Kanisa lataka wagombea wafanye kampeni kwa adabu

lLasema mbwembwe,matusi jukwaani havisaidii jamii

l'Wananchi wanataka sera sio matusi, taarabu na matarumbeta'

Na Josephs Sabinus

KANISA Katoliki limewataka wagombea viti vya urais, ubunge na udiwani, kuendesha mikutano ya kampeni kwa kuzingatia adabu na uadilifu na pia, limewataka wananchi kukomaa kwa kutowachagua wagombea wasio na adabu hata wanapokuwa jukwaani kuomba kura.

Akizungumza na KIONGOZI mwanzoni mwa juma juu ya hali ya kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao nchini, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Amedeus Msarikie, alisema inashangaza hivi sasa mikutano mingi ya kampeni imetawaliwa na matusi, kashfa na vitisho na akawataka wagombea kuepuka kufanya kampeni za namna hiyo kwa kuwa hazijengi isipokuwa, zinavuruga heshima ya Jamii.

Alisema ni aibu kwa mgombea kutoa matusi, au kashfa dhidi ya mwingine badala ya kueleza sera hali aliyoisema inatokana na mgombea au chama kujiingiza katika kinyang’anyiro kabla ya kujiaandaa na kuiva kisera na kisiasa.

"Kampeni bila kujali heshima mbele ya jamii, ni matokeo ya kuwa na sera zisizo wazi na kutokomaa kisiasa. Mbwembwe kwenye kampeni bila kutaja namna ya kutatua matatizo ya wananchi, haitusaidii sisi," alisema Mhashamu Msarikie.s

Alisema kiongozi anayekusanya watu kisha badala ya kueleza sera za chama chake, mapungufu yaliyopo na namna atakavyoyakabili ili kuboresha hali za watu wake, akaanza kutoa matusi, kashfa, matusi vitisho na kuimba hadharani nyimbo zisizo na maadili, anaidharau na halengi kuifanya jamii kazi kwa uadilifu.

Mhashamu Msarikie alisema hata kama mgombea ana mapungufu, mpinzani wake hana budi kumkosoa kwa lugha ya kiungwana na adabu badala ya kutoa matusi tu kwa kuwa ana uhuru na ni mpinzani wake.

"Mfano, mpaka sasa Mkapa ni Rais, kwa hiyo mpinzani wake atakayemkosoa kwa matusi ni yule asiye na adabu na asiye waheshimu wananchi. Wananchi lazima watumie hekima na busara zao kuchagua viongozi waadilifu, wachapakazi na wenye kujali utu. Wananchi wasitishwe na mbwembwe za matarumbeta," alisema.

Wakati taifa linaelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu, baadhi ya wagombea wa urais, ubunge na udiwani wa vyama kadhaa, wamekuwa badala ya kueleza sera za vyama vyao, wanatoa matusi, kashfa na vitisho dhidi ya wagombea wenzao na wapiga kura.

Viongozi wengine katika kuhamamsisha watu kwenye mikutano yao, wamekuwa wakiungana na wahamasishaji wao kuimba na kucheza hadharani nyimbo za taarabu na tarumbeta zisizo na maadili ya Kitanzania hadharani.

Majonzi yaligubika Baraza la Maaskofu

lLapoteza ‘nyota’ ya matumaini

Mwandishi Wetu

JUMANNE asubuhi, kila mmoja katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alionekana mwenye baridi, amejikunyata, hali yake si nzuri na wala si mbaya. Hakuna mgonjwa. Lakini, nini kimewasibu wasinyae na kugubikwa na majonzi huku wakionekana upweke namna hiyo?

Katika hali isiyo ya kawaida, mchana wa siku hiyo simu kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa TEC, zinapigwa katika ofisi mbalimbali ya Baraza hili zikimtaka kila mfanyakazi aende kanisani.

Bila kujua hili wala lile, wafanyakazi wote walielekea kanisani, si wafanyakazi peke yao bali hata watu kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki ambao walikuwa wanashiriki Mkutano wa Idara ya Uchungaji, nao pia waliunganika.

Kila mmoja akiwa ametulia kanisani humo, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura, akainuka na kutaka kusema kitu lakini, kabla hajafanya hivyo, akakumbwa na kigugumizi asichokuwa nacho siku zote.

Uso wa Padre Rutechura ambao siku zote huwa ni wenye furaha na matumaini awapo mbele ya wanaTEC wenzake, siku hiyo ukaonekana kinyume kabisa.

Kila mtu akawa na hamu ya kupata ujumbe kutoka kwa Padre Rutechura, ili ajue amekumbwa na masaibu gani.

Akasema kuwa, kipenzi cha wengi, Padre mcheshi, Padre mwenye huruma, Padre asiye mbinafsi, Padre mkarimu kwa watu wote, Padre mtaalamu wa mambo mengi yakiwamo mawasiliano na mambo muhimu ya kiroho, NORBERT KIJA, sasa eti ni MAREHEMU. Eti amefariki dunia. Huzuni na majonzi tupu.

Ni nani anayemfahamu Padre Kija ambaye hakulengwalengwa na machozi baada ya taarifa hiyo iliyotolewa katika kanisa la TEC?

Kisha, Katibu wa Idara ya Liturjia wa TEC, Padre Julian Kangalawe, akaongoza sala kumuombea Marehemu kipenzi cha watu, Padre Kija.

