Tusimwonee haya Dk. Salmin atuingize kwenye janga
Na Arnold Victor
ILIANZA kama utani na uzushi lakini sasa imekuwa kweli na hatari. Taarifa zilipoanza kuvuja, Rais wa Zanzibar Dk Salmin Amour alikana kwamba anaendesha mikakati ya kuibadili katiba ya Zanzibar ili aweze kugombea tena Urais visiwani humo. Lakini sasa kila kitu kiko wazi kwamba Dk. Salmin amedhamiria kubomoa kiota kinachomhifadhi.
Wenye haraka wanaweza kusema pengine amepania kufufua na kuuenzi Usultani wa aina yake ndiyo maana katika maadhimisho ya Mapinduzi Januari 12, mwaka huu alitangaza kumsamehe Sultani wa zamani wa Zanzibar aliyepinduliwa mwaka 1964.
Narudia tena kusema kwamba kila hali inaridhisha kwamba Dk. Salmin na mashabiki wake, pengine kwa kujikomba tu, wameazimia kwa dhati kubomoa misingi ya kuheshimu Katiba kama sheria mama ya nchi, misingi iliyojengwa na kulindwa kwa nguvu zote na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Siwezi kushawishika nikubali kwamba Dk. Salmin, CCM na viongozi wake hawajui ukweli kwamba Rais anapaswa kuongoza kwa mujibu wa Katiba na wala si Rais kuiongoza katiba kwa kufuata vionjo vyake binafsi. Kufanya hivyo ni kuua kabisa nguvu ya katiba na hivyo kuporomosha mfumo mzima wa utawala wa sheria na demokrasia.
Sababu zinazotolewa na wanaodai Katiba ya Zanzibar ibadilishwe ili kutoa fursa kwa Rais kuweza kugombea Urais kwa vipindi zaidi ya viwili ni kwamba eti ni Dk. Salmin pekee anayeweza kuwania Urais huko Zanzibar na kushinda na kwamba hakuna kiongozi yeyote anayefaa kuwa Rais wa Zanzibar isipokuwa Dk. Salmin!
Ikiwa CCM inakubaliana na dhana hii, basi hakuna ubishi kwamba CCM kama chama hakipo kabisa huko visiwani kwa sababu chama ni sera na wala si mtu. Chama chochote cha siasa kinadaiwa kunadi sera zake kwa wananchi ili wakizipenda wakichague na ikiwa chama kitategemea kunadi watu badala ya sera, basi kimekufa kwa vile binadamu ni kama ua ambalo leo lachanua na kesho lanyauka na kukauka.
Lililo wazi na dhahiri ni kwamba popote pale watawala wanapojaribu kwa namna yoyote kuwaaminisha watawaliwa au kuwalazimisha wakubali kwamba pasipo wao, mambo yote yatakwenda kombo, mbegu ya udikteta inakuwa imeshachipua na ikiendekezwa mwisho wake kamwe hauwezi kuwa mwingine ila maafa. Alama moja ya dikteta yeyote ni kutokujenga misingi endelevu ya inayoweza kuwaongoza watu hata pale ambapo yeye hayupo. Kwa mfano, baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere Oktoba, mwaka jana, Rais Mkapa, aliwatoa hofu Watanzania kwamba hakuna litakaloharibika kwa vile misingi aliyoijenga Baba wa Taifa kwa nchi hii itaifanya iendelee kuwa imara hata bila yeye kuwapo. Hiyo ndiyo misingi ambayo Watanzania wanapaswa kuienzi na kuilinda hata kwa damu, na si kujenga mfumo wa tamaa ya kudumu ikulu milele kwa manufaa binafsi.
Ni hatari kuanza kujenga msingi wa watawala kutumia madaraka waliyo nayo kubadili katiba ili ikidhi matakwa yao binafsi.
