Mapadre kuoa sio dawa ya matatizo - Pengo

l Ahoji: Mbona wanandoa wenye watoto, wataalamu wanabaka na kunajisi?

l Ataka wasigeuze sakramenti kuwa mali yao

Na Joseph Sabinus

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema licha ya mapadre kuonesha mfano bora wa kuithamini Sakramenti ya Upatanisho, hoja za baadhi ya watu kuwataka waoe ili kuepuka zinaa hazina msingi kwani watu wengine wameoa lakini wanabaka, kunajisi na kulawiti.

Akizungumza wakati wa Ibada ya Alhamisi Kuu, iliyokuwa Sikuku ya Makasisi duniani, Kardinali Pengo alisema makasisi hawana budi kuithamini Sakramenti ya Upatanisho ili waamini waige mfano wao badala ya ilivyo sasa ambapo makasisi wengine hudiriki hata kuwakaripia waamini na wengine kutoa kazi hiyo kwa kulipua.

Katika Ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam, ambapo mapadre walirudia ahadi zao za Upadre, Kardinali Pengo aliadhimisha misa ya kubariki mafuta ya wagonjwa, Krisima Takatifu na mafuta ya wakatekumeni.

Alisema baadhi ya makasisi katika Kanisa wamekuwa wakifanya makosa kuipuuzia Sakramenti ya Upatanisho na kwamba hali hiyo imekuwa kikwazo kwa waamini wengine.

Alisisitiza ukweli kuwa, katika Sakramenti ya Ekaristi, Kristo yupo kabisa kabisa kati ya wanadamu na anafika kila mahali kwa kuazima uso na sauti ya kila kuhani na hivyo, makasisi watoe nafasi kwa Kristo kufufuka na kufika kila mahali walipo.

"Ni kweli kabisa Ekaristi humuunganisha Mungu na mwanadamu. Hivyo, haiwezi kumuacha mwanadamu na dhambi kwani dhambi haikai pamoja na Mungu," alisema.

Akaongeza, "Lakini huwezi kupokea Ekaristi bila kuwa tayari. Hivyo, umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho unapuuzwa kwa uzembe na ukali wa kusulubu...ingawaje inapendwa hata na vijana".

Aidha, Kardinali Pengo alisema, "Makosa ambayo tumekuwa tukiyafanya makasisi, ni kwamba baadhi yetu tumekuwa wa kwanza kuipuuuza Sakramenti ya Upatanisho na sasa waamini wameona ikiwa hao wenyewe waliopewa jukumu hilo na Mungu wameipuuza sisi tufanye nini," alisema.

Alihimiza wito wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kwa makasisi kuwa makasisi hawana budi kujenga na kuonesha mfano bora kwa wao wenyewe kuithamini Sakramenti hiyo.

Alisema, "Ni makosa kama mtu atakuja anasema padre nahitaji Sakramenti ya Upatanisho, ukapuuza na kuona kuwa eti labda kuna jambo lingine la muhimu zaidi. Makasisi, sisi wenyewe tuanze kwa kuiandaa Sakaramenti hii kwa moyo wa furaha."

Akisisitiza katika kipengele cha kuipuuza Sakaramenti hiyo, Kardinali Pengo alisema baadhi ya makasisi wamekuwa hawazingatii hali aliyo nayo muumini wakati akiomba Upatanisho.

Alisema, kosa wanalolifanya baadhi ya makasisi ni kuwa wakali kiasi cha kuwafanya waamini waione Sakaramenti ya Upatanisho kama sehemu ya kuongezea mateso, uchungu na kupata hukumu.

"Usimsulibishe muumini mpaka akaona kama Sakramenti ya Upatanisho ni hivi, heri niende hivyo hivyo kwa Mungu na dhambi zangu atanisamehe mwenyewe kwa ukarimu wake," alisema.

Alisema kosa lingine wanalolifanya makasisi hao, ni kutoa maondoleo bila kuridhika vya kutosha kuwa muumini yuko katika hali ya toba ya kweli.

"Wengine wanafanya juu juu tu wakisema eti Mungu mwenyewe anajua. Wanasema umeondolewa dhambi bila kutafakari kama kweli huyu amejiweka tayari," alisema.

Aidha, Kardinali Pengo aliikemea tabia ya baadhi ya makasisi kujiona kama wanaostahili kutwaa mamlaka ya Mungu.

"...Wengine wanafanya kosa la kujifanya kwamba wewe ndiye unayeondoa dhambi kwa nguvu na tamko lako; sivyo. Wewe unamwakilisha Kristo aliye katika mazingira yako," alisema.

Alisema ni wajibu wa makasisi kuwatambua vema waamini wao ili kuwahudumia kulingana na mahitaji ya kila mmoja

"Wengine wanajificha, wengine wanakuja ili kupata nafasi za kueleza shida zao pia, wengine wanakuja kwa nia njema lakini hawajui waseme au wafanye nini. Hali hizo zisitufanye tuone kama ni udhia... lazima tuwe tayari kuwahudumia wote.

Alisema makasisi hawapaswi kuigeuza na kuiona Sakramenti ya Upatanisho kama mali yao binafsi, bali wazingatie kuwa ni mali ya Mungu.

"Tusigeuze Sakramenti hii kuwa yetu, kuwa mahali popote naweza kusema umeondolewa dhambi... Kila mtu ahudumiwe pamoja na mapungufu yake.

Alitaka kila mmoja wa makasisi atambue na kukubali kuwa anafanya kazi kwa nguvu za Mungu.