"Mungu akulaze Mahali Pema Father Kija. Lakini Father, tutakuona lini katika dunia hii? Huzuni tupu, majonzi na upweke.

Gazeti la KIONGOZI, Idara ya Mawasiliano, TEC, Tanzania na Kanisa kwa jumla, wanaamini kuwa ingawa kimwili umewatoka, lakini kiroho uko pamoja nao na wana matumaini mtakutana katika Ufalme wa Mungu kwa kuwa maombi yao kwako ni makubwa, vilio vyao ni vingi na hasahasa wanakiri kuwa ulimtumikia vema Mwenyezi Mungu.

Hivi ni nani hakumjua alivyo kuwa na utani kwa watu wengi? Ukiwa nae unajisikia umekaa pamoja na baba yako, umekaa na ndugu katika Yesu na hasahasa umekaa na Mkristo mwenzako?

Jumatano katika ibaada maalumu ya kumuombea kanisani hapo, kwa huzuni kabisa Padre Lucas Mzuanda akasema kuwa ni wazi hakuna ajuae kifo kitampata wapi na hivyo kila mmoja ajiandae wakati wowote kuingia mbinguni huku akiishi maisha mema na kudumu katika sala.

Kifo cha Padre Norbert Kija, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano wa TEC, na Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hili la KIONGOZI, kimetokea Septemba 19, mwaka huu baada ya kuugua akiwa jimboni kwake Shinyanga.

Baamedi nusura afanyiwe kituko na nyani

lAokolewa na askari magereza

Na Peter Dominic

NYANI dume anayefugwa katika Uwanja wa Maonesho ya Kimataifa wa Sabasaba jijini Dar-Es-Salaam, mali ya kampuni ya Buibui Investiment, amewatoroka walinzi na kumparamia mhudumu wa baa huku akimnyang’anya nguo zote alizovaa.

Tukio hilo la aina yake limemkuta mhudumu huyo wa baa iliyo mkabala na mazizi ya wafugaji hao maarufu wa wanyama wakali na wapole.

Ilikuwa majira ya saa moja za asubuhi mwanzoni mwa wiki wakati mhudumu huyo akichota maji kwa ajili ya kufanya usafi katika eneo lake la kazi.

Mhudumu huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Fatuma, alilipasha KIONGOZI kuwa wakati akiendelea na shughuli zake asubuhi hiyo, ghafla alishitushwa na kelele za mhudumu mwenzake ambaye alikuwa akimwita na kumwashiria hali ya hatari.

"Kabla sijageuka vizuri nijue kuna nini, ghafla nikashitukia nipo kwenye mikononi ya dume la nyani. Lilining’ang’ania mpaka likaninyang’anya khanga niliyokuwa nimejifunga. Nikabaki na nguo za ndani pekee." Alisema Bi. Fatuma na kuongeza,

"Nilijitahidi kung’ang’ania nguo yangu, lakini pia nilikuwa naogopa maana lina nguvu kuliko hata mtu. Lakini, likafanikiwa kunivua nguo na kuniacha uchi."

Mhudumu huyo aliendelea kueleza kuwa, kelele zake zilimshtua askari magereza ambaye alimkuta nyani huyo amebakiza kazi moja ya hatari aliyoikusudia ya kumbaka.

Bi. Fatuma alisisitiza kuwa maada wake ulitoka kwa askari magereza huyo ambaye alitumia ujasiri wake kupambana na kumdhibiti nyani huyo asitimize azma yake kwa ingawa nyani huyo alikuwa mbishi mno kwa kuwa alishaona amefanikiwa kumvua nguo.

Bi. Fatuma anasema alishindwa kuamini kwani japokuwa watu wengi walikwisha anza kusogea na kumweka katikati lakini nyani huyo alicharuka kwa kutaka kuwajeruhi wanaume hao mradi wasimzuie aweze kumshika Fatuma.

Hata hivyo Bi. Fatuma alisema dakika chache baadae, walikuja walinzi wa Mazizi ya Buibui Investment na kumkamata nyani huyo mwenye usongo na kumrudisha mahali pake.

hii ni mara ya pili kwa wanyama wakali kutoroka katika mabanda hayo. Wakati wa maandalizi ya maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba mwaka huu, chatu mkubwa alitoroka na kukutwa ndani ya uwanja akiwa juu ya dari hali iliyowalazimu wahudumu kuezua paa la banda hilo ili kumuondoa.

Haijulikani ni kwa jinsi gani wanyama hao wanafanikiwa kutoroka kwa vile kila mnyama anayefugwa hasa wale wakali, amejengewa kibanda chake kilichoimarishwa kwa vyuma,.

wanyama wengine wanaofungwa ndani ya uzio huo ni pamoja na chui, fisi na nyoka. Wengine ni wale wapole wakiwamo ngamia, pundamilia, mbuni na ndege wa aina mbalimbali.

Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili wamesema endapo walinzi wa wanyama hao hawatakuwa makini, ipo hatari ya wanyama wakali kama chui kutoroka na kuwashambulia bila huruma wananchi.

Kuweni macho Tanzania isipate 'vibwetere'- Pengo

lAonya vikundi vinavyotumia jina la Maria, Yesu kufanya maasi

Na Dalphina Rubyema

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewatahadharisha Watanzania kuwa makini na vikundi vinavyojitenga na makanisa yao ili kulinusuru taifa kukumbwa na maafa kama mauaji yaliyotokea Kanungu Uganda.