Hatua hii ya sasa si ya kwanza kufanywa na Serikali ya Dk. Salmin. Alianza zamani, lakini kwa bahati tulikuwa naye Mwalimu Nyerere ambaye aliweza kumdhibiti na kumkemea. Leo hii nina mashaka kama ndani ya CCM kuna anayeweza kumnyooshea kidole Komandoo Salmin na akamuweza.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 1995 yaliwekwa masharti visiwani humo kwamba mtu ambaye hajakaa katika eneo moja kwa miaka mitano mfululizo asiruhusiwe kupiga kura. Lengo la mpango huu lilikuwa kujaribu kuwadhibiti Wazanzibar walioko nje ya visiwa hivyo na wazawa wa Pemba waishio Unguja wakiwemo wanafunzi wasiweze kushiriki katika Uchaguzi huo kwa hofu kwamba wangeongezea upinzani kura.
Hatua hii ya sasa pamoja na hatua nyingine nyingi zinazoonyesha ubabe ambao Dk. Salmin amekuwa akichukua zinaonyesha kwamba ili Muungano uweze kudumu inabidi CCM nzima na Serikali ya Muungano zikubali kutawaliwa na mawazo ya Rais huyu wa Zanzibar na wala si Katiba iwe ya Jamhuri, ya Zanzibar wala ya CCM yenyewe, ikiwa haiwezekani kuchukua hatua za kijasiri za kumdhibiti. Ni Salmin huyu ambaye Mwalimu Nyerere alimfananisha na mbogo, ambaye anapocharuka wana-CCM wanashindwa kumdhibiti. Vitendo vya Dk. Salmin vinatia mashaka kwamba Uchaguzi Mkuu ujao utakuwa wa haki, kwa vile inaonekana Komandoo yuko tayari kufanya lolote mradi arudi madarakani, kwa imani kwamba bila yeye hakuna Zanzibar.
Najua kwamba wakati mwingine viongozi wa CCM wamelazimika(kama ilifaa kulazimika) kumuachia Komandoo Salmin afanye baadhi ya mambo yasiyokubalika ili tu kuunusuru Muungano. Kwa mfano wakati hakuna popote katika katiba ya Jamhuri wala ile ya Zanzibar panaporuhusu kuwepo kwa Maamiri Jeshi wawili, Dk. Salmin amekuwa akipigiwa mizinga 21 na Jeshi kana kwamba yeye ni Amiri Jeshi. Kikatiba Tanzania inaye Amiri Jeshi Mkuu mmoja ambaye ni Rais wa Jamhuri.
Zanzibar imekuwa ikidai iwe na utambulisho (identity) wa peke yeke kimataifa kama taifa, jambo ambalo haliingii kichwani kwa vile hata nchi kama Amerika ambazo ni muungano wa "nchi" 50, zinao utambulisho mmoja tu kimataifa; wimbo mmoja wa taifa, bendera moja, Rais mmoja anayetambulika kimataifa na kadhalika, mambo ambayo ndiyo yanayojenga umoja halisi wa kimuungano. Haya yote ni mambo ambayo Zanzibar haiyataki, lakini msingi wake mkuu ni vigumu kuutenganisha na tamaa ya ukubwa na kile wakiitacho vijana "ujiko"-yaani mbwembwe. Naamini kwamba sasa wakati umefika wa kutoogopana na badala yake ukweli usemwe, utetewe na ulindwe kwa gharama yoyote, kwa nia ya kujenga misingi ya haki na amani ya taifa letu, sasa na siku zijazo.
Kutambaa mapema huleta faida
Afya ya mtoto hujengwa tangu anapokuwa katika hali ya mimba. Katika mfululizo wa makala kutoka kitabu cha " Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo" cha Shirika la Uchapishaji wa Lugha za Kigeni la Beijing, China baada ya kuwaletea miiko 15, wanayopaswa kuwa nayo akina mama wajawazito, leo tunaendelea na kutambaa mapema kwa mtoto kunavyoleta faida kama ilivyoelezea wiki iliyopita sasa endelea..
Swali la pili siyo jambo rahisi.
kwa kuwa ni shida kwa watoto wanaonyonya kupokea chakula cha kawaida, pengine watoto hao watapata ugonjwa wa kutoweza kusaga chakula vizuri, kuvimbiwa, au kutopenda kula kabisa. Hii ni sababu ya uzuiaji wa utendaji kisaikolojia au ni sababu ya moyoni, kama vile neva fulani kuchukia jambo ambalo na kukataa kufanya kazi.
