Tuwe Wasamaria wema kwa wenzetu

DAIMA katika jamii, kuna watu ambao wamekuwa na shida mbalimbali. Tunaweza kutofautisha shida za kawaida na zile zisizo za kawaida.

Shida za kawaida na ambazo zimezoeleka, ni kama ukosefu wa maendeleo, ukosefu wa elimu, kutokuwa na huduma nzuri za afya, kutokuwa na huduma nzuri za mawasiliano, kama vile barabara, vyombo vya usafiri, vitendea kazi mbalimbali na nyingine kama hizo.

Zipo shida kadhaa zinazotokana na mazingira tofauti ambazo nyingine si za kawaida, kama vile kukabiliwa na njaa kutokana na hali mbaya ya hewa, kukumbwa na mafuriko na hivyo kusabisha hasara kubwa ya mali na ukosefu wa makazi.

Kuna shida zinazotokana na ukosefu wa amani, na hivyo kusababisha hali ya ukimbizi katika nchi. Pia zipo zinazotokana na kuingiliwa na magonjwa, mengine yakiwa ya kutisha kama gonjwa hili hatari la ukimwi.

Katika hali kama hiyo, binadamu akikabiliwa na matatizo kama hayo huhitaji msaada kutoka kwa majirani na marafiki na hasa wale wenye mapenzi mema. Katika

Injili ya Luka tunasoma jinsi mtu mmoja alivyoshambuliwa na watu wabaya na hivyo akawa katika hali mbaya. Lakini kwa bahati njema alisaidiwa na Msamaria mwema. Na kutokea wakati huo neno hili "Msamaria Mwema" limekuwa linatumika katika kuelezea mtu mwema, aliye tayari kumsaidia mwenzake katika shida. Mara kwa mara tunasikia kuwa fulani ni Msamaria mwema, kwa maana kuwa ni mtu mwenye huruma na mwenye kutoa msaada kwa yule mwenye shida.

Kanisa Katoliki limetambua kutokea zamani wajibu wake wa kuwasaidia wale wote wenye shida mbalimbali.

Ili kufanya kazi hiyo ya kuwasadia wenye shida na matatizo mbalimbali, Kanisa limeanzisha Shirika linalojulikana kama "CARITAS". Neno Caritas, kutokana na neno la Kilatini, lenye maana ya "upendo".

Shirika la Caritas lipo katika ngazi ya kimataifa, kitaifa, kijimbo, na pia katika ngazi ya kigango na hata jumuiya ndogondogo za Kikristu.

Kazi kubwa ya shirika hilo ni kusaidia penye matatizo katika jamii mbalimbali.

Kwa upande wa Kanisa la Tanzania, Jumapili ya Kwanza ya Mwezi Septemba hujulikana kama ni Siku ya Msamaria Mwema.

Katika siku hiyo, Ujumbe maalumu kuhusu Msamaria Mwema hutolewa na Idara ya Caritas ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Wazo kubwa ni lile kwamba "Kila binadamu ni ndugu".

Katika Siku ya Msamari Mwema, tunahimizwa kutoa michango yetu ya hali na mali kwa ajili ya wale wote wenye shida mbalimbali katika jamii yetu. Tuna watu wengi wenye shida katika taifa na nchi yetu kwa jumla.

Wenzetu wengi wameathiriwa na ugonjwa mbaya wa ukimwi. Hao, kwa kiasi kikubwa wanahitaji msaada wetu.

Tunao walemavu wengi katika nchi yetu, wanaohitaji huduma ya afya, tunao watoto yatima kutokana na ukimwi. Hao, wanahitaji wapewe malezi mazuri na elimu ya kuwafaa kwa maisha yao ya baadaye.

Tunao wakimbizi wengi sana katika nchi. wanahitaji pia huduma na misaada yetu mbalimbali.

Mwaka huu Tanzania imeathirika sana na njaa. Wote hao, wanahitaji huruma, upendo , ukarimu na misaada yetu. Kwa kifupi tunao wengi wenye shida wanaotuzunguka hapa na pale, tunapaswa na pia ni wajibu wetu kuwasaidia kila mtu kwa nafasi yake, kama ndugu zetu halisi.

Katika siku hii ya Msamaria Mwema, tunakumbushwa na kuhimizwa kuwa na moyo wa huruma kama alivyokuwa yule Msamaria.

Tunaambiwa kuwa kutoa ni moyo na siyo shauri la utajiri. Ni kweli kuwa hakuna mtu anayeweza kutoa kile asichokuwa nacho, lakini tunaamini kwamba wananchi na waamini wengi wanao uwezo wa kutoa cho chote kile kwa ajili ya hao wenzetu walio katika dhiki.

Daima tukiwa na hali nzuri tujiulize kama sisi tungekuwa katika shida hizo walizo nazo wenzetu, je, tungefurahi kuona hatupati misaada kutoka kwa wenzetu wenye uwezo.