Muadhama Pengo alitoa kauli hiyo Jumamosi iliyopita wakati akizungumza kwa Wanalegio Mariae Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam waliokuwa wanasheherekea Jubilei Kuu katika sherehe zilizofanyika katika kituo cha ofisi za Halmashauri ya Baraza la Walei Katoliki Taifa Bakanja, eneo la Ukonga jijini Dar-Es-Salaam.

Alisema hali ya vikundi kushindwa kufuata kanuni na taratibu za Kanisa, ikitokea inaweza kusababisha uhasama ndani ya Kanisa hivyo kusababisha mauaji ya watu kama ilivyotokea hivi karibuni nchini Uganda.

Akitahadharisha ili Kanisa nchini lisipatwe na mauaji kama hayo ya Uganda, Kardinali Pengo alikuwa na haya:

"Juzi tumetoka kwenye mkutano wa Halmashauri ya AMECEA (Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati) huko Uganda. Miongoni mwa mambo tuliyoongelea ni pamoja na suala la roho za wenzetu wale wa Kanungu nchini humo ambao roho zao ziliteketezwa kwa moto. Mungu wangu! Inasikitisha sana."

"Tena Kibwetere na huyo mwenzake mmoja, walikuwa ni mapadre wa Kanisa Katoliki nchini Uganda. Lakini kwa sababu zao, walianzisha kikundi chao wenyewe na kilikuwa kinafunga mara tatu kwa wiki na siku zilizobaki, walikuwa wanakula nusunusu.

Hao hao wakadai mwisho wa dunia ni mwaka 2000. Walipoona mwaka 2000 umefika na siyo mwisho wa dunia kama walivyokuwa wakidai, wakaona waangamize wasio na hatia kwa moto, Mungu wangu! Na watu waliouawa ni wale wasio na hatia kabisa"

Kardinali Pengo aliongeza, "Kikundi hicho cha Kibwetere kilidai kinafanya hayo mambo ya ajabu kwa kuongozwa na Mama Maria. Mama Maria kweli anaweza kukuongoza ufanye maasi? Mungu wangu!

Sijui utasema nini kwa Mama Maria! Bahati nzuri ni Mama wa Huruma."

Kardinali alilitaka Shirika la Legio Mariae lizidi kuwa kweli Legio ya Kanisa Katoliki na siyo Legio ya kufanya maasi na kusisitiza kuviombea vikundi mbalimbali vinavyoonekana kuwa na mwenendo ule wa akina Kibwetere, ili vibadilike na kumgeukia Mungu.

"Ufalme wetu ni tofauti na ule wa akina Kibwetere. Sisi hatuna nafasi ya kuyumbishana sisi kwa sisi kwani tayari Yesu Kristo alikwisha tutetea pale aliposulubiwa Msalabani" alisema Mwadhama.

"Kama kweli mtu anaamini kuna Ufalme wa Mungu, kwa nini asiwaache watu wafurahie kuuona ulimwengu walimoumbwa na badala yake, anaamua kuwachoma kwa moto."

"Hata hapa Tanzania kuna kikundi kama hiki na nafikiri kila mmoja anakifahamu. Hivyo, kiombeeni jamani," alisema Muadhama bila kutaja jina la kikundi chochote.

Nchini Uganda, Machi mwaka huu, waamini wanaosadikiwa kuwa zaidi ya 500 wa kikundi cha kidini cha The Movement for Restoration of Ten Commandments of God waliteketea kwa kuchomwa moto baada ya kufungiwa na kuchomwa ndani ya kanisa na viongozi wa kanisa hilo.

Baadaye maiti zaidi ziligundulika katika makaburi tofauti karibu na nyumba ya kiongozi mmoja wa kanisa hilo, Dominic Katalibawa.

Kikundi hicho kilikuwa chini ya joseph Kibwetere na mwenzake Dominic Katalibawa ambao zamani walikuwa mapadre wa kanisa katoliki na inasadikiwa kuwa ndio waliohusika na mauaji ya waamini hao wasio na hatia.

Katika sherehe zilizowashirikisha Wanalegio Mariae kutoka parokia mbalimbali na Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es Salaam, michezo mbalimbali ilioneshwa.

Risala ya PASADA yamtoa kigugumizi Kiongozi wa mbio za Mwenge

lAmkumbuka Nyerere, asema ni ndoto vijana kutawala, wanakufa kwa UKIMWI.

lDC atumia nafasi hiyo kumnadi mgombea Ubunge

Na Peter Dominic

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Bw. Jordan Lugimbana, amemlilia Marehemu Julius Nyerere kwa madai kuwa shabaha yake kupigania uhuru ili vijana watawale, haitatimia kwa kuwa sasa vijana wengi wa Kitanzania wanakufa kwa UKIMWI.

Bw. Lugimbana alitoa kauli hiyo wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika kituo cha Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, kinachotoa huduma za kimwili na kiroho kwa walioathirika na ukimwi(PASADA)mwanzoni mwa juma lililopita.