"Asiwepo anayesema kuwa mimi nisipotamka kwamba umeondolewa dhambi, dhambi zako hazitaondolewa; kama kwamba wewe ni Mungu.

Aidha, katika ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini, Kardinali Pengo alisema, makasisi watambue kuwa wanaangaliwa na jamii ya kitaifa na kimataifa hivyo, ni wajibu wao kudumu katika uadilifu na kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kushusha heshima ya Kanisa.

"Baadhi yetu mapadre duniani tumefanya vitu ambavyo ni ishara ya dhambi katika ngazi ya juu kabisa. Wengine wamekwisha shitakiwa kwa kubaka, kufanya mapenzi ya ajabu na wavulana hadi kufikia watu kusema ni heri Kanisa liruhusu makasisi wake kuoa," alisema.

Alisema kuwarushu mapadre kuoa sio suluhisho la vitendo hivyo viovu kwa kuwa hata wanataaluma mbalimbali wamekuwa wakisikika kwa kiwango kikubwa kushiriki kwao katika vitendo hivyo licha ya kuwa ni watu wenye wake zao.

Kardinali alitoa mfano wa baadhi ya watu ambao licha ya kuwa na wake zao nyumbani, lakini unashangaa anambaka au kufanya vitu vya ajabu na mtoto wake wa kuzaa" alisema.

Njoolay amlilia Askofu Mkatoliki

l Ataka Watanzania waige mfano wake

Na Reginald Barhe, Arusha

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Bw. Daniel Ole Njoolay, amewapa changamoto Watanzania waige mfano wa uongozi bora wa Askofu Mkatoliki mwanzilishi wa Jimbo la Arusha, Marehemu Dennis Durning.

Njoolay alitoa changamoto hiyo hivi karibuni wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali katika mazishi ya Hayati Askofu Dennis yaliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Ngarenaro, Jimbo Kuu Katoliki la Arusha.

Alisema Askofu Durning alikuwa kiongozi bora aliyejua kuongoza akijibu mahitaji ya Watanzania kwa wakati, mahali na hali mbalimbali huku akihudumia jamii bila kujali unyonge na umaskini wao.

Alisema kutokana na utumishi bora wa Askofu Durning, alitoa huduma mbalimbali za kiroho na kimwili ikiwa ni pamoja na kujenga hospitali katika maeneo magumu ambayo Serikali ilishindwa kwa wakati huo.

Alitaja mfano wa hospitali za Wasso Loliondo na Endulen katika maeneo ya Wamasai ambako hata serikali ilishindwa kuhudumia sababu ya mawasiliano mabaya na hatari mbalimbali kama wanyama pori na mazingira magumu ya kiuchumi.

"Hayati Askofu Durning alihudumia Watanzania hao katika mazingira ya kichungaji akianzishia miradi kuendeleza mifugo na shule kwa wataalamu mifugo, pia akabuni usafiri wa ndege kwa wagonjwa kwani hapakuwa na barabara kufikisha hospitali," alisema Njoolay.

Alisema kuwa, Taifa na Kanisa wamempoteza kiongozi ambaye nafasi yake haitazibika kwani huduma yake ilikuwa bado ikihitajika hususan ya waathirika wa kijamii na kitamaduni kutokana na ugumu wa mazingira.

Aidha, Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha Mhashamu Josephat Lebulu, alimwelezea Hayati Askofu Durning kuwa kiongopzi wa kiroho aliyekuwa mnyenyekevu, mvumilivu na mpenda watu.

Akisoma wasifu wa Marehemu Durning, Mwenyekiti wa WAWATA wa Bashay, Bi. Elizabeti Massinda, alisema pengo aliloliacha marehemu halizibiki kwani alikuwa kimbilio la wote waliokuwa na shida za kiroho na kimwili.

"Baba Dennis alikuwa chimbuko la kuwatambulisha umaana na ubora wa utume wa walei kama nyenzo maalumu ya kumfikia Mungu akiyaishi maisha haya kwa unyoofu, uwema na uaminifu bila kudharau binadamu kama mwenyewe alivyohudumia wote kwa usawa," alisema.

Taarifa toka ndani ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini zimeeleza Mhashamu Dennis kuwa mmoja wa viongozi wa Kanisa Katoliki nchini aliyehudhuria mtaguso II wa Vatikano akiwa Askofu baada ya kuteluliwa kwake na pia alikuwa Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa Ofisi ya AMECEA.

Taarifa imemtaja kuwa Mtaalamu wa Sheria za Kanisa na mpenzi wa uchungaji msingi wa Utume Walei na mmoja wa waanzilishi wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo nchini.

Mwakilishi wa jamaa za marehemu kutoka Philadelphia, Richard Mchomba, alisema familia ya Marehemu Durning imepata pigo kwa kifo cha ndugu yao, lakini wamesema pigo hilo ni kubwa kwa Watanzania.

Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu nchini hapa, Padre Evaristo Shayo, alimwelezea marehemu kuwa mwanashirika wao aliyekuwa makini kuienzi kazi bora na utumishi mwema alioufanya mwisho wa maisha yake.

Askofu Dennis alizaliwa Mei 18, 1923, Philadelphia, Pennsylvania Marekani. Alipadirishwa Juni 03, 1949. Alipata Daraja ya Uaskofu Mei 28, 1963. Alisimikwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo la Arusha, Septemba 08, 1963.

Alistaafu 1988 na mwaka 1990 alikaribishwa Mbulu na Askofu Nicodemus Hando. Akafungua Parokia ya Bashay Lambo alipohudumia hadi kifo chake Februari 21, 2002 baada ya kufariki katika Hospitali ya Rufaa KCMC na kuzikwa Machi 2, 2002.

