Watanzania
jifunzeni toka Ivory coast - Kardinali
Pengo
l Asema vurugu za kidini huanzishwa
na wanasiasa
l 'Wanasiasa
wengi ni wa kukimbilia Ikulu’
l Dar kuna washirikina wengi kuliko mikoani
wanakoua vikongwe
l Azungumzia uteuzi wake huko
Pd. Revocatus Makonge na Joseph Sabinus
MWADHAMA Polycarp Kardinali Pengo,
amehofia hali ya usalama nchini huku akiwahimiza wanasiasa, wanasayansi ya
jamii na waandishi wa habari, kuchunguza ili kubaini kama Tanzania itapona au
itaangamia kwa kile kilichosababisha machafuko nchini Ivory coast.
Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake
katikati ya juma juu ya hali ya siasa nchini, ushirikiano wa kidini na
kuteuliwa kwake kuwa Mjumbe katika Idara ya Mafundisho ya Imani ya Kanisa katoliki Duniani, yenye makao yake
makuu nchini Vatican.
Hivi
karibuni waasi nchini Ivory coast walifanya jaribio la Mapinduzi kumng'oa madarakani Rais Laurent Gbagbo, na
hivyo kuzuka ghasia nchini humo.
Hadi
mwishoni mwa juma, waasi walikuwa wamekataa wito wa Rais Gbagbo wa kuweka
silaha chini ili kufanya mazungumzo.
Msemaji
wa waasi hao alisema, Rais alitoa wito huo baada ya kuona ameshindwa kuwaondoa
katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo Bouake.
Alisema
anafurahi kuona kuwa hali imebadilika miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo.
Wananchi
wa Burkina Fasso waishio nchini humo wamekuwa wakionekana kama wavamizi na
wamekuwa wakitishiwa kila kukicha.
Naye
Kamanda wa waasi huko Bouake, Wo Tuo Foziem, alikaririwa akisema Rais huyo
alikuwa anafanya mchezo ambao alisema hawezi kuuamini.
"Hatuwezi
kuacha silaha kabla ya mazungumzo."
Katika mazungumzo hayo,
Kardinali Pengo ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,
alisema, “Matatizo yaliyozuka Ivory Coast yamenitia baridi na hofu sana kuhusu
siasa yetu hapa Tanzania hasa siku zijazo maana Ivory Coast ilikuwa moja ya
nchi zenye amani na utulivu kama Tanzania. Hukuwa unafikiria wala kuhofu juu ya
amani,” alisema.
Akaongeza, “Mimi nina
hofu kwamba tunaweza kuwa tunaelekea kule ambako wenzetu wa Ivory Coast
wamefikia bila sisi wenyewe kujua.Ndiyo maana natoa wito kwa wanasiasa,
wandishi wa habari, wataalamu wa sayansi ya jamii, na jamii kwa jumla, watafiti
ili waone ni kitu gani kimetokea kule na je, sisi tuko wapi? Kinachotokea kule
hakiwezi kutokea hapa kwetu?, ama sisi hatuelekei huko? Wote tulitafakari hilo
tuone kama tutapona ama tutaangamia ninayo hofu kubwa.”
Akizungumzia mang’amuzi
yake mintarafu uhusiano wa kidini nchini Tanzania,Kardinali Pengo,alisema hali
ya Tanzania ni nzuri ikilinganishwa na nchi nyingine ambazo dini zake zina
uhasama na chuki.
Alidokeza kuwa
kinacholeta vurugu katika uhusiano baina ya dini nchini, ni siasa kali za
kidini ambazo alisema ni hatari na hazina budi kukemewa na kila mwenye mapenzi
mema.
Alisema, “Watanzania
tujichunge sana tusiingie kwenye mkondo wa siasa kali kwani maafa kama
tunayosikia yakitokea Nigeria, na sehemu nyingine si vitu vya kufurahisha na
vinaweza kuanzishwa na sisi Wakristo au na wenzetu Waislamu endapo hatutakuwa
makini.”
Aidha, Kardinali Pengo alibainisha ukweli
kuwa, mara nyingi katika sehemu mbalimbali duniani, matatizo na machafuko ya
kidini, hutokana na wanasiasa wanaotumia dini kujinufaisha kisiasa.
“Baadhi ya wanasiasa
wanatafuta sababu ya kupendeka kwa watu hasa wanaoonekana kuwa ni wengi kwa
kutumia dini zao. Na ili waonekane kuwa wako upande wa dini hiyo, wanaanza
kuzusha maneno ya uhasama dhidi ya wanasiasa wenzao walio na dini tofauti kwa
kuwa wanajua wakipambana kisiasa moja kwa moja, hawawezi kuwashinda, lakini
wanaona wakipitia dini, wanaweza kuwashinda,” alisema.
Akaongeza, “Wanaifanya
dini kuwa mbinu tu, au chombo kinachotumiwa ili kufanikisha malengo ya kisiasa.
Unajua mara nyingi wanasiasa wanatumia dini kama ngao ambayo kazi yake ni
kumlinda mtu anayepigana. Akishafanikiwa, kama ngao imeharibika au
haikuharibika, haina maana tena; ataitupa pembeni. Na ndivyo unavyofanyika
uhasama baina ya dini mbalimbali unaojengwa na wanasiasa.”
Mwadhama Pengo alisema
inasikitisha kuona kuwa, pindi wanasiasa wanapotimiza malengo yao, huzisahau na
hata kuzitelekeza dini zao bila kuzifanyia chochote cha maana.
“Wataiweka huko kwenye
mizimu kama ngao iliyokwishatumika na kuchanika na itakaa huko mpaka
watakapoihitaji tena ndipo wataiokota, lakini sio kitu cha kubeba ngao kila
wakati, mpaka mtu anapojua kuna mashambulizi na anahitaji kujikinga,” alisema.
Alisema inatia moyo kwa
viongozi wa dini nchini Tanzania, kukataa kwa kauli moja, kutumiwa kama ngao ya
wanasiasa na akasema hiyo ni bahati kubwa kwa Watanzania.
Kuhusu vikundi vyenye itikadi
kali vinavyotumiwa kama ngao ya wanasiasa,
Kardinali Pengo, alisema
kama ingetokea bahati mbaya vikapata nguvu ya kujihesabu kuwa dini, hali ya
amani ingekuwa mbaya nchini.
“Kwa mfano tuseme Wakatoliki tungekuwa na msimamo huo wa
itikadi kali, halafu mmoja aje kwa upande wetu, hiyo ingekuwa ni mbaya kuliko
hali inayokuwapo kwa sasa. Na hata kwa Waislamu, kuna vikundi hivi vya siasa
kali, lakini si dini ya Kiislamu; viongozi wa Kiislamu wanahakikisha kwamba hao
si wenzao na hali hii imesaidia sana amani,” alibainisha.
