Hongera Masista wa Bukoba
TUMEPATA habari kutoka vyombo vya habari kuwa Masista wa Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu la kule Mkoani Kagera - Bukoba, wanaanzisha shule yenye kuendesha masomo kwa kutumia hasa lugha ya Kiingereza (English medium). Tumeambiwa kuwa shule hiyo inaanzishwa huko Ukonga, Jijini Dar Es Salaam. Ama kwa hakika tunalipongeza sana Shirika hilo la Masista kwa hatua hiyo kubwa ya kimaendeleo.
Ni dhahiri kuwa kuna wazazi wengi sana pamoja na watoto wao wana kiu kikali sana cha elimu siku hizi. Wazazi hao wanafanya kila jitihada ili kuweza kuwapatia watoto wao elimu ya juu kabisa yenye kuwafaa katika maisha yao ya halafu. Watu wengi wanaamini kwamba ni afadhali kumrithisha mtoto elimu kuliko mali kwani mali bila elimu haitaweza kuongezeka na hata pengine itakufa kabisa.
Wazazi wengi hapa Tanzania, na hasa wale wenye uwezo hufanya juu chini kutafuta shule zilizo bora kwa watoto wao. Pia hupenda kuwatafutia watoto wao shule za awali na hata za Secondari. Hivyo kuna wazazi ambao tayari wanawapeleka watoto wao kule Kenya na Uganda kwa lengo hasa watoto wafahamu zaidi lugha ya Kiingereza pamoja na maarifa mengine. Kutokana na mahangaiko hayo Masista wa Bukoba wa Mtakatifu Theresia wameona nao watoe mchango wao katika elimu na hasa kuwapunguzia mzigo na usumbufu baadhi wa wazazi na watoto kwa kuanzisha shule ya ina hiyo hapa nchini.
Juhudi hizi za kuanzisha shule zenye kuweka mkazo katika lugha ya Kiingereza zimepamba moto katika Jiji la Dar Es Salaam na hata katika miji mingine hapa nchini. Kuna shule nyingi za watu binafsi zenye kuwekea mkazo katika lugha hiyo ya Kiingereza. Lakini katika kufanya utafiti wa hapa na pale inaonekana kuwa shule hizo zinakazia sana lugha ya Kiingereza na masomo mengine, lakini hakuna masomo ya dini wala yale ya kimaadili. Hilo ni jambo la kusikitisha sana kwani kukazia masomo ya kawaida pamoja na lugha ya Kiingereza hatuwezi kujivunia vya kutosha kama watoto wetu wana msingi wa maisha ya kweli.
Ni matumaini yetu kuwa Shule hiyo inayoanzishwa na Masista wa Mtakatifu Theresia itatilia mkazo mkubwa sana katika vipindi vya dini pamoja na maadili, na lile somo la uraia litakuwemo katika ratiba ya vipindi. Kumekuwa na manung’uniko mengi sana katika taifa letu kuhusu maadili ya vijana wetu. Wale ambao wameketi chini na kufikiri natumaini wametambua kuwa kuna makosa au udhaifu katika malezi ya watoto na vijana wetu.
Serikali yetu imejitahidi kwa kurusu vipindi vya dini katika mashule yetu, lakini kwa bahati mbaya kuna walezi na hata walimu ambao hawatilii mkazo kuhusu jambo hilo. Imeshatokea kuwa vipindi vya dini huangaliwa kama ni vipindi vya ziada ambavyo visipokuwepo hakuna hasara. Kumbe mambo siyo hivyo!
Watoto wengi na vijana wengi wanafahamu maarifa ya dunia na kiiulimwengu, lakini kwa bahati mbaya hawana adabu wala heshima kwa wazee na wakubwa wengine. Mambo hayo yanapaswa kufundishwa na kuelekezwa huko shuleni licha ya kule nyumbani. Ni matumaini yetu kuwa shule ya Masista inayoanzishwa itakuwa ni ya mfano kwa shule hizo ambazo zinachukua Kiingereza kama ndiyo msingi wa mafunzo. Tunazidi kuwapongeza hao wazazi wanaohangaika kwa ajili ya elimu watoto wao, lakini tunapenda kuwashauri kuwa elimu ya Kiingereza na maarifa mengine bila dini na maadili itakuwa hatujengi taifa letu katika msingi wa kweli.
Tunapenda pia kutoa rai kwa Serikali na hasa ile Wizara ya Elimu kuona kuwa shule hizo za kukazia Kiingereza (English medium) zinakuwa na vipindi vya dini pamoja na urai katika ratiba zao. Mpaka sasa kuna tofauti sana kati ya watoto hao na watoto wengine hasa kuhusu maadili na hata ile elimu ya dini zao. Jambo linalotakiwa kwa kila mtoto wa mumini ni kwamba akue kielimu na pia kidini. Ni jambo la fedheha kuona kijana ametaalamika katika mambo ya kidunia, lakini kumbe ni maskini sana katika mambo ya kidini na kimaadili.
Tumesema kuwa tunawapongeza hao Masista wa Bukoba kwa jitihada yao hiyo ya kuanzisha shule ya pekee hapa Jijini. Masista hao wana shule nzuri sana ya Msingi kule Mwanza, Nyakahoga, na pia wanao Shule yao ya Secondari ya Hekima kule Bukoba, licha ya shule za nyingine. Tunapenda kuwapongeza hao Masista kwa mchango wao mkubwa katika uwanja huu wa elimu. Tunaona hilo ni changamoto kubwa sana kwa Mashirika mengine hapa nchini katika kutoa michango yao katika fani ya elimu. Hatuwezi kusema kuwa hilo ndilo Shirika pekee katika nchi yetu lenye uwezo, bali ni katika kuona wajibu wao na pia ndio utume wao katika Kanisa na Taifa letu. Tunaamini kuwa kuna Mashirika mengi ambayo yangeweza kabisa kutoa michango yao katika elimu. Tunahitaji shule za Kanisa kutoka ngazi ya chekechea hadi vyuo.