Sote tunapenda kupata misaada wakati tunapokuwa katika shida, basi nasi tuwe tayari kuwasaidia wenzetu walio katika shida. Hakuna mtu anayetafuta shida kwa makusudi katika maisha yake, mara nyingi matatizo huja kwa bahati mbaya na bila kutazamiwa.

Tunaambiwa kwamba kama yule Mwanasheria, twende tukatende kama alivyotenda yule Msamaria Mwema, yaani tukawe na haruma kwa wenzetu walio katika shida mbalimbali.

Tunaambiwa katika Maandiko Matakatifu kuwa, tuwe na huruma kama Baba wa mbinguni alivyo na huruma, ili siku moja tuweze kuhurumiwa.

Tunapenda kuchukua nafasi hii pia, kuipongeza Idara ya Caritas Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wale wote wenye shida na matatizo mbalimbali.

Caritas imewasaidia sana wakimbizi kutoka nchi jirani, imetoa misaada ya hali na mali kwa wasiojiweza. Caritas Tanzania, imewasaidia wale waliokabiliwa na njaa katika nchi yetu katika mikoa mbalimbali.

Aidha, Caritas Tanzania, imetoa misaada mingi na hata mikopo kwa ajili ya maendeleo, hasa maendeleo ya akina mama. Vile vile, Caritas Tanzania, imewasaidia walemavu na watoto wengi yatima katika nchi yetu. Kwa kifupi tunaweza kusema Caritas Tanzania imekuwa kweli ni Msamaria Mwema.

Lakini tunapaswa kukumbuka kuwa Caritas Tanzania haina mahali pa kupata misaada hiyo isipokuwa ni kutoka kwa wananchi wa Tanzania, au waamini wa Kanisa la Tanzania.

Ni wajibu wetu kutoa na kuchangia upatikanaji wa misaada hiyo ili Caritas wapate chochote cha kuwasaidia hao wenzetu wenye shida na matatizo.

Tutoe kwa moyo, tutoe kwa ukarimu na tuwe Wasamaria Wema kweli kweli. Maana kutoa ni moyo, usambe ni utajiri

Parokia ya Kibakwe yasherehekea jubilei kwa kishindo cha aina yake

Ndugu Mhariri,

Watu wengi wanasikika wakisema kuwa mambo kama haya bado hatujayaona tangu tumezaliwa. Hata hivyo, haikuwa rahisi kuamini mapokezi makubwa yaliyofanyika wakati Msalaba wa Jubilei ulipowasili Parokia ya Kibakwe.

Msalaba ulipokewa kwa pamoja na watu wasio wa madhehebu yetu na wasio Wakristo. Kila mahali Msalaba ulikofika ulianzisha hisia mpya ya matumaini kwa Yesu Kristo Msulibiwa. Waamini kwa wasiowaamini, walipata fursa ya kuushangilia na kukesha nao kwenye mitaa yao vigangoni kwa zamu.

Huu ulikuwa mwezi wa Julai na mwanzo wa Agosti, 2000. Mapokezi hayo, yalikuwa pia maandalizi ya Hija ya Kiparokia na Sikukuu ya Parokia ambayo somo wake, ni Bikira Maria, aliyepalizwa Mbinguni.

Sherehe hiyo ilifikia kilele chake tarehe 13.8.2000. Maandalizi yalifanyika kwa mafungo na Wiki ya Sala kwa waamini wote wa vigango 20 vya Parokia hiyo.

Siku hiyo ya sikukuu, ilikuwa na mshindo wa pekee. Hoi hoi, nderemo nyimbo - KRISTO, JANA, LEO NA DAIMA, ndizo zilizosikika zikivuma katika anga lote la Kibwakbwe ambako maandamano yalipitia.

Waamimi kutoka vigango vyote walikusanyika na wengine kwa kutembea kama mahujaji kwa kilometa zaidi ya 20. Ilikuwa ni siku ya Hija Kiparokia. Umati wa waliohudhuria ibada hiyo, wapatao elfu tano au sita hivi, ulilazimika kufanyia ibada nje ya Kanisa.

Hii ilikuwa siku ya kukumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo. Tukio hilo, lilikuwa la pekee kabisa.

Heka heka ilipamba moto siku ya Jumapili iliyofuata, ya tarehe 20/8/2000 ambapo Parokia iliweza kuwakusanya vijana karibu wote wa Parokia hii kutoka kila Kigango.

Vijana hao waliandamana hadi kanisani ambako Misa iliadhimishwa. Vijana walionesha umahiri wao wa kumkiri Kristo kwa shangwe ya aina yake.

Jambo hilo lilionesha imani thabiti na utayari wao wa kumjunga Kristo na bila woga. Wakati wa Injili katika ibada, Padre Leonard Amadori, ambaye ndiye Paroko, alihimiza vijana kumwiga kijana mwenzao Kristo ambaye, katika ujana wake wa miaka 33, alikuwa tayari kujitoa mhanga ili kuwakomboa wanadamu.

