanga wao wenyewe.

Ilinibidi nichukue mwili wa marehemu kutoka Cape Town kwenda nyumbani kwao na kwa kipindi chote hicho, sikuwa na mawasiliano ya karibu na mama mkwe wangu.

Hakunipigia simu na ilibidi nimtumie shangazi yangu kama mjumbe. Yote haya, yalikuwa muendelezo wa uhusiano wangu na yeye usioridhisha kwa muda mrefu. Nilipofika hakunikaribisha vizuri. hii ilinionesha wazi kuwa, hakufurahia chochote nilichokuwa ninafanya.”

“Kwenye mazishi sala zote zilikuwa zikielekezwa kwa Gerald na mama yake na wala si kwangu na watoto wangu. Niliumia sana na hata mjomba wake hakuwa akisikitika pamoja nami.

Baadaye, niliona banchi la maua yasiyo ya kawaida na niliposoma ujumbe ulikuwa umeandikwa hivi, “Kutoka kwa binti yako.” Nilichanganyikiwa lakini baadaye, nikadhani ni kutoka kwa kaka yake Gerald.

Mara nikagundua mwanamke mmoja akiwa na mtoto mdogo na nilivyomtazama huyo mtoto, alikuwa na sura iliyofanana na mume wangu. Nilipatwa na mfadhaiko wa ghafla, kumuona mke mdogo wa mume wangu na mtoto wake katika mazishi wakipewa heshima namna ile kuliko mimi.

Nilipigwa na butwaa wala sio hasira kwani nakumbuka mume wangu muda wote alikuwa analala nyumbani. Lakini, kilichonishangaza zaidi, mama mkwe alikuwa anamfahamu mwanamke huyo na kumkubali.

Baadaye, binamu wa mume wangu akanieleza kuwa, Gerald alishamkutanisha huyo mwanamke na familia yake.”

Aliendelea kulalamika akisema hivi sasa, alikuwa analaumiwa yeye kuhusiana na kifo cha mumewe wakidai kuwa, aliyemuua Gerald ni mpenzi wa mwanamke huyo.

Mwanamke huyu ni kiwakilishi cha wanawake wanaoteseka barani Afrika Tanzania ikiwamo kutokana na mila na tamaduni mbovu dhidi ya wajane.

Nchini Tanzania na hata kwingineko Afrika, utamaduni wa wazazi na ndugu wa mume kumchagulia kijana mke wa kuoa, ni mionhoni mwa vyanzo vya matatizo yanayowakabili wanawake wanaofiwa waume zao.

Hapo, ndipo kinyongo chote cha ndugu huishia kwa kumnyanyasa ikiwa ni pamoja na kumsingizia kuwa, umalaya wake ndio umesababisha kifo cha mumewe.

Wengi yakiwamo baadhi ya makabila ya Tanzania, wanaamini kuwa, kifo cha mwanaume daima lazima kina mkono wa mwanamke ama kwa ushirikina, au njama yoyote. Wazo hili ni hatari kiroho na kimwili hasa katika kipindi hiki ambacho watu wanamjua zaidi Mungu katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Si jambo geni kusikia ndugu wa mwanaume (marehemu) akiwamo mama au baba, wakiongoza jahazi la kudai mali zote za familia ya marehemu bila kujali mkewe na watoto wataishi vipi endapo watanyang’anywa haki zao.

Mfano mzuri ni pale mjane huyo anaposema kuwa, kuyokana na matatizo baina yake na mama mkwe yaliyoanza tangu kipindi Gerald anamchumbia, kutokana na mama huyokutaka kijana wake aoe mwanamke mwingine, ilifikia hatua hata akakataa kufika nyumbani kwao.

Anasema kitendo cha Gerald kumuoa yeye na kuhama, kulilimuuma sana maana aliona kama ameondolewa chanzo chake cha pesa.

Anasimulia kuwa, Mama yake Gerald alizidi kuchukizwa baada ya kugundua anapata pesa nyingi kuliko mwanae kwani nalikuwa mwanamke naliyesoma na mwenye elimu ya juu na hata wakati wa mahafari yake, alimwalika lakini, akakataa . ”… Gerald alijaribu kusuluhisha ugomvi huu wakati wa uhai wake lakini hakufanikiwa,” anasema.

Mjane wa Kiafrika pia katika jamii nyingi, anatakiwa aishi maisha fulani maalumu kwa kipindi kinachopangwa na familia ya marehemu. Mjane anatakiwa avae nguo nyeusi na kitambaa kwa muda wa kati ya miezi mitatu .

Mjane hulazimikakuzivaa kila wakati na hata unapopanda gari hutakiwi kukaa mbele kwani inaaminika kuwa, ni nuksi.

Anasema, “Familia ya Gerald iliniamulia kukaa eda kwa miezi tisa kitu kilichokuwa si kawaida. Ilibidi nimwombe shangazi yangu akawaeleze kuwa mimi sitakaa kwa miezi hiyo. Nilimtumia shangazi kwani ndiye aliyekuwa akijadiliana nao badala yangu.