... Wanawake tumieni karama zenu mlinusuru Kanisa- Kanisa Katoliki

Na Mwandishi Wetu

KANISA Katoliki limesema endapo wanawake hawatakuwa mstari wa mbele kukemea matumizi mabaya ya karama, ipo hatari Kanisa na Taifa likashuhudia wenye mali wakijigeuza kuwa kama miungu na kutaka kuabudiwa.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Pius Rutechura, aliyasema hayo wakati akitoa mada juu ya ujumbe usemao MMEPEWA BURE; TOENI BURE, katika mafungo ya siku moja ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), yaliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Kanisa Kuu la Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Alisema ni vema kila mwana jamii akatambua ukweli kuwa, hakuna kitu wala hali yoyote aliyopewa mwanadamu na Mungu, ili amringie, kunyanyasa wala kumtesa mwenzie, bali wazitumie kuwavuta na kuwaleta watu kwa Mungu.

Alisema katika kutenda kazi ya Mungu, kila mtu azingatie kuwa amepewa bure na ni wajibu wake kutoa bure na kwamba, hakuna anayepaswa kutenda jema kisha akasubiri heshima za kibinadamu au kulipwa wema.

"Hivi sasa watu wanatumia karama walizonazo kwa manufaa yao binafsi. Hili ni tatizo kwani wengine wanajaribu hata kuzitumia karama zao na kuziabudu na hata wenyewe kutaka waabudiwe kama miungu watu. Hii ni hatari sana," alisema.

Akaongeza, "WAWATA pigeni vita karama zote zinazowafanya watu wawe miungu wadogo na wanaotaka kuabudiwa."

Alisema wana WAWATA na wanajamii wengine, watambue kuwa umefika wakati ambapo hakuna anayepaswa kutumia mbinu zilizopitwa na wakati kama vita, ili kuleta amani, bali wanawake watumie karama zao za kike za uvumilivu, upole , upendo, huruma na msamaha.

Alisema, ni hatari kukataa kutoa msamaha kwa anayekukosea kwa kuwa kufanya hivyo ni kuendelea kujitwisha mzigo wa machungu pamoja na kujiongezea uwezekano wa kutenda dhambi kubwa zaidi.

Padre Rutechura aliilaumu tabia ya baadhi ya akinamama kutaka kutumia na kuumiliki mfumo dume bila kuzingatia karama zao za kike.

"Akinamama wengine wanaamini kuwa kuchukua majukumu na madaraka yote ya mume katika familia ndio njia sahihi ya kujikomboa; hayo ni makosa makubwa kutaka kuuchukua mfumo dume na kutaka kuumiliki maana mabadiliko siyo kwamba lazima uwe sawa na mume," alisema Katibu Mkuu huyo.

Wakati huo huo: Katibu Mkuu huyo wa TEC, amewataka Wakatoliki kuepukana na tabia ya kupokea mazuri tu, lakini mabaya yanakuwa chanzo cha kuiyumbisha imani yao.

Wengine wanajenga dhana ya kupokea mazuri tu na ndiyo maana utakuta wanasali sana lakini huwezi kuamini vitu walivyojifungia (hirizi) na njia wanazotumia kutatua matatizo yao," alisema.

Askofu Mtega ataka mapadre wajiendeleze kiimani

Na Martin Amlima, Songea

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Mhashamu Nobert Mtega, amewataka mapadre wachukue tahadhari kwa kujiendeleza zaidi katika mafundisho ya imani ili kwenda sambamba na waamini wa ulimwengu wa sasa.

Mhashamu Askofu Mtega alisema hayo hivi karibuni katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Mathias Mulumba, jimboni humo wakati wa Ibada ya Kubariki Mafuta.

Alisisitiza kuwa, padre hana budi kuwa imara katika kulilinda Neno la Mungu kwa nyakati zote ili wanakondoo wasije wakatetemeshwa na mabadiliko ya ulimwengu.

Aliwaambia mapadre, mashemasi, watawa na waamini walei waliofurika katika kanisa hilo kuwa waamini wengi wa siku hizi wanadadisi masuala mengi juu ya imani si kwa lengo baya bali kwa kutaka kujua zaidi tofauti.

Alisema hali hiyo ya sasa, ni tofauti na ilivyo kuwa awali hivyo, ni wajibu wa mapadre, mashemasi, watawa na waamini walei kuwa mstari wa mbele kuwaelewesha kwa usahihi kadiri wanavyohitaji ili waende sambamba na ulimwengu wa sasa.

"Ndugu zangu mapadre na mashemasi, napenda mfahamu kuwa leo NDIYO! NDIYO! hazipo na hata zamani ndiyo zilizokuwepo ni NDIYO zenye LAKINI," alibainisha Askofu Mkuu Mtega.

Aliongeza, "Ulimwengu wa sasa umebadilika kwani waamini wengi wanataka wafahamishwe juu ya imani yao ili wadumu katika imani hiyo".

Alizidi kusema kuwa, padre ni mtume na nabii hivyo, ni lazima ajiweke mikononi mwa Mungu kwa njia ya sala ili apambane na mambo yanayotetemesha na kuyumbisha imani ya Wakristo katika ulimwengu wa sasa.

Alisema ni muhimu mapadre wakazingatia hilo kwa kuwa kutokana mabadiliko ya ulimwenguni kwa sasa, zinaibuka dini mbalimbali mithili ya uyoga ambapo nyingine hutoa mafundisho potofu.