Alisema anashangazwa na
mtindo wa wanasiasa wa Tanzania kuwa wanaokimbilia ikulu, badala ya kutoa
changamoto kwa chama tawala ili kijikosoe na kuboresha maendeleo ya kijamii.
“Ndiyo maana utaona
tunapoelekea Uchaguzi wa Rais na Wabunge, ndipo vikundi vya siasa kali
vinapoibuka. Hii ni kwa sababu wanasiasa wetu kwa sasa hawaoni sababu ya
kugombana; siasa yao ni kutaka kuingia ikulu.”
Akitoa mfano wa
kuthibitisha namna wanasiasa wengi wa tanzania
walivyo, Kardinali Pengo alisema, “Katika kipindi hiki chote tutakuwa kimya,
tutakapokaribia uchaguzi, ndipo utaanza kuwasikia hata wakielezea sera zao huku
zikiendana na matusi kati ya vyama na vyama ndipo wanaanza kutumia chokochoko
za kidini. hali hii si ya kungoja
wakati wa kwenda ikulu ndipo waanze kueleza sera zao, haipendezi.”
Kuhusu mapambano na
migogoro ndani ya vyama vya siasa, alisema, “Badala ya kutumia muda huu kujenga
na kuimarisha vyama vyao, wanaanza kusambaratishana. Wanaona ni wakati wa
kucheza ndani kwa ndani, uchaguzi ukifika, tunajifanya kuwa ni chama kimoja.
Sasa tutaamini vipi kuwa nyie ni chama kimoja wakati juzi mlikuwa mnagombana
mmepatana lini, au mmehongana kitu gani ili tusadiki kuwa sasa mko pamoja.”
Alipoulizwa mtazamo wake
juu ya uinjilishaji kwa watu wenye imani za jadi, Kardinali Pengo alitoa wito
kwa wataalamu katika asasi mbalimbali za kanisa zikiwamo seminari na vyuo vikuu
vya Kanisa, vifanye uchunguzi wa kina ili kubaini tunu zinazowavuta waamini
mbalimbali wakiwamo wakristu na waislamu, kushiriki katika dini hizo kwa
kificho.
"Watalaamu, walimu
na wanafunzi wakiweza kujifunza na kueleza tunu ambazo watu wanazifuata kwa
siri, wakaeleza zinavyokaa, hapo tunaweza kujua na kusahihisha" Alisema .
Alisema moja ya mapungufu
yaliyopo katika dini za jadi nchini, tofauti na hali ilivyo huko Afrika
Magharibi, hapa Kanisa ni kama hakuna linachojifunza na kupata kutoka dini za
jadi maana zinafanyika kwa siri siri tu.
“Dini za jadi kule zina
mpangilio mzuri kuliko huku kwetu… huko unajua umuendee nani ili ufanye
uinjilishaji au kubadilishana naye mawazo. Lakini, hapa kwetu hujui uende kwa
nani; tumeshikilia kuwa dini ni Ukristo, Uislam na labda na Wahindu,” alisema.
Alibainisha kuwa ingawa
wengi wa Watanzania wako katika imani za kijidi, bado wanaonekana kama imani
zao wanazionea haya na pengine kujiona kama watu walioko safarini; kuelekea
kuchagua Uislamu ama Ukristo.
“Hivyo, ukimuita mmoja ni
mpagani au muumini wa dini za jadi, atajisikia kama umemdharau au
umemdhalilisha kinyume na ilivyo kule Afrika Magharibi. Wao wanavikundi kabisa
vya dini za jadi na wana viongozi wao wasomi,” alisema.
Alisema asasi za kanisa
zikibaini tunu zinazowavuta baadhi ya waamini wetu katika dini za jadi, Kanisa
litajiimarisha na kuziona kama zinafaa kupokelewa, na kama zinamchango wa
kumfanya Kristu aeleweke zaidi.
“Tunaenda kwa wachawi,
tunapiga bao ambalo kwa Waislamu hulipati na kwa Wakristo halipo, lakini lipo
kwa dini za jadi, lakini kwa sababu tunaenda kule na ni kitu hakiko katika
mpangilio, tunaenda kule kwa kujifichaficha watu wasione na vitu vinavyofanywa
kwa siri ni hatari kwa sababu tunaweza kusema tunachukua vinavyofaa kwa
utamadunisho kumbe tunachukua ngoma tunaanza kupiga kanisani kumbe ni ngoma
iliyokuwa inapigwa katika uchawi nasi tukaanza kuitumia katika Pasaka.
Alisema inashangaza kuwa
ingawa Dar es Salaam, kuna watu wengi wasomi, na walio katika dini
zinazojulikana, lakini bado kuna washirikina wakubwa zaidi kuliko hata sehemu
nyingine za mikoani wanakofanya mauaji ya vikongwe kwa imani za uchawi.
Kardinali Pengo ni
miongoni mwa Makardinali na Maaskofu saba ambao hivi karibuni Baba Mtakatifu
Yohane Paulo wa Pili, aliwateua kuwa wajumbe katika Idara ya Mafundisho ya
Imani ya Kanisa Katoliki yenye makao makuu yake nchini Vatican.
Alisema uteuzi huo,
unafuatia utaratibu wa kawaida ambapo zinapotokea nafasi zozote kuachwa wazi
katika idara mbalimbali, baba
Mtakatifu huchagua makardinali, maaskofu wakuu au Maaskofu kujaza nafasi zilizo wazi kwa
kipindi fulani.
"Makardinali
hatupigi kampeni hivyo, hata nafasi kama hiyo ni uteuzi tu, anaoufanya baba Mtakatifu kwa sababu zake
mwenyewe". Alisema.
Alisema miongoni mwa
sababu zinazoweza kuifanya idara ikawa na nafasi ya wazi, ni kung’atuka kwa
ajili ya umri, ama kufariki dunia..
“Kwa mujibu wa Kanisa,
Kardinali akifikisha umri wa miaka 80, anakuwa amestaafu shughuli zote hata
kama ni ushauri.
Baada ya miaka 80 hata
kukiwa na uchaguzi wa baba
Mtakatifu, haruhusiwi kuingia katika chumba cha kura.
Alikanusha hisia za
baadhi ya watu kuwa huenda yeye ndiye kiongozi mkuu wa idara hiyo kwani
kiongozi yupo na yeye ni mmoja wa wajumbe hao saba, wanaokwenda kuongezea
nafasi zilizokuwa wazi.