Wakati nikiwa eda, sikuendelea vema na maisha yangu na hata ilipofika siku ya kumaliza msiba, hawakuniruhusu kumwalika rafiki yangu yeyote katika sherehe, kitu ambacho kilikuwa muhimu katika maisha ya familia yangu, lakini mila na desturi ndizo zilizokuwa zikipewa kipaumbele zaidi.

Sikuwa najali kuomboleza msiba wa mume wangu, nilikuwa bado namuomboleza lakini kilichokuwa kinanisikitisha, ni jinsi hii jamii inavyonitenga na kunibagua kama mtu wa taifa jingine.”

Wakati wajane wa kike wanateswa na masaibu mengi ikiwa ni pamoja na kufukuzwa nyumbani, kunyimwa huduma zote muhimu na pengine kupigwa na ndugu wa marehemu, hali ni tofauti kwa mjane wa kiume (mwanaume anayefiwa mkewe). Yeye huishi anavyotaka baada ya mazishi na hata katika kipindi cha msiba.

Mwanaume hana mavazi maalumu katika kipindi cha maombolezo. Hali hii, inaonesha kuwa, bado waafrika wengi wakiwamo baadhi ya wanajamii wa Kitanzania, wamepitwa na wakati kwani wanaendekeza na kuendeleza ubaguzi. Hawalazimishwi kuvaa mavazi meusi; hawakatwi nywele! Kwanini ubaguzi uwepo?

Kwa kweli mila hizi zinahitaji marekebisho ya hali ya juu kulingana na maisha ya sasa kwani zinawakandamiza wanawake.

Kwa mjane wa kiume, anaruhusiwa kuoa wakati wowote lakini kwa mjane wa kike, ajaribu kuishi na mume baada ya kifo cha mumewe aone mateso atakayovuna toka kwa ndugu wa mume; usawa na haki katika ndoa viko wapi?

haieleweki ni kwanini mjane mwanamke anakuwa kichwa cha kupata uangalizi huu wa ajabu, na kwa nini maisha yao yanafanywa kuwa magumu baada ya kufiwa waume.

Wajane wa Kiafrika wanatakiwa kuamka na kutetea haki zao. Lazima waeleze kila mmoja kwamba, matarajio wanayoyapata kama wajane ni kutokutendewa haki na ni uonevu mkubwa.

Mama huyo Msouth anakaririwa akisema, “Nakumbuka siku ya harusi yetu. Mzee mmoja aliniasa kwamba, mume anaposema anakwenda  kazini au mkutano, hutakiwi kumuuliza ni wapi; anakwenda na nani au atarudi kwa sababu hata yeye mwenyewe hafahamu.” “Labda kauli hii ilinipumbaza.”

Umefika sasa wakati  jamii nzima ikaungana kuzipinga mila zozote zinatowabagua, kuwatenga na kuwanyanyasa wanajamii wakiwamo wanawake. Watu wote wajue kuwa, kila mtu ameumbwa kwa mfano na mapenzi ya Mungu na kwamba watu wote, wana haki sawa mbele za Mungu.

Hata hivyo, juhudi hizo za usawa, zisiwe zinazoelekea kukiuka mpango wa Mungu katika uumbaji.

 

 

HOJA ZA KIBIBLIA

 

Kwanini mitume wengine hawakuandika Injili?

 

Katika toleo hili, Mtaalamu wetu wa Biblia, Padri Titus Amigu, anajibu swali la msomaji wetu anayetaka kujua zaidi mintarafu Injili. Yeye aliuliza akisema, “Nafahamu kwamba mitume wa Yesu walikuwa 12 lakini, walioandika Injili walikuwa wanne tu. Kwanini hawakuandika wote? Au hao hawakuwa mitume, bali wandishi wa habari wa Yesu Kristo?

JIBU: Ndugu Msomaji, kuandika kitu licha ya kuwa ni kipaji cha mtu, pia ni hiari ya mtu mwenyewe anayejua kusoma na kuandika. Kwa mfano, wewe mwenyewe; je, umewahi kuandika kitabu juu ya matukio katika ukoo wenu? Kama umefanya hivyo, hiyo ni bahati yako lakini kama hujafanya hivyo, jiulize ni kwanini?

Basi waliaoamua kuandika habari za Yesu Kristo na kutuambia alivyoishi na kufanya mambo yake hapa duniani, walikuwa wengi sana. Soma na uhakikishe hilo katika Injli ya Luka (Lk 11-4). Walikuwamo mitume na wasio mitume yaani, wafuasi kadhalika. Hao, ni wengi sana walioamua kuandika.

Ndugu msomaji, wakati ule hakukuwa na mambo ya uandishi wa habari. Hayo ni maendeleo ya siku hizi tu. Ila kuandika, wale wenye hiari na vipaji walifanya hivyo kwa habari zile zilizowavutia. Basi kukawa na maandishi mengi sana.

