Makanisani Wiki hii
Mavazi 'nusu mlingoti', kandambili marufuku Kanisani
Na Steven Mchongi, Mwanza
MAVAZI nusu uchi kama "vimini, skin tight, truck suit" na kandambili yamepigwa marufuku kuvaliwa wakati wa ibada katika kanisa la Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ilemela jijini Mwanza kwa kuwa pamoja na mambo mengine, huchangia kuvuruga ibada.
Mkurugenzi wa Malezi ya miito kwa vijana Jimbo Katoliki la Mwanza, Padre Richard Makungu, amewaagiza wasimamizi kanisani hapo kuwazuia kuingia ndani wakati wa ibada waamini wote watakaovalia mavazi hayo yasiyo ya maadili.
Ametoa agizo hilo Septemba 10 kufuatia wimbi la waamini hasa wasichana parokiani hapo, kuingia kanisani wakati wa ibada wakiwa wamevaa sketi au gauni fupi kupita kiasai pamoja na blauzi zinazobana miili yao au kuacha sehemu kubwa ya maungo yakiwa wazi.
Alisema hali hiyo inaashiria kukosa adabu katika ibada na pia huwafanya waamini wengine wavuruge ibada zao kwa kujikuta pasipo kutarajia, kwanabaki wanaishangaa hali hiyo.
Akitoa agizo hilo, Padre Makungu alisema nidhamu kanisani imeshuka kwa baadhi ya waamini na hivyo inabidi sasa hata kama ni wasimamizi, wawazuie milangoni wenye nidhamu duni namna hiyo ili wasiingie kanisani kuvuruga ibada za wenzao.
Alisema mavazi hayo yastahili kuvaliwa katika maeneo ya burudani na michezo lakini siyo katika nyumba takatifu za ibada kama makanisa.
Alisema muamini yeyote atakayevaa mavazi ya aina hiyo, haina budi kuzuiwa kuingia kanisani na iwapo atakuwa tayari ameingia na akaonekana, atolewe nje mara moja.
Alisema Padre makungu alizielezea kandambili kuwa ni viatu vya kuendea chooni au bafuni wakati wa kuoga hivyo, muamini yeyote ambaye atakuwa amevivaa kanisani, hataruhusiwa kukomunika labda kama ataviacha kwenye benchi alikokalia.
Alisema kulingana na Maandiko Matakatifu na mapokeo kutoka kwa mitume, kanisa ni mahala pa takatifu, hivyo waamini hawanabudi kuzingatia hilo na basi, kuheshimu mahala pa ibada.
Agizo hilo limeanza kutekelezwa na waamini kanisani hapo, wametakiwa kutoa ushirikiano ili kurejesha nidhamu na maadili kanisani.
Hii ni hatua ya pili kuchukuliwa katika harakati za kurejesha nidhamu kanisani, ambapo hivi karibuni parokia hiyo ilipiga marufuku watoto wadogo kusimamia harusi wakati wa Sakramenti ya Ndoa.
Tayari makanisa ya madhehebu mbalimbali hapa Mwanza, yameshakua hatua kama hiyo ya kupiga marufuku waamini kuingia kanisani wakiwa wamevalia mavazi yasiyo ya heshima.
Makanisa unganeni kukemea maovu-Wito
Na Getrude Madembwe
KANISA la African Inland Church, limeyataka makanisa yote kutokaaa kimya pindi yanapoona makosa yakitokea katika jamii na badala yake, kuungana kwa nguvu moja kuyakemea yasizidi kujitokeza.
Askofu Charles Salala wa Kanisa hilo la AIC, Dayosisi ya Pwani, alitoa wito huo wakati akihubiri katika ibada mwanzoni mwa juma lililopita katika kanisa la Magomeni jijini Dar-Es-Salaam.
Alisema kanisa lolote ulimwenguni halipaswi kuwa bubu linapoona mambo yanakwenda kinyume katika jamii kwani kwa kufanya hivyo, linatakuwa linakwepa majukumu yake na kupoteza ladha na maana ya kuwepo kwake duniani.
"Kanisa linatakiwa likemee maovu yanayotokea katika nchi kama haya ya utoaji mimba na mengine mabaya ambayo yamo katika jamii yetu," alisema Askofu Salalah.