Bw. Lugimbana Alijiandaa kutoa ujumbe wake kwa kumuomba radhi Mkuu wa Wilaya ya Temeke na wageni wengine kwa namna atakavyotoa ujumbe wake kwa taifa,

"Samahani hapa nitakufuru kidogo, naamini wakati akipigania uhuru wa nchi, Baba wa Taifa alitegemea vijana ndio watakaoongoza nchi. Lakini la kusikitisha, sasa wanakufa kwa Ukimwi," alisema na kusisitiza kuwa Watanzania hawana budi kumuenzi Baba wa Taifa kwa vile ndiye aliyeleta mshikamano kwa kuunganisha makabila 21 na watu wenye imani tofauti za dini.

"Naamini hapa tulipo wapo Waislamu, lakini wamejumuika na sisi ingawa ni maeneo ya Kanisani."

Katika hali iliyodhihirisha ujumbe muhimu wa Mwenge juu ya UKIMWI, Bw. Lugimbana alizidi kumwomba Mkuu wa Wilaya kuona kwamba endapo ataona miongoni mwa wakimbiza mwenge yupo anayejihusisha na vitendo vya kisherati, basi awanyang’anye mwenge huo na kuukabidhi wilaya nyingine.

"Mkuu wa Wilaya kama Rais wa Wilaya hii, ukiona tunafanya mambo yasiyo katika mstari usitukabidhi tena. Watafute haraka vijana wengine watakaoutumikia Mwenge kwa uadilifu," alisema na kuwahimiza Watanzania kuungana pamoja kuupiga vita UKIMWI.

Bw. Lugimbana alisema kila Mtanzania atatakiwa kuusema UKIMWI kwa uwazi bila kuficha ili kuweza kufikia lengo la kuutokomeza ugonjwa kama ilivyo nchi jirani ya Uganda ambayo awali ilikuwa ikiongoza.

Hata hivyo kituo hicho cha PASADA pamoja na kuupokea Mwenge, kiligeuzwa uwanja wa kampeni pale Mkuu wa manispaa alipoamua kumnadi mgombea Ubunge wa chama Tawala (CCM) wa Temeke, Bi. Kasora Kusaga.

Hali hiyo ilizua minong’ono miongoni mwa wananchi.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia nafasi ndogo aliyopewa kumnyanyua mgombea wa kiti cha ubunge kupitia CCM ili watu wamfahamu hali iliyotafsriwa kuwa kampeni za kisiasa.

Hata hivyo, Mkuu huyo alitoa nafasi kwa vyama vingine kuwatambulisha wagombea wao ingawa hakuna hata kimoja kilichomsimamisha na kumnadi mgombea wake. Mkuu huyo alisema alishangazwa na hali hiyo kwa madai kuwa vyama vingine vilifahamishwa mapema kupewa nafasi hiyo.

Wakati huo huo: PASADA katika risala yake kwa mwenge wa uhuru, imeiomba Serikali na dini mbalimbali kuweka utaratibu wa kuzungumzia UKIMWI katika kila kikao, kiwe kikubwa au kidogo.

Risala hiyo iliueleza ukimwi kama kikwazo kikubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hivyo kuiomba serikali iweke utaratibu utakaokifanya kila kikao kiwe kikubwa au kidogo kuwa na ajenda ya Ukimwi.

Balozi wa Vatican kuzuru Jimbo la Mwanza

Na Steven Mchongi Mwanza

BALOZI wa Vatican nchini anayemwakilisha Papa John Paulo wa pili Mhashamu Askofu Mkuu Luigi Pezzuto atakuwa na ziara ya siku saba katika Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza Novemba mwaka huu.

Kufuatia ziara ya ujio wa Balozi huyo yenye ujumbe wa Jubilei ya miaka 2000 kutoka kwa Papa, Jimbo Katoliki la Mwanza limetoa ratiba ya ziara yake na maandalizi ya mapokezi tayari yameanza.

Taarifa iliyotolewa hapa jijini Mwanza na Mhashamu Askofu Anthony Mayalla wa jimbo hilo, imesema kuwa ziara hiyo ya Mhashamu Pezzuto itaanza Novemba 20 na kumalizika Novemba 26.

Taarifa hiyo yenye kumbukumbu namba JKM/298/2000 na ambayo KIONGOZI imepata nakala yake imesema kuwa Balozi huyo wa Papa akiwa hapa Mwanza atatembelea Parokia saba pamoja na kuzungumza na waamini.

Kulingana na taarifa hiyo Mhashamu Pezzuto atawasili jijini Mwanza mnamo Novemba 20 ambayo siku hiyo atakuwa na kikao cha pamoja na sekretariati ya Jimbo Kuu kabla ya kuanza ziara yake ya kuzitembelea baadhi ya parokia.

Ziara yake ya kuzitembelea parokia itaanza Novemba 21 ambapo atatembelea parokia ya mtakatifu Justine, Bujora katika Dineri ya Magu na siku inayofuata Novemba 22 atatembelea Parokia ya Mtakatifu Joseph, Sumve katika Dinari ya Kwimba.

Novemba 23, Mhashamu Pezzuto atatembelea Parokia ya Bukumbi katika Dineri ya Misungwi parokia ambayo ilikuwa ya kwanza kuanzishwa katika Jimbo la Mwanza.

Ziara hiyo ya Mhashamu Pezzuto itaendelea tena Novemba 24 katika parokia ya Mtakatifu Joseph, Nansio katika Dineri ya Kisiwa cha Ukerewe, ambapo Novemba 25 atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za mahafali ya wahitimu wa chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine, Nyegezi.

