Picha na mengine juu ya Fr. Kija
Toleo Maalum
HISTORIA FUPI YA MAREHEMU PADRE NORBERT JUMA KIJA TANGU KUZALIWA
1957 HADI KIFO 2000
Padre Norbert Juma Nimage Kija alizaliwa mwaka 1957 katika kijiji
cha Kijereshi wilaya ya Magu katika mkoa wa Mwanza.
Marehemu
Padre Norbert Juma Kija ni mtoto wa familia ya Mzee Seif Masanja na Mama
Modesta Kija.
Alizaliwa
katika familia ya Kiislamu na alikuwa Muislamu hadi alipoamua yeye mwenyewe
kubadili dini na kuwa Mkristo Mkatoliki.
Februari
27, 1974, alipata Sakramenti ya Ubatizo na Ekaristi Takatifu katika parokia ya
Malili. Machi 9, mwaka huohuo, alipata Sakramenti ya Kipaimara katika parokia
hiyo ya Malili.
Akiwa
kijana katika parokia hiyo, Marehemu Padre Norbet Kija alianza kutumikia kabla
ya kubatizwa. Wakati huo Mhashamu Askofu Aloysius Balina, akiwa Paroko.
Askofu
Aloysius Balina alivutiwa sana na mwenendo wake. Marehemu alipenda sana mambo
ya kanisa kiasi kwamba, Paroko wake alimpatia kazi ya kuuza magazeti ya Kanisa.
Marehemu
alipendezwa sana na jina la Frateri Norbet Ngusa, aliyekuwa mwaka wa kichungaji
ndipo marehemu alipoamua kubatizwa kwa jina hilo.
Marehemu
Padre Kija, alikuwa karibu sana na Padre Aloysius Balina, aliyekuwa Paroko wake
wakati huo.
Kwa
jinsi hiyo, Marehemu alimkabili Paroko wake na kumweleza nia yake wito wa
Upadre. Paroko wake alimwelekeza na akatuma maombi Makoko Seminari, kwa bahati
mbaya Gombera wa Seminari ya Makoko hakuweza kumjibu kwa sababu jina alilotumia
Marehemu lilikuwa la Kiislam, "Juma Seif."
Kwa
bahati sana Gombera huyo alitembelea Parokia ya Malili na ndipo hapo Padre
Aloysius Balina alipomfahamisha kuwa kijana huyo si Muislamu bali alishabatizwa
na kuwa Norbert.
Kwa
maelezo hayo, Gombera wa Seminari ya Makoko alikubali na kutoa fomu zilizomwezesha
marehemu kufanya mtihani wa kujiunga na Seminari hiyo.
Pamoja
na kuwa Gombera, Paroko wake aliendelea kumsaidia Marehemu katika kumlipia ada
na kumpatia maadili mazuri.
Hali
hiyo, iliendelea tangu wakati wa malezi na masomo yake hadi kifo chake.
Tunamshukuru
sana Baba Askofu Aloysius Balina kwa msaada wake huo, Mungu azidi kumbariki na
kumjalia ufanisi mwema katika kazi zake.
Marehemu Padre Norbert Juma Nimage Kija alipata elimu yake katika
shule zifuatazo:-
Ø Malili shule ya msingi mwaka
1967- 1974.
ØMakoko
Seminari kidato cha kwanza hadi cha nne 1975 hadi 1978.
ØNyegezi
Seminari kidato cha tano na cha sita mwaka 1979 hadi 1981.
Ø Jeshi la kujenga Taifa kwa
mujibu wa taifa mwaka mmoja 1981 hadi 1982 katika kambi ya Bulombora.
ØNtungamo
Seminari- Filosofia miaka miwili toka 1982 hadi 1984.
ØKipalapala
Seminari - Teolojia miaka mitano toka 1984 hadi 1989.
Padre
Kija alipewa Daraja ya Ushemasi Desemba 15, 1988 katika parokia ya Ng’wanangi
na baadaye, Daraja Takatifu ya Upadre Agosti 3, 1989 katika parokia ya
Chamugasa.
SHUGHULI ZA KITUME.
Mara
baada ya Upadrisho wake, Marehemu Padre Kija alipangiwa kufanya kazi za kitume
katika parokia ya Ng’wanangi.