Kwa bahati mbaya kwa wakati ule, waandishi hawakujitaja waziwazi labda kwa vile walitaka kuishi kinyenyekevu bila kujigamba kama waandishi. Kuhusu majina ya waandishi, basi yakawa yanatajwa mengi tu na ilipofika karne ya pili hadi ya nne na kuendelea, maandishi yote yalikusanywa na kuchaguliwa yale yaliyokuwa safi sana na yenye kuhimiza upendo na imani; yale yaliyokubalika na kupokelewa na Wakristo wengi; yale yasiyopingana na mafundisho ya msingi; yale yasiyotilia chumvi mambo wala mbwembwe.

Hayo yakachaguliwa na Uongozi wa Kanisa na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, yakawekwa pamoja na ndipo tukapata Biblia.

Hapo, yakapatikana maandishi safi yasiyo na mbwembwe wala jeuri ndani yake yaliyofika 27. Maandishi hayo ndiyo yaliyotimiza sifa zote zile nzuri.

Ndiyo hayo maandishi yaliyo katika Agano Jipya; Injili nne za Mathayo, Marko, Luka na Yohana. Mengine ni Kitabu kimoja cha Historia yaani MATENDO YA MITUME; Barua 14 yaani Barua kwa Warumi; Barua ya Kwanza na ya Pili kwa Wakorintho, Barua kwa wagalatia, Barua kwa Waefeso, Barua kwa Wafilipi, Barua ya Kwanza na ya Pili kwa Wathesolanike, Barua ya Kwanza na ya Pili kwa Timotheo, Barua kwa Tito, Barua kwa Filemoni na Barua kwa Waebrania na mwisho, kitabu kimoja cha kinabii; ndio UFUNUO WA YOHANA.

Basi, kimajina, mitume wengi walikuwa wamehusishwa na maandishi lakini, kama ni wenyewe waliandika, au la, au labda wanafunzi wao waliandika na wakatumia majina hayo, hakuna anayejua kwa uhakika. 

Maandishi yote yasiyokuwa mazuri hata yale yaliyokuwa na majina ya mitume, yakaachwa katika mchujo huo.

Ndipo  tukabakiwa na  maandishi yaliyopo katika vitabu hivyo 27 ambavyo vipo katika Agano Jipya. Kati ya maandishi hayo au vitabu hivyo, vichache vinaunganishwa hasa na mitume ambao tunaweza kutafuta habari zao kwa uhakika yaani Injili ya Yohane na Injili ya Mathayo.

Marko na Luka walikuwa wafuasi tu; sio mitume na tena wafuasi wa Mitume Petro na Paulo na wala hawakuwa wafuasi wa Yesu moja kwa moja. Barua nyingi zinaunganishwa na Paulo ambaye alikuwa Mtume, lakini sio kati ya wale mitume 12.

Kwa hiyo basi, unaona jinsi majina yanavyolegalega kidogo, lakini ujumbe wao ni mzuri katika vitabu hivi.

Kwa vyovyote, ni watu waliohusiana na Yesu Kristo kiimani, walioandika vitabu vya Biblia yetu yaani ,Agano Jipya na siyo waandishi wa habari maana, kwa enzi zile za kale, hawakuwapo waandishi wa habari.

Vitabu vingine viliandikwa na vilihusika pia na habari za Yesu Kristo kama vitabu vya Agano Jipya tulivyo navyo. Vitabu hivyo lakini, kwa kutokidhi haja na uadilifu uliotakiwa na wale waliochagua vitabu kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu, viliachwa.

Vitabu hivyo vina mbwembwe na maelezo mengi yasiyojenga lolote; vina habari nyingi zilizotiliwa chumvi na kadhalika.

Mfano ni kama vile vitabu vya Injili ya Filipo, Injili ya Petro, Injili ya Ukweli, Injili ya Ukamilifu, Injili ya Mikoa Minne ya Mbinguni, Injili ya Mitume Kumi na Mbili, Injili ya Wafusi Sabini, Injili ya Mathias, Injili ya Yuda, Injili ya Bathlomeo, Injili ya Maria na Injili ya Koritus.

Mifano mingine ni Injili ya Basilibesi, Injili ya Mwanzo wa Yakobo, Injili ya  Nikodemo, Matendo ya Paulo, Matendo ya Petro, Matendo ya Thomas, Barua kwa Leokardia, Barua Kati ya Seneka na Paulo, Barua ya Kughushi kwa Tito, Ufunuo wa Paulo, Ufunuo wa Thomas na kadhalika.  Hivyo vyote, havikukidhi sifa za Injili, basi vikaachwa.

Hivyo, ni wazi wengi waliandika kiasi hata haijulikana ni nani alikuwa mwandishi mtume kwelikweli.

Hata hivyo, kama nilivyosema, hawa walioandika hata kama hawakuwa ni mitume moja kwa moja, walikuwa wafuasi wa Kristo kwa maana  hii kwamba, walimsikiliza na kumpenda kwa namna moja ama nyingine.

Hawa hawakuwa waandishi wa habari maana enzi zile waandishi wa habari hawakuwapo kwa vile magazeti, televisheni na redio, hazikuwapo. Ni vyombo hivyo vinavyohitaji waandishi wa habari. Haya mambo ya kuwa na waandishi wa habari ni yetu siku hizi. Hayakuwa yao katika enzi zao zile.

