Magazetini Wiki Hii

Sijutii kukacha Muungano -Cheyo

Tanzania Leo Julai 13

MWENYEKITI wa Chama cha United Demecratic Party (UDP) Bw. John Cheyo, amesema ajutii uamuzi wa chama chake kujitoa katika muungano wa vyama vya upinzani vyenye lengo la kumsimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya Urais wa Jamuhuri katika uchaguzi mkuu ujao.

Cheyo alitoa kauli hiyo jijini jana katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MALEZO).

Cheyo aliwaambia waandishi wa Habari kwamba ilikuwa ni lazima UDP ijiondoe katika muungano huo kulingana hali jinsi ilivyokuwa.

Akitoa sababu zilizofanya UDP ujitoe Cheyo alisema kwamba hiyo ilitokana na kukithiri kwa sera zinazoshabikia udini na ukabila katika baadhi ya vyama viivyotaka kuungana.

"Sera ya jino kwa jino ndiyo chanzo kikubwa cha UDP kujiondoa kwenye muungano baina ya CHADEMA na CUF", alisema Cheyo.

Tanga wadanganywa Mrema karudi CCM

Majira Julai 12

WANANCHI wa Kijiji cha Churwa kilichopo tarafa ya Maramba mjini hapa juzi walimshangaa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Bw. Agustine Mrema akiwa anatangaza sera ya Chama hicho kufuatia wananchi hao kuwa na habari kwamba kiongozi huyo amerudi Chama cha Mapinduzi.

Wananchi hao walimshangaa Bw. Mrema aliyekuwa na mkutano wa hadhara kijijini hapo kutokana na habari walizoelekezwa na viongozi wa vijiji wa CCM kuwa Mwenyekiti huyo amerejea CCM kujinusuru na kesi zinazomkabili.

Mshangao huo uliamsha hali ya wananchi na kumshangilia Bw. Mrema kwa kuimba nyimbo za kuikejeri CCM huku wakirukaruka na kumtaja kuwa ni Rais wao na Milenia.

Maiti wakutwa wakielea Ziwa Victoria

Majira Julai12

MAITI wawili wanaume ambao hawajatambuliwa wakiwa wameharibika wamekutwa wakielea katika Ziwa Victoria kwenye mwalo wa Mwinga ulio kati kati ya Rubafu tarafa ya Mugabo wilaya ya Bukoba Julai 9 mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Bw. Eliyuko Elihaki aliwambia waandishi wa habari jana kuwa maiti hao waligunduliwa na mwenyekiti wa kijiji cha Rubafu Bw. Eleeza Kashaga.

Mkuu wa Wilaya Bukoka Bw. Mussa Changa aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa maiti hao ambao walishindikana kutambuliwa, mmoja alikuwa ni kijana anayesadikiwa kuwa na umri wa miaka 25, alikuwa amevaa suruali aina ya jinzi na fulana ambako katika mifuko yake alikutwa na sh. 4,200 na wa pili alikuwa ameliwa upande.

Mkuu wa Wilaya aliwashukuru wananchi wa eneo hilo kwa uaminifu wa kutunza fedha zilizokutwa katika mifuko ya marehemu, na akaamuru zitumike kununulia sanda kwa ajili ya kuwazika maiti hao.

Alichowaahidi Mkapa Polisi ni sawa na Hongo - CUF

Mtanzania Julai 14

CHAMA cha CUF kimedai kwamba serikali inajaribu kuwahonga polisi ili waipendelee CCM katika uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Wilfred Lwakatare alisema kwamba kitendo cha Rais Benjamin Mkapa kuahidi kuwa atawaongezea posho polisi wakati tunaelekea kwenye uchaguzi Mkuu ni hatua ya kuwarubuni ili walipendelee CCM.

"CCM inatafuta mbinu za kushinda kirahisi kwa kuwarubuni polisi ili wakipendelee chama hicho kwenye uchaguzi mkuu alikuwa wapi muda wote huo hadi anasubiri uchaguzi ukaribie, ndipo atoe ahadi hizo?" Alihoji Lwakatare.

Alisema kitendo hicho cha Mkapa kuwapa matumaini polisi ni hatua ya kuwatisha na kuwaogofya wananchi ili waipigie kura CCM katika uchaguzi mkuu ujao wa madiwani, wawakilishi, wabunge na Rais.

Mwanamke mbaroni kwa kumuua mumewe

Mtanzania Julai 14

MWANAMKE mmoja, Mwatatu Mohamed (25), mkazi wa Wilayani Kiteto, Mkoa wa Arusha, amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mumewe kwa kumpiga na fimbo kichwani.

Kamanda wa polisi Mkoani Arusha Alfred Tibaigana alisema jana ya kuwa, mtuhumiwa huyo alimuua mume wake aliyemtaja kwa jina la Bakari Juma (30), kufuatia ugomvi baina yao uliodaiwa ulitokana na wivu wa kimapenzi kati ya wapenzi hao.

Alisema, kabla ya mauaji hayo kutokea Jumamosi wiki iliyopita katika kijiji cha Machinga walipokuwa wanaishi kulizuka mabishano na hatimaye ugomvi ndipo mtuhumiwa alipompiga mume wake huyo kwa kutumia fimbo na kufa papo hapo.

"Upelelezi wa awali umebaini, Kifo cha marehemu kilisababishwa na kupigwa na fimbo kichwani, lakini tunapeleleza zaidi kujua ugomvi ulitokana na chanzo gani" alisema.

Hata hivyo alisema mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa na polisi wakati akisubiri kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma ya mauaji.