Kilele cha ziara hiyo kitakuwa Novemba 26 ambapo Mhashamu Pezzuto ataongoza misa kubwa katika kanisa Kuu la Bugando hapa jijini Mwanza.

Katika taarifa ya ziara hiyo iliyosambazwa pia kwa parokia zote za jimbo la Mwanza, Mhashamu Mayalla amewataka waamini wote jimboni kuanza maandalizi ya kumpokea mwakilishi huyo wa Papa.

Mhashamu Pezzuto ambaye ana makao yake jijini Dar es Salaam, ndiye mwakilishi wa Papa na pia balozi wa Serikali ya Vatican hapa nchini.

Tanzania kuchimba mafuta baharini?

Na Dalphina Rubyema

HUENDA Tanzania ikaondokana na tatizo sugu la kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuendeshea mitambo na matumizi mengine,endapo itahakikishwa kuwa na mafuta hayo yanayosadikiwa kuwa chini ya miamba ya bahari.

Akihojiana na shirika la Utangazaji la Uingireza (BBC) Waziri wa Maji, Nishati na Madini nchini Bw. Abdalah Kigoda alisema kuwa hadi hivi sasa utafiti uliokwisha fanywa na wataalam nchini, umeonesha kuwa ni kweli mafuta hayo yapo.

Alisema hadi hivi sasa utafiti umekwisha fanywa kuanzia Ruvuma hadi Dar-Es-Salaam na kwa hivi sasa, serikali ipo katika mikakati ya kufanya utafiti wa kuanzia Dar-Es-Salaam kwenda mpakani.

"Awamu ya kwanza utafiti ulifanyika Ruvuma hadi Dar-Es-Salaam.

Awamu ya pili, itakuwa Dar-Es-Salaam kwenda mpakani. Hii ikiwa na maana kutoka Dar kwenda maeneo ya Pemba na Unguja," alisema.

Bw. Kigoda ambaye yupo nchini Uingereza kutafuta makampuni na wataalam zaidi wa kufanya utafiti, alisema kuwa hadi kufika mwanzoni mwa mwaka 2001 Taifa litakuwa na takwimu ambazo zina uwezo kueleweka.

Alisema serikali imetoa nafasi kwa makampuni makubwa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta hiyo ya mafuta.

Wamachinga wa Morogoro wailalamikia Manispaa

Na Gerald Kamia, Morogoro

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo katika Manisapaa ya Morogo, wamelaumu uongozi wa manisapaa hiyo kwa kuwaondoa katika maeneo ya biashara kabla ya kuwatafutia maeneo mengine ya kufanyia shughuli zao.

Malalamiko ya wafanyabiashara hayo yamekuja siku moja baada ya Serikali ya manispaa ya Morogoro kuwataka wafanyabiashara hao kuacha kuendesha biashara kandokando ya barabara za manisapaa hiyo ili kutoa nafasi ya ukarabati wa barabara hizo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa niaba ya wenzao, masha Hassani Mfinanga na Hassan Ali Hassan, wanaofanya biashara yao katika barabara ya Morogoro , wamesema wameshitushwa na agizo hilo la walililosema limekuja ghafla bila wao kuandaliwa.

Wamesema hali hiyo imewafanya washindwe kumudu kujua ni vipi na ni wapi wataendesha hali wanayodai wananyanyaswa kwa kuwa uongozi wa manispaa ulipaswa kuwaandalia mahali pengine kabla ya uamuzi wa kuwaondoa mahali hapo.

Wamesema wengi wao wanategemewa na familia zao na hawajui ni vipi wataendesha maisha yao yakila siku na hivyo, kuutaka uongozi wa manisapaa kutoa tamko linalowaelekeza mahali pa kufanyia shughuli zao.

Katibu Tarafa wa Manispaa ya Morogoro, Bw. Sulpicius Pakalapakala Mlenge, Jumatano iliyopita alitoa agizo la kuwataka wafanyabiashara hao kutoendesha shughuli zao kuanzia Siku iliyofuatia (Alhamisi)

Kwa mujibu wa Pakalapakala, lengo la kufanya hivyo, ni kumuwezesha mkandarasi wa ujenzi kufanya ukarabati wa barabara kwa nafasi na uhuru zaidi.

Barabara zinazohusishwa na mpango huo ni Madaraka, Mazimbu, Mtaa wa Mindu na eneo la

sabasaba.

Polisi wanafurahia mikutano yetu - TLP

Na Peter Dominic

CHAMA cha Siasa nchini Tanzania Labour Party (TLP) jimboni Temeke kimesema kinashirikiana vizuri na polisi katika mikutano yake kufuatia amani, utulivu na demokrasia ndani ya chama.

Akizungumza na Gazeti hili katika ofisi za chama chake jimboni Temeke,

Temeke Katibu wa chama jimboni wilayani humo Bw. Kwaller Amully alitamba kuwa chama chake hakina ugomvi wala migogoro na Jeshi la Polisi wala vyama vingine kwa kuwa hata wanachama wake wanazingatia amani, utulivu na demokrasia ya kweli.

