Tunapaswa kujitegemea
Kwa miaka mingi Serikali za nchi zile zinazoendeleaa zimekuwa zikitegemea sana nchi zile zilizoendelea za huko Ulaya na Marekani. Serikali hizo zimekuwa zikitoa misaada mbalimbali ya maendeleo kwa nchi nyingi hasa barani Afrika. Hivyo pia imekuwa kwa upande wa madhehebu ya kidini. Makanisa mengi baada ya kuanzishwa yamekuwa yakitegemea sana misaada ya kuyaendesha kutoka huko Ulaya na Marekani hasa.
Lakini kumbe mambo sasa yameanza kubadilika. Misaada kutoka kwa nchi zinazoendelea huzidi kupungua, na ikiwa misaada hiyo inatolewa, basi mara nyingi haikosi kuwa na masherti mbalimbali. Pengine misaada hiyo karibu inahatarisha uhuru wa nchi hizo, jambo ambalo halipendezi sana. Kwa upande wa kanisa wale wafadhili wetu wanazidi kupungua na hivyo misaada karibu inakwisha na hivyo tunachodaiwa ni kujitegemea na kujaribu kuacha tabia au ile hali ya kutegemea ufadhili wa kutoka ng,ambo. Kanisa hasa katika Afrika limekuwa tegemezi mno na hivyo ni wakati mwafaka wa kila mwanakanisa kulitegemeza kanisa lake la mahali.
Kutokea mwanzoni mwa siku zetu za uhuru, sisi Watanzania tuliambiwa na viongozi wetu kuwa inatupasa kujitegemea na hivyo tukawa na yale maneno yasemayo "Uhuru na kujitegemea au Uhuru na Kazi".
Daima tumekuwa tukikumbushwa juu ya shughuli za kujitegemea na kujitolea hapa na pale. Wale ambao waliitikia mwito huo wa kufanya kazi za maendeleo kwa kujituma na kujitegemea mapato yake yanazidi kuonekana. Tunaposhuhudia tofauti ya maendeleo katika taifa letu tukumbuke kuwa nyuma ya ufanisi huo wote ni kutokana hasa na moyo pamoja na juhudi za kujitolea katika shughuli hizo za maendeleo. Kuna baaadhi ya Watanzania ambao wameitikia mwito huo wa kujitolea, na mapato ya juhudi hizo huonekana waziwazi. Lakini kuna baadhi ya wananchi ambao wameamuwa kupiga uvivu na kutokuwa tayari kuchangia maendeleo kwa njia ya kufanya kazi na kujituma. Nao mapato yao yanaonekana waziwazi kabisa.
Tunaona ni kwa jinsi gani wananchi katika sehemu mbalimbali walivyo na maisha duni, licha ya kusaidiwa na serikali na hata mashirika ya kidini. Wengi baada ya kupata misaada kutoka kwa waafadhili hawakuweza kuzalisha cho chote na hivyo hali zao zimebakia duni, na hata pengine zimezidi kudidimia siku hata siku. Tunao Watanzania wengi wenye nguvu, wenye afya njema kabisa, lakini hawazalishi cho chote, yaani hawafanyi kazi ya maendeleo yao binafsi na hata ya kitaifa. Wataalam hutuambia kuwa unaweza kumlazimisha punda kwenda mtoni kunywa maji, lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji. Ndivyo ilivyo na kwa wananchi wetu.
Viongozi wetu wa serikali na hata wa kidini wamejitahidi kutuhimiza katika shughuli za maendeleo, lakini inashindikana kwa vile tuko wavivu na hatutakia kufanya kazi. Badala ya kufanya kazi tunazubazubaa tu mitaani na kufunga safari kwenda kwa ndugu na jamaa ili tukapate cho chote.
Hapo jana tumesherehekea siku ya wafanyakazi ulimwenguni, lakini nina mashaka kama kweli sote tunaelewa maana ya siku hiyo ya wafanyakazi ulimwenguni. Ni siku ambapo tunahimizwa kuangalia nyuma na kupanga mipango ya mbele. Tumekuwa tukifanya hivyo kwa miaka mingi sana. Lakini kwa wengi wetu hakuna mabadiliko tuliyoyafanya kwa muda wote huo kwani hali zetu zimezidi kuwa duni siku hata siku badala ya kwenda mbele. Tumeelezwa viongozi wetu kuhusu umuhimu wa kufanya kazi, lakini wengi wanaendelea kuridhika na maisha duni.
Ni jambo la kushangaza kuona kuwa kuna baadhi ya wananchi ambao hawana hamu wala wivu wa kimaendeleo. Wananchi hao licha ya kuridhika na hali zao duni, wanazidi kuwa kikwazo cha maendeleo kwa watu wengine. Tunapaswa kujifunza kutoka kwa wenzetu walioendelea kama vile kutoka kule Ulaya au Marekani. Wameendelea siyo kwa njia ya miujiza bali ni hasa kutokana na juhudi pamoja na maarifa katika kufanya kazi. Tunatambua kuwa nchi yetu siyo maskini bali ni yenye utajiri mkubwa sana. Ni sawa kama nilivyoambiwa siku moja na mmisionari moja kwamba sisi Watanzania tunakalia mali na hivyo tunapata shida na mahangaiko ya kimaisha. Tulishaambiwa kuwa hali ya nchi yetu ni nzuri sana. Kuna sehemu nyingi sana katika nchi yetu ambazo hufaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali, yawe ni ya chakula au biashara.
Kuna shughuli nyingi kama vile ufundi, uvuvi na ufugaji nk. Tunalohitaji sasa hivi ni ule moyo wa kujituma katika utendaji wa kazi.
Wengi tunalia kuhusu hali ngumu ya kiuchumi siku ya leo, lakini ikiwa haatutafanya kazi kilio hicho kitazidi kudumu. Tunaweza kubadilisha hali yetu duni kuwa nzuri kwa njia ya kazi na siyo vingine. Tuwaangalie hao wenzetu tunaosema kuwa wameendelea. Wamefikia hali hiyo siyo kwa miujiza bali kwa kufanya kazi. Uvumbuzi na maendeleo katika mambo ya sayansi na tekinolojia yasingeweza kufika katika nchi hizo zilizoendelea kama kusingekuwa na utendaji wa hali ya juu. Binadamu wenzetu hao wameendelea kutokana hasa na juhudi katika kazi.
Tunawapongeza wale wananchi ambao wamejitahidi sana kuwaiga hao wenzetu walioendelea katika kufanya kazi na hivyo wanajitegemea vikubwa sana. Tunapaswa kuwaonea wivu wa kimaendeleo, yaani nasi tuwe tayari kuwaiga kwa njia ya kujituma na kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Ni kweli jambo la kushangaza unapoona kuwa kuna nyumba zinazokaribiana sana lakini zenye tofauti kubwa mno ya kimaendeleo.
Tunaweza kusema mmoja ameridhika kabisa na mwingine anapenda kuwa na hali bora zaidi.