Mwaka
1991 alihamishiwa katika parokia ya Shinyanga Mjini kama Paroko Msaidizi,
Mkurugenzi wa Baraza la Walei na Idara ya Upashanaji Habari wa Jimbo hadi mwaka
1993, alipohamia Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania huko
Dar-Es-Salaam.
Marehemu
alikuwa na vipaji vingi sana, kati ya vipaji hivyo alipenda sana kusaidia
vijana katika kujiandaa kukabiliana na maisha.
Upendo
huo ulijionesha katika kuwabana vijana na kuwaeleza ukweli na kukemea mambo
mabaya yaliyojionesha katika matendo na maneno yao ilipobidi kufanya hivyo.
Padre
Kija hakuogopa kusema ukweli juu ya baya aliloliona kwa mtu yeyote yule bila
kujali umri au wadhifa alionao.
Pamoja
na tabia hiyo, yeye mwenyewe alikuwa ni mpole na mtu wa tabasamu siku zote,
mtii na mnyenyekevu wa kukubali na kurekebisha makosa aliyonayo endapo
ataambiwa na mtu yeyote yule.
Daima
alipenda kusikiliza ushauri na maelekezo mbalimbali aliyoambiwa na wenzake.
Hakumpuuza
mtu yeyote wala kubagua, bali wote walikuwa ni wake bila kujali busara ya mtu,
wadhifa wala umri.
Mtu
yeyote alipomwendea kwa ukali alipenda sana kumwomba wasalimiane kwanza kabla
ya kumgombeza. Hali hiyo, inaonesha ni jinsi gani Marehemu alivyokuwa
mnyenyekevu.
Marehemu
Padre Kija alikuwa na karama ya ubunifu wa maendeleo na hasa mbinu mpya za
Sayansi na Teknolojia.
Ubunifu
huo ulianza kujionesha mara tu, alipohamia Parokia ya Shinyanga mjini na kuwa
Mkurugenzi wa Idara mbili zilizotajwa awali.
Katika
kipindi kifupi alichokuwa hapo, aliziwezesha idara hizo kupata usafiri wa gari.
Na zaidi ya hilo alifufua Idara ya Upashanaji Habari iliyokuwa imefungwa kwa
muda.
Kutokana
na mbinu zake mwenyewe aliiwezesha idara hiyo kufungua duka la vitabu pamoja na
uuzaji wa picha za Watakatifu, Rozari na Visakramenti mbalimbali. Hali
iliyopelekea kupata mafanikio makubwa, kwani kwa muda mfupi ofisi hiyo ilikuwa
tayari na mashine za kisasa za kurudufu makaratasi na fotokopi.
Yote
haya yanaonesha kuwa, alikuwa na tabia ya kujisomea na kuelewa dunia
ianavyokwenda. Marehemu Padre Kija hakuwa mchoyo, bali alikuwa mkarimu na
mpenda maendeleo kwa vijana na Kanisa kwa jumla.
Hali
ya kupenda maendeleo haikuishia jimboni kwake tu, iliendelea kujionesha hadi
alipohamia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Akiwa
huko Marehemu Padre Norbert Juma Kija, alipelekwa Chuo cha Jamii, Nyegezi
kilichopo jijini Mwanza (sasa hivi Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino).
Marehemu
alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uandishi wa Habari na kuwa mwanafunzi bora
wa mwaka huo wa 1995. Aliwasaidia wanafunzi wenzake kuwafundisha kompyuta.
Ujuzi
wake wa kutumia kompyuta, uliwafanya walimu wake waendelee kumuita kuja chuoni
hapo kufundisha somo hilo.
Baada
ya kuhitimu masomo yake hayo, alirudi Dar-Es-Salaam, katika ofisi za Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania na kufanya kazi ya Afisa wa Habari (Press -
Secretary) wa Baraza hilo.
Kutokana
na utendaji wake bora Maaskofu walimteua kuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya
Upashanaji Habari. Akiwa na wadhifa huo aliimarisha vema idara hiyo na kuleta
mafanikio makubwa ya kulifanya gazeti la KIONGOZI litoke kila wiki badala ya
mara moja kwa mwezi.
Gazeti
hilo limekuwa na mafanikio makubwa hadi hivi sasa.