Aidha, alisema ingawa
nafasi hiyo itamfanya mara nyingine asiwepo jimboni kwake, bado uteuzi huo ni
heshima kubwa kwa Kanisa la Tanzania kwani ufanisi wa Utume wake unatokana kwa
kiasi kikubwa, na ushirikiano uliopo ndani ya Kanisa zima la Tanzania.
Aidha alisema, nafasi hiyo inampa nafasi
ya kujifunza mazuri na kurekebisha mabaya kutokana na uzoefu wa nchi zingine.
Waislamu sasa kumpata Mufti
Na Dalphina Rubyema
WAISLAMU
nchini kote wapo katika kitendawili kinachopata jibu Jumapili hii mkoani Dodoma
katika Uchaguzi wa atakayerithi kiti cha Marehemu Sheikh Mkuu Mufti Bin Jumaa
Bin Hemed, aliyefariki dunia hivi karibuni.
Mufti Hamed Bin Jumaa Bin
Hemed, alifariki dunia Aprili 8, mwaka huu katika Hopitali ya Taifa Muhimbili
alikokuwa amelazwa baada ya kuugua muda
mfupi.
Taarifa kutoka Baraza
Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), zinasema kuwa Uchaguzi huo utakaosimamiwa
na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi huo,
Sheikh Salim Gereza, utawashirikishika Masheikh wote wa Tanzania.
Taarifa hizo
zilizothibitishwa na Kiongozi wa Masuala ya Dini wa BAKWATA, Sheikh Hassan
Chizenda, zinasema kuwa hadi sasa (tunapokwenda mitamboni), idadi ya wagombea
wa nafasi hiyo ya Sheikh Mkuu wa Tanzania ni 11.
Aliwataja wagombea hao na Mikoa wanakotoka ikiwa katika
mabano kuwa ni Sheikh Suleiman Amran Kilemile, Sheikh Hemed Masoud Jongo,
Sheikh Twarib Ahmad Abdalah, Sheikh Abubakar Zuberi na Sheikh Twaha Omar Majaliwa (wote wa Dar es
Salaam).
Wengine ni Sheikh Suleiman Gorogosi (Lindi), Seikh Profesa
Jumaa Mikidadi (Kilwa), Sheikh Taufiq Ibrahim Malilo (Kigoma), Sheikh Mohamed
Ally Mkanga (Tanga), Sheikh Ahmad Zuber (Dodoma) na Sheikh Issa Shaban Simba (Shinyanga).
Sheikh Chizenga alisema kuwa Masheikh mbalimbali tayari
wamekwisha wasili mkoani Dodoma ambapo wamefikia eneo la Chuo cha Biashara
(CBE).
“Uchaguzi huu utawahusisha Masheikh wote wa Tanzania na
tayari baadhi yao wameisha wasili Dodoma tayari kushiriki uchaguzi huo
utakaofanyika Jumapili,” alisema Sheikh Chizenga.
Gazeti hili pia lilishuhudia Masheikh kutoka sehemu
mbalimbali wakiingia na kutoka katika ofisi za BAKWATA kuangalia taratibu za
safari.
Mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Sheikh Twaha Omar Majaliwa
(Dar es Salaam), aliliambia KIONGOZI kuwa anawataka wagombea wenzake watambue
kuwa kugombea huku isiwe ni kujenga husuda na chuki miongoni mwa Waislamu na
badala yake, uchaguzi ukisha waendelee kuonana kama watu wa jamii moja.
Pia, alisema matokeo ya uchaguzi huo yawe ni mwanzo wa
mabadiliko ndani ya Uislamu ambapo alisema kwa sasa duniani Waisalamu
wamefarakana jambo linalomfanya hata Mwenyezi Mungu akatae kupokea dua zao
mbalimbali.
“Baada ya uchaguzi,yule atakayeshinda na watakaoshindwa, wote
turudi katika hali zetu za awali, lengo ni kuuendeleza Uislamu ambao kwa kweli
tusipokuwa makini, unaonekana kuporomoka,”alisema.
Alisema, tangu awali lengo lake la kusoma ni kwa ajili ya
kuwa Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania na si vinginevyo.
Marehemu Mufti, Hemed Bin Jumaa Bin Hemed alifariki akiwa na
miaka 74. Alizikwa Aprili 8, 2002 mkoani Tanga.
Baada ya kufariki kwa Mufti, Baraza la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) lilitangaza nafasi ya mtu wa kushika nafasi.
Mgombea mmoja wa nafasi hiyo, Sheikh Mohamed Basafar (Dar es
Salaam), kujitoa katika kinyang’anyiro hicho na hivyo, kubaki wagombea 11.
Wakatoliki na
namba 666 katika Ufunuo wa Yohana
Na Mwandishi Wetu
Katika Ulimwengu wa kidini kuna mafundisho mengi
kuhusu ‘namba ndani ya Biblia’kwa mfano yapo baadhi ya madhehebu ya dini
yanayohusisha namba 666 inayotajwa katika kitabu cha Ufunuo cha Yohana na
mamlaka ya Kipapa. Katika Makala hii, MWANDISHI WETU anaelezea maana ya namba
katika mafundisho ya Kanisa Katoliki ikiwa ni sehemu ya pili ya mfululizo wa
makala yake juu ya namba ndani ya Biblia.
Kadiri ya Wayahudi (Waebrania) na mataifa mengine ya
nyakati hizo, kila neno liliweza kugeuzwa kuwa namba na kila namba iliweza
kubadilishwa kuwa neno! Mfano mzuri ni ile namba iletayo malumbano mengi, siku
hizi, namba 666 inayotajwa katika kitabu cha Ufunuo wa Yohane.
Je namba hii 666 inawakilisha maneno gani?
1. Historia fupi ya namba
hii 666 :
- Yohane aliandika barua au maandishi
haya wakati wa utawala wa mfalem, Domitiani wa Roma. Alikumbuka ule udhalimu na
madhulumu dhidi ya Wakristo yaliyofanywa na NERO kama Kaisari (NERON CEASER),
mwaka 54-68 baada ya kristu.
- Yohane alimfikiria Nero kuwa dhalimu
na fashisti mkubwa kuliko wote wa Ukristu na Kanisa mwanzo mwaka 64B.K Tazama
Uf.
- Hivyo basi, Yohane alitamani sana
kuweka kifupisho cha jina la Kaisari Nero katika lugha ya Kiyunani (Kigiriki)
kuwakilisha yule hayawani anayetajwa katika kitabu chake (Ufunuo) kama
ifuatavyo:-
2. Kifupi
cha Neron Caeser kwa Kigiriki ni Konsonanti hizi:
NRWN/OSR
Namba zinazowakilisha konsonati hizo:
N- 50
R- 200
W- 6
N- 50
Q- 100
S- 60
R- +200
Jumla
yake – 666
Hivyo konsonati hizi NRWN/QRS zinazowakilisha jina la Kirumi la Kaisari Nero zina muhtasari
wake kama 666 (Mia sita na sitini na sita).
