'Wanaosema wameponywa wakatupa magongo ni waongo'
l
Yadaiwa wengine husafiri na wahubiri toka nchi nyingineNa Elizabeth Steven
KIONGOZI mmoja wa Kanisa, amewatahadharisha waamini wa Kikristo kutoiga mkumbo kwani viongozi wengine wa makanisa husafiri na watu ili "kucheza maigizo" madhabahuni wakidai wameponywa na kutupa magongo yao lakini, baadaye walioponywa huwa hawaonekani.
Pia, ameitahadharisha jamii kuwa makini na kujiepusha na watu wanao anzisha kiholela makanisa mithili ya utitiri baada ya kushindwa kusuluhisha migogoro ndani ya makanisa yao ya asili.
Tahadhari hizo zimetolewa na Padre Ireneus Mbahulila wa Kanisa Katoliki, parokia ya Makuburi katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam, alipokuwa akizungumza katika ibada iliyofanyika katika kanisa hilo la Mwenyeheri Anuarite, siku moja kabla ya Sikukuu ya Krismasi.
Alisema kumezuka mtindo wa watu kutokuelewana katika makanisa yao, wakaamua kuanzisha makanisa kila mtu lake na hata kuwashawishi kwa njia mbalimbali watu wajiunge nao bila kujua undani wao kwa kuwa wengi wanaiga mkumbo wa wale wanaoandamana na wahubiri hao ili kusaidia kuhamasisha.
"Hawa wanaotupa magongo wakidai wameponywa, ni waongo wanaotoka nchi nyingine halafu wanakuja kudanganya eti wameponywa. Hebu watafute hapa dar-Es-salaam kama utampata, hawapo kabisa, sasa jiulize wakishaponywa huwa wanakwenda wapi," alihoji.
Kauli ya padre huyo Mkatoliki, imefuatia taarifa zilizoandikwa katika gazeti moja la kidini litolewalo mara moja kwa juma kuwa mmoja wa wachungaji waliojiengua toka kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Ayubu Mwakatobe, ambaye alikuwa mshauri wa Kiongozi Mkuu wa kanisa hilo, Zacharia Kakobe, tayari ameanzisha kanisa lake mwenyewe eneo la mwenge Kijijini.
Aidha, katika ibada hiyo, Padre Mbahulila, aliwaasa waamini wenye tabia ya kutumia sikukuu kumuweka mungu kando waachane na tabia hiyo kwa kuwa ni kinyume na Ukristo halisi.
Alisema jamii nyingi katika siku za sikukuu, huelekeza juhudi zao katika kuhangaika kununua nguo, viatu vipya na vitu vya dhahabu lakini, wanasahau umuhimu wa sadaka.
Bado vyama vinatia hofu- Kardinali
Na Dalphina Rubyema
WATANZANIA wametakiwa kuelewa kuwa bado taifa halijapona kabisa katika hofu ya kuvunjika kwa amani kama ilivyohofiwa hapo awali, kabla ya Uchaguzi Mkuu, kwani baadhi ya vyama vya siasa bado vinaonesha kutoridhika na matokeo kwa kutumia lugha ya kutishia amani na hivyo wawe makini.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, wakati wa Misa ya Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jimboni humo.
Alisema vyama hivyo vinavyoonesha kutoridhishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba -Novemba mwaka 2000, vinaashiria uvunjaji wa amani.
"Tanzania tulihofia Uchaguzi Mkuu, tulihofia zaidi pale uchaguzi huo ulipo karibia na zaidi, ni pale udini ulipoonekana kushamili. Bado hatujapona kabisa katika wasiwasi huu kwani, wanasiasa wengine bado wanaonesha wasiwasi wa kutoridhika na matokeo na wanatumia lugha za kutishia amani", alisema Kardinali Pengo.
Askofu Mkuu huyo pia aliitaka jamii ijipongeze na kumshukuru Mungu kwa kufikia kilele cha Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 na kuumaliza vema mwaka kwa kuwa ni tangu awali, ujio wa mwaka huu, ulijawa na maswali mbalimbali yakiwamo ya hofu.