Kwa mtoto anayenyonya maziwa ya mama huachishwa maziwa kuanzia wakati huo.
Katika mwaka uliopita kunyonya maziwa ya mama ni kiungo cha kupelekeana hisia kati ya mtoto na mama, naye huona usalama moyoni mwake. Anapoachishwa kiubgi hicho atafadhaika, hivyo atashikwa na wasiwasi kwa kuachana na mama yake.
Wasiwasi huo unasababisha kilio na uchokozi .
Wakati huo wazazi wasiwe na wasiwasi, bali wajue namna ya kutanzua swali hilo.
Mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja anaruhusiwa kulia na kufanya uchokozi, katika hali ya namna hii watu wazima inawabidi wamtunze vya kutosha ili kuondoa wasiwasi wake.
Kama mtoto amekuwa mwema sana bila kufanya uchokozi, inatupasa kuwa naye karibu zaidi.
Kwa kuwa silika hii hailingani na tabia ya saikolijia ya mtoto mchanga mwenye umri wa mwaka mmoja. kwa hivyo, baada ya mtoto kuachishwa kunyonya, tunamfundisha kuwa ma moyo wa kujitegemea ili kumsaidia apige vizuri hatua ya kwanza ya kuyakabili maisha.
Kwa desturi, watoto wachanga wenye umri wa mwaka mmoja hivi huanza kujaribu kusimama dede na kutembea.
Kutoka kukaa kitako hadi kusimama wima watoto hawa huona duania yake imebadilika.
Kwa kutembea wanaweza kuangalia dunia kutoka upande wowote. Kwa hiyo kipindi hichi ni fursa nzuri kwao kuchipuza uwezo wa akili, wazazi wanaweza kucheza na watoto kwa kutumia picha na vitu vingine.
Zaidi ya hayo, kutembea kunaweza kufanya watoto wachanga kuona na kugusa vitu vingi ambavyo hawajawahi kuviona tangu zamani, wazazi wanapaswa kutumia nafasi hii kupanua maeneo yao ya ujuzi wa utambuzi wa mambo.
Watoto wenye umri wa mwaka mmoja hivi wanaanza kujaribu kusema, ingawa mwanzoni wanasema silabi moja moja, lakini jambo hilo linamaanisha kwamba wameagana na kipindi cha ububu na kuonyesha hisia zao kwa kutumia kilio au kicheko. "Lugha ni chombo cha watu wanachotumia kwa kubadilishana maoni na kupelekeana hisia".
Wazazi wanapokuwa pamoja na watoto wanapaswa kujua namna ya kutumia lugha ya watoto kubadilisha maoni na kupelekeana hisia. Watoto wachanga wanahitajiwa kujifunza kutumia maneno wanapotaka kujisaidia na kula chakula.
Ni jambo la kawaida kwa watoto wachanga kujaribu kusema, lakini ni kazi ngumu kwa wazazi kujua namna ya kutumia vizuri lugha ya watoto.
Tunaposheherekea siku ya kuzaliwa kwa watoto kwa mwaka mmoja, hatuna budi kufahamu maana ya umri wao.
Mtakatifu Adelaida: Mwanamke aliyeandamwa na mikosi
Na Joseph Sabinus
Yule mwanae wa kambo Mfalme mpya akamtimua na kumlazimisha ahame; aondoke ikulu
Adelaida wa Burgondia aliyezaliwa mwaka 931 akiwa mtoto wa mfalme wa nchi ya Burgondia ambayo siku hizi ni sehemu ya Ufaransa, ni mwanamke ambaye maisha yake yanashangaza, huhuzunisha na hata hudhihirisha kuwa si wote wenye vyeo na mali kuwa na raha.
