NGUVU YA HOJAFr. P. Haule...

Tofauti za maisha huzidi kuwa kubwa mno

WAKATI nchi yetu ilipojipatia Uhuru wake,Viongozi wetu walituletea ile Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Siasa hiyo ilikuwa hasa na lengo la kujaribu kuleta usawa kati ya wananchi.Kwa namna fulani siasa na hali hiyo ikawa imefaulu na pia kushindwa. Kwa wengi siasa hiyo ilikuwa ngumu na hivyo wakaona ni afadhali kuchukua aina nyingine ya siasa nayo ni ya Kibepari. Kwa hiyo nchi yetu kwa sasa hivi kwa vikubwa imeachana na kiasi kikubwa imeachana siasa ile ya kijamaa na kuambatana na hiyo ya kibepari.

Katika siasa hiyo ya kibepali, ni kwamba kila mwananchi ajitahidi kufanya kazi kwa juhudi,na kwa kutumia nguvu na uwezo alio nao ili kuweza kujipatia riziki na mahitaji yake ya kila siku. Kumbe hapo mafanikio ya mtu hutegemea sana juhudi za mtu binafsi. Na kwa hiyo kumekuwa na biashara huria, pia na hata masoko huria kwani kila mmoja anao uhuru wa kujipatia mali na riziki kwa kiwango kikubwa kwa kadiri anavyoweza bila kuangalia kama kuna mwingine mwenye shida kando yake.

Hilo ni jambo na hali nzuri kwa upande fulani. Kumekuwa na watu ambao kwa sasa hivi hali zao ni nzuri mno kwani wana miradi mikubwa sana. Kuna wengine wenye makampuni binafsi, na huyaendesha vizuri na tena kwa faida kubwa sana. Wako wananchi ambao wamefungua mashamba makubwa sana na humo kuna mazao mazuri, na kuna mifugo kama vile ng’ombe, mbuzi, kuku, nguruwe nk. Shughuli hizo kwa kweli huleta matumaini makubwa sana kwao wenyewe binafsi na hivyo hali zao za maisha ni nzuri sana. Mambo yamefikia kiwango cha kusema kuwa kitu cho chote cha mtu binafsi ni kweli kinaleta faida kubwa sana na kinapata huduma nzuri zaidi kuliko kile cha ujamaa.

Katika hali hiyo, kwa upande mwingine tunashuhudia pia hali mbaya ya maisha kwa wananchi wengi. Tunaona kuwa kuna umaskini unazidi kushamiri katika taifa letu na huo ubepari unazidi kutukuka siku hata siku. Tofauti kati ya wale wenye uwezo na wasio na uwezo inazidi mno. Kwa mfano kwa sasa hivi kuna wananchi ambao wanashindwa kabisa kuwapeleka watoto wao shuleni na kuwalipia ada, lakini kuna wale wenye uwezo ambao huwalipia watoto wao siyo tu ada ya hapa nchini, bali wanadiriki hata kuwapeleka watoto wao nchi za nje. Kuna wale ambao wako tayari kuwapeleka nchi za nje watoto wao kutoka shule za awali hadi vyuo vikukuu.

Isitoshe kuna wale wenye uwezo wa kifedha ambao wako tayari kutumia pesa hata katika mambo ya kutafuta haki zao na hapo wanyonge hubakia katika hali duni. Ingawaje ni kweli kuwa Serikali yetu inafanya juu chini katika kupinga rushwa na hogo, lakini hali ilivyo mambo huzidi kuwa magumu siku hata siku kutokana na hiyo tofauti kubwa iliyoko. Waingereza walishatuambia kuwa "money is power", yaani hela ina nguvu kubwa sana. Kwa hiyo tusione ajabu kuwa vita vya rushwa haviishi katika taifa letu kwa kuwa kuna tofauti mno kati ya wale wenye kitu na wale ambao hawana chochote.

Jambo ambalo tunaliona sisi kama lingeweza kusaidia walao kuondoa ile hofu ya maisha kutoka upande wa hao wenzetu wenye uwezo ni kule kuwa na moyo wa kizalendo. Tunaposema juu ya moyo wa kizalendo, ni kwamba wale wananchi wenye uwezo sharti wawe na huruma kwa wale wenzao ambao hali zao ni duni. Ikiwa hawatafanya hivyo basi mambo ya ujambazi, vibaka, na wizi vitazidi kushamiri katika taifa letu. Si jambo rahisi kibinadamu kuona kuwa jirani anakula na kusaza na kando yake kuna mtu hana hata kile kidogo cha kutuliza njaa yake. Pengine watu hufanya uhalifu, siyo hasa kutoka na tabia walio nayo mbaya ya uhalifu, bali mara nyingi ni kwa sababu ya njaa waliyo nayona tabu walizonazo. Hata kama jambo ambalo tunalishuhudia au linakuja ni ile tofauti inayozidi kukua kati ya hao wenye uwezo na wale ambao hawana uwezo wa kujipatia mahitaji ya kawaida.