 

 

 

 

NIONAVYO MIMI

 

‘Tunataka Mwaka Mpya, Mtazamo Mpya’

Na Pd. Baptist Mapunda (M.Afr)

Tunaposherekea sikukuu ya kuanza mwaka, tena mwaka mpya wa 2005, lazima tukumbuke kitu kimoja kwamba, hii ni siku ya kuombea Amani Duniani kadiri ya utamaduni wa Kanisa Katoliki duniani.  Kwa mantiki hii, ni vema kurejea ujumbe wa  Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika siku hii.

Ujumbe wenyewe ni huu unasema kwamba, “Msishindwe  na uovu, bali ushindeni uovu kwa kutenda wema.”  Maneno hayo ya Baba Mtakatifu ameyatoa katika Barua ya Mtakatifu Paulo kwa Warumi (Rum 12:21).  Baba mtakatifu anaendelea kusema kwamba, “Huwezi kuushinda uovu kwa kutumia uovu.”

Watanzania tunapoanza mwaka mpya na kuiombea dunia amani ikiwemo Tanzania, tukumbuke kuwa, “Amani inapatikana tu, iwapo tutadumu katika kutenda wema.” Hii ni changamoto kubwa kwa Watanzania hasa tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.

Nikiwa katika likizo ya Krismasi nyumbani Mbinga, Ruvuma, nilisoma magazeti kadhaa yalikuwa yamesheheni jumbe mbalimbali za Sikukuu ya Kuzaliwa Bwana Wetu Yesu Kristo.

Ujumbe mmoja  ulionifurahisha, ni ule wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliposema, “Watu wenye uchu wa madaraka na uroho wa mali hawawezi hata siku moja, kudumisha amani, mshikamano wa kitaifa, upendo na undugu kati ya Watanzania.” Nami daima nimeamini hivyo, kwani uongozi bora unahitaji sadaka kubwa.

Kwa muda mrefu nchi yetu imejulikana kama nchi yenye amani na mshikamano wa kitaifa.  Lakini, matukio ya hivi karibuni haoneshi kuwa, tunaendeleza tunu hiyo, bali sasa nchi inaonekana wazi kuelekea kubaya.

NIONAVYO MIMI, amani ya kweli inaambatana na Ukweli maana ni kwa ukweli, tutawekwa huru. Ukisoma magazeti na kusikiliza mazungmzo ya watu nchi nzima, unapata picha kwamba uhuru unakosekana katika sehemu nyingi.

Uhuru unakosekana kwa vyombo vya habari katika sehemu za nchi yetu, wandishi wa habari wanawoga mkubwa kuripoti matukio maovu kwa hatari ya kufuatwa na vyombo vya dola. Kuna kukosekana kwa uhuru wa watu kueleza yale wanayoyaona, wanayoyaishi, na kadhalika.

Hali hii haiashirii kudumu kwa amani inayoanzia mioyoni mwetu, na kama mioyo yetu inakuwa na woga na malalamiko kila wakati, basi hii ni shida kubwa katika jamii; kwani amani itakuwa ya maneno tu, huku wengine wakiwa kama mshumaa unaongua ili kuangazie wengine.

 Kamati ya Haki na Amani imetoa bango lisemalo, “HOFU NI SUMU.” Hivyo, tunapoanza mwaka mpya, tuuanze kwa kubadili mitazamo ili tujitafiti ni kwa nini watu wengi wasomi na wasiosoma, wote tumegubikwa na hofu na hivyo, kutosema ukweli.  

Kwa mang’amuzi yangu, moja ya sababu ni kukosa kufahamu haki za msingi katika jamii. Nikiwa Mbinga katika likizo hiyo, nilijifunza mengi toka kwa Wana Mbinga, jinsi hofu ilivyotanda katika maisha ya watu. Hii inanipa picha kwamba, maendeleo huko hakika ni ndoto ya mchana maana, bado watu hawataki kubadili mtazamo.

Jitihada kubwa zinatakiwa ili kuwakwamua watu kutoka katika wimbi la hofu. Mtu akieleza ukweli juu ya jamii, siasa, uongozi na umasikini, anaonekana kuwa adui wa chama fulani au Serikali. Ni kwa nini? Hapa, elimu ya uraia inahitajika sana katika jamii ili kusaidia kuendeleza  amani.

NIONAVYO MIMI, Tunapoanza Mwaka Mpya, Watanzania tuwe na mtazamo mpya wa Kuupenda Ukweli na kupenda kusikiliza maoni ya wengine hasa kwa viongozi wetu.  

Sio siri, siku hizi katika nchi yetu inaonekana kama vile kusema ukweli ni kutenda dhambi. Rais Benjamin Mkapa aliyebakiwa na miezi kumi akiwa ofisini, alipochukua madaraka ya nchi hii alitangaza sera, sera aya “Uwazi na Ukweli.” Je, inakumbukwa? Inaheshimiwa na kutekelezwa?