Maisha yake yanatudhihirishia bayana kuwa hao nao wanayo matatizo makubwa; ya mambo mbalimbali yanayowakabili. Tena pengine kutokana na mali na vyeo vyao , labda wana misukosuko mingi inayowafanya wayaone maisha yao kuwa ni magumu na ya tabu kutokana na kutendewa vibaya na watu mbalimbali kutokana na sababu kadhaa na hata pengine kwa makusudio ya Mungu.
Kwa kadri ya mila za wafalme wa zama zile, Adelaida aliyefariki akiwa na miaka miwili tu toka kuzaliwa kwake.
Hata hivyo licha ya maafikiano,Adelaida aliolewa na mfalme wa Italia akiwa na umri wa miaka kumi na sita .Lakini ,mfulululizo wa matesowa mikosi na bahati mbaya nyingi ulianza kumuandama haraka haraka.
Tunasema hivi kwani inaelezwa kuwa haukupita muda mrefu tangu kuolewa kwake,Adelaida baada ya kuendelea na "cheo" chake cha MKE WA MTU akabadili jina na kuitwa MJANE baada ya kufiwa mmewe.
Lakini kibaya zaidi,Adelaida alifungwa ngomeni na mfalme mpya.
Ni bahati kuwa baada ya miaka mitatu,Otto aliyekuwa mfalme wa Ujerumani alifanya jitihada kubwa kumuokoa na kisha akafanikiwa kumuoa Adelaida.
Mfalme huyo aliyekuwa pia mjane mwenye mtoto mmoja baada ya kufiwa na mke wake, alimuoa Adelaida akiwa na umri wa miaka Ishirini sasa.Wakazaa watoto watano.
Ingawa uhusiano kati ya mtakatifu Adelaida na mtoto wake wa kambo haukuwa mzuri walau miaka hii ilikuwa ya heri kwa Adelaida kwani alipendwa na raia zake baada ya kuhangaika muda mrefu.
Hakuna marefu yasiyo kuwa na ncha; na hivyo huo haukuwa mwisho wa mikosi ya Adelaida. Heri na unafuu wa masumbuko katika maisha yake ilikoma ghafla mumewe alipofariki na yule mtoto wa kambo kuwa mfalme mpya.
Yule mwanae wa kambo Mfalme mpya akamtimua na kumlazimisha ahame; aondoke ikulu.
Lakini wakosanao ndio wapatanao. Ni kweli maana baada ya muda kidogo, wawili hao yaani mama na mwana wa kambo wakapatana na kurudiana katika mahusiano mema kabisa.
Siku ya kifo cha nyani; miti yote huteleza na ndiyo maana hata ng'ombe wa maskini hazai, akizaa anazaa dume.
Uhusiano baina yao haukudumu muda mrefu kwani mfalme mpya yaani mtoto wake wa kambo alifariki dunia. Mke wa Mfalme huyo aliposhika utawala wa nchi hiyo, alimchukia kabisa mama mkwe wake (Adelaida) na hakuwa akitaka kabisa kumuona katika mboni za macho yake. Hali hiyo ikamfanya kwa mara nyingine Adelaida alazimishwe kuondoka na kwenda mbali.
Hata hivyo kifo cha ghafla cha malkia huyo kikawa 'tiketi isiyolowa' kwa Adelaida kurudi ikulu; sasa akiwa na miaka sitini.
Sasa akakabidhiwa hiyo iliyomzidi nguvu hasa ukizingatia ile tabia yake ya upole.
Mungu akamsaidia akajitahidi kwa kadri ya uwezo wake; akifanya yote aliyoweza kwa kadri ya vipaji na uwezo wake kwa ajili ya raia wake.
Kidini, Mtakatifu Adelaida alijenga nyumba nyingi kwa ajili ya wamonaki na watawa akiwasihihi maaskofu kuwafundisha na kuwaongoa waliokaa mipakani mwa Mashariki ambao mara kwa mara walikuwa wakihatarisha amani.
Mbali na magumu hayo aliyoyavumilia kwa muda mrefu, shughuli nyingi alizokuwa nazo zilimdhoofisha hata akafariki dunia Desemba 16, mwaka 999 na tarehe hiyo ndiyo Kanisa linamkumbuka Mtakatifu huyo.