Yule Paroko wa Kanisa la Bagamoyo alinisimulia kwamba wakati akifika kule Bagamoyo alikuwa amekumbana na vibaka ambao walikuwa wakimwibia mali yake pale Parokiani. Alijaribu kuwashika na kuwaweka ndani, lakini baada ya kutolewa waliendelea na uhalifu huo kwani walikuwa hawana cho chote. Baadaye huyo Padre aliamua kufungua shule ya Ufundi ambamo aliweza kuwaingiza vijana hao shuleni, na hivyo wakawa ni vijana wake na wakawa walinzi wakubwa wa mali ya hapo Parokiani. Hivyo ndivyo alivyoweza kuwashinda hao vijana vibaka. Kwa maneno mengine tunasema kuwa wale wenye mali hawawezi kamwe kuwa na uhakika wa mali zao ikiwa wale walio kando yao wanakuwa katika hali ya umaskini.

Haitoshi kabisa kwa wale wenye mali kuweka mageti na magrili kuzunguka nyumba zao bila kuwa na uhusiano mzuri wa kizalendo na hao wanaowazunguka. Binadamu kama binadamu hupenda naye apate chakula na mambo mengi ya muhimu, na hayo huweza kuyapata kutokana na juhudi zake binafsi pamoja na kusaidiwa na majirani. Ni kweli kuwa wako wananchi ambao ni wavivu, na hivyo hawajishughulishi na kazi yo yote. Kuna watu ambao wangeweza wakafanya kazi kama wangepewa msimamo fulani. Kwa hiyo kwa namna fulani ni wajibu wa hao wenye uwezo kuwapatia msimamo hao wanaowazunguka kwani kwa kufanya hivyo wataweza kujenga uhusiano mzuri na mali zao zitakuwa ni salama kwa kiasi fulani.

Tunasema kuwa binadamu siyo kisiwa, bali ameumbwa ili kuweza kuhusiana na binadamu mwenzake hata kama ni mnyonge. Wengi tumeshuhudia jinsi majirani walivyoweza kutusaidia wakati tukikabiliwa na tatizo fulani katika maisha yetu, na pia imeshatutokea kuwa pale ambapo hatukuwa na uhusiano mzuri na majrani zetu, basi tumepata shida na majirani wakatuacha katika shida hizo. Tunapenda kurudia kwa kusema kwamba hata kama tumeiacha siasa ya ujamaa, lakini bado tunahitaji maisha ya kijamaa, yaani kuweza kujaliana licha ya tofauti za kiuchumi tulizo nazo. Tunapaswa kutambua kuwa uhai na usalama wa mali zetu hutegemea sana mahusiano yetu na majirani tunaoishi nayo.

Hapo tunapaswa kuiga mifano ya wenzetu wa huko Ulaya au Marekani na penginepo ambao wanakuwa tayari kuwasaidia hata watu wale ambao hawawafahamu kabisa. Kumbe sembuse kwa hao ndugu zetu ambao wanao uwezo mkubwa na hawataki kabisa kuwasaidia Watanzania wenzao wenye shida na matatizo. Uungwana wetu utakuwa wa kweli ikiwa tutafikia kile kiwango cha kuweza kuwasaidia wenzetu walio katika shida. Ikiwa hao wenye uwezo watatujengea mashule, watatujengea mahospitali na vituo vingi vya afya.

Tungetazamia kuwa hao wenye uwezo wangechukua hatua za kuwasaidia vijana wale ambao hawana uwezo wa kulipia ada. Tunasema kuwa hayo yotokane lakini na ule moyo wa kizalendo au kiungwana.Ni wakati sasa kwa hao wenye uwezo kujenga majina yao kwa Mungu na taifa kwa njia ya kutoa misaada kwa wale ambao hawana uwezo.

Hatusemi kuwa hilo ni jambo lazima, la hasha.

Tunamalizia kwa kuwasihi hao wenye uwezo wawe na moyo wa kutoa kile kinachowazidia kwa ajili ya faida ya wale wasiojiweza.

Maendeleo yetu yanapaswa yawe ni kwa ajili ya wale wote wanaotuzunguka. Binadamu tusiishi kama visiwa bali tunapaswa kuhusiana na wenzetu hasa linapofikia hilo suala la maendeleo.