Naamini sera hii ni nzuri, lakini je, Watanzania tunaifuata? Mwaka huu 2005 uwe mwaka wa uwazi na ukweli na hasa katika kupendekeza, kukampeni na kuchagua viongozi mbali mbali wa taifa akiwemo Rais wa nchi atakayefuata nyayo za Rais Mkapa huko Ikulu

Hata hivyo inaanza kutia moyo kuona kuwa, kadri siku zinavyopita, watu wanazidi kupata uelewa juu ya maisha yao, siasa, uongozi, maendeleo, halikadhalika,  imani yao. Maendeleo ya kisayansi na teknolojia, nayo yanawasaidia watu kuuelewa ulimwengu na kujifunza namna wenzetu katika nchi nyingine, wanavyoendesha demokrasia ya vyama vingi bila uoga, chuki wala uadui toka pande zote za watawala na wataliwa.

Mawasiliano ya mtandao  nayo  yanapanua uelewa wa kiakili pamoja na kwamba wakati mwingine, mtandao huo unaleta mambo yaliyo kinyume na utamaduni wetu. Kiongozi wa Tanzania ya leo asijidanganye kuwa watu wamelala la hasha! Watu wanaelewa mambo mengi sana, ila tu hawana nguvu na nafasi ya kusema ukweli huo bila kutiwa matatani.

Kusema ukweli kunadai sadaka, tunajua yaliyompata Yesu Kristo, alikufa kwa sababu ya kusema na kutetea ukweli. Nchi yetu kama nilivyosema awali, inahitaji manabii. Kadri tunavyouelekea Uchaguzi Mkuu, manabii hao wanazidi kuhitajika kwa nguvu zaidi.

Watanzania tuna misamiati mingi sana ya kutufundisha mathalani, “Tenda wema uende zako, usingoje shukrani.” Hivyo, sote tutambue ukweli kuwa, “uongozi” ni utumishi siyo “utawala.” Hii ni kuanzia makanisani, serikalini, katika chama, taasisi na jamii kwa jumla.

Si mara chanche tunawasikia watu wanalalamikia uongozi kuwa ni wa kiutawala zaidi kuliko kiutumishi. Kwa mtindo huo, nidhahiri kuwa amani itatoweka tu; kwa vile hakuna masikilizano wala heshima kwa wale wanaoongozwa maana wanaburuzwa kama bakuri linaloelea baharini.

Sasa, Watanzania tubaki kuwa watu wa kuburuzwa tu!? Hapana! Sasa tuanze Mwaka Mpya na mtazamo unaotekezeleka kuwa, watu wenye uchu wa madaraka na uroho wa mali hawatufai na hatuwataki.

Kwa msingi huo, tusiwe vinyonga unababilika rangi ghafla baada ya kuona shilingi 2000, au T-Shirt yenye picha ya mgombea hata kama hafai kukuondoa katika ugumu wa maisha unaokukwaza. Hivi tunapodanganywa kwa bei rahisi namna hii, anayeumia ni nani?

Ni wazi kuwa, uongozi ni dhamana anayopewa mtu au kikundi kwa manufaa ya jamii nzima hivyo, watanzania tuuige mfano bora wa wajumbe wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuamua kufanya mabadiliko ya dhati na kweli, wakatekeleza nia yao.

Watanzania tukubali kuwa, watoa rushwa hawatufai, wala rushwa, hawatufai na hata wanaotoa amri za kijeshi bila kutaka maoni ya wengine, pia hatufai.

Kwa mtazamo wangu, Mwaka Mpya uanze kwa kuipa PCB meno ya kumng’ata mwizi bila kujali mwizi ana umbo la tembo, simba au chui eti huyo asionwe, lakini sungura na dagaa kwa mwili mdogo na upole wao, wanaswe kwa mitego ya shilingi 10,000/=

Katika Barua hiyo ya Mtakatifu Paulo katika ujumbe wa Baba Mtakarifu, tunamwona akikazia kwamba, “Usilipe uovu kwa uovu” (Rum 12:17).  Hivyo basi, tuushinde uovu kwa kutenda wema.

Yesu Kristo anasema, “Achaneni na utamaduni wa “jino kwa jino.” Upendo ndiyo njia ya Kristo hivyo, tuwapendeni hata adui zetu. Kwa kulijua hilo ni gumu katika maisha yetu anasema, hiyo ni “Amri” wala siyo “ombi.”

NIONAVYO MIMI, Tunapoanza Mwaka Mpya wa 2005 wa Uchaguzi Mkuu, viongozi wa siasa waache  visasi kati yao, na maneno ya kuchochea chuki kwa wananchi. Tukumbuke kuwa, amani iliyopo ni zawadi toka kwa Mungu; ni mpango wake Mungu kama alivyotuasa Kardinali  Pengo katika  mahubiri yake ya Noeli.

Katika mwaka huu tuliouanza, wapiga kura tuwachuje watakaogombea katika nafasi mbalimbali za uongozi na tukitambua kuwa, huyu ni mtu wa kisasi, basi tumtupilie mbali kwani atakuwa kichocheo na chanzo cha kutoweka kwa amani yetu ambayo ni zawadi ya Mungu.