3. Je
namba hii inaweza ikawa na maana gain nje ya Biblia?
Katika
fani ya hisabati namba hii 666 ni jumla ya namba zote nzima (Whole numbers)
kuanzia 1 hadi 36 yaani 1+2+3+4+5+6…+36 = 666
Jaribu
kufanya na kuhakikisha ukweli huu.
4. Mifano
mingine ya Kibilia:
a) Katika
Injili ya Matayo 1:1-7 ukoo wa Yesu unaonyeshwa katika makundi matatu yenye
vizazi 14. kila kundi limepewa tafsiri ya namba ya jina la Mfalme Daudi! Kwa
Kiebrania jina daudi linawkailishwa na herufi au konsonati hizi tatu DWD.
Yaani:
D- 4
W-6
D-+4
Jumla
= 14
i. Namba hii 14, ni mara mbili ya ile
namba kamilifu yaani 7. hivyo 14 = 2X7.
ii. Makundi
hayo matatu ni herufi tatu DWD za jina la Daudi!
B. Mfano wa
Pili : kwa Kiebrania neno mimba linawakilishwa na konsonanti hizi :
HRYWN
Hii inawakilisha nini kibiblia ?
H – 2
R – 200
Y- 10
W- 6
N- + 50
Jumla 268
Maana yake : Mimba ya kawaida hukaa
kwa muda wa siku 268. yaani miezi 9 = (268)
C. Mfano wa
tatu : kwa Waisraeli (Waebrania) waliamini kabisa kuwa ‘kisirani chema’
(good omen) kwa mtu kilikuwa ni kubadili divai iwe maji !!!. hii ni ajabu
kabisa kwa nini ? je Konsonati za maji ni zipi ? Na je zinawakilisha
nini ? ama kweli Wayahudi walikuwa na divai nyingi kuliko maji.
Jangwa
lilikuwa kubwa.
Hapa kwetu Tanzania
huenda tungalitamani kubadili mito
yote inayotiririka kutoka milimani
iwe divai !!
Kwa
Waisraeli maji yaliwakilishwa na konsonati hizi
M-
40
Y-
10
M-
+40
Jumla
– 90
Hivyo, kumtakia mtu uwezo wa kubadili Divai iwe maji
ni kumtakia maisha marefu hadi miaka 90. kama Walatini wasemavyo (Ad Multons
Annos).
Tafsiri, kauli
inayojenga na kubomoa unyumba
l Maneno yanaweza kuficha au kufichua kilichofichwa
Joseph Sabinus
MTAALAM mmoja wa mambo ya Kisaikolojia, aliwahi kusema kuwa ulimi ni
nyama nzuri kuliko zote, na ndiyo nyama mbaya kuliko zote duniani, lakini
mwingine akasema unaweza kuwadanganya watu fulani kwa muda wote, lakini huwezi
kuwadanganya watu wote kwa muda wote.
Kwa asili, Fema alikuwa ni mtu wa mambo ya
kisaikolojia, yeye mwenyewe hakulijua hilo na hivyo, kila alipoitumia elimu
hiyo ambayo hakuipata darasani, alipofanikiwa alitamba na kujiita mtoto wa
mjini.
Ni kwa mtindo huo, alikuwa maarufu kwa kutumia ulimi
(maneno) wake kupata huduma mbalimbali zilizokuwa ngumu kupatikana kwa watu
wengine.
Wakati ikijulikana kuwa huwezi kupata tiketi ya treni
bila kutoa kitu kidogo, kwa wauzaji yeye alikuwa na mbinu
aliyotumia kuwadanganya na kuvuna kwa ndugu zake kile asichopanda kwao.
Kila mgeni walipotaka tiketi ya treni kwenda Bara ni
yeye aliyepewa shilingi 20,000/= kwa ajili ya tiketi badala ya shilingi
12,900/=.
Siku moja, uchunguzi ukafanywa kwa abiria wengine.
Kila aliyefika dirishani aliambiwa tiketi zimekwisha kwa wakati huo, nao
wengine walitoka wakisema, “Huo ni ulanguzi tu, watu wawili tu, zimekwisha,
hiyo ni rushwa tu.” “Tanzania rushwa haitaisha.” Hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya
wengi na mara nyingi ilihitimishwa na ugomvi.
Lakini kilichoshangaza Uchunguzi huu, ni kwamba Fema
alipofika licha ya wengi kukosa tikiti, yeye alipata mbili tena kwa ulaini tu.
Mwandishi wa makala akajenga urafiki wa kujikomba
mradi tu, ajue mbinu anazotumia. Fema akaona si vema agawe bure hazina yake ya
uelewa. Akagoma.
Ikabidi mbinu nyingine itumike. Mwandishi siku
nyingine akampa ndugu wa Bw. Fema kinasa sauti chake (tape recorder)
ambayo hakujua kilichofanyika. Alimwambia, “Naomba unishikie kidogo”. Kisha
yule bwana akabaki kwenye benchi akimtazama.
Tape recorder ilikuwa imewashwa na inarekodi.
Baada ya kurudi, akaeleza wageni pale nyumbani kuwa badala
ya kulipa shilling 12,9000 amelipa shillingi 20,000 baada ya kudaiwa kitu
kidogo.
Lakini, tuliposikiliza kaseti tulibaini
maneno na kauli alizotumia, alisikika akisema dirishani, “Poleni sana
inaonekana anti leo mmebanwa sana; na watu ni wengi. Hiviina mana shirika halioni umuhimu wa kuwaongeza wasaidizi; huu
sio ubinadamu kabisa.”
Yule dada pale dirishani akasema, “Tunashangaa na sisi
tunalia tu.” Kisha bwana akasema, “Yaani kwa hali kama hii, hata kusema kitu ni
sawa na kuzidi kukuonea tu na kukuchanganya,” yule dada akavutwa na maneno ya
kaka yule, akaona kuwa ni afadhali yake yeye anatambua shida zao na kama
angeweza, angewasaidia.
Hivyo, nae akataka kuonesha ukarimu na kulipa fadhila
akasema; “Kwani kuna mtu ulikuwa unamhitaji au una shida gani?” “Hapana anti,
nisikuchoshe bure nami nilikuwa natafuta tikiti, lakini kwa hali ilivyo,
nitakuwa ninakuonea endapo nitakuomba msaada kama huo.”