"Jiwekeni mikononi mwa Kristo aliyepigwa mijeledi akatemewa mate, lakini yeye ndiye Kuhani Mkuu. Tumwendee yeye atufundishe namna ya kuwa makuhani wanaojiweka mikononi mwa Mungu," alisisitiza.

Pia, aliwaomba waamini walei kuwaombea mapadre wao ili waweze kutekeleza vema majukumu waliyokabidhiwa.

MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

Serikali yashauriwa kutotumia mamilioni ya pesa kuandaa mabango

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeshauriwa kutotumia mamilioni ya pesa kwaajili ya kugharamia mabango yenye ujumbe wa kujihadhari na UKIMWI na badala yake pesa hiyo wapewe wahamasishaji ambao wataweza kufikisha vijijini ujumbe wa ugonjwa huu.

Ushauri huu ulitolewa katikati ya juma na mmoja wa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI,Bi.Antonia Kilegu wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam.

Bi.Kilegu alisema kuwa hivi sasa hakuna haja ya kupoteza mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuandika mabango kwani hakuna mtu asiye fahamu kuwa UKIMWI unaua.

Alisema "Mabango ya gharama mjini hayafai,bango moja karibu linagharimu karibu mamilioni ya shilingi. Kama pesa zilizotumika kutengeneza mabango hayo wangepewa wahamasishaji ambao wangetumwa vijijini,naamini kampeni ya UKIMWI ingefanikiwa kwa kiasi kikubwa,"alisema Bi Kilegu.

Vile vile alipongeza msimamo wa viongozi wa dini wa kupinga matumizi ya kondomu ambapo alisema wao kama viongozi wa kiroho hawawezi kumwambia mtu asiue kwa bunduki huku wanamkabidhi rungu.

"Ni haki ya viongozi wa dini kusisitiza juu ya kuacha zinaa,huwezi kumwambia mtu asifanye mauji kwa kutumia bunduki huku wanamkabidhi zinaa,kuua ni kuua tu"alisema.

Wakati huo huo; Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA),Bi.Ananilea Nkya ameitaka jamii kutolipa kipaumbele suala la ngono kwa kulifananisha na chakula ambacho ukikikosa unaweza kufa kwa njaa.

Bi.Nkya alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Idara ya Habari (MAELEZO) hivi karibuni ambapo alisema kuwa baadhi ya watu wamelichukulia suala la ngono kama sehemu ya chakula.

"Ukiacha kufanya ngono huwezi kufa ila ukiacha kula utakufa" alisema Bi.Nkya.

New Life Crusade wafurahishwa kusimamishwa kwa Askofu Mgwamba

l Wataka Mchungaji Mtegile naye akae ‘mkao wa kula’

  • Waliokuwa wamehama kanisa sasa warejea tena

Na Dalphina Rubyema

KIKUNDI cha Kilokole cha New Life Crusade,kimefurahishwa na hatua ya uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ya kumsimamisha uongozi kiongozi wa kanisa hilo, Dayosisi ya Mashariki na Pwani,Askofu Jerry Mgwamba.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti,baadhi ya wanakikundi hao walisema kuwa hatua hiyo itainusuru Dayosisi hiyo ambayo walidai kuwa ilikuwa inaelekea kuteketea kutokana na uongozi mbovu wa Askofu huyo.

Walisema Askofu Mgwamba licha ya kwamba alikuwa hataki kusikia ushauri kutoka kwa watu ambao yeye binafsi hakuona umuhimu wao,vile vile alijiona ni mungu mdogo katika ulimwengu.

"Askofu Mgwamba,alijiona yeye ni mungu mdogo, akisema kitu fulani basi,ni basi kweli,hatanii"alisema Bw.Mathias Mbenna ambaye ni miongoni mwa wanakikundi hao kutoka KKKT Usharika wa Temeke.

Naye Bw.Dickson Mongi wa Usharika wa Mwananyamala alimfananisha Askofu Mgwamba kama mtu ambaye alikuwa anaongoza Dayosisi kimabavu bila kujali kama alikuwa akifanya kazi ya Mungu.

Nao baadhi ya Wananew Life Crusade kutoka Usharika wa Tabata walimtaka Mchungaji wa usharika huo, Emmanuel Mtegile kuchukua hatua za haraka kurekebisha mwenendo wake ambao walidai kuwa hauko tofauti na ule wa Askofu Mgwamba,kinyume na hapo naye ajiandae kutimliwa.

Walidai kuwa Mchungaji huyo amekuwa akiendesha usharika huo kinyume na kanuni na taratibu za KKKT,huku akikumbatiwa na Askofu Mgwamba.

Walitaja moja ya vitu ambavyo mchungaji huyo aliendesha kinyume kuwa ni pamoja na kuwasimamisha uongozi wazee wa kanisa bila sababu maalumu.

Vile vile wanakikundi hao walidai kuwa kutokana na tamko ambalo uongozi wa Dayosisi ulisambaza katika Sharika zake ,la kukitaka kikundi hicho cha New Life Crusade kiendeshe shughuli zake chini ya uongozi wa mchungaji wa usharika husika na Mchungaji mwenyewe kuendesha usharika kinyume na taratibu,baadhi yao walikuwa wameisha hamia makanisa mengine likiwemo Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG).

Hata hivyo walisema kuwa sasa kwa vile uongozi wa juu wa kanisa hilo la KKKT umeingilia kati suala hilo,wako tayari kurudi kwenye usharika wao na kuendelea kufanya kazi ya kulitangaza neno la Bwana.

