Viongozi wa dini tajirisheni watu - Askofu
l
Padre ataka watu waache anasa, stareheNa Mwandishi Wetu
WAKATI Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi amewataka viongozi wa dini na waamini kufanya kazi kwa uaminifu na kutumia mapaji yao bila majivuno ili kuwatajirisha wengine, Padre mmoja amewataka Wakatoliki kuitumia Kwaresima kwa kuacha anasa na starehe .
Askofu wa Jimbo katoliki la Moshi, Mhashamu Amedeus Msarikie, alitoa wito huo wakati akihubiri katika Ibada ya Majivu, katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katokliki Tanzania (TEC), Jumatano iliyopita.
Akinukuu Ujumbe wa Kwaresima wa Baba Mtakatifu Yohane Paul wa Pili kwa mwaka huu wenye wazo kuu lisemalo: MMPEWA BURE TOENI BURE, Mhashamu Msarikie alisema, "Tumepewa mwaliko wa kutambua mapaji ya Mungu na kuyapitisha kwa wengine...basi na sisi tuyatoe kwa wengine na tusiyang’ang’anie kama yetu na wala tusijivunie, bali tuyatumie kuwatajirisha wengine kiroho na kimwili."
Alisema watumishi wa Mungu wajitazame namna utumishi wao ulivyo huku wakijitoa kwa moyokatika kumtumikia Mungu kwa uaminifu. "Moyo wetu uwe pale katika kazi zetu na ugundue namna ya kufanya kazi ile kwa ufanisi zaidi...uwe katika utumishi wako kiakili na kiroho na siyo kuwapo kimwili pekee," alisema.
Alisema ni muhimu kwa kila mtumishi kujitoa ili kufanya kazi kwa moyo wa ufanisi na uaminifu mbele ya Mungu bila kujali kama wakubwa wa kikazi wapo au hawapo. "Tuwe waaminifu katika utumishi wetu yaani, tujitoe bila kuangalia kama wakubwa wetu wataona au vipi. Lazima tuzingatie uaminifu mbele ya Mungu... Kila mmoja awe mkweli katika utendaji wake," alisisitiza.
Mhashamu Msarikie alisisitiza jamii ya Wakristo kukitumia kipindi cha Kwaresima kujisahihisha makosa yao na kujitoa kwa wengine ili hao wengine watajirike kiroho.
Aidha, habari zilizopatikana toka katika Parokia ya Kurasini, Jimbo Kuu katoliki la Dar es Salaam, zinasema Katibu wa Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padre Andrew Luanda, amesema Wakatoliki wazingatie umuhimu wa Mfungo wa Kwaresima kwa kuyakana na kuyaepuka matendo ya dhambi badala ya kukazania kufunga kula chakula.
Padre Luanda alikuwa akihubiri katika Ibada ya Majivu parokiani hapo Jumatano iliyopita.
Alisema ni makosa kwa waamini kukazania kujinyima chakula pekee huku wakiendelea kushiriki katika vitendo vinavyokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu."
"Fungeni vilema (dhambi ) vyenu msikazanie tu kufunga kula cha msije mkafa na njaa bure. Kama una ndoa ya mitala nje ya ndoa yako, kuanza sasa acha," alisema.
Aidha, Padre Luanda alisema uwingi wa waamini ulioonekana katika ibada hiyo, uendelezwe siku zote badala ya kusubiri siku za sikukuu pekee.
"Wengine wamekuja leo Siku ya Majivu mpaka kanisa limejaa mpaka nje na kurudi kwao tena ni mpaka siku ya Pasaka. Jengeni utaratibu wa kuhudhuria ibada katika siku zote," alisema.
Wachungaji Moravian wahimizwa kuzingatia elimu ya kujitegemea
l
M/kiti asema dhambi nyingi hutokana na njaal
Awalilia chonde chonde wenye UKIMWI wasijiue,l
‘Roho zenu zina thamani kubwa kwa MunguNa Joseph Sabinus
LICHA ya kuwalilia chondechonde wenye UKIMWI wasijiue kwani roho zao zina thamani kwa Mungu, Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), limewataka wachungaji wake kutilia mkazo elimu ya kujitegemea kwa waamini ili kulitegemeza Kanisa huku wachungaji nao wakijishirikisha kujiongezea mapato bila kukiuka maadili ya kichungaji.