“Usijali tu, hebu leta hiyo pesa nijaribu kukutafutia
tuone kama tutafanikiwa… una bahati.”
Hivyo ndivyo Fema alivyopata dawa ya kisaikolojia ingawa
naye siri yake iligunduliwa.
Kwa mtindo huo, pia wanawake wawili wenye ndoa wanaweza
kuwa na tatizo la aina moja kwa wakati mmoja, lakini kwa wengine tatizo hilo
likajenga na kuimarisha ndoa huku kwa upande mwingine likibomoa.
Jesca na Janeth, labda ni marafiki wakubwa pia waume zao
Jacob na James ni marafiki wasioachana.
Marafiki hawa kwa kawaida hutembea na kurudi usiku wa
manane huku wanawake na watoto wamelala fofofo.
Hebu tujiulize kuwa inakuwaje wakati mwanaume anaporudi
nyumbani akiwa amechelewa usiku? Ni dhahiri kuna kuwa na maswali mengi.
Jesca yeye humuuliza mmewe, “Hivi unapochelewa kurudi
nyumbani namna hii unakuwa na maana gani? Au basi unaona ugumu gani, si
ungenipigia simu sasa wewe unauchuna tu, unategemea mimi nitakueleweje?”
Kwa mtindo huo maswali hayo yanasikika vingine masikioni
mwa mumewe, Jacob, yeye anayasikia, anayapokea na kuyatafsiri kuwa ameambiwa
hivi. “Ulipitia sehemu unazojua mwenyewe na hukuwa na sababu yoyote ya maana
kukufanya uchelewe; kazi gani hadi usiku. Wewe sema ukweli tu, na hata hivyo
sikuamini kabisa.”
Sasa, kama kweli mwanaume ni mwaminifu na amechelewa kwa
sababu za uaminifu mbele za Mungu, mbele
yake mwenyewe na mbele ya familia yake, lazima atasema maneno kama haya;
“Mihangaiko mingi; ni muhimu kutafuta dili hapa mjini tutaishije.” “Foleni leo
ilikuwa kubwa.”
Pia, mwanaume anaweza kusema, “Yaani kuchelewa leo tu,
ndiyo inakuwa nongwa namna hiyo?! Aaah!”
Hapo, kibao tena kinageuka majibu ya mwanaume nayo
yanapokewa kwa namna, hisia na tafsiri tofauti.Mwanamke anajisikia kama vile
labda ameambiwa hivi, “Huna sababu ya
kuchukia kwa hilo, nadhani unajua kuwa kazi ni muhimu kuliko wewe. Halafu
tatizo lako unataka tukae nyumbani muda wote tukitazamana.” Ndiyo mwanamke
anavyofikiri sasa.
Wote wako sahihi kwani kila mmoja anajaribu kuonesha
namna anavyomjali mwenzake isipokuwa ndimi (lugha) zinazotumika ndizo
zinachochea sumu katika uelewano wa wanandoa hao.Hali ya kuhisi na kutafsiri
kwamba unaambiwa mambo mengine tofauti na ulivyotarajia ndiyo husababisha
migogoro hata kusambaratika kwa ndoa baina ya watu kama Jacob na Jesca.
Bahati ni kwamba kila mgogoro huo ulipotokea Janeth
aliufahamu. Akamfuata na kumsaili polepole ili ajue namna shoga yake alivyoanza kumuuliza mumewe.Jesca
akawa anayaweka yote hadharani kwa Janeth.
Akamwambia, ”Shoga yangu, ngoja leo nikueleze namna ya
kumuuliza au kumuonya mmeo juu ya tabia kama hiyo. Si unaona mume wangu mie
siku hizi ameiacha. Unajua mume hapendi umkaripie wala kumkosoa wazi wazi. Wao
ukiwafanyia hivyo, wanajiona kama kwamba umemgeuza kuwa mtoto mdogo. Au eti
umechukua madaraka ya nyumba na sasa unamtawala.
Ni haki yako kufanya hivyo, lakini lazima umsome vizuri
na kumjua mwenzio ili ujue uwezo wake wa kupokea, kubeba, kutafsiri na
kutekeleza mambo.”
Akaendelea, “Kama mume akikukosea kwa lolote, njia bora
ya kumrudi ni ile ya kutambua hadhi yako ya kuwa MKE WAKE. Yaani, uoneshe,
upendo, heshima, upole, unyenyekevu na pia, uwe mtu wa subira.
Mumeo asichelewe kurudi nyumbani ukamfungulia mlango huku
ukimshambulia kwa maneno hata hamjasalimiana, hajakaa na wala hajala.
Ukimjua vizuri mmeo, ukamfanyia mambo kwa ufundi wa namna
ya kuishi na mume, akizidi kuwa mbogo, basi ujue lazima atakuwa na matatizo ya
akili.
Siwatetei, lakini mwanaume akioneshwa upendo wa dhahiri,
na wenye sura ya mashindano, na kwa kuwa ni kawaida wanaume huwa hawapendi
kuonekana wameshindwa mbele ya wanawake, atajitahidi na yeye akufanyie mazuri
ili akushinde kwa upendo.
Na hii wanaifanya kwa vile mara nyingi wanaume hawataki
watazamwe na jamii kuwa ndio chanzo cha kulegalega katika familia.
Hiyo ndiyo siri ya wanaume wengi, mkifanya mashindano ya
upendo katika ndoa, anataka akushinde, mkitaka mashindano ya ushetani, anataka akushinde,
mkifanya mashindano ya darasani, wanaona vibaya kushindwa na mwanamke.
Kwa kawaida, wanaume wanaoridhika na kufurahia kushindwa
na wanawake katika nyanja hizo, hata kiuchumi, ni dhahiri huwa wana dosari
katika ubongo.
Janeth akafichua, “Unajua mimi kinachofanya hatugombani
na mume wangu hata kama atachelewana badala yake tunazidi kupendana? “…Ni kwamba akichelewa kurudi, kwanza nampa
pole, namuuliza kama angependa kunywa chai, kula au aanze kwanza kuoga. Anachagua
alitakalo huku akivua viatu na kuendelea kuitazama television kwa kuibia na kwa
hali ya kuchoka.
Akishafanya hayo sasa ametulia, ndipo ninapomwambuia,
“Mume wangu, baba …naomba ikitokea unachelewa, unijulishe. Unajua ukifika muda
huu haujafika na sijui ulipo, ninakuwa na wasiwasi sana juu yako. Ukifanya hivi
baba… utakuwa umenisaidia sana.