Licha ya hayo wanakikundi hao walisema kuwa Askofu Mgwamba huenda ana agenda ya siri ya kulivuruga kanisa hilo na akishaona amefanikisha adhma yake,yeye yuko tayari kukimbilia nchini Marekani ambako walidai tayari ana uraia wa huko.

Oktoba mwaka jana kulitokea kutokuelewana baina ya wanakikundi hao kutoka KKKT Usharika wa Tabata na Mchungaji wa usharika huo,Emmanuel Mtegile.

Kutoelewana huko kulikuja baada ya mchungaji Mtegile kutoa tamko hilo kutoka kwa uongozi wa Dayosisi lililowataka wanakikundi hao wafanye shughuli zao chini ya mchungaji.

Hata hivyo Askofu Mgwamba katika kulizungumzia suala hili kwa vyombo mbalimbali vya habari nchini,alisema kuwa lililotamkwa limetamkwa na kama wanakikundi hao wanakataa kutii amri hiyo, basi wahame kanisa na kuunda madhehebu yao wenyewe.

Kikundi cha New Life Crusade kinawajumuisha walokole wa madhehebu mbalimbali nchini wengi wakiwemo walutheri.

Machi 21 mwaka huu kikao cha Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kilichofanyika mjini Morogoro chini ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo nchini,Askofu Samson Mushemba,kilimsimamisha kazi Askofu wa kanisa hilo,Dayosisi ya Mashariki na Pwani,Askofu Jerry Mgwamba kutokana na kile kilichodaiwa kuwa utendaji wake ulikuwa unaenda kinyume na taratibu na kanuni za kanisa hilo.

Askofu ashutumu Umoja wa mataifa kuruhusu kondomu mbovu kuingia Tanzania

Na Peter Dominic

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini, ameyashutumu mashirika ya umoja wa mataifa kwa madai kuwa yanachezea maisha ya Watanzania kwa kuruhusu kondomu mbovu kuletwa nchini.

Akijibu risala ya vijana katika Siku ya Vijana iliyofanyika Jumapili ya Matawi, katika Kituo cha Malezi ya Vijana cha Don Bosco Upanga, Da es Salaam, alisema kitendo cha mashirika hayo kuruhusu usafirishaji wa shehena ya kondomu mbovu kuja nchini, kinalenga kuangamiza maisha ya watu duniani na hasa Watanzania na siyo kuyaokoa.

Alisema, kama Umoja wa Mataifa unaweza kuruhusu vitu vibovu kusambazwa, ni hatari kwa kuwa watu wengi wataangamia.

Aliongeza kuwa, hata kama kondomu hizo zingelikuwa salama, bado mpango na msisitizo wa matumizi ya kondomu ni hatari kiroho na kimwili na ndiyo maana kanisa Katoliki linapinga vikali matumizi ya kondomu kama njia sahihi ya kupambana na UKIMWI.

Mhashamu Kilaini alisema anatambua matatizo yanayo wakabili vijana likiwemo suala la ajira na ugonjwa wa UKIMWI, lakini waepuke kujiangamiza kiroho na kimwili kwa kuupoteza utume wao kwa kutawaliwa na mambo ya ulimwengu.

"...Afadhali hata ukimkosea Mungu anaweza kukusamehe endapo utafanya toba ya kweli, lakini UKIMWI, hata ufanye vipi hausamehi kamwe," alisema.

Akaongeza, "Mumesikia juu ya kondomu; ni mbovu lakini zinaingizwa nchini, ni makontena mawili, hata kama zingekuwa zinafaa bado watu wangeangamia. Hii ni mbaya sana kwa jamii. Vijana wangu hakuna usalama bila kusema (no) wanawaletea mipira ili mtumie, mtaangamia. Kijana mzuri kama wewe kwanini ufe!" Alisema Kilaini.

Askofu Kilaini aliwafaraji vijana akisema, "Sijawakataza kuwa na urafiki, lakini linapofika suala la kujamiina sema NO, kwani nikiwakataza urafiki mtapataje wachumba."

Hivi karibuni mashirika ya umoja wa mataifa yaliingiza nchini makontena mawili yenye shehena za kondomu ambazo baada ya kufanyiwa uchunguzi ziligundulika kuwa ni mbovu.

Kanisa katoliki pamoja na asasi kadha za dini nchini zinapinga matumizi ya kondom kama kinga dhidi ya UKIMWI.

Katika risala yao, vijana hao walisema umoja wao ulioanzishwa mwaka 2000, umekuwa na mafanikio licha ya kukabiliwa na matatizo mbalimbali likiwemo la ajira, kushamiri kwa tamaduni za nchi za Magharibi pamoja na janga la UKIMWI.

Walizitaja baadhi ya athari mbaya za tamaduni wa Magharibi kuwa ni pamoja na kuwafanya vijana kushiriki vitendo vya utoaji mimba, matumizi ya dawa za kulevya na UKIMWI.

Vyama vya kitume vya vijana katika Kanisa Katoliki nchini, vinahitaji muda zaidi ili vifikie malengo yaliyokusudiwa kutokana na ushirikiano mdogo uliojitokeza katika siku ya kitaifa ya vijana juma lililopita.

Mkurugenzi na Mratibu wa Mafundisho ya Dini, jimboni Dar es Salaam, na Mlezi wa Umoja wa Walimu Wakatoliki wa Sekondari na Vyuo nchini, Padre Simon Kusunga, alielezea wasiwasi wake kuwa kulingana na mahudhurio ya vijana katika maadhimisho ya Siku ya Vijana ambayo pia ilikuwa Siku ya Matawi, alisema vijana walivyoendesha mipango yao, inaonesha kuwa ushirikiano wao haujakomaa.