"Kiulimwengu watu walihofia kuzimika kwa kompyuta na wengine kuhofia kwamba utakuwa mwisho wa dunia. Hofu hiyo ilizaa mauaji makubwa kama yale ya Kanungu nchini Uganda," alisema.
Alisema Tanzania ina kila sababu ya kujivunia kufanya adhimisho la Krismasi kwa utulivu na amani kwani baadhi ya nchi, zinatamani zifanye adhimisho hilo ingawa zinashindwa kufuatia vita na machafuko.
"Nchi kama Angola, Kongo, Msumbiji na nchi nyingine za Maziwa Makuu zinatamani zifanye adhimisho hili lakini, zinashindwa kufuatia hali ya vita ambayo bado inaendelea hadi hivi sasa. Hii inasababisha kuvurugika kwa amani na uchumi kushuka katika nchi hizo," alisema.
Aliwashukuru waamini wa Kanisa Katoliki jimboni humo kwa kutoa michango yake ya hali na mali hali iliyosababisha Jimbo hilo sasa kuanza kujitegemea badala ya kutegemea Mfuko wa Baba Mtakatifu.
Alisema kwa mwaka 2000, Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam lilikadiria kukusanya milioni 60 za mavuno na hadi kufika siku hiyo ya mkesha wa Krismas, jumla ya shilingi milioni 53 zilikuwa tayari zimekwisha kusanywa.
"Natoa shukrani zangu binafsi na kwa niaba ya Baba Mtakatifu kwa wanajimbo wote. Shukrani za pekee pia ziwafikie wanaparokia wa Mtakatifu Yosefu, Mwenge, Chuo Kikuu na parokia ya Kibiti ambazo ni miongoni mwa parokia zilizodhihirisha jitihada za pekee katika kutoa mavuno hayo," alisema.
Wachungaji ombaomba kwa Maaskofu marufuku Kanisani kwa Kakobe
l
Waambiwa uzeni saa na nguo mlipe madenil
'Kwanini mkope nyie walipe wengine?’l
Wachungaji walioandika barua za mapenzi nao matataniNa Mwandishi Wetu
KIONGOZI Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe, amepiga marufuku mchungaji wa kanisa lake kuomba msaada toka kwa maaskofu na amewataka wote wenye madeni, wauze saa na vitu walivyo navyo zikiwamo nguo ili walipe kwa kuwa walikopa wenyewe.
Pia, wachungaji waliowaandikia barua za mapenzi wasichana watendakazi wa makao makuu au mahali pengine kwa madai ya kuwa wachumba wao, wametakiwa kujisalimisha kwa kuandika barua ya kujieleza kabla hatua hazijachukuliwa dhidi yao.
Kwa mujibu wa barua ya kanisa hilo la F.G.B.F, iliyosainiwa na kakobe mwenyewe yenye Kumb. Na. FGBF/MISSIONS/CIRCULAR/00/3, ya januari 30, mwaka 2000 iliyochapishwa katika toleo la mwisho la gazeti moja la Kiswahili litolewalo kwa juma, wachungaji waliokopa wametakiwa kulipa wenyewe madeni yao.
"Kumezuka wimbi la wachungaji ombaomba wanaoandika barua kwa Askofu Mkuu, maaskofu wa majimbo na waangalizi wa wilaya na kwa wachungaji wengine wa makanisa mengine yasiyo ya F.G.B.F, na wengine kwa washiriki wa jimboni, wilayani, makao makuu n.k wakiomba mabati, sementi, fedha n.k,. Ombaomba hawa pia, hawatavumiliwa...nimesema wakati wote mimi sijaomba kitu chochote kwa mtu yeyote tangu kanisa hili lianze," inasema sehemu ya barua hiyo na kuongeza, "...watu wanaoishi kwa kukopakopa na kuzungukwa na madeni kila upande hawatavumiliwa! Kukopa kunaharibu ushuhuda wa watumishi wa Mungu kama uasherati na uzinzi... Wengine wana madeni, lakini, wanavaa saa na nguo nzuri na wanataka eti maaskofu wa majimbo wawalipie madeni! Uzeni saa hizo na nguo zenu mlipe madeni enyi msio haki... Iweje wewe ndiye uliyekopa halafu unataka mwingine ndiye akulipie deni?"