Sasa, hebu tujadili kinachotokea wakati mwanamke
akitamani kitu na kumbe mumewe akakisahau; hali inakuwaje. Kwa kawaida hapa
huwa kuna namna fulani ya zogo au mgomo baridi kwa mwanamke dhidi ya mwanamme.
Tabia hubadilika japo siyo sana na kwa wazi zaidi. Hakika
hali hii huwa ni kovu dogo, lakini lenye sumu kali katika maisha ya ndoa.
Mara nyingi mwanaume anaposahau kitu kilichotegemewa na
mwanamke, mwanamke huweza kutoa kauli kama hizi, “Kweli hicho tu, ndicho
unachosahau vingine hausahau; unavikumbuka hata bila kuambiwa. Unafanya hata
nishindwe kukuamini maana naona…”
Ugonjwa unakuja kwamba kwa mwanaume, kauli kama hiyo
inapenya na kusikika vingine masikioni, inaweza kuwa inasikika na kutafsirika
vibaya kama hivi, “Huna sababu ya
kusahau kitu kama hicho, labda una matatizo ya akili na wewe sio mtu wa
kuaminika kabisa.”
Pia, kauli kama hiyo ya mwanamke japo hakupanga isikike
wala kueleweka hivyo, lakini inaweza kusikika masikioni mwa mwanaume kama hivi,
“Inaonenkana kama mimi (mwanamke) ndiye ninajikomba kwako (mwanaume) na pengine
inaonekana mimi ndiye ninayetoa zaidi kwenye uhusiano wetu kuliko wewe
mwanaume.”
Sasa, mwanaume naye anaposikia maneno hayo huku yakiingia
masikioni kwake na kutafsiriwa kwa namna hiyo hapo juu, hujaribu kujibu mapigo
kwa staili anayoijua yeye.
Mara nyingi wengi wanaweza kujibu hivi, “Lakini mbona
hilo ni jambo dogo kuliko unavyolichukulia? Siyo kwamba sikujali hapana, ni
kusahau tu, ni kitu ambacho ni cha kawaida maana nilikuwa nimetingwa sana na
majukumu.”
Kwa mwanamke nayo haya yanatafsiriwa vingine, yeye
anajisikia kana kwamba ameambiwa vibaya zaidi, anakuwa mbogo na kusema,
“Utasikitishwaje na mtu mdogo kama mimi, si ndiyo maana unaona ni kitu kidogo
na cha kawaida.”
Sasa, matokeo ya tafsiri za namna hii, zinazotokana na
usikivu, uchambuzi na uamuzi wa maana ipi itumike kwa manufaa yako na mwenzio
kuwa tofauti na ilivyotolewa, huwa ni songombingo katika ndoa.
Lakini, kama mtu anajua kutoa kauli nzuri hata kwa jambo
baya, hivi ni vitu vidogo sana kwa
mwanandoa mwenzio na kwa mshirika wako wa namna yoyote, kazini, shuleni na
katika maeneo ya makazi ikiwa pamoja na
katika biashara.
Janeth yeye alisema
kuwa yanapomtokea mazingira ya mumewe kusahau kile ambacho yeye Janeth
alitarajia kupata toka kwa mumewe, au amesahau kufanya jambo fulani, humwambia,
“Mume wangu siku ukininunulia kitu fulani nitafurahi,” “Mwenzangu ninatamani
uninulie kitu hiki, nikipata nitashukuru kweli, lakini usihangaike kama kwa
sasa huwezi ila, ukipata nafasi siku yoyote.”
Janeth anaonya kuwa, “Kamwe usimwambie mumeo kuwa
amesahau, wewe jifanye kuwa hujui kwamba kasahau. Hii ni kwa sababu ukimwambia
hivyo mumeo wakati anajua ulishamwambia, au alishapanga hivyo, atajua kuwa
amesahau na atajitahidi mara nyingine akumbuke.”
Lakini, ili kujenga ushindani wa upendo na mvuto wa
wanandoa kwa hali iliyo sawa, ni wajibu mwanaume anapobaini ukweli juu ya
kusahau kwake, basi ajue namna ya kumwambia mkewe ili ajenge nguzo thabiti ya
upendo na imani.
Anaweza kusema hivi, “Kwa kweli mke wangu au mama fulani,
hicho kitu nilikuwa ninakikumbuka sana, lakini sijui nimeghafirika vipi
nikasahau, naomba unisamehe bwana ni bahati mbaya. Nadhani umechukia sana,
usichukie bwana ni bahati mbaya nisamehe.”
Akishasema maneno kwa namna hiyo, mwanamke atajisikia
vizuri na huru. vibaya.
Sasa, wakati huu pia, mwanaume hana budi asiseme kitu.
Akitulia tu, mwanamke akimaliza atajisikia vizuri kwa kuwa amesikilizwa maana
miongoni mwa vitu anavyovipenda mwanamke katika ndoa, ni haki ya kusikilizwa.
Ni vema kuzingatia kuwa ndoa ni kitu muhimu
kisichohitaji mchezo, mzaha, majaribio wala kutiana vishawishini.
Dawa yake kubwa ni kila mmoja kujitoa kuwa zawadi kwa
mwenzake kwa kila jambo, kiroho na
kimwili.
Ni muhimu wanandoa wakajuana kwa ukaribu na uwazi
zaidi kuwa kila mmoja anapenda na kuchukia nini, na kwa wakati gani.
Wanandoa wasipozingatia hayo, na kuimarisha upendo wa
kweli, uvumilivu na kusameheana, wote wanaweza kujikuta katika hatari ya kuwa
mazao sumu, badala ya kuwa mazao yanayoza matunda ya upendo na matumaini.
Kila mmoja ajue
kuwa kosa moja linaweza kuwa na hasara kubwa kwa mwenzio kutokana na kauli
zilizotumika na namna zilivyotafsiriwa.
Msomi wa KKKT ataka vijana matajiri
wasipotoshe maskini
Na Brown Sunza
MSOMI mmoja wa Chuo
Kikuu cha Huduma
ya Kiroho kilichopo Makumira , Arusha , Heko Pori, amesema vijana wenye uwezo
wa kifedha waache kuwadanganya na kuwapotosha vijana wa familia duni
kiuchumi kwa sababu hali hiyo inaziongezea matatizo familia masikini.
Aliyasema hayo hivi
karibuni wakati akizungumza na KIONGOZI katika Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara katika Dayosisi ya
Mashariki ya Pwani, Jijini Dar es Salaam.
“Baadhi ya vijana
wanaotoka katika mazingira magumu
kimaisha wamekuwa wepesi wa kudanganywa na vijana
wenye uwezo wa kifedha na kujikuta wanajihusisha na vitendo viovu na
vyenye madhara makubwa katika jamii kiroho na kimwili,” alisema.
