Mchimba Kisima Huingia Mwenyewe (2)
Mpenzi msomaji wiki iliyopita tuliona jinsi Dickson na mwenzake Kizito walivyomwelezea mganga shida yao na mganga naye anawatengenezea, je watafanikiwa kumuua James, ungana naye Erasto Duwe katika sehemu hii ya Mwisho.
Akachukua manyoya ya aina mbalimbali yakiwamo ya mbuni yaliyoshonewa juu ya kofia ya ngozi ya kenge.
Akaivaa kichwani. Akakichukua kibuyu kiliochokuwa pembeni ndani ya kibuyu kikiwa na chura mkubwa aliyesikika mara kwa mara akikoroma, "Kroooh!, Krooo!"
Akakiweka kichwani halafu akakisogeza puani na kukinusa. Kisha akajitanda kwa nguo nyeupe akajifukiza kwa ubani huku akiimba nyimbo kadhaa za kikabila.
Akisha kuimba kana kwamba anaita au kuwasiliana na mizimu ya kwao, akasema, "Hapa mmefika. Tatizo lenu ni kubwa sana lakini, kwangu ni dogo sana mkifuata masharti yangu."
"Kesho, kiumbe mnayemtaka nimtoe roho hatakuwepo duniani."
Akawasisitiza kuzingatia kuwa jambo ni la siri mno na hivyo, waitunze siri, ikae sirini na wala isivuje hata kwa tone maana ina ubaya na hatari zake kubwa na nyingi.
Akawafungia dawa ya unga na mizizi na kuwapa maelekezo ya namna ya kuitumia. Eti wakaimwage dawa mlangoni katika ofisi ya James na nyingine, waichimbie.
Akawahimiza ile mizizi ya mizizi, nayo waichimbie katika sehemu ambazo James anapendelea kupita anapokagua kazi ili airuke na kuikanyaga maana hapo, itakuwa inafanya kazi vizuri.
Kisha akasema, "Kuutoa uhai wa mtu, shio mchesho. Hasha mtu mkubwa kama yeye anayetambuliwa na watu wengi. Maana inawezekana na yeye alisha jiweka shawashawa."
"Kwa shasha mtaacha sh.100,000 (laki moja) kwa ajili ya kuendea porini ili "wazee" wafurahi na kufanya kazi. Hii ndiyo pamoja na kummaliza na shilingi 100,000 nyingine, kwa ajili ya ninyi kupata hiyo nafasi."
Akaongeza, "Hata hivyo, nimewapungushieni shana shasha. Nipeni halafu muendeni shenu mukashubiriye matokeo".
Vijana hao hawakuwa na hiyana, wakatoa na kumpa. Wakaahidi pia kumzawadia zaidi iwapo mambo yangetimia.
Walipofika kwenye kampuni yao, hawakuchelewa kufanya waliyotakiwa kufanya. Wakamwaga madawa mlangoni na mengine kuchimbia ardhini na kufukia kwa lengo la kuutoa uhai wa James.
Kisha wakatega masikio kujua kulikoni sasa juu ya uhai wa James. Siku waliyoitarajia, ikapita bila ya James kufikwa lolote, walijipa moyo wakazidi kutazamia.
Muda ukazidi na siku zikapita na kupita bila dalili yoyote ya James kudhurika.
Ni katika juma lilelile baada ya uchunguzi kukamilika kuonekana kuwa Nickson na Kizito ni wasaliti wa James ambaye ni Meneja Mkuu, na wahujumu wa kampuni wa jumla.
Kikaitishwa kikao kilichojadili kwa kina juu ya jambo hilo na kuwatahadharisha vijana hao wajihadhari kwani tabia yao ni mbaya kupindukia. Walisemwa waziwazi na kuelezwa ukweli juu ya njama zao mbele ya wafanyakazi wote wa kampuni. Ilikuwa ni aibu iliyoje iliyowagubika.
Jambo hilo la kuelezwa ukweli liliwauma sana. Baada ya kikao walikutana wakapanga kurudi tena kwa Mgongomhawi kwani waliona mambo yanazidi kuchelewa na siri zao zinazidi kufichuka.
Haukupita muda, wakakodi gari dogo aina ya TOYOTA MARK ll, wakaanza safari ya kueleka tena Tunguli wikiendi iliyofuata baada ya kikao kile.
Walisafiri vizuri wakiwa watatu ndani ya gari lile dogo. Walipofika sehemu iliyofahamika kama Mto wa Mbu kilometa mbili na nusu kabla ya kufika kijijini kwa Mgongomhawi.
Ghafla, tairi la gari likachomoka mara na gari lile kikaanza kuyumba na hatimaye kuviringika kuelekea gemani lilipotua kwa kishindo cha "Puu" na kutulia likiwa limepondeka na kuathirika vibaya sana.
Watu waliopita karibu, walistaajabu kuona alama za matairi ya gari zilizoonesha kuserereka bila uangalizi wala uthibiti bora kuelekea gemani.
Wakaamua kufuatilia waone kulikoni huko gemani ambako kwa umbali kidogo waliona kitu waliona kitu mithili ya gari lililobinuka na kulala chali.
Wakaingia gemani na kushuhudia kwa macho yao halisi, maiti mbili zilizokuwa zimelala kando ya lile gari lililobondeka na hali wale maiti wakiwa wameharibika vibaya.
Dereva ambaye alikuwa amebanwa na usukani ndani ya gari lile kifuani, yeye alikuwa amekwisha kata roho na kubaki akionekana mithili ya dereva anayejipumzisha huku akimsubiri bosi wake.