barua hiyo imewataka wachungaji waliowahi kuandika barua kwa wasichana kwa sababu yoyote, wawasilishe haraka barua za kujieleza kwanini wasitimuliwe katika kazi ya uchungji kanisani humo.
"wachungaji wanaoandikiana barua za mapenzi na wasichana watendakazi wa makao makuu au popote pengine kwa kisingizio kwamba wanataka baadaye wawe wachumba wao, hawatavumiliwa. Huu ni uasherati...Nimeletewa barua nyingi na wasichana walioandikiwa barua hizi na ninazo.
Kwa waraka huu, kabla sijachukua hatua kwa wote walioandika barua kwa wasichana kwa sababu yoyote ile, walete kwangu haraka barua za kujieleza kwanini wasitimuliwe, wakikaa kimya wakifikiri sijui, nitawatimua mara moja bila maulizo yoyote...wakati wa kubembelezana umekwisha...Yeyote anayeona utumishi umemshinda, au alikuja kutafuta kazi baada ya kushindwa maisha, alikosea, utumishi ni kwa wale wenye wito tu."
Juhudi za kumtafuta askofu Mkuu huyo wa F.G.B.F ili azungumzie barua hiyo hususan wachungaji waliojisalimisha kwa kipindi hiki cha takriban mwaka mzima sasa, hazikufanikiwa kwa kuwa gazeti hili lilipofika kanisani kwake, liliambiwa na mmoja wa watumishi kuwa hayupo na juhudi za kumtafuta kwa njia ya simu hazikufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni kwa kuwa kila alipotafutwa simu yake ilikutwa imefungwa.
Wamoravian wa Temeke wamuonyesha 'jeuri' Mlutheri mwenye kansa
Na. Mwandishi Wetu
WAAMINI wa Kanisa la Moravian Tanzania, Ushirika wa Temeke, katika Jimbo la Kusini, wilaya ya Mashariki, wameonesha jeuri ya upendo baada ya kumsaidia Mlutheri mmoja shilingi 100,010/=, wakati yeye alikwenda kanisani kwao kuomba 30,000/=.
Kwa mujibu wa Mchungaji wa kanisa hilo, Tuntufye Mkumbwa, tukio hilo lilitokea katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani hapo, baada ya Mlutheri huyo Zacharia Thobius, kufika hapo akiwa na shida ya shilingi 30,000/=, alizokuwa akitafuta ili kuongezea kiasi alichokuwa nacho kwa ajili ya matibabu ya kidonda.
Kwa kadiri ya mazungumzo na mchungaji huyo, Bw. Thobius mwenye umri kati ya miaka 25 na 30, alipata matatizo ya kidonda hicho kinachoaminika kuwa kansa, baada ya kujikwaa kidole yapata miaka miwili iliyopita akiwa matembezini katika jiji la Dar-Es-Salaam.
Katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi jijini katikati ya juma lililopita, Mchungaji Mkumbwa, alisema baada ya kujikwaa, Bw. Thobius mwenyewe alieleza kuwa, aliamua kuweka mbolea ya chumvi chumvi katika jeraha lake kama njia rahisi ya kulitibu.
"Anasema alipoweka hiyo mbolea sasa sijui kumbe alikuwa na matatizo ya kansa, kila siku anaona kidonda kinakauka, kumbe ni kwa juu tu, ndani kinazidi kuoza kabisa na kuzidi kupanda kuja juu ya mguu," alisema Mchungaji.