"Mikutano yetu ni ya amani hatubebi watu kutoka majimbo mengine. Kazi yetu ni kusimama jukwaani kueleza sera za chama na kufungua matawi tofauti na vyama vingine vinavyosomba watu kutoka mbali. Na hiyo ndiyo inayosababisha vurugu," alisema. na kuongeza kuwa TLP inafuata taratibu hizo kwa kuwa sera zake hazishauri kuvunjika kwa amani nchini.

Alidai TLP kina matumaini makubwa ya kushinda kwa asilimia 80 katika jimbo hilo kwa vile kimewasimamisha wagombea udiwani katika kata na kimekwishafanya mikutano mara tatu kila kata na wananchi kuwa na mwitikio mzuri.

Bw. Kwaller alisema chama chake bado kina mbinu nyingi za hoja kwa hoja na mtandao katika nchi nzima na akaongeza kwamba, hivi sasa katika jimbo hilo anasubiriwa mgombea wa urais kwa tiketi ya TLP ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama kitaifa Bw. Augustine Mrema.

Hata hivyo Katibu huyo ameishutumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi jimboni humo kwa kuchelewesha takwimu za watu waliojiandikisha kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 29,mwaka huu.

"Kama Tume ya Uchaguzi imeshindwa kutoa takwimu ya idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura, itakuwaje siku ya kuhesabu kura?" alihoji Bw. Kwaller na kuongeza kuwa anatarajia kulifikisha suala hilo katika ngazi za juu za chama chake ili watafute namna ya kulitafutia ufumbuzi.

Zaidi ya asilimia 50 watoa mimba Dar

Na Josephs Sabinus

IMEELEZWA kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wanawake jijini Dar-Es salaam, wenye umri tofauti, walitoa mimba kwa njia mbalimbali katika kipindi cha mwaka juzi.

Muuguzi Mkuu wa Kituo cha Mafunzo cha Mweka (Mweka Training Center), kilichopo Kigogo-Mbuyuni, jijini Dar-Es-Salaam, Kilian Mlangwa, aliyasema hayo wakati akitoa mada katika semina ya wanandoa watarajiwa wa Kanisa Katoliki Jimboni dar-Es-Salaam, katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha Msimbazi jijini hapo, Jumapili iliyopita.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka huo wa 1998, wanawake wa rika mbalimbali wakiwamo wana ndoa, wanafunzi na mabinti wa nyumbani, waligundulika kutoa mimba kwa sababu na njia mbalimbali.

Alisema baadhi yao walitoa mimba kwa kutumia sindano na madawa ya kisasa na miti shamba wakati wengine walitoa mimba kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao kiafya.

Aliwataka wanawake wanaokimbilia kwa wauguzi wa vichochoroni kutoa mimba kwa sababu yoyote kujua kuwa, huko wanahatarisha afya na maisha yao kutokana na utaalamu duni na vifaa hafifu wanavyotumia.

"Huko vichochoroni, kuna hatari sana kwa kuwa hakuna wataalamu. Sasa wataalamu hao wa vichochoroni wanaweza kupasua hata mfuko wa uzazi, au wakatumia vyombo hata visivyochemshwa vizuri na kusababisha maambukizo katika mji wa mimba," alisema.

Aliongeza kuwa, utoaji wa mimba haupaswi kuwa njia ya kuepuka migogoro ya kijamii, bali labda endapo kuna ulazima ili kuepuka hatari ya kifo.

Aliwahimiza akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ili kupimwa afya zao na kupewa ushauri wa kitaalamu.

Akifunga semina hiyo ya siku mbili tangu Septemba 16, mwaka huu, Katibu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es Salaam, Padre Andrew Luanda, aliwataka wanandoa kubeba msalaba wa kuvumiliana katika maisha yao.

"Dini ya kweli ni ile inayoonekana kwa imani na matendo mema hivyo, maisha ya Kikristo ni lazima yawe ya kubeba misalaba. Hata nyie mnaoingia maisha ya ndoa." Alisema Padre Luanda.

Kuweni mashahidi kuutakatifuza ulimwengu-Wito

Na Dalphina Rubyema

WAKATI Ulimwengu mzima upo katika vuguvugu la Karne ya Sayansi na Teknolojia, Walei wote wametakiwa kuutakatifuza na kuwa mashahidi wa kuutakatifuza ulimwengu.

Hayo yalisemwa na Katibu Mtendaji wa Idara ya Walei katika Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Padre Nicholous Segeja wakati wa sherehe za maadhimisho ya Jubilei Kuu ya miaka 2000 iliyofanywa na chama cha kitume cha Legio Mariae Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye ofisi za Halmashauri ya Baraza la Walei Taifa zilizopo Ukonga jijini Dar-Es-Salaam, Padre Segeja aliwahimiza wakristo kuishi maisha mema kwa kuwa Ukristo ni mahali popote na wala siyo kusubiri mahubiri kutoka kwa maaskofu na mapadre.

Hata hivyo mbali na kutoa ujumbe huo uliovutia umati wa watu walihudhuria sherehe hizo, Padre Segeja aliwasisitiza walei kutoa michango yao ya hali na mali kumalizia ujenzi huo wa kituo cha Halmashauri ya Baraza la Walei ambacho kitakuwa ni cha kuratibu shughuli za kilei na kitakuwa na kutatua matatizo yao.

