NGUVU YA HOJA - Na Padre P. Haule

Wale wenye uwezo wasiwe wachoyo

Tunaambiwa na kushuhudia kuwa hakuna binadamu anayeweza kujitosheleza kabisa Kwa maneno mengine ni kwamba hakuna binadamu ambaye ana kila kitu na anao uwezo wa kila kitu hata asimhitaji binadamu mwenzake.

Binadamu hawezi akajitosheleza kiakili, kiuchumi, kielimu na hata furaha yake haiwezi kuwa timilifu bila kuwashirikisha binadamu wenzake. Hatuna ukamilifu wa kiakili, wa kiuchumi, wa kiafya, wa kimawazo, wa kielimu na kadhalika. Mungu ametugawia sisi binadamu karama mbalimbali na pia kwa namna fulani hakutupatia kila karama kwa kiasi kikubwa sawasawa.

Mara kwa mara vijana na wanafunzi huko mashuleni tunashuhudia kwamba wanafaulu mitihani yao kwa namna tofauti. Kuna wengine wanaweza labda masomo ya hisabati, au ya sayansi, wengine masomo ya lugha, wengine masomo ya historia na siasa.

Lakini kwa vile wako huko shuleni huwapasa wafanye jitihada katika masomo yote. Njia inayotumika katika kuwafanya hao wasiokuwa na uwezo katika somo fulani, basi ni ule mtindo wa kujifunza katika vikundi.

Hapo wale wenye uwezo katika somo fulani huwa tayari kuwasaidia wenzao wasio na uwezo katika somo hilo. Hutokea lakini kunakuwa na wanafunzi wengine wenye uwezo ambao hawatakia kuwasaidia wenzao katika shida hiyo ya masomo. Basi hao wanafunzi wasiopenda kuwasaidia wenzao tunawaita ni wanafunzi wachoyo, na wenye kiburi cha elimu.

Tabia ya kusaidiana ni katika jadi ya binadamu na hasa kwetu sisi Waafrika na hasa hasa kwetu sisi Watanzania.

Mababu na mababa zetu wamezaliwa na kulelewa katika maisha ya kijamaa yaliyojaa tabia na desturi ya kusaidiana. Kuna baadhi ya Watanzania ambao wamebahatika kuwa na mali, tungeweza kusema ni matajiri kutosh kulingnisha na Watanznia wengine.

Kwa bahati njema hawataki kuitumia mali hiyo pekee yao bali wanapenda kuwashirikisha na wengine ingawaje kwa mitindo mbalimbali.

Wale ndugu ambao wako radhi kununua mabasi yakafanya kazi ya kupunguza matatizo ya usafiri hapa nchini tungeweza kusema kuwa ni wakarimu kwa namna fulani kwani hata kama wanapata hela kutoka kwa wasafiri wa mabasi hayo, bado tunahesabu kama ni ukarimu kwani wangeweza wakatumia mali yao hiyo kwa njia nyingine ambayo isingewafaidia watu wengi.

Hivyo pia hivi sasa kuna Watanzania ambao wanapenda kutushirikisha bahati waliyo nayo katika kuanzisha vituo vya radio, televisheni, viwanda vya uchapaji nakadhalika. Hao nao tunaweza pia kusema kuwa ni wakarimu kwa namna fulani.

Wamependa kuwashirikisha wengine mali waliyo nayo katika kuanzisha vyombo hivyo vya habaria ambavyo huwasaidia na kuwanufaisha watu wengi katika nchi.

Kwa hiyo tunapoamuwa kuanzisha au kununua kitu fulania ambacho ni kwa matumizi ya watu wengi, hapo tukumbuke kuwa tunawakirimia wenzetu pia na hivyo tunaondokana na uchoyo.

Tunaondokana na ile hali ya kutaka kushiba mwenyewe na kutokuwa tayari kuwshibisha na wengine.

Tunawaomba wale wenye mali kuitumia mali waliyo nayo katika kutujengea mashule, mazahanati, na vituo mbalimbali vya maendeleo.

Hao wenzetu waliobahatika kupata mali wakumbuke kuwa wamebahatika kuipata hiyo mali kwa sababu kumekuwa na watu wengine wanaowajua na wasiowajua waliowasaidia kwa namna moja au nyingine.

Tunawaomba wasiwe wachoyo na ubinafsi bali waonyeshe ukarimu unaoonekana.

Kwa kufanya hivyo hawatajenga tu majina yao katika ulimwengu huu bali watazisdi kutuletea maendeleo ya kweli katika taifa letu.

Tunaambiwa kwamba binadamu si kisiwa, bali huishi na kuhangaika pamoja na binadamu wenzake. Mtu hawezi akawa salama kama hana mahusiano mazuri na wenzake.

Nakumbuka siku chache zilizopita Padre moja alinisimulia kwamba alipokuwa amepelekwa kwenye Parokia aliko sasa hivi alikuta vijana wengi vibaka kuzunguka ile Parokia.

Aliwashika vibaka wengi na kuwapeleka polisi. Lakini bado wale vibaka waliendelea kumsumbua yule Padre. Baadaye akapata wazo, nalo likawa ni kufungua Shule Ufundi pale Parokiani, na wale vijana akawakusanya na kuanza kuwafunza kazi mbalimbali za kifundi.

Kwa namna hiyo alifanikiwa kukomesha ile tabia mbaya ya vijana mahali hapo. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa ni kwa nia ya ukarimu yule Padre aliweza kuondokana na lile balaa la kuhangaishwa na vibaka.

Weengi tunaweza kuondokana na vijana na hata watu wazima walio na tabia mbaya kwa njia ya kuwa wakrimu kwa namna mbalimbali.

Tutumie kile tulicho nacho kwa ajili ya wenzetu pia kwani kwa kufanya hivyo tutaweza kwanza kuwatoa katika shida zao, na pia tutaweza kujenga mahusiano mazuri nao.

Tunapoamua kuishi kama visiwa katika bahari, hapo ndipo na mali zetu zinazidi kuwa hatarini, lakini kunakuwa na unafuu pale ambapo tunaweza kuwashirikisha wenzetu kile tulicho nacho.

Ninapenda kumalizia hoja yangu hii kwa kuwataka wale wote wenye bahati katika maisha wazitumie bahati hizo ziwazo zote kwa ajili ya kuwajenga pia wale walio kando yao.

Wakati umefika wa kila mmoja aliye na chochote kukitumia kwa ajili ya manufaa ya taifa zima. Makabila mengi hapa nchini yamekuwa nyuma kutokana na ule uchoyo ambao wale waliobahatika kupata elimu au mali hawakuweza kuwasaidia wenzao.

Huo ni ukweli ambao unajidhihirisha na kuonekana kabisa ukipitapita hapa na pale katika nchi yetu. Tuwashauri hao wenye uwezo mbalimbali wajitahidi kuwa wakarimu kama ambavyo baadhi ya Watanzania walivyotuonyesha kwa kutujengea mambo mbalimbali tuyaonayo hapa na pale.

Wahenga wanasema chakula ambacho unakula peke yako hakinogi, bali ule na wenzako na kitanoga.