Mtazamo wetu uwe wa kuchagua watu wanaoendeleza nchi yetu kwa masilahi ya wote,  ya siyo ya kikundi fulani tu, au mtu binafsi. Watu wenye uchu wa madaraka na mali, chuki na uchochezi ni wa kuepukwa kama ukoma, ebola na magonjwa mengine hatari.

NIONAVYO MIMI, Kila chama cha siasa kipendekeze watu wanaokubalika  na jamii na siyo vyama vyao. Tusipendekeze watu kutokana na hisia HUYU NI MWENZETU, bali tutazame amani, umoja, mshikamno na maendeleo ya Taifa.

Kila Mtanzania aombe kuongozwa na Roho Mtakatifu katika kutekeleza wajibu huu. Tujiulize; HUYU MWENZETU NI NANI na KWA MANUFAA YA NANI?

Mwaka huu uwe wa kutazama maslahi ya wote hasa maskini huko vijijini ambao wapo hoi kabisa. Asiyeamini niyasemayo, aende kijijini aishi huko kwa wiki mbili tu, kasha arudi aniambie alichobaini huko.

Mwaka 2004 ulikuwa wa matukio mengi sana, ambapo maovu yalizidi, mathalani; ubakaji, uvutaji bangi,  ubadhirifu wa mali ya umma, wizi wa fedha katika mabenki, malumbano ya kisiasa, ugaidi, na kadhalika.  Haya sasa, tuyaache yaende; sisi tuanze upya, ya kale yamepita, tusonge mbele kwa matumaini na Imani, kwamba Yote tutayashinda pamoja na Mwokozi  Wetu  Yesu Kristo.

NAWATAKIENI HERI YA  MWAKA MPYA NA  BARAKA TELE 

 

 

SHERIA

Mtu binafsi, Vyama vinaruhusiwa kumiliki Majeshi ya Ulinzi?

Na Dotto Shashi

 

HIVI karibuni kulitokea mjadala mkubwa wa umma uliosabishwa na tamko la Kiongozi mmoja wa Chama cha Siasa nchini, ambaye alieleza nia ya chama chake kutaka kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya kulinda mali za chama hicho.

Kauli ya kiongozi huyo iliifanya Serikali iingilie kati  suala hilo na mpaka ikafikia hatua ya kutoa ufafanuzi wa kisheria dhidi ya tamko la kiongozi huyo.

Japokuwa kiongozi huyo alieleza moja kwa moja majukumu ya kikundi hicho cha ulinzi kuwa, ni kulinda mali za chama hicho. Kwa mtazamo halisi na wa kimsingi, kikundi hicho hakitofautiani kimaana na jeshi lililopo hivi sasa nchi la ulinzi kama inavyoainishiwa katika katiba yetu.

Katika mada ya toleo hili, tutaangalia katiba inaeleza nini juu ya Majeshi ya Ulinzi nchini, yaani “The Armed Forces.” Ikiwa ni pamoja na mambo mengine kuhusiana na majeshi hayo.

Sura ya Tisa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho mbalimbali, inaeleza kuhusu Majeshi ya Ulinzi.

Kifungu cha 147 Ibara ndogo ya Kwanza (1) cha Katiba kinaeleza kuhusu katazo kwa mtu au kikundi cha watu au serikali, kuanzisha au kuwa na Jeshi la Ulinzi la aina yeyote ile nchini Tanzania, isipokuwa serikali pekee.

Katika ibara ndogo ya Pili (2) yaani “Sub Article (2),” inaeleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano inaweza kwa mujibu wa sheria, kuanzisha au kumiliki majeshi ya aina yeyote Tanzania, kwa makusudi ya ulinzi na usalama wa nchi (kwa maana ya mipaka) pamoja na watu wa Tanzania.

Kimsingi hapa tunaona kuwa, ni serikali pekee yenye uwezo wa kuanzisha na kumiliki jeshi, hivyo kwa mtu binafsi kama tulivyoona hapo mwanzo, sheria inamkataza, vivyo hivyo kwa chama cha siasa.

Tukiendelea kutazama zaidi sifa za majeshi ya ulinzi na usalama, tunaona kuwa, Ibara ndogo ya tatu, katika kifungu hicho cha 147 cha Katiba, inaeleza kukatazwa kwa askari yeyote wa jeshi la ulinzi na usalama kujiunga katika chama chochote cha siasa, isipokuwa katiba inampa haki ya kupiga kura askari huyo, kama ilivyoainishwa katika kifungu cha Tano (5) cha Katiba.

Labda mpaka hapo mtu anaweza kuwa anajiuliza swali kuwa je, askari wa majeshi ya ulinzi na usalama ambaye amekatazwa na katiba yetu kujiunga na chama cha siasa ni yupi?