Mwenyekiti wa Kanisa hilo katika Wilaya ya Mashariki, Jimbo la Kusini, Mchungaji Eli Douglas Ambukege, alisema hayo mwishoni mwa juma wakati akizungimza na KIONGOZI, jijini Dar es Salaam.
Alisema, dhambi nyingi zinakuja duniani kwa sababu ya njaa ambayo hutokana na uvivu wa kutofanya kazi na hivyo, ni wajibu wa viongozi hao wa dini kutilia mkazo elimu ya kujitegemea ili iwasaidie waamini katika kujitegemea na kujiletea maendeleo.
Alifafanua kuwa, endapo waamini watafundishwa vema na kujitegemea katika kujiletea maendeleo, Kanisa pia litajitegemea kwa kuwa waamini hao watalichangia na kuliwajibikia ipasavyo.
"Mkristo akijitegemea, ni rahisi kulifanya Kanisa nalo lijitegemee, pia ni wazi kuwa uchumi ukiimarika nyumbani watoto wakala, wakatibiwa na kusoma vizuri na huku pato likibaki, atakuwa na kitu cha kutoa kanisani kama shukurani kwa Mungu wake.
"Hata hivyo, wachungaji hao wajali mpangilio mwema wa kazi. Wawe na bidii na watoe kipaumbele katika wito waliotumwa ili kuchunga kondoo wa Mungu," alisema.
Alikiri kuwa baadhi ya wachungaji wanabanwa na tatizo la ufinyu wa maeneo na hivyo kukosa sehemu za kufanyia miradi ya kuwaendeleza kimapato.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa KMT Wilaya ya Mashariki, amesema waathirika wa virusi vya UKIMWI wasijiue kwa kuwa roho zao bado zina thamani mbele ya Mungu.
Alisema jamii inao wajibu wa kuwapenda, kuwashauri, kuwajali na kuwatunza waathirika wa virusi vya UKIMWI.
"Ingawa wameathirika, lakini huo sio mwisho wa matumaini; bado roho zao mbele ya Mungu zina thamani kubwa na hivyo waamini kuwa siku moja watasimama mbele za Mungu kwa furaha kuliko kukata tamaa na kujiua," alisema.
Aliwataka wakazi wa mijini, kuiga mfano wa baadhi ya wakazi wa vijijini ambao huonesha moyo wa kuwajali wagonjwa hadi wanapofariki.
Aliwasisitiza wanadamu kuzingatia matumizi ya dawa ya UKIMWI ambayo alisema ni kumfuata Yesu Kristo kwani hakuna dawa nyingine.
Mchungaji Ambukege, aliilaumu tabia ya watu kutokuelewa vema njia zote za maambukizi ya UKIMWI hivyo, kuwachukulia waathirika wote wa virusi vya UKIMWI kuwa ni wazinzi na hali aliyosema ni makosa.
"Watu wametawaliwa na tatizo moja la kuamini kuwa UKIMWI unaenezwa kwa njia ya zinaa pekee na hivyo, kufanya kosa lingine la kuwahukumu na kuwatenga waathirika; sio vizuri kabisa kuwatenga," alisema.
Ugonjwa wa UKIMWI huenezwa kwa njia ya zinaa, kuongezwa damu yenye virusi vya UKIMWI, kuchangia vyombo vya kotogea visivyochemshwa sawi na mjamzito kumuambukiza mwanae tumboni.
Mnaowaombea wengine mabaya msipoteze muda- Mch. TAG
Na Benjamin Mwakibinga
MCHUNGAJI mmoja wa Kanisa la TAG amesema wanaofanya maombi ya kuwatakia wenzao mabaya, waache tabia hiyo kwani wanapoteza muda wao bure na kwamba anakerwa na Wakristo wanaoogopa wachawi.