Alisema kufuatia hali hiyo, watu walimshauri akatibiwe Nairobi nchini Kenya ambako kila walipokata sehemu iliyoathirika, ilizidi kupanda tena, baada ya kujaribu matibabu katika hospitali kadha hapa nchini kwa msaada wa watu mbalimbali nahali kuzidi kuwa mbaya.
"Hivi sasa kimebaki hiki chenyewe(anaonesha sehemu ya kisigino) na kuja huku juu pameoza kweli," alisema bila kutaja ni mkazi na muumini wa usharika gani wa kanisa hilo la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) hapa jijini.
"Sasa alipoeleza mbele ya kanisa matatizo yake na hata kufungua suruali, watu walipoona tu, wakamwambia acha! Rudisha kabisa! Funika. Hapo hapo wakaanza kutoa pesa za kumsaidia bila kujali alitaka ngapi."
"Yeye mwenyewe alisema alikuwa amekwisha pitapita sehemu mbalimbali akiomba msaada ili arudi kwao Zambia. Sasa, alikuwa amepungukiwa 30,000/= lakini watu walivyotoa, hapohapo akapata 100,010/= badala ya zile alizotaka. Akaondoka kwenda kutafuta pasipoti."
"Yani ule mguu wake namna ulivyoathirika, akikuonesha tu, uko radhi kama hauna huruma, umpe pesa ulizo nazo lakini aondoke asikae kwako. Hata sijui ni msamaria gani anayekaa nae," alisema Mchungaji Mkumbwa.
Aliwapongeza waamini wake na kuwataka Wakristo wote kuwa na moyo wa kuwasadia wenye shida bila kujali tofauti za kikabilia, kisiasa wala kimadhehebu.
KKKT wataka jamii izaliwe tena
Na Leocardia Moswery
MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT), usharika wa Mtoni katika dayosisi ya Mashariki na Pwani, ameitaka jamii kuzaliwa upya na hivyo, kuachana na matendo yote yanayojenga ukuta wa mahusiano na mungu.
Mchungaji huyo Samweli Chuma, aliyasema hayo wakati akihubiri katika ibada ya mchana katika sikukuu ya Krismasi, iliyofanyika usharikani hapo.
Alisema njia pekee ya kuzaliwa upya na kwa usahihi, ni kuishi ndani ya Yesu kwa kubadili matendo toka yale maovu, kuelekea yanayompendeza Mungu.
Aliionya jamii kuepukana na vitendo vya rushwa, chuki, fitina, wivu na uasherati ambavyo vimeshamiri ndani ya jamii.
Alisema katika wakati jamii inamaliza mwaka wa 2000, jamii haina budi kutafakari na kuchuja matendo yao ili kuyaendeleza yaliyo mema huku wakijua wanaingia katika mwaka mpya unahitaji amani, upendo na kumujua Mungu zaidi.
Wakati huo huo: Katibu Mtendaji wa Idara ya Habari wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Raphael Kilumanga, amewahimiza Wakatoliki kujenga tabia ya kuondokana na uvivu wa kusoma Maandiko Matakatifu(Biblia).
Padre Kilumanga alikuwa akizungumza wakati wa ibada ya mkesha wa Krismasi, iliyofanyika katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.
Jamii yatakiwa kuwaheshimu akinamama
Na Festus Mangwangi, Arusha
JAMII imeelezwa kuwa haina budi kuheshimu na kuipa kipaumbele nafasi ya wakinamama katika malezi ili kuzinusuru familia nyingi nchini kutoka katika wimbi la kusambaratisha maendeleo ya mwanadamu kiroho na kimwili.
Hayo yamesemwa na Paroko wa Parokia ya Ngaramtoni, Padre Pastory Kijuu, wakati wa semina ya siku nne ya Wakinamama Wakatoliki iliyofanyika parokiani hapo kwa malengo ya kuwaandaa wakinamama kuziwezesha familia zao kusherehekea vema sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.