Katika Injili ya siku hiyo, tulimsikia kijana aliyekuwa na mali nyingi iliyomfanya asiitiikie mwaliko mwanana wa Kristo.

Vile vile huwa si rahisi kwa vijana kumkiri na kumfuata Kristo kwa dhati kwa visingizio vya aina aina kama starehe au anasa pamoja na kujilimbikizia vikwazo vingi vyenye kuharibu uadilifu.

Vijana walipata hamasa na changamoto kubwa ya kuuishi Ukristo wao na kujipima upya mwelekeo wao kama vijana wafuasi wa Kristo.

Baada ya ibada, vijana walipata nafasi ya kuonesha michezo iliyofanyika kwa ushindani, ambapo washndi walipewa zawadi mbalimbali.

Matukio ya Jubilei Kuu katika Parokia yetu yamedhihirisha umoja na mshikamano wa hali ya juu kiimani.

Vile vile imeweka kumbukumbu nzuri ya kudumu kwa waamini na wasio Wakristo kuhusu maana ya Kristo kutimiza miaka elfu mbili kuzaliwa kwake.

Ambrosi S. Kawala

Katibu wa Halmashari

Parokia ya Kibakwe.

Mahubiri ya Wakatoliki Jangwani, yasiishie Dar pekee

Ndugu Mhariri,

Kwa furaha kubwa, napenda kuungana na Msomaji wako Bw. Brigger wa Switzerland katika toleo la Agosti 5-11, 2000, alipoonesha furaha yake akisema kuwa mahubiri ya Wakatoliki, ni kielelezo tosha cha kutimiza Habari ya Yesu kwa wanadamu.

Nichukue nafasi hii pia kuwapongeza wale wote walioshiriki kuhubiri Injili pale Jangwani(Jijini Dar-Es-Salaam) na kwa hakika bila kumsahau Mhubiri, Padre John Baptist Bashobora kutoka Uganda.

Kwa kweli kwa ujumbe huu, moyo wangu ulifarijika sana. Ingawa mimi sikuwapo kwenye mahubiri hayo, lakini kwa kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari, naambiwa kuwa lilikuwa kongamano lilioandaliwa kwa makini mno.

Naamini mahubiri hayo yaliziinua nyoyo za watu kadhaa wa madhehebu yote walioshuhudia uwepo wa Kristo mahali pale.

Kwa barua hii na kwa namna ya pekee kabisa, namuomba Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini pamoja na Chama cha Kitume cha Uamisho, waandae mahubiri mengine kama hayo.

Tunaomba mahubiri kama hayo yatufikie mikoani na yasiishie Jangwani tu.

Na kama yatahitaji gharama za uendeshaji kongamano hili basi Baraza la Walei jimboni kwetu lifahamishwe ili suala hilo lijadiliwe kwa hatua za utekelezaji.

Mungu awabariki wote, Mungu awabariki wasomaji wako pia.

Edward Wataye,

Box 55,

Nwanhuzi

MEATU.

KIONGOZI: Changanyeni habari za makanisa

Ndugu Mhariri,

Nitafurahi sana pale utaponipa nafasi katika gazeti lako hili ili nami niweze kutoa maoni yangu.

Kwanza kabisa, napenda kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya katika gazeti lenu na nawaomba msichoke katika kuielimisha jamii na kuwajenga wanadamu kiroho.

Mimi maoni yangu ni kwamba, ningependa kuwashauri hasa katika kipindi hiki taifa letu linapoelekea katika Uchaguzi Mkuu ujao, angalau basi gazeti lenu lijitahidi kuchanganya viongozi mbalimbali katika habari ili kupata mawazo tofauti ya kuielimisha jamii.

Mfano, Mgombea wa Urais kupitia chama cha TLP amesema nini au Ali Idd Ali amehaidi nini pindi atakapopata nafasi ya urais au Askofu ameshauri au kuitaka nini jamii.

Tusielekee upande mmoja tu wa viongozi wa dini hasa katika kipindi hiki jamii inapotaka kujua huyu kafanya nini na mwisho, nawashauri muongeze nakala za magazeti hasa mitaani ili tunaoshindwa kuyapata makanisani, tuyapate mitaani.

Nawatakia kazi njema,

Elly Mpiana

Box 6202

Dar-Es-Salaam.

 

Asante kwa ushauri wako. Tutazingatia ushauri wako lakini , ni muhimu kujua kuwa kila chombo cha habari kina sera zake.

Kama kweli wewe ni msomaji wa KIONGOZI, utakubaliana nasi kuwa licha ya ukurasa wa 9,MAKANISANI WIKI HII kuwa maalumu kwa habari za makanisa mbalimbali, bado

viongozi wa makanisa yote wanapewa nafasi katika kurasa nyingine.

ASANTE-MHARIRI