Mbaya sana hakosi wema, mwema sana naye hakosi ubaya

lZiko aina kuu tatu za tabia za watu watazamapo mambo

KATIKA maisha ya binadamu tunao watu wenye tabia tatu tofauti. Kuna wale wenye tabia au hali ya kuona mazuri tu kwa wenzao. Hao hawajui kulaumu na hata wenyewe hawapendi kulaumiwa.

Wako wale ambao hawaoni jambo lolote zuri kwa binadamu wenzao. Hao wana tabia ya kulaumu daima. Tunasema hao wanaangalia upande mbaya tu wa binadamu mwenzao. Hao wengine kazi yao au tabia yao ni kuangalia tu upande mbaya wa wenzao.

Lakini pia kuna wale wenye msimamo wa katikati. Hao binadamu daima watakuwa na hukumu za katikati.

Tuna binadamu ambao ni raia na ni waumini wa dini na madhehebu fulani. Kwao hakuna kitu chema chochote kwa viongozi wao. Daima ni kulaumu tu.

Mara kwa mara watawalaumu viongozi wao wa kidini na serikali . Kazi yao ni kutoa kasoro kwa viongozi na hata uongozi mzima. Kwao hakuna kiongozi mzuri labda wangekuwa wao wenyewe (ambao mara nyingi hawafai kabisa).

Ni kweli kuwa hakuna kiongozi aliye "malaika: au mwenye ukamilifu kwa kila hali. Viongozi wetu ni binadamu. Hivyo wana kila sababu ya kukosea pale wanapokosea.

Tabia hiyo ya kutoona mazuri kwa wengine siyo tu kwa viongozi hata kwa majirani na wafanyakazi wenzetu. Wako binadamu ambao hawana tabia wala mazowea ya kuthamini matendo ya wengine. Hawana kabisa nguvu na ujasiri wa kuwasifu wengine. Hawafanyi hivyo au kutokana na tabia yao ya wivu na ubinafsi au dharau tu.

Pengine tabia hiyo mbaya huwapata wakubwa au viongozi. Wanashindwa kuona mazuri ya baadhi ya wale walio chini yao.

Ni jambo la kusikitisha kushuhudia kama kiongozi au mkuu akamwona yule wa chini ni mbaya moja kwa moja na wala hana zuri lolote. Kwa yule mdogo huwa jambo hilo linakatisha tamaa na kuua kabisa juhudi.

Kinyume chake lakini kuna binadamu ambao hawawezi kuona ubaya kwa mtu mwingine. Tabia hiyo nayo siyo nzuri. Kumwona mtu kuwa ni mkamilifu kabisa na hawezi kufanya vibaya ni kumharibu huyo binadamu.

Tunajua kuwa hakuna binadamu aliye mkamilifu hapa duniani. Kila mmoja ana mapungufu yake. tunapaswa daima kutoa nafasi ya uzuri na hata ya kukosea kwa wenzetu kwani ni binadamu.

Hata wale tunaowatambua leo kuwa watakatifu waliishi kwa hofu ya kukosa na kuanguka.

Mtume Paulo anasema: "Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata ile tuzo....."(Wafilipi 3:12).

Tabia au hali inayotakiwa tuonyeshe kwa wenzetu ni ile ya kuwa katikati. Daima tuone uzuri wa wenzetu na kuusifia inapowezekana. Pia tuone ubaya wao, lakini tuuhurumie na kuwasaidia waondokane na ubaya huo.

Hukumu zetu kwa binadamu wenzetu zisiwe zile "hukumu tangulizi" yaani "prejudice". Tusione kuwa fulani hawezi akafanya ubaya wa namna hii. Na yule fulani hawezi akafanya jema la namna hii.

Daima tukumbuke kuwa binadamu hubadilika kimaumbile na pia kitabia kulingana na umri pia mazingira. Wako binadamu ambao labda katika ujana wao wameonyesha tabia njema na wengine wakawaona ni wakamilifu, wale hawahitaji ushauri au uongozi wa namna yoyote ile, kumbe mambo yakageuka na hawakuwa na wa kuwasaidia. Wamepotoka moja kwa moja. Pia kumekuwa na watu wengine, licha ya kuonekana ni wabaya, kama wangesaidiwa na kupewa misaada wangeweza kuongoka na kuwa watu wema na kuiletea jamii faida kubwa sana.

Kuna kanuni isemayo kuwa "hakuna mtu aliye mwema kabisa kwa watu wote; na hakuna binadamu aliye mbaya kabisa kwa watu wote". Kila binadamu hata angekuwa mbaya namna gani bado hakosi chembe ya uzuri, na pia kila binadamu, hata angekuwa mzuri namna gani anayo pia chembe ya ubaya.

Licha ya kuangalia tabia na hali za watu, tunapaswa pia kuangalia maisha yetu kwa mtazamo wa matumaini. Kuna raia ambao wamekata tamaa kabisa na hivyo hawaoni ule uzuri na faida toka kwa viongozi wao au wasaidizi wao. Hao tunasema huangalia mambo kutoka ule mtazamo usio wa matumaini.

Tunasema kuwa kila kiongozi awaye yeyote yule sharti awe ni mcha Mungu. Hivyo atapaswa kuiongoza nchi, jumuiya au jamii, siyo tu kwa kufuata katiba bali pia kwa kumwogopa Mungu. Atatambua kuwa uongozi aliopewa ni dhamana. Hataweza kuchezea madaraka yake kwa hasara ya nchi.

Kwa hiyo tunaamini kuwa kila mwenye kushika uongozi humcha Mungu na sisi wengine tunapasika kumheshimu na kumtii. Na ndivyo anavyotufundisha na kutuhimiza Mtume Paulo anapowaandikia ndugu Waroma: "Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali, maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. Anayeyapinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu, nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe " (Waroma 13:1-2).

Ni kweli hao viongozi wetu wanaweza kuwa na kasoro zao. Lakini kasoro hizo hazitakiwi zitufanye sisi raia tusiwaheshimu na kuwapa ule ushirikiano unaotakiwa. Tunapaswa kuwa watiii na watu wa heshima.

Mambo ndivyo yalivyo pia hata kwa upande wa viongozi wetu wa kidini. Mamlaka na madaraka yao yametoka kwa Mungu. Na kwa kuwa wao ni viongozi wetu wa kiroho, basi tunapaswa kuwa na heshima na utii zaidi. Hatuwezi kuanza ubishi kuhusu uhalali wao na hasa kuhusu hali zao.

Mwenyezi Mungu kawateua na kuwaweka wawe viongozi wa kiroho akifahamu ukamilifu na mapungufu yao. Tunapaswa kuwapokea kama walivyo nao wakiwa na nia njema ya kututumikia.

Kama tulivyosema hapo juu ni kwamba kila mmoja anao mchango wake katika kila jami alimo.

Kwa hiyo tunapaswa kumwangalia kwa jicho la tamaa na la kufanikisha au kuendeleza pale alipowekwa na Mwenyezi Mungu kuwapitia binadamu viumbe vyake. Hatuna sababu ya kuangalia upande wa kasoro tu katika binadamu wenzetu tunaofanya nao kazi. Wala tusikatishwe tamaa kutokana na kasoro tunazoziona kwao.