Wapita njia wale walisambaza taarifa za ajali ile na watu walipokuja kushuhudia tukio, wakagundua kuwa, maiti wale wengine, walikuwa Nickson na Kizito.
Mungu si athumani Fitina na hila zao Nick na Kizito ziliishia gemani James aliendelea kustawi na mambo yakamnyokea barabara hata baadae akapandishwa tena cheo.
Dunia haina siri ni kwanini wamepata ajali na walikuwa wanakwenda wapi na kufanya nini, yote hayo tayari yalikwisha jibika vichwani mwa watu na ndipo kila mmoja kwa wakati wake alikuwa akisikika akijisemea, "MCHIMBA KISIMA, HUINGIA MWENYEWE".
Sikutarajia Yawe Haya (1)
Na Emmanuel Boniface
N
AFSA naye alijua dhahiri kuwa ni urembo pamoja na unadhifu wake ndio uliopelekea vijana wengi mtaani pale, wamtamani na kumpapatikia namna ile tangu ahamie mtaa ule wa Suna pale Magomeni-Mapipa kutoka nyumbani kwao Tanga.Nadhani kile kioo chake kikubwa cha ukutani, ndicho alichotumia na kumfanya ajishuhudie urefu wake wa kadiri uliomfanya aonekane kama chombo kilichotengenezwa kutokana na madini na vito vya thamani na kutiwa nakshi na mafundi wa kimataifa.
Nafsa; chombo cha watu chenye rangi ya maji ya machungwa uso wake umeyabeba macho yake meupe na tena laini yenye dalili za usingizi, mdomo wake ulioyakusanya meno yake meupe mithili ya punje za mahindi machanga; hata yeye alikiri kuwa ile ngozi yake nyororo mithili ya manyoya ya njiwa, pamoja na vile vilemba alivyopenda kujitanda, vilizidisha uzuri wake hasa pale anapotembea na kuonekana kama nguva awapo ndani ya bahari.
Vyote hivyo vilizidisha uzuri wake na kufanya azidi "kunata" na kuwazingua vijana wengi.
Hata hivyo, kama wanawake wengi wasivyojiamini, Nafsa hakuridhika na uzuri wake. Alizidi "kujipiga deki" kwa mikorogo ya aina aina na kujipamba kwa vikorombwezo visivyo na idadi.
Pia, Nafsa alitumia marashi ambayo hata sikupata kuyasikia harufu yake tangu kuzaliwa kwangu. Ndiyo hayo yaliyozidi kuwamaliza vijana wengi na kuwaacha wakiteseka kwa matamanio ya huba mioyoni mwao.
Yeye alizidi kuongeza mikogo, minenguo na madaha ili kuwakomoa. Wakome; wakomae.
Bahati, nilikuwa ni miongoni mwa hao vijana lukuki walioteswa na binti huyo mara tu, baada ya kutoka kijijini kwetu Nyambiri wilayani Kasulu huko Kigoma huku tukikosa ujasiri wa kumwaga sera zetu za mtoni.
Basi, tukazidi kuchomwa na mishale ya maumivu ya uchu wa mapenzi mioyoni mwetu.
XXXXXXXX
Ninatoka Mbagala, hatua chache toka ilipokuwa daladala ile. Ninamuona mwanadada aliyekuwa amevalia viatu vya mtindo wa Yondo na mavazi yale wanayovaa wale wanawake wa ki-Pemba na Kiarabu; sijui yanaitwaje.
Alikuwa akipekuapekua kile kitabu alichokuwa nacho kama mtu aliyetunzia humo hundi yake ya kuchukulia pesa benki.
Mwanadada huyo ambaye sikuchelewa kumtambua kuwa ni Nafsa aliyekuwa tamanio la kila mwanaume pale mtaani, aliyenifanya nichukie hata chakula, nikalala njaa huku ndoto zangu zote zikiwa juu yake, alionesha uso uliobainisha kuwa, alikuwa kapoteza kitu.
Huku nimemtumbulia macho ya huba na ulimbukeni, nikamwona kwa huzuni na taratibu akivuta hatua toka kituo kile cha daladala cha Mbagala- Kariakoo. Mara nikaona kitu kama bahasha ikidondoka toka kitabuni pasipo yeye kushtuka.
Nilipatwa na mshawasha wa kutaka kujua ni kitu gani, basi nikaisogelea na kuiokota bahasha ile.
Nikaangaza macho huku na kule kwa tahadhari ili kuona kama kuna mtu aliyeniona.
Nikaridhika kuwa hakuna aliyeniona. Naye Nafsa alikuwa anatokomea mtaa maarufu wa Kongo hapo Kariakoo. Nikaifungua ile bahasha huku kiroho kikinidunda kidogo.
"Yarabi nipe salama," nikajisemea mara nilipoiona ile noti ya shilingi elfu kumi ikiwa na picha moja ndogo (passport size).
Picha ile ilizidi kunidhihirishia ulimbwende wa Nafsa, inaufanya moyo wangu kubaki njia panda huku wazo moja likinishawishi nimkimbizie dada yule pesa zake. Nalo wazo la pili linapingana na lile la kwanza.
"Sheria duniani, haki mbinguni, Mungu akupe nini" nikajiwazia huku nikiwazia noti ile mfukoni na kuishikilia ile bahasha ikiwa na picha tu.
Basi, nikakata shauri kupitapita kwenye mitumba ili walau na mimi nipate mtumba mmoja mzuri utakalolipumzisha hilo shati langu chakavu linalotumika kama kitambulisho cha ufukara wangu, ambalo watu huliita,"kauka nikuvae" au "chanika nikushone".
Haya mpenzi msomaji mambo ndio hayo je ni nini kitatokea usikose toleo lijalo