Pia, aliongeza kusema, "Hata Bwana Yesu Kristo aliwataka wanafunzi wake wawe chumvi yaani, wawe mfano bora kwa wengine. Sasa, ikiwa Kanisa litapoteza ladha yake au nuru yake kwa maovu hayo na likasema liko neutral(katikati), hali itakuwa nzuri kweli?"
Askofu huyo aliwataka Wakristo kuishi katika ulimwengu kwa maadili yanayompendeza Bwana kwa kuwa wao si wa ulimwengu, bali ni watu wa Mungu.
Akiongea katika ibada ya kubariki watoto wadogo zaidi ya 20, Mchungaji wa Kanisa hilo, Rubeni Ng’wala, aliwataka wazazi kote nchini kuwalea watoto wao katika misingi ya maadili mema.
Alisema ni wajibu wa kila mzazi kumlea na kumuelekeza mtoto wake katika matendo ya Bwana kwani wakifanya hivyo, watakuwa wamewaepusha na maovu mengi ambayo huwa rahisi kwa mtoto kuyasikia.
"Ukimlea mtoto wako katika njia za Bwana, utakuwa unamuepusha na vitendo viovu vinavyotokea katika jamii yetu kwani watoto hao huweza kuviona vitendo vibaya au kuvisikia katika video na redio na hata katika baadhi ya magazeti," alisema Mchungaji Ng’wala.
Jamii yakumbushwa kuwa upendo siyo hiari
Na Mwandishi Wetu, Tarime
WAAMINI wa madhehebu mbalimbali, wamekumbushwa kuwa upendo kwa jirani siyo jambo la hiari, bali ni Amri ya Mungu inayomtaka kila mmoja kuitekeleza ili auone Ufalme wa Mbingu.
Hayo yamo ndani ya barua aliyotumiwa Paroko wa parokia ya Tarime katika Jimbo Katoliki la Musoma, Padre Mathew Burra wakati wa maadhimisho ya Siku ya Msamaria Mwema.
Akisoma barua hiyo iliyoambatanishwa na ujumbe uliotoka kwa Mwenyekiti wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki (CARITAS-Tanzania), Mhashamu Askofu Agapit Ndorobo, kwa ajili ya siku hiyo, Padre Burra, alisema kuwa ni wajibu wa kila Mkristo na kila mwanadamu kuona kuwa anampenda kwa kiasi kikubwa jirani yake na kuitendea mema jamii nzima.
Ujumbe huo uliotumwa parokiani hapo kupitia kwa Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Justin Samba, ulisema Wakristo hususani Wakatoliki, hawana budi kuwahurumia na kuwasaidia wenye shida mbalimbali.
Pia, ujumbe ulihimiza kuwapa huduma mbalimbali wanazohitaji watu hao walioko katika shida na mateso kwa kuwatunza vema na kuwapa chochote kinachopatikana kwa ukarimu.
Watu wenye shida ni pamoja na wanaokumbwa na majanga mbalimbali wakiwamo wagonjwa wa UKIMWI ambao ni janga linalosababisha watoto wengi kupoteza wazazi na walezi wao na hivyo, kubaki yatima.
Pia, UKIMWI husababisha familia nyingi kubaki maskini kwa kuwa hutumia mali nyingi kuwahudumia wagonjwa.
Wengine ni wagonjwa wasiojiweza, walemavu, waliofikwa na majanga kama njaa, mafuriko na ajali mbaya zikiwamo zza moto.
Kwa mujibu wa mazungumzo ya Paroko, ujumbe huo uliwahimiza watu binafsi, familia, jumuiya ndogondogo za Kikristo, vikundi mbalimbali na vyama vya kitume, kuendeleza moyo wa ukarimu kwa wahitaji waote.
Padre Burra, alisema kuyafanya matendo hayo si tu kwamba kunadhihirisha ukomavu wa kiimani hasa Kikristo, bali kunaivuta huruma ya Mungu kuwarudia wanadamu zaidi.
Kisiwa cha Mafia chagubikwa na nderemo
Na Padre Andrew Luanda, Mafia
JIMBO Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, limeadhimisha kwa furaha na shangwe kilele cha sherehe za Msalaba wa Jubilei katika parokia ya Mafia iliyopo ndani ya jimbo hilo.
Sherehe hizo zilizofanyika Siku ya Kutukuka kwa Msalaba (Septemba 14), ziliongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mhashamu Method Kilaini.
Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa pia na wageni kutoka Ujerumani, jozi 15 za wanandoa na ndoa mpya 4, zilifungwa na kubarikiwa siku hiyo.