Padre Kijuu alisema kuwa, jukumu alilonalo kila mama katika familia juu ya malezi ya jamii, ni kubwa na muhimu na hivyo, si vema wala busara kutowasikiliza kwani hata Mwenyezi Mungu kwa namna ya pekee, amemthamini mwanamke na ndiyo maana alimshirikisha kwa namna ya pikee katika kuendeleza kazi ya uumbaji.
"Wakati tunapoihamasisha jamii iwaheshimu na kuwatambua, mnapaswa pia wenyewe mfahamu nafasi na wajibu wenu. Kila familia iweze kuzaliwa upya na Mtoto Yesu na kuishi naye kadiri ya mapenzi ya Mungu na uongozi wa Roho Mtakatifu," alisema Padre Kijuu.
Mmoja wa watoa mada kutoka kikundi cha uamsho wa Imani cha parokia ya Mtakatifu Joseph katika Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, Bi, Verediana Chisunga, aliwataka wakinamama kujenga tabia ya kujiamini na kuondoa hofu ambayo mara nyingi inawafanya washindwe kutekeleza kikamilifu wajibu wao katika nafasi mbalimbali ijapokuwa uwezo wa kufanya hivyo wanao.
Naye Bi. Cecilia Kashanga, wa kikundi hicho hicho, amefafanua kuwa kama mama wa familia asipokuwa mstari wa mbele katika kudhihirisha uwepo na upendo wa Mungu, kwa maneno na matendo, basi uwezekano wa wanafamilia kutokuwa na mawasiliano mazuri ni mkubwa na hali hiyo huweza kuleta athari siyo tu kwa familia husika, bali pia taifa kwa jumla.
Aidha, Padre Kijuu alisema kuwa semina hiyo ililenga pia kuwahamasisha wakinamama waweze kutambua jukumu lao la kuwa vyombo bora mikononi mwa Mungu katika kupambana na maovu mbalimbali ili kila mwanajamii aweze kuona sura na upendo wa Mungu kwa mwingine.
KATIKA KUSHEREHEKEA KUZALIWA YESU KRISTO
Watoto 30 'wazaliwa' mtoni - Dar
Na Frank Mtwanzi
WAAMINI wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Bakhita Parokia ya Mtoni iliyopo wilaya ya Temeke, jijini Dar-Es-Salaam, Siku ya Pili ya Sikukuu ya Krismasi walisherehekea kuzaliwa kwa mara ya pili kwa watoto wao yaani ubatizo, katika misa iliyoongozwa na paroko wa Parokia hiyo Padre John Wardrop.
Kwa mujibu wa Mkatekista wa Parokia hiyo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwalimu Stanslaus Machege, mwezi huu parokia hiyo imebatiza watoto wengi wenye umri kati ya miezi 6 hadi miaka 5.
"Idadi hii ni kubwa kabisa ukilinganisha na idadi za watoto waliowahi kubatizwa katika kipindi cha nyuma, yaani toka kanisa liwe parokia inayojitegemea," alieleza mwalimu huyo.
Aliongeza kusema, "Kuanzia mwaka 2001 na kuendelea, tunatarajia kubatiza watoto wengi zaidi tofauti na idadi ya mwaka 1999-2000."
Awali katika mahubiri yake, Padre John aliwahimiza wazazi wa watoto waliobatizwa kuishi vema na kuwalea watoto wao katika tumaini la ubatizo.
Aliwaasa wazazi wengi kutowachelewesha watoto wao kupata sakramenti hiyo ya Ubatizo kwa kuwa ni muhimu katika maisha ya mwandamu hasa Mkatoliki.
Sherehe hizo pia ziliunganishwa na tamasha la vijana wa parokia hiyo.
Wazazi wawajibike kulea watoto - kauli
Na Leocardia Moswery
MKURUGENZI wa Masoko wa Kampuni ya Kompyuta Limited Tanzania (CATS) Bi. Scholastica Ponera, amewataka wazazi kote nchini kuwajibika kulea watoto hao badala ya kuwazaa na kutupa majalalani.