"Hata kama kweli Mama Bikira Maria hataki makuu, lakini sasa jamani kufanyia shughuli za walei taifa kwenye sehemu kama hii ambayo imejengwa sehemu ndogo tu na sehemu iliyobaki kuwa matofali peke yake ni jambo la kuangalia kwa upana," alisema.

alisema katika miaka ya nyuma, Walei wameweza kuchangia vitu mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha Bakanja lakini, kwa Mwaka huu Mtakatifu hakuna kitu chochote kilichokwisha tolewa.

"Toeni michango yenu kwa dhati kabisa ili tuweze na sura gani’ alisema.

Hivi sasa kituo hicho kimejaa matofali ambayo kwa siku hiyo ya sherehe za Legio Maria yalitumika kama viti na muonekano wa matofali hayo yamekaa kwa kipindi kisichopungua miaka mitano.

Ili ujenzi wa kituo hicho ukamilike kila mwamini mlei wa Kanisa Katoliki nchini anatakiwa kutoa sh. 100-500, sh 10,000 kwa makundi mbalimbali na sh 25,000 - 100,000 kutoka kwa watu maalum na fomu za michango hiyo zitakuwa zikipitishwa kwenye jumuiya ndogondogo na maparokiani.

Mamia ya watu wamzika Padre Kija

Na Charles Hililla, Shinyanga

MAMIA ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wamejitokeza kwa wingi kumzika aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,Padre Norbet Kija aliyefariki dunia Septemba 19 na kuzikwa Septemba 22 mwaka huu Jimboni kwake Shinyanga.

Akizungumza katika misa ya mazishi ya Padre huyo,Askofu wa Jimbo la Shinyanga,Askofu Aloysius Balina alisema kuwa Binadamu siku zote anatakiwa kuishi maisha yanayompendeza Mungu ili kuleta heshima na maana ya uwepo wake hapa duniani kwani hajui siku wala saa atakayoitwa kwa Mungu

"Uwepo wa binadamu hapa duniani ni pamoja na kumjua Mungu na kufanya mambo yanayoendana na mapenzi yake na siyo kuishi kwa vile ulijikuta upo duniani"alionya Askofu Balina.

Askofu Balina alimtaja marehemu padre Kija kuwa alikuwa na tabia ya upole na unyenyekevu tabia ambayo alisema ni mfano wa kuigwa na jamii.

Aliendelea kusema kuwa moyo wa marehemu wa kuwafikiria zaidi na kujitoa kwa ajili ya wengine kuliko kujifikiria mwenyewe ni moja ya sifa zilizompa mafanikio katika shughuli zake mahali pote alipofanya kazi au kuhudumia.

Misa hiyo ya kumuombea marehemu padre Kija ilitanguliwa na ibada fupi ya kupokea mwili huo iliyofanyika nje ya mlango wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Shinyanga ambapo iliongozwa na padre Norbert Ngussa.

Baada ya ibada hiyo jeneza lililokuwa limewekwa mwili wa marehemu liliingizwa kanisani kwa ajili ya watu mbalimbali kutoa heshima zao za mwisho.

Marehemu Padre Kija amezikwa kwenye makaburi ya mapadri yaliyopo nyuma ya Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Shinyanga.

Nasaha,utani wa Padre Kija sasa basi

Na waandishi Wetu

YAANI nyie Waandishi wa Kiongozi mmeisha nigeuza mimi kama babu yenu! nawambia msiingie kwenye chumba cha kompyuta nyie mnaingia!ngoja,sasa nikimkuta mtu namchapa kabisa,maana sasa naona nikiongea kwa mdomo hamnielewi".

"Hasa wewe ‘Warioba’na ‘Jangala’ndiyo mnaopenda kuingia huko,huyu Dembwe sasa kapunguza ,msiingie jamani kwenye chumba cha Kompyuta, nikiwakuta, wewe Page Maker ndiye utakayeanza kuadhibiwa".

Hayo ni baadhi tu ya maneno tuliyozoea kutoka kinywani mwa baba yetu mpendwa,Padre Norbet Kija ambaye jana Ijumaa Mwenyezi Mungu amemwita kwenye nyumba yake ya milele.

Alipoona Waandishi wake wanaonyesha woga kila akiingia chumba cha habari, Marehemu Padre Norbet Kija alisikika akisema "Mnaniogopa ehe!, kwanini mnaniogopa? Mimi ni mtu kama nyie, ongeeni tu, mimi nilichowakataza ni kuingia chumba cha kompyuta na wala sikuwakataza msiongee kila mnaponiona ninakuja kwenu kuwatembelea".

Alivyoona kimya kati yake na waandishi kinazidi ,alisikika "Mbona siku hizi waandishi wangu hamji ofisini kwangu kunisalimu? Au mmechukia baada ya kuwazuia msiingie kwenye chumba cha kompyuta? Sawa bwana, lakini mimi wanangu nawapenda sana ,nitakuwa nakuja Newsroom kuwajulia hali kabla sijaingia ofisini kwangu".

"Kitendo cha kuwazuia msiingie kwenye chumba cha kompyuta kisiwakasilishe, au nilitumia ukali? Mliogopa ehee!, poleni kama nilitumia maneno makali, lakini sasa nasema kwa sauti iliyotulia kabisa, jamani msiingie chumba cha kompyuta, tumieni hii kompyuta yenu iliyopo Newsroom, sawa ehee, haya mimi naelekea ofisini, nawatakia kazi njema kwa siku ya leo".