Akiishi katika mazingira ya ikulu ya mfalme kabla ya kifo chake, daima Mtakatifu Adelaida aliulinda moyo wake wa kidini, ulimfanya ayavumilie kishujaa magumu mengi toka kwa ndugu zake na maumivu mengine.
Licha ya hayo, Mtakatifu Adelaida ambaye uvumilivu wa mateso na chuki zilizomuandama ni somo kubwa kwetu wanadamu wa sasa kusimama imara kwenye imani na kutokata tamaa, aliwapenda watu na kubaki kuwa mtu mwema na mpole.
Alipendwa na watu walioiona mifano mingi ya upendo wa kidugu.
Makaburi yenye uwezo wa kugandisha maziwa au mvinyo
Na Ignatio Obuombe
JE kuna uhusiano gani kati ya harufu ya binadamu aliyekufa na maziwa au mvinyo? Je harufu hiyo yaweza kupelekea maziwa na mvinyo kuganda?.
Jumba la Makumbusho lililo chini ya ardhi ndani ya mfereji mkubwa kabisa ulioko kando ya mto Seine ni mashuhuri sana jijini Paris na pia lina mambo ya kushangaza.
Unapotembea ndani ya mfereji huu uliobatizwa jina la Musee des Egouts kwa Kifaransa au jumba la makumbusho la mifereji kwa kiswahili, mwishoni mwake kabisa unakumbana na mrundiko wa mafuvu na mifupa lukuki ya binadamu walio kufa miaka mingi iliyopita. Watu wengi wanaotembelea mifereji hii jijini Paris leo wanajiuliza mifupa na mafuvu haya yalitoka wapi?
Hakika mifupa hiyo haikutolewa sehemu nyingine mbali isipokuwa hapo hapo jijini Paris katika makaburi ya Kanisa mashuhuri kama Saints Innocents. Yaaminika kuwa baada ya watu kuzikwa kupita kiasi katika makaburi hayo kunako zama za kati mabaki ya watu yaliyotokeza nje kiasi cha kutoa harufu iliyoweza kugandisha maziwa au mvinyo yalitupwa humo.
Jarida la News of World linayaelezea makaburi hayo kwa maneno yafuatayo
"About two million bodies ,stacked sometimes 30 feet deep, had raised the ground level by more than 6 feet. The Cemetery was a breeding ground for infection, and it gave off a putrid smell, said to turn milk or wine sour"
"Zaidi ya miili milioni mbili ilinasa umbali wa futi 30 ndani ya makaburi hayo wingi wa maiti hizo ulipelekea ardhi kutuma na kuinuka zaidi juu kwa futi 6 zaidi maiti zilichomoza nje na kupelekea makaburi hayo kutoa harufu iliyoweza kugandisha maziwa au mvinyo"
Kufuatia harufu kutoka kwenye makaburi hayo kukera na kugandisha vyakula majumbani na kuvipelekea kuchacha wananchi walilalamikia kanisa lililoyamiliki ili yafungwe.
Lakini malalamishi yao yaligonga ukuta kwa sababu kanisa ilikuwa ikijiingizia pato kubwa ya maiti kwenye makaburi yake.
Kuongezeka kwa maiti kwenye makaburi hayo kulianza mwaka 1418 wakati ugonjwa wa mkumbo wa Black Death uliopelekea vifo vingi sana nchini Ufaransa. Katika mwaka huo huo maiti zipatazo 50,000 zilizikwa katika makaburi ya Saints Innocent
Ulipofika mwaka wa 1572 maafa mengine yaliikumba Ufaransa yaliyoitwa Saints Bartholomew's Massacre mauaji hayo yalikumba maelfu ya Wafaransa ambao nao pia wakuja kuzikwa kwenye makaburi hayo hayo ya Saint Innocent.
Mwaka 1780 makaburi hayo baada ya kuelemewa na maiti yalipasuka.
Miili ya mamilioni ya watu waliozikwa hapo ikatapakaa kwenye mitaa ya jiji la Paris, kwa sababu makaburi hayo yalikuwa yapo katikati ya jiji.