Sherehe za kutukuka kwa Msalaba Kisiwani Mafia, zilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo walei, mapadre na watawa.
Kabla ya kuanza kwa Misa ya Msalaba saa 11 jioni, kulikuwa na maandamano ya Msalaba wa Jubilei.
Kisiwa hicho cha Mafia kiligubikwa na vigelegele, hoihoi, nderemo na kila aina ya ushangiliaji kuushangilia Msalaba ambao ni ishara ya ushindi na ukombozi kwa wanadamu.
Askofu Kilaini katika mahubiri yake, aliwaasa waamini hao wa Mafia, kujivunia kutembea kifua mbele huku wakijivunia Msalaba ambao ni ishara ya Kristo Mshindi.
Alisema Parokia ya Mafia kupewa kupatiwa Msalaba wake wa Jubilei, huku jimbo zima likitumia Msalaba mmoja na kupewa heshima yakuadhimisha kilele cha sherehe za Msalaba wa Jubilei, ni upendeleo wa pekee na heshima kubwa inayowataka wautumie kweli kuifanya kazi ya Mungu.
Askofu Kilaini aliwapongeza wanandoa hao na kuwahimiza kuishi maisha matakatifu ya ndani ya Sakramenti ya Ndoa na akasema hayo yanawezekana kutokana na nguvu za Msalaba.
Kivutio kikubwa kilikuwa kurudia ahadi ya ndoa iliyofungwa kanisani hapo miaka 34, iliyopita.
Askofu aliwasifia waamini wa Mafia kwa juhudi wanazozifanya kujiletea maendeleo chini ya uongozi wa Paroko Padre Beno Kikudo.
Wakati huo huo: Idara ya CARITAS parokiani hapo chini ya ya uongozi wa Sista Alexander, imeanzisha miradi ya kilimo na maji.
Wamenonite wasema: Tunataka kiongozi aliye na dini siyo udini, ukabila
Na Christopher Gamaina, Tarime
WAKRISTO nchini wameshauriwa kumwomba Mungu awachagulie kiongozi bora ambaye ni mcha Mungu wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao, atakayekuwa tayari kuyasikiliza matatizo ya umma na kuyatafutia ufumbuzi.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya Uchaguzi Mkuu ujao, Mchungaji Chris Kateti wa Kanisa la Mennonite, Parishi ya Tarime alisema, "Hata kama kwenye kura yako utakuwa umempigia mgombea wa chama hiki, kisha akachaguliwa na chama kile, basi elewa huyo ndiye uliyemwomba Mungu akuchagulie." Alisema Mchungaji Kateti na kuongeza,
"Tunahitaji kiongozi aliye na dini lakini asiwe na udini katika uongozi wake. Asitumie dini yake kuongoza mwananchi. Aongoze bila upendeleo bila kujali au kuangalia dini, chama au kabila," alisema.
Aliwataka watu wasirubunike kuuza kura zao kwani mbali na kupoteza haki zao, za kidemokrasia, pia ni kufanya hivyo ni kutenda dhambi.
Mchungaji huyo wa kanisa la Menonite katika mazungumzo hayo ya hivi karibui alisema hata kwa kiongozi au mgombea yeyote anayetegemea kununua kura ili achaguliwe, ni dhahiri anajijua hafai na si mcha Mungu.
Aliwataka wananchi wote kuhudhuria mikutano ya kampeni ili kuwasikiliza kwa makini wagombea, kuwahoji na hatimaye, waweze kuwang’amua walio bora.
Mchungaji huyo aliwataka wagombea kueleza sera zao waziwazi ili wananchi wenyewe wapate nafasi ya kuwachambua, wajue "pumba na mchele" na pia, wagombea wasikubali kuona wanachama wao wakifanya fujo.
Alisema kitendo cha kiongozi wa chama chochote awe mgombea au la, kufumbia macho vurugu wakati wa kampeni, kinaashiria kuwa kiongozi huyo si mpenda amani na atakapo chaguliwa, nchi itakuwa katika vurugu na kukosa amani.
"Sisi kama Kanisa, tunapenda kuona amani, utulivu na haki vikifanyika katika Uchaguzi Mkuu wa 2000. Tunapenda kuona viongozi watakaochaguliwa wanasimamia haki na kulinda Katiba ili kuleta maendeleo nchini," alisema Mchungaji Kateti.