Bi. Ponera alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea kituo cha watoto wenye shida kilichopo Kurasini jijini Dar-Es-Salaam.
Ziara ya Mkurugenzi huyo iliambatana na kazi ya Matendo ya Huruma, iliyofanywa na Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Desemba 26 mwaka huu.
"Wazazi wanapaswa kuwajibika kulea watoto wao na hii ni kwa wote wenye ndoa na wanaoishi uchumba wa muda mrefu, siyo kuzaa tu na, kutupia serikali wakidhani watalelewa," alisema na kuongeza kuwa,
"Watoto kama hawa 75 wa kituo hiki wakiwa rika mbalimbali na wazazi wote hawana budi kuwalea. Ni jukumu la kila mtu."
Aliongeza kuwa, kumsaidia mtoto asiye wako, ni kulisaidia Taifa na kuleta maendeleo na pia kuondokana na watoto wa mitaani," alisema.
Mkurugenzi huyo pia amewataka wasichana kutofanya mapenzi kabla ya ndoa na pia wenye ndoa, wawe waaminifu ili kuepukana na tatizo la watoto yatima na wa mitaani.
Shirika hilo la Kipapa la Utoto Mtakatifu, lilishiriki kwa Matendo ya Huruma yaliyofanywa na watoto wa parokia ya Kurasini, Mbagala na Chang’ombe zote za Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.
Parokia tatu zilitoa msaada wa vyakula mbalimbali kama juisi dazeni 16, kilo 50 za sembe, sukari kilo 50, mchele 80 kilo, sabuni miche 46, mafuta lita 30, kanda mbili dazeni 18, sambusa 150, pamoja na nguo boksi moja.
Matendo ya huruma yalifanywa na Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam kwa kila parokia tatu kutembelea watoto wasiojiweza na kuwasaidia.
...Msiwageuze watoto kuwa watumwa
Na. Mwandishi Wetu
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka wazazi na jamii kutowatumikisha kama watumwa, watoto wanaookotwa baada ya kutupwa.
Akiongoza Ibada ya Jubilei ya Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Msimbazi jijini hivi karibuni, Mwadhama Pengo, alisema ni wajibu wa jamii kuwatunza kwa mapenzi mema, watoto yatima na wanaookotwa.
"Tukiweza kuwalilia wazazi wanao talekeza watoto wakaondokana na dhana potofu ya kinyama, basi tunaweza kupunguza makali ya watoto wa mitaani na shida za utumwa wanazofanyiwa wanao okotwa," alisema.Akifafanua kauli yake, Pengo alisema, hapa Tanzania wapo watoto wanakosa wazazi kwa kutupwa, lakini, wanaowaokota, huwatumikisha kama watumwa badala ya kuwafanya kama sehemu ya familia yao halisi.
"Watoto wengine wanalazimishwa kuolewa, wengine hufanywa watumwa wa kuwalinda adui na hata wanapokuwa wakubwa huuzwa kama watumwa," alisema Mwadhama.
Kardinali Pengo amewataka wazazi kuchangia shirika hilo ili lisaidie watoto wengine wenye shida zaidi ya hao ulimwenguni kote.
"Nyie watoto muwaombe wazazi wenu wawasaidie kuchangia mfuko huu ili tupeleke kilicho kidogo kwa Baba Mtakatifu, Mwanzilishi wa shirika hili, ili aweze kuwasaidia watoto wengine wenye shida zaidi ulimwenguni," alisema.
TEC yatangaza Kamati ya Nidhamu na Uajiri
Na. Waandishi Wetu
BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC), limetangaza Kamati ya Nidhamu na Uajiri ambayo itakuwa chini ya Mwenyekiti, Padre Elias Msemwa.
Akitangaza kamati hiyo katika kikao cha wafanyakazi wa TEC kilichofanyika hivi karibuni, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura, alisema kamati hiyo itashughulikia masuala yanayohusu ajira na nidhamu kwa wafanyakazi wote.
