Yanga kuuburuza uongozi kortini
l
Ni kupinga klabu kutofanya uchaguziNa Mwandishi Wetu
BAADHI ya wanachama wa klabu ya soka ya Yanga jijini Dar-Es-salaam, wamesema wanakusudia kufungua kesi mahakamani Jumatatu hii kupinga hatua ya uongozi wa klabu hiyo kufuta Uchaguzi mkuu.
Wanachama hao waliokusanyika mwishoni mwa juma yalipo makao makuu ya klabu hiyo, mtaa wa jangwani Kariakoo, walisema wanapinga kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Issack Shekiondo ya kufuta uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo.
Walisema kauli hiyo ya kufuta Uchaguzi Mkuu kwa kisingizio cha Yanga kuwa kampuni, ni hila ya kutaka kujinyakulia madaraka yote kinyemela.
Makamu mwenyekiti huyo wa Yanga Alhamisi iliyopita alitangaza kuwa klabu hiyo ya soka haitafanya tena uchaguzi kwa kuwa sasa imesajiliwa kama kampuni na inaongozwa na mfumo wa Rais na sio Mwenyekiti tena.
Alisema klabu yake tayari imepata hati ya usajili wa makampuni nchini na inahalalisha mfumo huo mpya.
Hata hivyo, wanachama wanadai kuwa katika mkutano wao wa awali iilikubaliwa kuwa Yanga ianzishe kampuni lakini, iendelee na mfumo wake wa sasa.
Wanachama hao wakiongozwa na Hussein Ally, walisema kuwa uamuzi wao wa kwenda mahakamani ili kuiomba mahakama iwalazimishe viongozi waitishe mkutano wa uchaguzi, haitokani na tukio la hivi karibuni la yanga kufungwa na Simba.
Historia ya soka tanzania inaonesha kuwa moja kati ya Simba na Yanga inapofungwa, basi hufumuka mgogoro mkubwa na pengine hata viongozi kupinduliwa
.Siachi ndondi mpaka nimkung’ute Tyson-Lewis
LONDON, Uingereza
BONDIA Lennox Lewis, ambaye ni bingwa wa mataji mawili ya Dunia, amesema kuwa ingawa anapigana pambano la mwisho Jumamosi hii, nchini kwake, hatastaafu ndondi hadi pale atakapombonda Mike Tyson.
Akizungumza mbele ya wandishi wa habari mwishoni mwa juma mjini London, Lowis alisema hataki kuacha ngumi kwa aibu na hivyo ni lazima kwanza amtwange Tyson na kwamba hapo ndipo atajisikia raha ya kustaafu ndondi.
Bingwa huyo wa dunia ambaye anapanda ulingoni Jumamosi hii kupambana na Mwafrika Kusini mwenye makao yake marekani, Franscois Botha, ana uhakika wa kushinda pambano hilo kirahisi kutokana na kile anachodai ni ubovu wa mpinzani wake.
Botha alipigwa na tyson, katika raundi za kwanza na akakiri kuwa Tyson alimtwanga kihalali.
Iwapo Botha atamshinda Lonnex, basi hataweza kupigana na Tyson baadaye mwaka huu kama ilivyopangwa.
Katika michezo yao kuhusu pambano hilo la leo, Lonnex alisema ni lazima ashinde ingawa hana lazima ya kushinda kwa "Knock out".
Naye Botha alisema lengo lake si tu kwamba anataka kushinda pambano, bali pia kulinda hadhi ya ya bara la Afrika ambayo aliharibika pale alipopigwa kirahisi na Tyson.
"Napigana kwa ajili ya Afrika nzima na si kwa ajili yangu mwenyewe, nitajitahidi kwa jinsi yoyote ili kulinda hadhi yetu na Mungu atanisaidia," alisema.
Jengo la Walokole kutumika kwa ndondi
Na Dalphina Rubyema
KATIKA hali isiyoaminika kiurahisi, Kituo cha Walokole, maarufu kwa jina la Christian Centre kilichopo jijini Dar-Es-Salaam, Jumapili hii kinatumika kwa ajili ya pambano la mchezo wa ngumi kati ya mabondia Fike Wilson na Mwakasinga John; imefahamika
Akizungumza na Waandishi wa habari mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini, Mkurugenzi wa ngumi za kulipwa nchini,(TPBC),Titus, alisema kuwa pambano hilo Midle weight ,kati ya miamba hao wa ndondi litashuhudiwa pia Mwenyekiti wa chama hicho, Onesimo Ngowi, atakayekuwa mgeni rasmi.
Alisema pambano hilo litakuwa la raundi kumi na kutakuwepo na pambano la utangulizi kati ya Ramadhani Ali na Julius Junet wanaopigana uzito wa Super Weight ambapo Said Chidi atazitwanga na Hamza Seif, wote wa uzito wa light weight.
Wadhamini wa shindano hilo zito ni Heavy D. Promotion.
Wakati huo huo:
Rais wa Shirikisho la Ngumi Duniani (IBF), Hiawatha Knight anatarajiwa kuwasili nchini Julai 21, mwaka huu ambapo pamoja na kufanya mambo mbalimbali, pia atatembelea kituo cha watoto yatima cha Mtakatifu Theresia kilichopo Mburahati Jijini Dar-Es-Salaam.Ligi daraja la Kwanza netiboli kuanza Julai 23
Na Widimi Elinewinga DSJ
LIGI Daraja la Kwanza ya Netiboli inatarajiwa kuanza 23 Julai hadi Agosti 6, mwaka huu mjini Arusha.
Akizungumza na gazeti hili, Mweka Hazina wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) Anna Kibira, alisema jana kuwa timu zitakazo shiriki katika mashindano hayo ni Bandari, Jeshi Stars(DAR), Kakakuona, Mapinduzi na Jitegemee.
Nyingine ni timu za JKT kutoka Mbweni, Mlalakuwa na Mafinga pamoja na timu za Reli kutoka Tanga, Morogoro na Dar-Es-Salaam.
"Timu za Polisi hazitashiriki mashindano ya mwaka huu kwa sababu wachezaji wake wengi wako masomoni," alisema Kibira.
Aidha Kibira alisema timu ambazo hazijathibitisa kushiriki mashindano ya mwaka huu ni pamoja na Majimaji ya Songea, Hamli Ranger ya Lindi na Vatican kutoka Dar-Es-Salaam.
Ligi hiyo itatoa washindi wanne wa juu ambao watapata nafasi ya kushiriki ligi ya Muungano ambapo mwaka jana nafasi ya kushiriki hiyo, timu za Jeshi Stars, JKT Mbweni na Bandari, zilishiriki ligi ya Muungano.
Mpaka sasa ligi ya Zanzibar imeshamalizika na timu za JKU, Bandari Zanzibar Mafunzo na Chipukizi zimezibitisha kushiriki.