Ndipo Kampeni ya kukusanya mabaki ya watu ilipoanza kwa miezi 15 usiku na mchana mifupa na mafuvu yalikusanywa. Baadhi ya mabaki hayo ya binadamu yalirundikwa ndani ya mfereji mkubwa wa chini ya ardhi ambao sasa umegeuzwa jumba la makumbusho.
Leo ukiembelea mfereji huo ulio jijini Paris unapofika mwishoni mwake utakutana na mifupa na mafuvu yaliyowekwa kwa kupangwa katika umbo la msalaba.
Unapoyataza yanakukumbusha miujiza. Je, haishangazi ya harufu ya maiti kugandisha maziwa na mvinyo?!
Wamfahamu aliyekuwa wa kwanza kukwea kilele cha mlima mrefu kupita yote duniani?
l
Alifikia kilele hicho Mei 29Na Mwandishi Wetu
EVAREST ndio kilele cha mlima ulio mrefu kupita yote duniani. Kilele hiki kipo kwenye safu ya milima ya Himalaya.
Ukiwa na urefu wa futi 29,002 kwa miaka mingi katika karne iliyopita watu mbalimbali walijaribu kuweka historia kwa kutaka kufikia kilele cha mlima huu mrefu kupita yote duniani lakini wasiweze.
Mwaka 1921 Howard Bury pamoja na wenzake walijaribu bahati yao kwa kukwea mlima Evarest wakitokea upande wa Kaskazini mwa milima ya Himalayas.
Mwaka uliofuata wa 1922 Jenerali Bruce pamoja na kundi lake nao pia walifunga safari kuelekea kilele cha mlima wa Evarest na wasifike walikofika akina Bruce. Umbali wa urefu ambao Jenerali Bruce na wenzake waliweza kukwea na kufikia ilikuwa ni futi 27,000 na hawakuweza kusogea zaidi ya hapo.
Walipojaribu tena waliishia njiani,. moja ya vikwazo walivyokabiliana navyo wakati wa kukwea Evarest vikiwa ni upepo mzito uliovuma kutoka Kusini Magharibi mwa mlima huo.
Upepo huo ulipoanza kuvuma majira ya mwanzoni ya kiangazi, hewa ya unyevunyevu ilipelekea kuwapo kwa theluji nyingi sana iliyodondoka sehemu za kando kando mwa mlima huo. Sehemu ambazo awali zilikuwa salama ziligeuka kuwa za hatari. Wakati Jenerali Bruce alipojaribu safari ya pili ni wenzake 9 ili kukwea na kufikia kilele cha mlima huo mrefu, watu saba miongoni mwao walifariki kwa kuangukiwa na theluji.
Mwaka 1924 Bw. Somervell na Bw. Norton walijaribu bahati yao na kufanikiwa kuukwea "Everest" kwa futi 28,200, lakini wote baridi kali iliwasababishia kuugua sana. Wawili miongoni mwao Bw. Mallory na Irvine na watu wengine wawili katika kundi hilo walijaribu kuendelea kukwea zaidi na walipotelea juu ya mlima huo mrefu na hawajaonekana hadi leo nikiandika makala hii.
Kundi jingine lilijaribu tena safari tatu kukwea mlima huo hadi kileleni na likashindwa. Baadaye vita vya pili vya dunia na vile vya kwanza vilifumuka. Vita vilichangia kuchelewesha harakati za wapanda milima kutaka kutimiza azma yao ya kufikia kilele cha Evarest.
Mwaka 1951 Bw.Shipton aligundua njia ambayo ingeliwezesha kufika kileleni hasa ukitokea upande wa Kusini mwa mlima huo. Watu wote ambao juhudi zao za kufika kileleni zilishindwa walijaribu kukwea wakitokea upande wa Kaskazini, ndipo kundi toka Uswisi lilijaribu kwa kutumia njia hii mpya iliyogunduliwa upande wa Kusini nalo likashindwa.