Hakuna asiyefahamu kuwa shule zinazoendeshwa na Kanisa na hasa Masista huwa ni zenye kiwango kikubwa sana cha elimu pamoja na maadili.Mpaka sasa tunapenda kutoa shukrani nyingi sana kwa Mashirika mbalimbali kwa kuendesha shule za awali, yaani chekechea. Hata hivyo kama tulivyosema hapo awali, Mashirika hayo yasikomee tu kwenye hizo shule za awali,bali yaendelee kama Shirika la Mt. Theresia linavyotufundisha.
Ni dhahiri kuwa kutakuwa na watoto wengi ambao watapenda kujiunga na shule hiyo na hivyo siyo watoto wote anaotarajia kujiunga na shule hiyo watapata nafasi hapo. Tunapenda pia kutoa rai kwa watu binafsi kuwekeza katika mambo ya elimu kwa kuanzisha shule za aina kama hiyo iliyoanzishwa na Masista. Hapa nchini kuna watu wengi wenye uwezo na hivyo wangeweza kuanza shule na hivyo kupunguza tatizo la shule katika nchi yetu.
Kuna baadhi ya watu ambao wanaanzisha shule hizo za pekee, lakini pengine wanafanya hivyo kama vitega uchumi na siyo hasa kama mchango wao katika elimu. Jambo ambalo litadhihirisha kuwa shule hizo ni kwa ajili ya kujenga taifa letu, ni kule kuwa na sehemu ya mafundisho ya dini katika shule hizo. Lakini kama inatokea kuwa vipindi vya dini hakuna, na wala hakuna somo uraia na maadili, basi hapo tuwe na mashaka kama watoto wetu watalelewa pia kitabia licha ya kupata maarifa mengine.
Tunapenda kumalizia Kauli Yetu hii kwa kuzidi kuwapongeza Masista hao wa Mt. Theresia wa Bukoba kwa juhudi zao kubwa katika kuleta mwanga ndani ya akili za Watanzania kwa kuzingazitia umuhimu wa elimu. Hapo tunaombwa Watanzania wote tuwaunge mkono hao Masista kwa jitihada zao hizo kwa hali na mali.
Walutheri wa Mwanga tukubalini suluhu
Ndugu Mhariri,
Naomba nami unipatie nafasi katika gazeti lako nitoe wosia wangu kwa wenzangu wana -Mwanga wanaodai kupatiwa Dayosisi yao, kuwa tukubali suluhu na tukubali tamko la Halmashauri Kuu ya KKKT kuwa hakuna uwezekano wa kuanzishwa kwa Dayosisi ya Mwanga.
Walutheri wa Mwanga tukumbuke kuwa kila mamlaka imewekwa na Mungu hivyo hatuna budi kuheshimu mamlaka iliyotoa tamko hilo.
Tuache malumbano na wenye mamlaka na badala yake tuungane na wote wapenda amani, tushikamane na tuendelee kumwabudu Mungu bila kubaguana.
Tunaiomba inayojiita Kamati ya Maendeleo ya Walutheri wa Mwanga ikubali suluhu, na kama imekusudia kweli kuleta maendeleo ya Walutheri wa Mwanga, basi iungane na uongozi uliopo wa Dayosisi halali ya Pare, kuleta maendeleo, sio ya kimwili tu, bali hasa ya Kiroho; jambo ambalo ndilo lengo kubwa la dini kwa watu wa Mungu.
Ikiwa ni shughuli za maendeleo ya kimwili, basi tuiachie Serikali ya Wilaya na Halmashauri ya Wilaya kuendesha mipango hiyo na kamwe tusichanganye mipango ya Serikali ya kupelekea wananchi maji, hospitali, barabara na.kadhalika na mipango ya madhehebu ambayo hasa ni kueneza Injili, na kusaidia maendeleo pale tu inapolazimu.
Wazee wetu wanasiasa, acheni kutudanganya kuwa tukipata Dayosisi yetu tutapata maendeleo, kwani kazi hiyo ni ya vyama vyenu vya siasa na wala sio ya madhehebu. Dini kazi yake kuu ni kuelekeza watu wafike peponi?
Viongozi wetu waheshimiwa na wachungaji tunawategemea kulisha kondoo wa Bwana; sasa mnapowashawishi vijana kuchoma nyumba za watu au kupiga makelele ibadani na kutukana viongozi na watu wanaowazidi umri, mnatufundisha nini? mnataka tusiwaheshimu viongozi wetu na wale wanaotuzidi umri?
Wana Mwanga turejee na kumwomba Mungu aturudishie tena Umoja na uvumilivu, tuweze kueneza neno la Mwenyezi Mungu ulimwenguni mwote.
Daima tuheshimu Katiba za madhehebu yetu na ikiwa kuna dosari iliyoko katika katiba hizo tutumie vikao halali kujadili vipengele hivyo na sio kuchukua madaraka ya kuvunja katiba na taratibu zinazotambulika.
Tunaomba waumini warejee na kuwa kitu kimoja na ikiwa yapo matatizo tukae kwa amani na kujadiliana, kusameheana na kuchukuliana mizigo.
Matatizo makubwa ya Wapare ni pale wanapopenda sana (Mburi) vijikesikesi visivyoisha. Tuache tabia hizo na kutumia Biblia kutatua matatizo yetu na kamwe tusifikiri kuwa Dayosisi itatatua matatizo yetu.
Mungu Ibariki Mwanga
Mimi Mpenda Amani,
Naoah. M. Msuya
S.l.P 7080,
Mwanga- Ugweno