Swali hili linajibiwa na ibara ndogo ya nne (4) ya kifungu cha 147 cha katiba. Kwa mujibu wa ibara hiyo, askari wa majeshi ya ulinzi na usalama, maana yake ni askari aliye katika ajira ya ama Jeshi la Ulinzi, yaani “Defence Forces,” Jeshi la Polisi (Police Force), Magereza, yaani (Prisons Service) au Jeshi la Kujenga Taifa, Yaani “The  National Service” aliyekatika ajira hiyo ama kwa masharti ya muda au masharti ya kudumu yaani “Temporary or Permanent terms.”

Sasa tuangalie mamlaka ya Amiri Jeshi Mkuu, yaani, “Powers of Commander in – chief.”

Katika kifungu cha 148 Ibara ndogo ya kwanza kinaelezea mamlaka ya Amiri Jeshi Mkuu, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Ibara hiyo ndogo inaeleza kama ifuatavyo:-

“Bila kuathiri sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge, miongoni mwa mamlaka ya Rais kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, ni pamoja na kuamrisha majeshi ya ulinzi. Kujiingiza au kufanya shughuli za Operesheni za kijeshi zihusianazo na ulinzi wa Jamhuri ya Muungano, kufanya shughuli za uokoaji (Rescue) kwa ajili ya kuokoa maisha na mali nyakati za hatari na au masuala mengine yoyote endapo Amiri Jeshi Mkuu ataona inafaa na lazima.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, shughuli/operesheni hizo Amiri Jeshi Mkuu, anaweza kuamrisha zifanyike ndani au nje ya Tanzania, mfano ushiriki wa jeshi la wananchi la Tanzania katika kulinda amani nchini Liberia, miaka michache iliyopita, kushiriki Kongo baada ya Mabutu kuondolewa Msumbiji wakati wa vita vya ukombozi n.k.

Katiba pia imeeleza mamlaka mengine ya Amiri Jeshi Mkuu ambaye ndiye Rais katika Ibara ndogo ya Pili (2) ya kifungu cha 148 kuwa ni pamoja na:-

 (a)  Mamlaka ya kuwateua makamanda wa juu katika majeshi ya ulinzi ya Jamhuri ya Muungano.

(b)   Kuajiri au kuachisha watu kutoka majeshi ya ulinzi.

(c)   Mamlaka ya kuteua makamanda wa vikosi mbalimbali vya majeshi ya ulinzi na kusimamisha mamlaka ya askari yeyote katika majeshi ya Ulinzi na kuhusiana na utumishi wa askari katika jeshi.

Ibara ndogo ya tatu (3) ya kifungu cha 148, inaeleza kuwa chochote kitakacho fanywa na askari katika majeshi ya ulinzi, kinyume na amri zilizotolewa na Amiri Jeshi Mkuu kama zilivyoainishwa katika Ibara ndogo ya kwanza (1) na Ibara ndogo ya Pili (2) ya kifungu cha 148 cha Katiba kitakuwa ni batili.

Tumeona kwa kifupi sheria inavyoelekeza kuhusu majeshi na jinsi ya uanzishwaji wake kwa mujibu wa katiba.

Ki msingi, katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, inaelekeza kwa ujumla juu ya majeshi ya ulinzi na usalama nchini, lakini kwa sheria maalumu zihusianazo na miundo na utendaji wa majeshi hayo.

Mfano kuna sheria inayohusu jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania, yaani “Tanzania Peoples Defence Act.” Sheria ya Jeshi la Polisi yaani, “The Police Force Ordinance” na au Jeshi la Magereza, yaani “The Prisons Services Ordinance.”

Tukirejea katika suala zima la uwezo wa kuanzisha Jeshi, kwa mtu binafsi, kikundi cha watu au shirika kama tulivyoona katika utangulizi wa mada ya toleo hili, tunaona kuwa ni vigumu kisheria kufanya hivyo.

Jambo hili ni tofauti kabisa na suala la uanzishwaji wa makampuni ya ulinzi, yaani “Security Companies,” kwani makampuni ya ulinzi husajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na wala si majeshi katika maana nzima ya majeshi ya ulinzi na usalama.

 

SHERIA ZA KANISA

 

Wanaokwenda vitani wanaweza kupewa Sakramenti ya Mpako?

 

Na Pd. David Mubirigi

Katika Toleo lililopita tuliishia katika kipengele kilichokuwa kikizungumzia kanuni ya 1003, namna Mhudumu wa Sakramenti anavyoweza kuhudumia. Sasa endelea na mada hii kama anavyoifafanua Mwandishi.

Baadhi yao au wote wanaweza kushiriki katika kupaka mafuta iwapo idadi ya wagonjwa ni kubwa.

Sala inayosomwa na kiongoza-Ibada tu ni, “Kwa mpako huu mtakatifu na kwa pendo lake kuu, Bwana akujaze/awajaze na nguvu ya Roho Mtakatifu”. Baada ya jibu la “Amina”, anaendelea kusema: “Akuondoe/awaondoe katika enzi ya dhambi, akuweke/awaweke huru.

Kwa wema wake akupe/awape nafuu katika mateso yako/yenu na kukujalia/kuwajalia neema”. Jibu ni: “Amina”.