Kwa takribani miaka 30 juhudi zote zilizofanywa kufikia kilele cha Evarest hazikuzaa matunda. Mwaka 1953 kundi jingine lililoongozwa na John Hunt lilijaribu nalo laikini lilikwamishwa njiani na hali mbaya ya hewa iliyopelekea kuugua hovyo.
Biblia husema "kila jambo na wakati wake", ilipofika Mei 29, 1953 historia iliwekwa. Katika kundi hilo la Hunt watu wawili miongoni mwao, Hillary na Tensing waliagana na wenzao majira ya saa 6:30, ili wapate kujaribu kukwea sehemu ya mwisho kufikia kilele, sehemu iliyoshinda wengi. Saa tano walizotumia toka walipotengana na wenzao Hillary na Tensing walikuwa wamesimama kwenye kilele cha Evarest. Historia ya kufikia kilele cha Mlima mrefu kuliko yote duniani ikawa imewekwa.
ZIJUE IMANI ZA WENGINE
Wajaluo wanachoamini juu ya wafu
Na Ignatio Obuombe JR.
PANDE zote za kijiji zimetawaliwa na milio ya ngoma, filimbi na parapanda. Watu waliojikwatua kwa rangi mbalimbali usoni huku wakiwa wamevalia ngozi za wanyama, pembe na kufunga njuga miguuni wanacheza kwa midadi.
Milio hiyo ya ngoma husindikizwa na wanenguaji wanaocheza kwa kufuata midundo,. mikononi wakiwa na mkuki na marungu ambayo wanakimbia nayo wanapopandwa na mori na kuirusha hatimaye huiokota huku wakijigamba kwa kutaja majina yao yote ya ukoo na kutoa maneno ya kujitapa.
Mbwembe zote hizi hufungwa huku watekelezaji wake wakiswaga ng'ombe ambao ni sharti wakapite na kukanyaga juu ya kaburi la mmoja wa wanaukoo aliyekufa.
Watu hawa hutumia kutwa nzima kuyafanya hayo katika maeneo ya makondeni wakiwa na mifugo. Majira ya alasiri hurejea nyumbani kwa marehemu kwa mbwembwe zote za kutambika katika makaburi ya wanaukoo.
Hiyo ndiyo "Teroburu" sherehe ya matambiko ya asili iliyo mashuhuri sana miongoni mwa jamii ya Wajaluo kiasi cha kupelekea jamii kujiliza, je, Wajaluo wanaabudu wafu?
Kwa kawaida matambiko ya "Teroburu" hufanyika juma moja toka kufariki kwa marehemu. Ikiwa marehemu ni kijana, wanaoshiriki kumtambikia mwanamke ni wanawake wenzake na ikiwa ni mtu mzima watu wazima wenzake.
Ng'ombe wa kafara anayechinjwa siku hiyo huitwa Dher Alap na hutolewa na mmoja wa wazee wa makamo na wenye busara katika jamii.
Nyama ya ng'ombe huyo akishachinjwa hugombaniwa na waliohusika katika tambiko na mara nyingi wababe peke yao ndio huambulia nyama iliyonona na baadhi kukosa kabisa kwa sababu usipokaa sawa wakati wa kuigomabania unaweza hata ukakatwa panga.
Wajaluo wana imani kuwa mtu akifa halafu asifanyiwe matambiko hayo basi, roho yake itarejea duniani na kuleta balaa katika jamii yake. Na kama marehemu akifanyiwa matambiko ya Tero Burn, wanaamini kuwa roho yake itarejea duniani na kuwabariki wahusika.
Mara nyingi kumezuka migogoro na mivutano baina ya Wajaluo walioongoka na kuwa Wakristo na wale wanaoshikilia mila za matambiko pale wanapolazimisha Wajaluo Wakristo kushiriki matambiko hayo ya Tero Buru .
Wajaluo wanaoshikilia mila hizo huweza pia kumshurutisha mtu anayedai ameokoka au Mkristo awatolee ng'ombe wa kafara na hapo huwa kwa njia moja ama nyingine wamempelekea mtu aliyeleta ubishi kushiriki matambiko hayo kwa kutoa ng'ombe wa kafara, akikataa huhesabiwa kwamba ametengwa na ukoo.