Mchungaji huyo wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), aliyasema hayo Jumapili iliyopita wakati akihubiri katika Usharika wa Ubungo-Rubada jijini Dar es Salaam.
Alisema Mkristo mzuri ni yule anayejiombea mema kwa imani ya kimungu na kuwaombea wengine mafanikio ya kimwili na kiroho.
Alisema maombi bila imani ni sababu kubwa inayowafanya baadhi ya Wakristo kulalamika kwamba maombi yao hayajibiwi na akawasihi kudumu katika kufanya maandalizi mema kabla ya maombi yao.
Aidha, kiongozi huyo wa kiroho alisema anasikitishwa na tabia ya watu wengine kuwaogopa wachawi badala ya kujitoa na kumtegemea Yesu Kristo.
Alisema maisha ya Ukristo yanahitaji mtu kuwa na moyo wa uvumilivu na kwamba dawa ya matatizo ni Mkristo kudumu katika maombi na sala.
"Ikiwa Yesu Kristo mwenyewe aliomba na kufunga ili apate kushinda majaribu ya shetani; je wewe ni Mkristo gani unaezembea katika suala la maombi?" alihoji.
Aidha, Mchungaji huyo aliwahimiza Wakristo kuimarisha imani na kuondokana na woga juu ya vitisho vya shetani.
Alisema imani thabiti itasaidia kumshinda ibilisi. "Ni wakati wa kukua na kuanza kujitegemea kiimani," alisema.
Alisema Wakristo duniani waonekane kuwa ni taa ya ulimwengu na hivyo, walete mwanga mahali palipo na giza na hivyo, wathibitishe ukweli kuwa Ukristo ni nuru ya ulimwengu.
Uguzeni wagonjwa msisubiri kuchangia misiba
l
Paroko adai Watanzania wana Huruma, hawana upendo kwa wagonjwaNa Neema Dawson
WATANZANIA wameshauriwa kuwajali na kuwasaidia wagonjwa kwa upendo kwa kutumia mali waliyo nayo kuwahudumia wapone badala ya kusubiri kuchangia katika vifo na kujipatia umaarufu katika misiba.
Paroko wa Parokia ya Yombo, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padre Camile Neuray, aliyasema hayo katika siku maalumu ya kuwaombea wagonjwa iliyofanyika parokiani Yombo, Jumapili iliyopita.
Siku hiyo zaidi ya wagonjwa 250 kutoka maeneo mbalimbali walihudhuria ibada kanisani hapo.
Alisema inasikitisha kuona kuwa baadhi ya Watanzania wana huruma lakini hawana upendo kwa wagonjwa wao hali inayowafanya kuwachoka haraka wagonjwa na hata kuwatelekeza na kuwatenga.
"Inashangaza Watanzania wengi wana huruma lakini hawana upendo kwani mtu aliye na upendo humhudumia mgonjwa bila kujali hata kama anaumwa sana; ameoza na anatoa harufu..." alisema.
Akaongeza, "Mwenye huruma, humhurumia mgonjwa au mwenye shida nyingine na kumsaidia kwa muda tu.
Tena wengine hufanya hivyo ili asiendelee kumsumbua. Hivyo, kuwa na huruma bila upendo ni vibaya sana na kwa hali hiyo wenye upendo ni wachache na ndio watakaoingia katika Ufalme wa Mungu."
Alisema baadhi ya watu hupata pesa nyingi kupitia vyanzo vyao vya mapato, lakini wanashindwa kuzitumia kuutafuta Ufalme wa Mungu kwa kuwasaidia na kuwahudumia wenye shida mbalimbali kikamilifu.
Alisema kama wenye huruma na mali nyingi wangekuwa na upendo, wangetumia mali zao kuwahudumia wagonjwa hadi wapone kuliko kusubiri kutoa misaada ya michango katika misiba hali ambayo haisaidii kuokoa uhai wa mtu.