Akiwa
katika ofisi hiyo, Marehemu Padre Kija alitumia vyanzo vyake vyote vya pesa,
ikiwa ni pamoja na wafadhili wake binafsi kwa ajili ya matumizi ya ofisi.
Baadhi
ya vitu alivyofanya ni pamoja na ununuzi wa kompyuta mpya za kisasa pamoja na
mashine ya kuchapia (Printer) mpya na ya kisasa ya yenye nguvu na uwezo mkubwa
wa kufanya kazi kwa haraka zaidi na nadhifu.
Aidha,
alitumia ujuzi wake wa kompyuta kuingiza programu mbalimbali na kuwafundisha
wafanyakazi namna ya kuzitumia. Sababu ya utendaji wake mzuri wa kazi
aliteuliwa pia kuwa Katibu wa mikutano ya wakuu wa idara, pia aliombwa
kusimamia mawasiliano na matumizi ya simu katika idara zote za TEC.
Aliteuliwa
pia kuwa mjumbe katika kamati ya kufufua bodi ya TMP huko Kipalapala. Kwa
kumbukumbu kubwa siku za hivi karibuni ameiwezesha ofisi hiyo kupata gari
jipya.
Marehemu
Padre Norbert Kija, hatasahaulika pia katika majimbo mengi ya Kanisa katoliki
nchini.
Alisafiri
katika majimbo mbalimbali kufunga kompyuta na kuziwekea programu pamoja na
kuwafundisha matumizi yake. Aliwaungia na kuwaungaishia mawasiliano kwa njia ya
Internet na hasa E-mail.
Pamoja
na hayo, alitumia muda wake mwingi kuwezesha ufungaji wa vituo mbalimbali vya
kurushia matangazo vikiwemo vituo vya Morogoro, SAUT Mwanza na Sumbawanga.
Aliwezesha
miradi mbalimbali kupata wafadhili. Nia yake hasa ilikuwa kuwezesha maendeleo
ya mtu binafsi kwa nia ya kuiendeleza jumuiya ya Kanisa na chini nzima ya Tanzania.
Aidha
alisaidia kupata fedha zilizowawezesha wajumbe mbalimbali wa majimbo yote
nchini kuhudhuria warsha, semina na masomo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa
juhudi hizo, yeye mwenyewe aliweza kuhudhuria mikutano mbalimbali ya kimataifa.
Baadhi ya mikutano hiyo ni ule mjadala wa kufutiwa madeni nchi ambazo
hazijaendelea huko Cologne - Ujerumani.
Katika
mkutano huo yeye mwenyewe alitoa mawazo na hoja zake binafsi kwa niaba ya
wananchi wa Tanzania na kutetea mada hiyo.
Marehemu
Padre Kija baada ya kurudi jimboni Shinyanga mwezi Aprili Mwaka huu,
alijishughulisha sana katika ujenzi wa kituo cha kurushia matangazo cha jimbo
‘REDIO FARAJA FM STEREO’. Pia, alijitolea muda wake pamoja na fedha zake
kuharakisha ujenzi wa jengo la Redio hiyo unafanikiwa.
Pamoja
na udhaifu wa mwili aliendelea kufanya kazi hasa za kompyuta, ujenzi, usimikaji
wa mnara wa kurushia matangazo na kuandaa wafanyakazi wa Redio Faraja.
Cha
ajabu mno, katika usaili wa kuajiri, hakujali wafanyakazi katika redio hiyo,
aliweza kugundua mara moja kipaji cha kila mtahiniwa na kukiheshimu.
Na
kama alikuwa na wazo lolote juu ya mtahiniwa na wasimamizi wa redio, alilisema
mara moja bila kusita endapo ana uhakika nalo.
Na
kama hakuwa na uhakika mara moja alikwenda kulisoma kwenye vitabu na kufanya
mawasiliano mbalimbali na wataalam kwa njia ya Internet na hivyo, kupata
uhakika wa swala hilo.
Hali
hiyo alimfanya marehemu kuamua kufunga simu yake yeye mwenyewe chumbani mwake.
Marehemu aliendelea hivyo hivyo bila kujihurumia wala kunung’unika bali
alivumilia mateso na mahangaiko kwa utulivu na amani hadi hapo alipoaga dunia tarehe
Septemba 19, 2000 majira ya saa nne asubuhi.
RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA,
APUMZIKE KWA AMANI
AMINA.