Alisema kwa kuwa kwa sasa kamati haijampata afisa maslahi, baadhi ya kazi za afisa huyo ikiwa ni pamoja na utoaji ruhusa kwa mfanyakazi itafanywa na Katibu wa kamati, Bw. Peter Maduki.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo kama ilivyotangazwa na Katibu Mkuu, ni Deogratius Makoye, Sista Claudia Mashambo na Sista Flora Chuma.
Wakati huo huo: Katibu Mkuu huyo amesema katika mipango yake ya mika mitatu ijayo, TEC itatumia mbinu zaidi kujiendeleza na kuwaendeleza wafanyakazi kulingana na vitengo vyao kwa kuwa hali hii, itasawaidia wafanyakazi hao kuongeza ufanisi zaidi katika utendaji wao.
Akitaja mafanikio ambayo Baraza limeyapata katika kipindi cha Mwaka Mtakatifu wa 2000, Padre Rutechura alisema kuwa ni pamoja na baadhi ya wafanyakazi kufunga pingu za maisha na Baraza kupokea wageni wapya.
Kingine ni Baraza kupata maaskofu wapya watatu akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa TEC, Padre Method Kilaini, ambaye sasa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, Askofu wa Jimbo la Geita, Mhashamu Damian Dallu na Askofu Mteule wa Jimbo la Mpanda, Mhashamu Pascal Kikoti.
Mbali na mafanikio hayo Baraza pia limepoteza wafanyakazi wake watatu katika kipindi cha kuanzia Agosti hadi Desemba mwaka huu.
Wafanyakazi hao ni aliyekuwa katibu mtendaji wa Idara ya Mawasiliano Padre Norbert Kija, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Kichungaji Padre Theobald Kyambo na Bw. Ngaga aliyekuwa katika kitengo cha Wakala wa Meli cha TEC.
Baraza pia limewaaga wafanyakazi kadhaa baadhi yao wakirudi katika mashirika yao ya kitawa, na wengine kustaafu kazi akiwemo aliyekuwa katibu Mtendaji wa Shirika la Misaada la CARITAS, Tawi la Tanzania Bw. Clement Rwelamila.
Padre Pius ametoa changamoto kwa wafanyakazi hao kudumu katika imani na kuzidisha bidii katika kazi.
Na.Josephs Sabinus
WAKATI Kituo cha kulelea watoto cha YCIC, kimekwisha somesha takriban watoto 30 katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ufundi stadi, watoto 4 kati ya 20 waliokopeshwa na kituo hicho, ndio wanaoendelea na miradi yao tangu mwaka jana, imefahamika.
Taarifa hiyo ilitolewa kwa pamoja na maofisa wa Kituo cha Habari na Utamaduni(YCIC) cha jijini Dar-Es-Salaam, wakati watoto na wawakilishi wa Shirika la Kipapa lla Utoto Mtakatifu wa parokia Mwenge na Manzese za Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, walipotembelea kituo hicho kuwapa zawadi wenzao wanaolelewa kituoni hapo na kushirikiana katika michezo na mazungumzo, Jumanne iliyopita.
Maofisa hao, Bw. Sigsbert Kansabala, ambaye ni Afisa Utumishi, Mkuu wa Idara ya Elimu, Bi. Sabina Balisius, Mkuu wa Idara ya Ustawi wa jamii, Bw. Ojuku Mgedzi na Kaimu Mkuu wa Idara ya Mafunzo, Bi. Hadija Nyambasi, walisema kuwa, sababu kubwa ya watoto hao kushindwa kuendelea na miradi wanayokusudia ni tamaa ya kuishi kiufahari wanaposhika pesa nyingi kwa mkupuo.
"Tatizo ni kwamba hawakuzoea kushika pesa nyingi. Mfano ukimpa hata 10,000/=, matumizi yake yataongezeka ghafla na kusahau kufanya mradi alioukusudia," alisema Bw. Kansabala na kuongeza, " walioendelea ni wale waliofanya miradi ambayo bidhaa zake sio za kuuza na kununua, mfano, vinyozi wameendelea vizuri sana. Wapo mpaka sasa."