"Kuna sababu gani kutunza pesa na kushindwa kuwasadia wagonjwa na kisha kutumia pesa hizo kwa mazishi; unakuwa umepata faida gani au umeokoa nini?" alihoji Padre Camile.
Parokia ya Yombo ambayo ni somo wa Mtakatifu Kamili, huwahudumia wagonjwa bila ubaguzi wowote. Pia huwafariji na kuwapa matumaini ya kuuona Ufalme wa Mbingu.
"Ninashukuru kuona baadhi ya waamini wana moyo wa upendo kwani mara kwa mara ninapotembelea wagonjwa nyumbani, ninafuatana nao na wala hawaoni shida kuwahudumia wagonjwa wenye hali mbaya ingawa wagonjwa wengine huwa na magonjwa yanayosababisha uozo na kutoa harufu mbaya," alisema.
Aliongeza, "...Lakini tunawatembelea na kuwahudumia bila kuogopa na wengi wao wanapona hivyo Watanzania wote wangekuwa na moyo kama huo wa kuhudumia wagonjwa kwa upendo, kusingekuwa na vifo vingi ambavyo vingi vingeupukika."
Alisema yeye anapowatembelea wagonjwa, habagui dini wala kabila na kuongeza kuwa hali hiyo inathibitishwa na kufika kwa wagonjwa toka katika dini na madhehebu mbalimbali katika siku hiyo parokiani hapo. Wagonjwa hao walipewa mchele, unga na sabuni ili viwasaidie.
Siku ya Wagonjwa parokiani Yombo huadhimishwa Februari 11 kila mwaka.
Tutakosa cha kumjibu Mungu tusipounganisha Kanisa -Padre, Mchungaji
l
‘Vyombo vya habari vijenge Ukristo’Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa dini katika madhehebu ya Kikristo wamesema vyombo vya habari vya kikristo vishirikiane na viongozi wa makanisa kueneza Ukristo badala ya kuchangia utengano katika madhehebu kwani bila kuunganisha Kanisa, wanahabari hao na viongozi wa dini watakosa cha kujibu kwa Mungu.
Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Raphael Kilumanga na Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT) Wilaya ya Mashariki, katika Jimbo la Kusini, Mchungaji Eli Ambukege, waliyasema hayo katika mazungumzo yao yaliyofanyika TEC jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa juma.
Walisema umoja wa makanisa ni kitu muhimu katika kazi ya kuhubiri Injili ya Kristo na hata katika mipango mbalimbali ya serikali na hivyo, hauna budi kujengwa na kuimarishwa ili kudumisha amani, upendo, na kuboresha maendeleo ya nchi.
"Vyombo vya habari vya Kikristo vizingatie habari zenye kueneza Ukristo na kujenga maadili ya kiroho na kimwili," alisema Mchungaji Ambukege.
Naye Padre Kilumanga alisema, "...ndani ya gazet la kikristoi, mwanga wa Kristo uonekane. Hakuna faida yoyote kutumia vyombo vya habari kushambuliana badala ya kuimarisha Ukristo...Oh! Hii siyo dini. Oh! Hii inafanya hivi, hayo hayasaidii kiroho".
Wakiungana mkono, viongozi hao wa kiroho walisema kwa pamoja, "Lazima hata viongozi wa haya makanisa yetu tujue kuwa tutakuwa na jambo la kujibu kwa mMungu kama tumeunganisha Kanisa au tumelitenganisha".
Wakati huo huo: Licha ya kuwashukuru, Mchungaji Ambukege amesema waamini wilayani kwake waendeleze moyo walioanzisha ili kukamilisha miradi ya ujenzi katika wa makao makuu ya Wilaya katika eneo la Chamazi jijini Dar es Salaam.