"Kanisa linatakiwa kuyapa kipaumbele malezi ya vijana, bila malezi mazuri Kanisa litakosa viongozi imara," alisema na kuogeza, "Ushirikiano wa vijana haujawa mzuri, hata mahudhurio yao hayakuwa ya kuridhisha. Tulitarajia wawe wengi zaidi ya hapa." alisema.

Kauli yake haikutofautiana na Mwenyekiti wa Youth Alive wa jimbo la Dar es salaa Bi Ohana Gerad ambaye alisema, vijana walio wengi hawajaijua Jumapili ya Matawi. Akashauri juhudi zaidi zifanyike kuwaelimisha vijana waielewe.

Wakati huo huo: Baba Mtakatifu ametuma ujumbe kwa vijana na kuwaelezea kuwa vijana ni "Chumvi na Nuru ya ulimwengu."

Ametuma ujumbe huo kufuatia Siku ya Vijana iliyofanyika kitaifa, Upanga, Dar es Salaam.

Vijana katika sherehe hizo zilizoanza na ibada ya matawi pamoja na kufanya michezo mbalimbali na maigizo waliusoma ujumbe huo mbele ya Askofu Kilaini.

Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu aliwataka vijana kuisoma na kuifahamu vema Historia ya Kanisa Katoliki.

Waalikeni wajane, yatima katika sherehe - Makamba

Na Richard Timotht, RCJ,

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Luteni Yusufu Makamba, ameitaka jamii hususan wakristo wenye uwezo, kuwathamini na kuwaalika katika sherehe mbalimbali wajane na watoto yatima badala ya kukazania marafiki na matajiri pekee.

Makamba alitoa ushauri huo hivi karibuni wakati akizungumza katika Tamasha la kuadhimisha Pasaka, lililoandaliwa na Umoja wa Akina Mama wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Jimbo la Kinondoni, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Tamasha hilo lilifanyika katika kiwanja kinachotarajiwa kujengwa Kituo cha

Kulelea Watoto yatima kilichopo maeneo ya Wazo Hill na kuwajumuisha akina mama toka makanisa ya KKKT, Jimbo la Kinondoni. Lilihudhuriwa pia na watoto wanaolelewa na umoja huo wa kina mama walioimba nyimbo na kucheza ngonjera za kuhuzunisha.

Watoto hao walimuomba Luteni Makamba awe Mlezi wao ombi ambalo Makamba alilikubali na kuahidi kutoa matofali elfu moja kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Pia, alichanga shilingi 50,000/=.

Ujenzi wa kituo hicho cha kulelea watoto yatima, unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 58.5 hadi kukamilika. Fedha hizo zinatarajiwa kupatikana kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na michango, matamasha, minada na misaada ndani na nje ya nchi.

Majambazi yawapora mapadre, masista wakienda kumzika Askofu

Na Peter Dominic

WAKATI Jeshi la Polisi nchini, likijitahidi kuimarisha ulinzi katika maeneo kadhaa nchini kudhibiti uhalifu, huko Mbulu majambazi yamevamia msafara wa mapadre, watawa na walei wakati wakielekea kwenye mazishi ya Askofu Dennis V. Durning kisha wakapora gari na pesa.

Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo aliyezungumza na KIONGOZI hivi karibuni kwa sharti la kutotajwa jina, alisema majambazi hao waliokuwa na silaha, yaliuvamia msafara wa watumishi hao wa Mungu wakati wakielekea katika mazishi.

Alisema, msafara huo wa magari matatu uliokuwa umetanguliwa na gari aina ya Landcruiser TZG 8330 lililokuwa likiendeshwa na Bw. Bura, ulijikuta ukikwama ulipofika katika kona ya mwisho kabla ya kuingia Mto Magara, maeneo ya Mbuyuni kuelekea Arusha.

Alisema msafara ulikwama kutokana na kikwazo cha gogo lililowekwa kukingama barabara.

Alisema gari la mbele liliposimama, jambazi mmoja aliyekuwa pembeni mwa barabara alifyatua risasi hewani na kuwaashiria majambazi mengine kujitokeza zaidi toka vichakani.

Alisema baada ya majambazi hao kuwaamuru walale chini, dereva wa gari la pili (Land Cruiser) Bw. Josephat Habye, alisimamisha gari ghafla na kuwaarifu waombolezaji wengine.

Habari zaidi zinasema, waombolezaji hao waliteremka na kukimbilia vichakani na

majambazi hayo yalianza kuyapekuwa magari na kuchukua baadhi ya vitu vya thamani zikiwemo pesa na (Radio Call) mbili.

Alisema, kwa kuwa majambazi hayo yalikuwa na silaha iliwawia vigumu waombolezaji kukabiliana nayo kwani yalikuwa yakifyatua risasi mar kwa mara.

"Tulifikiri tungeweza kutoa msaada lakini, gari letu lilipigwa risasi katika kioo na kutufanya tuogope zaidi," alisema.

Aliongeza kuwa majambazi hayo yalitokomea na gari na vitu vingine ambavyo idadi yake haikufahamika mara moja, lakini chanzo hicho kilisema thamani halisi ya vitu na pesa inakadiriwa kuwa zaidi ya milioni mbili.

Dereva wa gari lililoibwa, alijeruhiwa shingoni na mkononi baada ya kukataa kuyapa funguo za gari majambazi hayo.

Alisema baada ya dakika kadha ilibainika kuwa majambazi hayo yalikuwa yametokome hivyo watu walikusanyika pamoja na kuamua kurudi jimboni ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Babati Mbulu. ambacho kilitoa taarifa Mkoani Arusha.