Alisema tamaa ya fedha ni
miongoni mwa vitu sugu vinavyowaingiza
vijana katika ushawishi wa kushiriki vitendo vya uhalifu vikiwamo vya wizi,
utumiaji wa dawa za kulevya na ufuska na hivyo, kusababisha kupungua kwa nguvu kazi ya taifa.
Alibainisha kuwa,
matokeo ya kujihusisha na udanganyifu miongoni mwa
jamii ni kuwa tegemezi, nakurudi nyuma
kimaendeleo ikiwa ni pamoja na
kuambukizana magonjwa mbalimbali ya zinaa yakiwamo ya kisonono, kaswende
na UKIMWI.
“Baadhi ya vijana hujihusisha
na ngono kama starehe na hii inawafanya wasichana wapate mimba zisizotarajiwa
na katika umri mdogo,” alisema.
Aidha, alisema kuwa kutokana
na udanganyifu huo, baadhi ya vijana wamekuwa wakihatarisha afya zao kiakili
kwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya zikiwemo bangi.
Bw. Pori alisema, jamii
inayoamini mila potofu za kishirikina, haina budi kuombewa ili epukane na
madhara ya kushiriki uhalifu ukiwamo ulevi ambao huugeuza na kuona kama
wanarogwa.
Watendaji
wa kata Serengeti waelimishwa kuhusu UKIMWI
Na Christopher Gamaina, Serengeti
WATU 26 wakiwamo watendaji 18 wa kata
zote katika Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, wamepata mafunzo ya siku 10 ya
upembuzi shirikishi ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni, Mratibu
wa Kudhibiti UKIMWI wilayani hapa, Bw. Jackson Thoya, alisema kuwa mafunzo hayo
yaliyowashirikisha pia wajumbe wanane kutoka asasi mbalimbali wilayani hapa,
yaliandaliwa na Shirika la Tafiti za Dawa Afrika (AMREF) na kufanyika katika
Kijiji cha Isenye wilayani hapa.
Alisema kuwa, mafunzo hayo yametolewa kwa watendaji hao ili baadaye nao
waweze kufundisha watendaji wa vijiji ambao nao watatakiwa kufundisha wananchi
vijijini juu ya kuanzisha miradi ya maendeleo yenye lengo la kukabiliana na
maambukizi ya UKIMWI na magonjwa ya
zinaa.
Alifafanua kuwa hivi sasa magonjwa hayo yanaongezeka kwa kasi kubwa
wilayani hapa kutokana na kuwa bado wananchi wana uelewa mdogo na wengine
wanakuwa wagumu kubadili tabia.
Alisema, pamoja na mambo mengine, watendaji hao watafundishwa namna ya
kuweza kutambua hali halisi iliyo katika jamii, kuamini kuwapo kwa UKIMWI na
kufahamishwa vyanzo, madhara na kinga thabiti ya ugonjwa huo.
Mratibu huyo alisema kuwa, hatua ya kuishirikisha jamii yenyewe kwa
kuifahamisha mbinu mbalimbali za kukabiliana na janga la UKIMWI, itasaidia
kuwashawishi watu kuepukana na vitendo vinavyoweza kuchangia kusambaa kwa
UKIMWI katika jamii.
Thoya aliongeza kuwa, baada ya mafunzo hayo, watendaji hao watapatiwa
mafunzo mengine kuhusu UKIMWI yatakayowawezesha kufahamu jinsi virusi vya
UKIMWI vilivyo na jinsi wanavyotakiwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi wote
vijijini.
Ametoa wito kwa jamii kutosita kutumia watendaji hao katika kujua hali
halisi kuhusu UKIMWI.
CWT Mara yataka walimu wasiadhibiwe nje ya Katiba
Na Christopher Gamaina, Tarime
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Mara, kimewataka viongozi wake
kutumia sheria na Katiba yake kuwaadhibu walimu wanapopatikana na makosa badala
ya kuadhibiwa kiholela.
Wito huo ulitolewa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa CWT
mkoani Mara, Shadrack Tembe, alipokuwa akifunga semina ya siku tano juu ya
uongozi bora ndani ya C.W.T.
Semina hiyo iliwashirikisha walimu 35 kutoka shule
mbalimbali za msingi mkoani Mara na kufanyika katika ukumbi wa CMG Motel mjini
hapa.
Tembe alisema kuwa, baadhi ya viongozi wa Chama hicho
wamejenga tabia ya kuwachukulia hatua za haraka walimu ikiwa ni pamoja na
kuwafukuza kazi kabla ya kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma
zinazowakabili.
Aliongeza kuwa, hali hiyo inakwenda kinyume na Katiba
ya C.W.T.
Naye Mratibu wa semina hiyo kutoka makao makuu,
Nalonga Shani, aliwataka walimu hao kuzingatia waliyojifunza katika semina hiyo
ili kuboresha utendaji kazi kwa kuelewa mipaka ya uongozi na hivyo, kuepuka
migogoro ndani ya CWT.
Aidha, aliwataka viongozi wa Chama hicho kushirikiana
katika kazi na kuwashirikisha wanachama katika maamuzi ya Chama ili kuhakikisha
walimu wanajiendeleza kitaaluma.
Shani alisema kuwa, ni vema kuwaelimisha pia, walimu
wasio wanachama kuhusu malengo ya C.W. T na faida zake kwa wanachama ili nao
wavutike kujiunga na Chama hicho.
Wakati huo
huo: Afisa Elimu wa Wilaya ya Tarime, Michael Igogo ametoa wito kwa
wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kufichua walimu wabadhilifu, wazembe
na wanaoenda kinyume na maadili ya kazi zao.
Igogo alisema kuwa tatizo la kuwapo kwa baadhi ya
walimu wanaokiuka taratibu na maadili ya taaluma yao halitatokomezwa kama
wananchi watakaa kulilalamikia tu mitaani bila kufichua kwa kuwasilisha kwenye
vyombo husika majina ya walimu wa aina hiyo ili wachunguzwe kwa kina.
Makamu wa Askofu ahamishiwa
Roma
Na Pd. Pamphilius Kitondo, Rulenge
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la
Rulenge, Mhashamu Severine NiweMugizi, amemteua Padre Respicius Rugemalira kuwa
Makamu wa Askofu wa Jimbo hilo badala ya Padre Protas Rugambwa anayekwenda Roma
kufanya kazi katika Ofisi ya Kipapa ya Uenezaji wa Injili.