Kanisa la Moravian Wilaya ya Mashariki linaendesha ujenzi wa ofisi na nyumba ya mwenyekiti katika eneo hilo la eka zipatazo tano. Jengo la ofisi linagharimu shilingi 20,000,000/= wakati nyumba ya mwenyekiti inagharimu shilingi 12,000,000/=. Kwa sasa makao makuu ya Wilaya hiyo yapo Ilala sehemu ambayo ni finyu na imezingirwa na wakazi wengi hivyo kuwa na ugumu wa shughuli za kiibada.
Mchungaji Ambukege alisema KMT wilayani kwake pia inaendesha ujenzi wa kisima cha maji kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa eneo hilo ambao alisema wanapata shida kupata maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kisima hicho kinagharimu shilingi 2,500,000/=. "Tuliamua tutangaze Neno la Mungu kwa kuwasaidia wakazi wa pale maana wanapata taabu sana kupata maji na pia kwa matumizi yetu ya Kanisa," alisema.
Aliongeza kuwa KMT wilayani kwake inalenga pia kujenga hosteli, zahanati, shule ya awali, ukumbi na uwanja wa michezo katika eneo hilo.
Alipoulizwa na gazeti hili juu ya vyanzo vya mapato katika kuendesha miradi hiyo, Mchungaji Ambukege alisema, "Kanisa Makao Makuu (Rungwe, Tukuyu) linatusaidia sana na hata waamini wenyewe ninawapongeza sana kwani wanatambua umuhimu wa kuitegemea ndio maana ninawapongeza kwa kuchangia kwa hali na mali".
Wilaya ya Mashariki ya Kanisa la Moravian Tanzani, katika Jimbo la Kusini inazihusisha sharika 21zilizopo Dar es Salaam, Morogoro na Pwani , pamoja na sharika ndogo za uinjilisti sita.
Umaskini si tatizo la Kimungu - Padre
Na Eric Samba
KIONGOZI mmoja wa Kanisa Katoliki nchini amewataka Wakristo wote nchini kupambana na umaskini kwa kusaidiana na kuinuana kiuchumi kwani umaskini si tatizo kwa Mungu.
Kiongozi huyo Padre George Sai aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika misa takatifu iliyofanyika katika Kanisa la Mwenyeheri Anwarite parokia ya Makuburi, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Alisema umaskini ambao unawakabili watu wengi siku hizi si tatizo la Kimungu bali la ulimwengu kwa sababu ya ubinafsi uliokithiri miongoni mwa watu katika jamii.
"Umaskini kwa Mungu si tatizo. Wewe kama una pato la shilingi milioni moja jumlisha na huyo anayepata elfu ishirini, halafu gawa katikati kila mmoja atapata laki tano na elfu kumi. Hapo maskini watatoka wapi tena?" alihoji Padre Sai.
Alishanga watu hasa Wakristo kuwashangaa wenzao ambao hawana vitu fulani huku wao wamejilimbikizia vitu hivyo zaidi ya mahitaji yao.
Alisema, "Wewe ni mama una masanduku mawili yamejaa nguo zako nyumbani, lakini unamshangaa mwenzako ambaye anavaa kaniki. Au una viatu pea tano uvunguni, lakini unamshangaa mwenzako anayetembea pekupeku. Chukua pea moja mpe avae."
Alisema Mungu aligawa vitu sawa na idadi ya watu ili asipungukiwe hata mmoja, lakini kwa sababu ya ubinafsi wa baadhi yao ndiyo maana wengine ni matajiri na wengine ni maskini.
Aidha, aliwataka vijana wote kuacha tabia ya kuamua kuishi pamoja na kuzaa watoto kabla ya kufunga ndoa, kwa madai ya kuona kama wanaweza kuzaa, kwani hiyo inawapa matatizo wakati wakitaka kubatiza watoto wao.
"Hivi lazima kama unataka kujua uwezo wako wa kuzaa ujaribie kwa mtu? Nenda Muhimbili ukapime, watakwambia. Mapenzi ya Mungu ni kwamba vijana inabidi wakutane kanisani, wafunge ndoa na baada ya hapo, waanze maisha ya ndoa takatifu," alisema.