Aidha alisema, msafara huo wa mazishi uliendelea baada ya jimbo kutoa magari mengine mawili yaliyoshirikiana bega kwa bega na Polisi kwa kutoa taarifa katika maeneo ya jirani; na polisi waliweka vizuizi barabarani.

Hata hivyo ilipotimu majira ya jioni majambazi hayo yaliamua kulitelekeza gari hilo.

Askofu Denis Durning alifariki Februari 21, mwaka huu. Mazishi yalifanyika Parokia ya Ngarenaro Arusha.

KIWOHEDE yawatafutia wanawake soko la kuuzia takataka kavu

Na Meryna Chillonji

SHIRIKA moja lisilo la kiserikali linalotoaji ushauri nasaha kuhusu magonjwa ya zinaa, ukiwemo UKIMWI, uzazi wa mpango na watoto wa mitaani maarufu kwa jina KIWOHEDE, limewapatia wanawake jinni Dar es Salaam, soko la kuuzia taka ngumu

Ili liwasaidie kujikwamua kimaisha.

Afisa Miradi Msaidizi wa Miradi ya Wanawake na Mazingira, Bi. Stella Mwambeja, alizitaja kata zilizonufaika na soko hilo kuwa ni pamoja na Buguruni Kisiwani, Vingunguti, na Kiwalani zote za jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yake na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake hivi karibuni, Bi. Mwambeja, alisema lengo la KIWOHEDE kufanya hivyo ni kuwasaidia na kuwaepusha wanawake na wasichana dhidi ya hatari ya kuingia katika vishawishi vitakavyowapelekea kupata maambukizi ya UKIMWI.

Alisema kabla ya kuwapatia masoko, KIWOHEDE ilitoa semina maalumu juu ya namna ya kufanya shughuli hiyo.

Hadi sasa, wanawake 23 kati ya 360 waliokuwemo katika mradi huo ndiyo wameonesha kufanya vizuri na wamepewa mikopo ya shilingi 50,000/= kila mmoja kwa ajili ya kuendeshea miradi yao.

Alisema lengo la KIWOHEDE kuoa mikopo hiyo ni kuwapa moyo na motisha ili waongeze ufanisi katika kazi.

Alisema, walionufaika na mpango huo, watoe elimu kwa wengine ili nao wanufaike.

Shirika hilo lilofadhiliwa na shirika moja la nchini Norway lijulikanalo kwa jina la Norwaygian People Aid (NPA), tayari limekwishachimba visima viwili vya maji.

Visima hivyo vipo Kiwalani na vimekuwa msaada mkubwa katika kupambana na tatizo sugu la maji.

Pamoja na kushughulikia usafi wa mazingira wameweza kutoa ushauri nasaha kwa wasichana walio katika hatari ya kutenda vitendo viovu na kuwapa elimu ya vitendo kama vile ufundi cherehani pamoja na upishi wa vyakula mbalimbali kwa muda wa miezi mitatu ili waweze kujiajiri wenyewe.

BORA kuwasaidia walemavu mataili

l Yataka bidhaa za nchini zithaminiwe

Na Anthony Ngonyani.

WATANZANA wameshauriwa kununua bidhaa zinazozalishwa nchini ili kuinua uchumi wa nchi na kuongeza uwezekano wa kupanua ajira nchini.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Utumishi wa Kiwanda cha

Viatu cha Bora, Devid Mwasomola, wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Alisema, ili kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi, ni wajibu wa wananchi hao kununua bidhaa zinazozalishwa nchini ili pamoja na mambo mengine, hali hiyo iongeze soko la wafugaji, wakulima na wazalishaji mbalimbali nchin.

Alisema kwa kufanya hivyo, Watanzania watafanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

Alifafanua kuwa, kosa linalofanywa na baadhi ya wananchi kukimbilia bidhaa za nje ya nchi bila hata kuzingatia ubora, linadidimiza ajira nchini na kukuza ajira hiyo katika nchi za nje ambapo hawawezi kunufaika nayo.

"Ni vema wananchi wakazipenda bidhaa za hapa nchini na kuacha kukimbilia zinazotoka nje. Kwanza hawajui tu, bidhaa nyingi za Tanzania ni bora kuliko zinazoagizwa toka nje," alisema.

Aidha, Afisa Utumishi huyo wa Kiwanda cha Bora, aliishauri Serikali kusitisha uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ili kukuza viwanda vya nchini na kutoa ajira kwa vijana.

Naye, Meneja Utawala wa kiwanda hicho, Bipin Bhatia, alisema kiwanda cha Bora kina mpango wa kutoa matairi ya baiskeri 300 kwa chama cha Walemavu Wilaya ya Temeke.

Bhatia, alisema, mwaka jana kiwanda chake kilitoa matairi 300 kwa Chama hicho na kwa walemavu mbalimbali waliokwenda kuomba msaada huo kwa nyakati tofauti.

Alisema walemavu wanapopata misaada, waitumie ipasavyo badala ya kuuza.

Alisema walemavu wanaouza misaada wanahatarisha uwezkano wa kiwanda kuendelea kuwasaidia.

VIBINDO yaitaka TRA kuwaomba radhi

Na Joseph Kiboga

JUMUIYA ya Vikundi vya Wenye Viwanda na Biashara ndogo ndogo (VIBINDO society) imeutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuwaomba radhi wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kile kilichodaiwa kuwa wamesababishiwa usumbufu.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa VIBINDO,Bw.Akida Mwaimu wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni.