Juu ya masomo, Bi. Sabina alisema mwaka ujao tawi la kituo hicho lililopo Kigamboni, linatarajia kuwaingiza darasa la kwanza watoto 200 ambao tayari wamekwisha andikishwa katika shule mbalimbali za msingi.
Wakizungumzia matatizo, viongozi hao wa kituo cha YCIC, walisema kupenda kuishi maisha ya uhuru na kujitawala mno, kumewafanya watoto hao washindikane kurudi katika familia zao na badala yake sasa wamekuwa wakikamatwa ovyo na polisi ingawa kituo kinajitahidi kuwatatulia tatizo hilo linapotokea.
"Watoto wengi wamezoea kuishi ‘free’ huru. Hata ufanyeje hawakubali kurudi. Wengine mnakubaliana hata kumpeleka kwao mikoani lakini akifika njiani anarudi. Ingawa tunawaambia asiye na uhakika wa kula au kulala akubali tumpeleke kwenye kituo kinachotoa huduma zote, lakini hawakubali," alisema afisa mmoja.
Kituo cha Habari na Utamaduni(YCIC), kilisajiliwa mwaka 1995. Hutoa huduma za elimu, afya,kutetea haki za watoto,kupatanisha na kuwarudisha watoto na vijana katika familia zao, na kujenga uaminifu, kujiamini na maarifa kwa watoto na vijana ili kuboresha maisha yao.Kituo hiki ambacho pia hutoa taarifa, kuepusha wimbi la watoto kuhamia mijini na kuwapatia mafunzo katika taasisi nyingine, huhudumia watoto na vijana wote wenye umri kati ya miaka 5na 25 kutoka familia mbalimbali walikopata mifarakano.
Vijana na watoto hupatikana kutoka katika familia kubwa na maskini, mitaaniwakiwa peke yao au na wazazi wao,watoto wasiojiweza katika familia na hata wanaoishi katika magenge mitaani.
Kituo hiki hufanya kazi kwa ushirikiano wa ufadhili wa mashirika kama Concern Worldwide, Save the Children UK and Christian Aid na UNICEF, DRDP, UNHCR na taasisi nyingine za kibinafsi.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa CPL, Padre Raphael Kilumanga, aliwaasa watoto na vijana wanaolelewa katika kituo hicho kuzingatia malezi na utamaduni wa Kitanzania na akawapongeza kwa maonesho ya michezo mbali mbali zikiwamo ngoma za asili.
"Endelezeni utamaduni wa kusaidiana kwa kuwa ndio utamaduni wa Watanzania huku mkizingatia kuwa taifa bila utamaduni, limekufa."
Mabibo kujenga madarasa ya milioni 12/=
Na Getrude Madembwe
SHULE ya Msingi Mabibo ya jijini Dar-Es-Salaam, inatarajia kuanza ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa vitakavyogharimu shilingi milioni 12, imefahamika.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Rubegga M. Rubegga, aliliambia KIONGOZI hivi karibuni kuwa, mpango huo ulifikiwa katika kikao cha pamoja na wazazi kilichofanyika shuleni hapo Desemba 10, mwaka huu na kuamriwa kuwa kila mzazi wa mwanafunzi, wa darasa la kwanza, atachangia shilingi 20,000/=
"Mchango huu hautawahusu wanafunzi wa madarasa mengine bali ni wale tu, wanaoandikishwa kuanza darasa la kwanza mwakani," alisema.
Alisema ujenzi huo unaotarajiwa kuanza mapema ili januari 15, 2001, madarasa hayo yaweze kutumika, utakuwa ni awamu ya kwanza wakati ujenzi wa awamu ya pili utafanyika Juni mwaka 2001.
Shule hiyo ina jumla ya vyumba vya madarasa 17, wakati mahitaji ni vyumba 48.