Kwa mujibu wa Mhashamu NiweMugizi, Padre Rugambwa anakwenda
Roma katika Ofisi ya Uenezaji Injili katika upande wa Lugha ya Kiingereza.
Mhashamu NiweMugizi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), alitangaza mabadiliko hayo katika hitimisho la mafunzo endelevu
ya mapadre wa Jimbo la Rulenge, waliokusanyika katika Makao Makuu ya Jimbo.
Padre Rugemalira (38), ni mzaliwa wa
Parokia ya Rubya.
Naye Padre Rugambwa (42) ni mzaliwa wa
Parokia ya Nyaishozi, Karagwe.
Tangu Askofu NiweMugizi aingie madarakani,Jimbo la Rulenge limekuwa na utaratibu wa kuendesha semina maalumu za malezi endelevu ya kila mwaka kwa ajili ya mapadre wote jimboni.
Mafundi kuweni waaminifu kama vinyozi,
wasusi
Na Getrude Madembwe, Iringa
“HUKO mitaani nasikia watu wakisema kuwa fundi mkweli ni kinyozi au
msusi kwani hawezi kukuambia uache kichwa ukifuate kesho sasa hapa inaonesha ni
jinsi gani mafundi wa nguo wasivyowaaminifu, lakini ninyi mliomaliza mafunzo haya
msije mkawa mafundi wa aina hiyo; kuweni waaminifu kwa wateja wenu”.
Padre Fransisko
Msofu, aliyasema hayo wakati wa Misa ya Mahafali ya Wanafunzi wa Chuo cha
Ufundi cha Sanaa House yaliyofanyika chuoni hapo mwanzoni mwa juma.
Chuo cha Sanaa House kinamilikiwa na Jimbo Katoliki la
Iringa na kipo chini ya ofisi ya CARITAS, Kitengo cha Maendeleo ya Akinamama.
Alisema kuwa mara kwa mara watu wanakuwa hawaamini
baadhi ya mafundi kwani hutoa visingizio vingi endapo hajamaliza kushona nguo
ya mteja.
“Sasa nyie mfute hiyo dhana kuwa fundi mkweli ni msusi
au kinyozi. Nanyi kuweni waaminifu katika ufundi wenu,” aliasa.
Akaongeza, “Huko mnako kwenda, jamii inataka kuona
kile ambacho mmekivuna mnapaswa kuwasaidia na kuwaelekeza vizuri.”
Padre Msofu aliyekuwa mgeni rasmi, alisema katika kila
roho ya mtu kuna mbegu bora na mchango kwa jamii, hivyo wahitimu wasiukalie
ufundi wao bali wanautumie vizuri.
Akijibu risala
ya wanachuo iliyoeleza matatizo waliyonayo likiwemo la ukosefu wa vyumba vya
kulia chakula na mabweni, Padre Msofu alisema kuwa uongozi wa chuo hicho una
mpango wa kuongeza chumba kwa ajili ya kulia chakula, ofisi ya walimu pamoja na
mabweni.
Walimshukuru Mlezi na Mkuu wa Chuo kwa malezi
waliyoyapata tangu walipokuwa chuoni hapo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mkuu wa Chuo ni Sista Sabina Witnes (CST) na Padre
Gasper Makombe, ndiye Mlezi wa Chuo.
Chuo hicho pia hutoa mafunzo ya upishi wa vyakula vya
aina mbalimbali, ufumaji wa vitambaa pamoja na kudarizi nguo za kike na za
kiume na hutoa mafunzo ya bila kujali jinsia au dhehebu lolote.
Wataalamu sasa wanatumia elimu kuleta vurugu si
maendeleo –Padre
Na Lilian
Timbuka
IMEELEZWA kuwa
mwanadamu wa sasa amekuwa akiitumia vibaya elimu ya Sayansi ya jamii kwa kuleta vurugu ulimwenguni badala ya
kuitumia kwa manufaa ya umma.
Kauli hiyo
ilitolewa hivi karibuni na Padre Leo Aman wa Kanisa Katoliki nchini wakati wa
uzinduzi wa majengo ya Shule ya Sekondari ya Loyola iliyopo katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Alisema elimu
haitakuwa na maana endapo wasomi wenyewe
ndio watakuwa chanzo cha vurugu, mauaji, uchochezi wa vita na kutengeneza
silaha za ajabu ajabu kwa ajili ya maangamizi ya vita kunakopelekea uvunjwaji wa amani duniani.
Alisema wazazi
wanapowapeleka watoto wao shule mara zote huwa wanategemea kuwa mtoto anakwenda
kujifunza mambo ambayo yatamsaidia
baadaye kwa kuwa na busara zaidi kuchangia kuleta nuru, amani na upendo
miongoni mwa jamii.
Aidha,Padre huyo
aliitaka jamii itambue kuwa siku zote elimu huanzia nyumbani kwa wazazi
kuwafundisha watoto wao jinsi ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na namna ya
kuwasaidia watoto wenzao wasiojiweza.
“Daima msingi
mzuri au urithi mzuri ambao mtoto hataweza
kuusahau katika maisha yake
duniani, ni urithi wa elimu. Sisi kama wazazi na wanajamii kwa jumla
tusidharau kuwasomesha watoto wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa
katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia, wasomi wengi wanapendelea kujifunza
masomo yanayowasaidia kujiajiri wenyewe kuliko kutegemea ajira kutoka sehemu
nyingine.
“Hivyo si budi wazazi
wakaangalia shule ambazo watawapeleka watoto wao ambako watapata elimu ya
kutosha kuwawezesha kujitegemea wenyewe hapo baadaye baada ya kuhitimu,”
alisema.
Majengo
yaliyozinduliwa yalijengwa kwa msaada ya Mapadre na Masista wa Shirika wa
Jesuiti ambalo lipo chini ya Kanisa Katoliki.
Wakati huo huo; Waziri wa Elimu na Utamaduni,Bw. Joseph Mungai
katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa majengo hayo, aliliomba Shirika la
Wajesuiti kuendelea kutoa misaada zaidi
ya ujenzi wa shule hususan zile za msingi zenye uhaba wa majengo.
Alisema Tanzaniai
inaupungufu mkubwa wa shule za msingi hali inayosababisha mlundikano wa
wanafunzi katika madarasa.
“Darasa moja lenye
uwezo wa kubeba wanafunzi 40, hivi sasa linakaliwa na wanafunzi zaidi ya 120,”
alisema.
Shule ya Sekondari
Loyola ilianza rasmi kutoa mafunzo mwaka 1995 kwa kuanza na wanafunzi wapatao
140.
Nusu ikiwa ni
wasichana na nusu nyingine wavulana
ambapo hadi sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,100 wanasoma kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Sita.