Kauli hiyo ya Bw.Mwaimu imekuja baada ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato nchini (TRA) kuendesha zoezi lenye lengo la kuwabana wakwepa kodi katika eneo la katikati ya jiji ambapo katika zoezi hilo VIBINDO inadai kuwa baadhi ya mali za vikundi mbalimbali ambavyo ni wanachama wa jumuiya hiyo ,ziliporwa kwa madai kuwa hazijalipiwa kodi.

Mwenyekiti alivitaja vikundi hivyo kuwa ni pamoja na Kiwaku,Kiwavi,Wanyonge na Umoja wa wauza khanga katika mitaa ya Uhuru.

Alivita baadhi ya vitu vilivyoibiwa kuwa ni pamoja na doti zaidi ya 2000 za khanga kutoka India.

Alisema ukweli ni kwamba wafanyabiashara hao hawahusiki na ulipaji kodi kutokana na ukweli kwamba wao hawaingizi mizigo kutoka nje na badala yake wananunua bidhaa zao kwa bei ya jumla kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa wa hapa hapa nchini.

"Mimi kama msemaji wa VIBINDO society,siamini kama ni kweli kwamba bidhaa hizo hazikulipiwa kodi kwa sababu bidhaa hizo kwa vyovyote vile ziliingizwa kupitia Bandari ama Viwanja vya ndege na mipakani, katika maeneo yote haya kuna maofisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato"alisema Bw.Maimu.

Alisema kama kweli bidhaa hizo hazikulipiwa kodi,basi ni dhahiri kwamba maafisa wa TRA katika maeneo hayo wamehusika kwa kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa na kutaka serikali iwawajibishe wahusika pindi itakapo bainika kwamba wameenda kinyume.

"Kitendo hicho kimewafilisi wanachama katika vikundi hivyo na kimewaacha wakiwa hawana kazi,hawana mtaji na baadhi yao huku wakiwa na madeni" alisema Bw.Maimu.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa VIBINDO alisema kuwa kitendo kama hicho kinaweza kuwasukuma wanachama hao kujiingiza katika vitendo viovu kama wizi,ukahaba na utumiaji wa mihadarati.

"TRA irejeshe bidhaa zote ilizopora kwa wanachama wetu pamoja na kutuomba radhi kwa usumbufu" alisema.

'Uzazi wa mpango mauaji tupu '

Na Lilian Timbuka

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema njia za kisasa zinazotumiwa na wanawake nchini kupanga uzazi kwa kisingizio cha ugumu wa maisha, ni mauaji tupu na hivyo, wanawake waepuke shinikizo lolote linalowataka kuzitumia.

Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati wa Ibada ya ufungumzi wa mafungo ya siku moja ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyofanyika Jumamosi iliyopita katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, jijini Dar es Salaam.

Alisema njia za kisasa za kupanga uzazi hazipaswi kufuatwa na Mkatoliki, Mkristo au mtu yeyote mwenye mapenzi mema kwa kuwa zinapingana na mapenzi ya Mungu na ni mauji mtupu ya moja kwa moja kwa watoto ambao hawajazaliwa.

"Hivyo inawapasa wanawake watambue wazi kuwa wanafanya dhambi kubwa ya mauaji. Ikiwa mama umeamua kutumia njia hizi ambazo nasikia ni nyingi ikiwa ni pamoja na kutumia vidonge, kitanzi, kondomu na vijiti, mnaamini vipi kuwa hamharibu mimba?" alihoji.

Alisema Mungu anao mpango wake maalumu hata kutoa uhai na kuruhusu kuzaliana na kwamba ndiyo sababu alimuumba mtu mke na mume ili wazae watoto watakaowasaidia wao na jamii nyingine hapo baadaye.

Akahoji, "IIkiwa Mungu aliwapa thawabu ya uzazi bure, kwanini na ninyi msiitoe bure kwa waume zenu ili mzidi kuongezewa?"

Alisema ingawa hali ya uchumi ni ngumu, inayowabidi Watanzania kupanga idadi ya watoto katika familia ili kuwahudumia ipasavyo, hiyo haipaswi kuwa sababu ya kisingizio cha kutumia njia za mauaji ili kupanga uzazi.

"Kama mwanamke anajiamini kuwa yeye ni Mkristo na Mkatoliki safi, kwa nini ashindwe njia za asili ili kupanga uzazi ambazo ni nzuri na zimekuwa zikitumika hata toka enzi za mababu zetu?" Alihoji.

Aliwaasa akina mama hao kuwa waangalifu na maamuzi ambayo yanaendelea kutolewa siku hadi siku na wanasayansi wa mabara mengine kuhusu njia muafaka za kupanga uzazi zinazohimiza matumizi ya dawa na mipira.

Alisema umefika wakati sasa kwa wakristo kumpigania Mungu katika maamuzi wanayofanya siku hadi siku na hata ikibidi, wafe kwa ajili ya Mungu.

"Akinamama hamna budi kukataa kushinikizwa kutumia njia hizo za mauaji eti kama njia ya kupambana na hali mbaya ya uchumi. Epukeni mauaji hayo ambayo adhabu yake mtakuja kuipata huko mbele ya Mwenyezi aliyewaweka hapa duniani kwa nia ya kuzaliana. Ikibidi kuzaa uzae, lakini ikishindikana kabisa kulea, tumia njia za asili za kupanga uzazi ambazo hata Kanisa linakubaliana nazo," alisema Kardinali Pengo.

Mwadhama Pengo aliwaomba WAWATA pia kutumia mafungo yao kuliombea Kanisa Katoliki na wachungaji wake ili wafanye vema na kwa ufanisi kazi ya Mungu.