Changomoto hiyo ya Padre Sai imekuja wakati ambapo umaskini uliokithiri unazidi kuongezeka miongoni mwa watu katika jamii na huku vitendo vya vijana kuamua kuishi wote bila ndoa kwa madai ya kuona kama wanaweza kuishi wote vikiongezeka siku hadi siku.
Mch. KKKT alia na rushwa
Na Steven Charles
MCHUNGAJI Ibrahimu Loweza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Usharika wa Temeke, jijini Dares Salaam, amesema bila kukomesha rushwa, ni vigumu Watanzania kupata maendeleo ya kweli.
Aliyasema hayo wakati akizungumza katika ibada ya Jumapili iliyopita ushirikani kwake, katika dayosisi ya Mashariki na Pwani.
Alisema ni wajibu wa jamii yote kushirikiana kuvipiga vita vitendo vya rushwa ambavyo alisema, vimeshamiri katika sekta mbalimbali.
Alisema inashangaza mtu anapokwenda kuomba huduma na kudaiwa kutoa rushwa ili anunue haki yake.
"Mtu anaumwa, anafika hospitali anaombwa atoe kitu kidogo, mgonjwa huyo atapata wapi?"
Alihoji na kuongeza, "...Au mzazi anampeleka mtoto shuleni, anaombwa kitu kidogo ili apokewe. Hivi kweli tutafika?"
Vitendo vya rushwa vimekuwa vikilaumiwa na watu, Serikali, asasi mbalimbali za kibinafsi pamoja na vikundi mbalimbali vya kidini lakini, bado inashamiri.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Kapten John Chiligati, alisema polisi wajiepushe na vitendo vya rushwa kwani kila lalamiko juu ya askari polisi kujihusisha na rushwa, ni kura moja wapo inayoweza kuchangia askari polisi huyo kuwajibishwa kwa mujibu wa taratibu za polisi.
Mnaojiweza wasaidieni watoto yatima wasome -Wito
Lilian Timbuka na Neema Dawson
WAZAZI wa familia zinazojiweza kiuchumi, wamepewa wito wa kuwasaidia kwa upendo watoto yatima na ambao wazazi wao hawajiwezi kiuchumi ili wote wapate elimu.
Wito huo ulitolewa na Mbunge wa Busanda Geita(CCM), Faustine Kabuzi Mbaye, katika hafla iliyoandaliwa na Umoja wa Makanisa ya Kiprotestanti Tanzania, ili kukabidhi msaada wa vifaa vya shule kwa watoto zaidi ya 700 mkoani Dar es Salaam ambao wengi ni yatima.
Msaada huo uliandaliwa na watoto wa nchini Uholanzi wanaosoma katika shule za Kikristo na kutumwa hapa nchini ikiwa ni njia mojawapo ya kuwasaidia watoto wenzao wasio na uwezo.
Msaada huo una thamani ya shilingi milioni 540/= za Kitanzania.
Alisema Tanzania inao watoto wengi mayatima na ambao wazazi wao hawana uwezo hivyo, ni wajibu wa wazazi kuwaonesha upendo watoto hao kwa kuwasaidia katika mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kupata elimu.
Alisema ingawa Serikali imefuta ada kwa shule za msingi, bado watoto wengine watashindwa kusoma kwa kukosa zana muhimu za masomo ikiwa ni pamoja na kalamu, madaftari, vitabu na sare za shule.
"Hivyo Watanzania wanalo jukumu la kuwa na upendo na kumuona mtoto wa jirani yako kama mtoto wwako na kumsaidia," alisema.
Aliishukuru Serikali kwa kusamehe ushuru kwa vifaa hivyo ambavyo ni maboksi yapatayo 36,000 vitakavyowasaidia watoto wengi nchini kwani hata walio katika mikoa mingine watanufaika nayo.
Alizitaja baadhi ya wilaya zitakazonufaika na msaada huo kuwa ni pamoja na Mwanga, Same, Korogwe, Muheza, Handeni, Kilosa, Bukoba-Mjini, Kambi ya Wakimbizi wa DRC ya Lugufu Kigoma, Geita, Sengerema na Tumbatu Zanzibar.