Kuhusu utayari wa kuadhimisha sakramenti hii, kila Padri ameruhusiwa kusafiri na mafuta matakatifu.

Lengo ni kumwezesha kuadhimisha sakramenti hii wakati wowote wa ulazima (SC Rit, Decr., ‘Pientissima mater ecclesia’, Mar. 4,1965;AAS 57(1965),409;DOL 3314; SCC, general directory, ‘Peregrinans in terra’, Apr. 30,1969:AAS 61 (1969),3605; DOL 2616).

Chimbuko la mwongozo huu ni hati ‘Pientissima Mater Ecclesia’ ya mwaka 1965 iliyotolewa na Idara ya Kiti cha Kitume kuhusu Ibada.

Lakini, mwongozo huu umepoteza uzito wake kutokana na ruhusa iliyotolewa na Kanuni ya 999 inayomruhusu padri yeyote kubariki mafuta ya mpako wakati wa adhimisho la Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Ruhusa imetolewa wakati wa ulazima, kama vile, hatari ya kifo.

 

WAPOKEAJI WA SAKRAMENTI: Kan. 1004-1007.

Sehemu hii ya sheria ya kanisa inazo kanuni 4. Kanuni ya 1004 inahusu adhimisho halali na marudio ya sakramenti. Kanuni ya 1005-1006 zinahusu kesi za mashaka na dhana katika adhimisho la sakramenti. Mwisho, kanuni ya 1007 inawataja wale wanaozuiliwa kupokea sakramenti hii.

Adhimisho halali:

kan. 1004

Kuhusu uhalali wa adhimisho la sakramenti, Sheria ya Kanisa imetaja masharti 5 ambayo ni pamoja na ubatizo, umri wa mang’amuzi, nia ya mpokeaji (kan. 1006), ugonjwa mbaya au uzee na hali ya kiroho. Kutokana na uwazi wa baadhi ya masharti hayo, nitajaribu kueleza baadhi tu ya masharti, kama vile, umri wa mang’amuzi na ugonjwa au uzee.

Kwa kuwa lengo la kwanza la adhimisho la sakramenti hii ni kuondoa dhambi na kukamilisha kitubio, kuongeza neema au kurudisha neema iliyopotea kwa sababu dhambi, mpokeaji hana budi kuwa na uwezo wa kutenda dhambi.

Kwa hiyo sakramenti hii, haitolewi kwa watoto wachanga au watu waliozaliwa punguani (kan.99) kwa sababu hawana uwezo wa kutenda dhambi.

Hawajapoteza neema ya Mungu waliyoipata wakati wa ubatizo (DZ,3536).

Badala yake, sakramenti hii inatolewa kwa muumini aliyefikia umri wa mang’amuzi au zaidi. Hata mtu mzima aliyebatizwa wakati wa hatari ya kifo na ameelezwa maana na umuhimu wa sakramenti hii katika maisha ya waamini, anaweza kupewa sakramenti hii.

Iwapo kuna mashaka kama muumini amekwishafikia umri wa mang’amuzi apewe sakramenti hii kwa masharti, “sub conditione” (kan. 1005).

Sharti la pili ni ugonjwa mbaya au mkubwa au uzee. Ndiyo maana Mtume Yakobo anasema, “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? na awaite Wazee wa Kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana”, (Yak. 5:14). Hayo, pia, ndiyo mafundisho na desturi ya kanisa (Dz,1698).

Kwa bahati mbaya, kanuni hii haielezi kuhusu hali ya ugonjwa au uzee ambapo muamini anapaswa kupokea sakramenti hii. Inataja tu kuwa muumini apewe sakramenti hii pale ambapo hali yake inaanza kuwa hatarini kwa sababu ya ugonjwa au uzee, “….ob infirmitatem vel senium in periculo incipit versari”.

Kwa hiyo, kanuni hii inatoa nafasi kwa waamini (kan.1001) kutumia busara na hekima zao katika kuamua kuwa afya ya muumini fulani imeanza kuwa hatarini.

            Aidha, kanuni haitaji aina ya ugonjwa, ndiyo maana, hata magonjwa ya akili yanahusishwa. Siku hizi magonjwa ya akili yameanza kuwa tatizo na tishio kubwa kwa wanadamu. Kwa hiyo, waumini wenye magonjwa mabaya au makubwa ya akili wanahitaji kuimarishwa na Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa (Pastoral Care, 27, n. 53). Mgonjwa anaweza kupakwa kabla ya kufanyiwa upasuaji hospitalini iwapo upasuaji unasababiswa na ugonjwa (Rituale Romanum, Ordo, 10). Lakini, siyo maaskari wanaokwenda vitani au watu wakunyongwa kwa sababu hali hizo hazisababishwi na magonjwa au uzee. Maaskari walio vitani wanaweza kupakwa iwapo wamepata majeraha mabaya. Kuhusu uzee, muumini  mzee anaweza kupakwa iwapo ameanza kuwa dhaifu ingawa uzee siyo ugonjwa (Rituale Romanum, Ordo unctionis infirmorum eorumqe pastoralis curae, vaticanis, 1972, n. 11).