"Umefika wakati sasa kwa Watanzania kuiga yaliyofanywa na watoto wa Uholanzi katika kuwasaidia watoto wenzao," alisema.
Sambamba na msaada huo, pia wabunge watano kutoka katika Majimbo ya Muheza, Busanda Geita, Buchosa Geita, Mwanga, na Geita Mjini, walikabidhiwa baiskeli za wagonjwa ili ziwasaidie wagonjwa katika hospitali mbalimbali majimboni kwao.
KIWOHEDE
yawasikitikia watoto wanaolipwa ukokoNa Peter Dominic
ENEO la Manzese jijini Dar es Salaam limeelezwa kuwa linaongoza kwa jira za watoto wadogo jijini na kulipwa ujira mdogo ukiwamo ukoko wa chakula.
Mshauri Nasaha wa kituo kinachoshughulikia afya na maendeleo ya wanawake na watoto (KIWOHEDE) katika kituo cha Manzese jijini Dar es Salaam, Bibi Joyce Milinga, alisema utafiti wao unaonesha kuwa eneo la Manzese jijini Dar es Salaam, linaongoza kwa ajira hiyo haramu.
Alikuwa akizungumza katika Warsha ya Siku Tatu juu ya mikakati ya elimu
Na shughuli za CARITAS.
Warsha hiyo iliandaliwa na Kitengo cha Akinamama na Maendeleo ya Watoto(WID), kilicho chini ya Shirika la Misaada la kanisa Katoliki CARITAS(T). Ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), wiki iliyopita.
Alisema watoto wengi katika eneo hilo la Manzese, wanafanyishwa kazi ngumu katika ajira haramu ikiwa ni pamoja na kuhusishwa katika biashara haramu ya ukahaba.
Alisema licha ya kufanya kazi ngumu, watoto hao hulipwa ujira mdogo ukilinganisha na kazi wanazofanya.
Alisema kutokana na uwezo mdogo walionao, watoto hao hukoseshwa haki ya kupata elimu na kukabidhiwa majukumu ya kutunza familia na kufanyishwa ukahaba ili wakidhi mahitaji ya.
"Manzese imekithiri kwa kuajiri watoto wenye umri mdogo, wanalala nje kwenye mabenchi, wengine wanafanya kazi ambazo hazilingani na umri wao. Mtoto anaajiriwa kwa kuosha masufuria kutwa ili alipwe chakula cha ukoko. Watoto wa kike na wa kiume hujikuta wakinajisiwa na kulawitiwa na imefikia hatua sasa wanaiona hali hiyo kama ya kawaida," alisema Bibi Millinga.
Alisema watoto wengi wanatoka katika familia maskini.
Aliongeza kuwa tabia mbaya walizonazo zinatokana na kuathiriwa na mazingira, hivyo, akawataka wazazi na jamii kwa jumla kuwalea vizuri watoto wao kwa vile hakuna mahali ambapo mtoto anapata malezi mazuri kama nyumbani.
Mratibu wa Mradi wa Maendeleo ya Akina mama na Watoto wa CARITAS, Oliva Kinabo, alisema mradi huo wa miezi 15 ulioanza mwaka jana kwa ushirikiano na Shirika la Kazi Duniani (ILO), unalenga kuvitumia vyuo vya ufundi stadi vya Kanisa Katoliki.
Alisema katika mpango huo, walimu watapata mafunzo na kuviwezesha vyuo kutoa mafunzo kwa watoto watakaotolewa katika ajira za watoto.
"Ili kuhakikisha tunafanikiwa katika hili tumeyashirikisha mashirika ambayo yanashughulika na watoto, watoto wakiletwa kwetu watapata mafunzo na ushauri." alisema
Alitaja mafunzo yaliyolengwa kutolewa kuwa ni pamoja na ushonaji, ufundi seremala, umakanika, mafunzo ya komputa, pamoja na utengenzaji wa batiki.
Mafunzo hayo yatatolewa kulingana na mahitaji ya watoto na kwamba mradi huo utafanyika katika mikoa ya Marogoro, Dar es Salaam, Dodoma na Iringa. Mikoa mingine ni Singida, Songea, Mbeya na Arusha.
Awali akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa TEC, Pius Rutechera, Katibu Mtendaji wa CARITAS(T), Bw. Peter Maduki, aliwataka washiriki hao kuimarsha ushirikiano ili kufikia lengo liliokusudiwa.
"Warsha hii ni kujadili namna ya kutekeleza malengo tuliyojiwekea ili kuwasaidia watoto wa Tanzania," alisema Maduki.
Akifunga warsha hiyo, Katibu wa Idara ya Liturujia ya TEC, Monsinyori Julian Kangalawe aliuelezea mpango huo kuwa ni mgumu kwa vile taifa linakabiliwa na idadi kubwa ya watoto wanaohitaji msaada.
"Inatisha inafikia mahala watoto wa kike wanatembea uchi wakiuza miili yao! Inabidi sisi kama Watanzania tujiulize kwa nini inakuwa hivi," alisema Monsinyoro Kangalawe.
Alisema matatizo mengi ya watoto kufanyishwa kazi yametokana na ufukara ambao unaosababishwa na tabaka la matajiri na masikini ambapo aliyenacho anazidi kuongezewa na asiyekuwa nacho anazidi kudidimia.
Aliwataka kuzingatia kwa dhati jukumu walilolikusudia ili misaada iwafikie walengwa.
Wanaojitangaza wana UKIMWI hawana jipya - SHDEPHA+
Na Dalphina Rubyema
CHAMA cha Afya ya Maendeleo kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (SHDEPHA+), kimedai kuwa watu wanaojitokeza kwa sasa na kudai kuwa wanaishi na Virusi vya UKIMWI hawana jipya.
Akizungumza na gazeti hili mwanzoni mwa juma, Mwenyekiti wa SHDEPHA+ kitaifa, Bw. Joseph Katto, alisema wapo baadhi ya watu ambao alisema kuwa ni kweli wameambukizwa virusi vya UKIMWI kwani wengine walikwisha fika ofisini kwake miaka michache iliyopita kutaka kujiunga na SHDEPHA+.
Alisema ofisi yake kweli ilithibitisha na kupata uhakika kwamba watu hao kweli walikuwa wameathirika na kukubali kuwapa uanachama.
Alisema licha ya ofisini yake kuwapa uanachama, wengine walianza kuwa watoto na hivyo kutofika kabisa ofisi hali iliyokifanya chama hicho kidhani kuwa pengine watu hao wamefariki dunia.
Alisema katika hali ya kustaajabisha, hivi sasa baada ya baadhi ya asasi na vyama kuanza kuwashawishi waathirika kujitokeza na kujitangaza hadharani, watu hao nao wameibuka tena.
Alisema baadhi yao ambao wakati wanajisajili SHDEPHA+, walikuwa hawana watoto lakini hivi sasa anashangaa kuwaona wananyonyesha hali inayo ashiria kwamba kipindi hicho walichopotea, walikuwa wameolewa na kupata watoto.
Alisema katika kuolewa huko bila shaka wamezidi kuongeza usambazaji na uenezaji wa UKIMWI kwa jamii hali ambayo ni mbaya zaidi.
"Mimi nashangaa sijui huku ni kujitangaza kwa namna gani. Hapa miaka ya nyuma walifika watu wengi sana ofisini kwetu na kutueleza kuwa wanaishi na virusi nasi tulipata uhakika baada ya kukamilisha taratibu zote za kuwapima. Baada ya hapo walipotea na hivi sasa ndiyo wanaibukia katika taasisi na vyama vingine na kujitangaza kuwa wameambukizwa," alisema.
Aliitaka Serikali iwachunguze watu hawa kwani kwa hivi sasa wamejitokeza na watapotea tena hivyo kuendeleza maambukizi mengine.