Kabla hajaondoka kuelekea ofisini kwake, tulimsikia marehemu Padre Kija akimwita mmoja wa wa Waandishi ambaye angemuona mbele yake na kumwambia "Wewe...mbona unaoneka una swali la kuniuliza,uliza basi kabla ya kuondoka" kabla hata huyo aliyeulizwa hajaulizwa swali yeye Padre Kija aliingilia kati "Warioba msaidie mwenzio kuuliza swali au mimi naondoka zangu.

Maneno haya ya utani alipenda kuyatumia mara kwa mara marehemu Kija, zaidi ni pale alipoona Waandishi wake wanaonyesha moyo wa woga kwake,hata siku moja hakupenda Waandishi wake waonekane wenye huzuni eti kutokana na kuwakemea.

Baba Kija ambaye alipenda kuwaita Waandishi wake majina ya utani kama "Jangala"," Warioba" na mengine mengi alipenda sana kuyapokea na kuyasikiliza matatizo ya Waandishi wake na kila wakati alikuwa tayari kuyatatua.

"Sasa nyie ni lini mtaisha kulalamika,kila siku ni watu wa kulia lia tu,,najua mnafanya kazi ngumu ya kutafuta habari lakini mambo yatakuwa mazuri hapo baadae, fanyeni kazi yenu kwa bidii na utii na matakuja kufurahia matunda yake.

Wakati Wanakiongozi wakiendelea kufanya kazi yao kwa bidii kama walivyoshauriwa na Baba yao,afya ya Padre Kija ilibadilika lakini alikuwa akipata nafuu siku hadi siku.

Katika namna ya kuwaondoa hofu Waandishi wake,Padre Kija aliitisha kikao cha ghafla cha Wafanyakazi wa Kiongozi.

Katika kikao hicho kilichofanyika Februari mwaka huu kwenye ofisi ya Mhariri Mkuu wa Gazeti la Kiongozi,Marehemu Padre Kija aliongelea zaidi juu ya suala la kuliendeleza gazeti la Kiongozi.

Miongoni mwa mikakati aliyoitoa ni juu ya upatikanaji wa gari aina ya Hiace kwa ajili ya shughuli za habari.

"Nafurahi kuarifu kuwa nimeomba msaada wa gari kutoka kwa wafadhili nao wamekubali kutupatia Hiace liatakalokuwa likitumika kwa ajili ya shughuli nzima za habari"maneno hayo yalisemawa na Padre Kija.

Taarifa hiyo nzuri iliwafanya waliohudhuria kikao hicho, kushangilia kwa furaha huku kila mmoja akikofi kama ishara ya kumpongeza Padre Kija kwa kazi yake nzuri.

Baada ya washiriki wa kikao hicho kutulia,Padre Kija aliendelea kusema "Gari letu tukisha lipokea ,wafanyakazi wote tutaenda Bagamoyo kujipongeza ambapo tutakwenda na gari letu hilo jipya kama uzinduzi wake".

"Kabla ya kwenda huko Bagamoyo,tutaandika vijikaratasi ambavyo vitaandikwa majina yetu ambavyo tutavirusha juu, kila mmoja ataokota karatasi moja na atakuta jina mojawapo la wanaKiongozi, hilo jina utakalolikuta usilitaje ,itakuwa siri yako na utaandaa zawadi yako ambayo utaenda nayo Bagamoyo na huko ndiko kila mmoja utakapotaja jina la mtu uliyemkuta kwenye karatasi ile uliyookota na kumkabidhi zawadi yake".

Wanakongozi wakiwa wanasubiri kwa hamu kubwa siku hiyo ya kwenda Bagamoyo,Padre Kija aliendelea kuumwa na kupelekwa Morogoro ambapo baada ya kukaa siku chache alirudi TEC na hatimaye kwenda Jimboni kwake Shinyanga kwa mapumziko.

Huko Shinyanga Baba Kija amekuwa akiwasiliana mara kwa mara kwa simu na Waandishi wake na Fax akiwafahamisha kuwa anaendelea vizuri.

Miongoni mwa salamu zake ni Fax aliyo watumia Waandishi mwishoni mwa Agosti mwaka huu ambayo pamoja na ujumbe mwingine ,vile vile aliandikwa:

"Msiwe na wasiwasi ,hivi sasa hali yangu ni nzuri na ninatarajia kurudi huko Dar-Es-Salaam mwezi ujao (Septemba)".

Ujumbe huo uliwaondolea giza Waandishi lililokuwa limetanda kwenye macho yao kwa kutomuona kwa muda mrefu Baba yao mpendwa.

Wakiwa wapo katika hamu kubwa ya kumuona baba yao akiingia Dar kama alivyo ahidi,ghafla matumaini hayo yalitoweka mnamo Septemba 19 mwaka huu majira ya saa 6.30 mchana pale Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura alipowatangazia wana TEC kuwa Padre Kija hatunaye tena ,ametutoka,amefariki!!!

"Baba Kija kumbe ulikuwa unatuliwaza wanao! ulivyotoka TEC kuelekea Shinyanga ndio ulikuwa unatuaga!!!!".

Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi Baba.Tutayaenzi mazuri yote uliyotutendea.Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake libarikiwe .Pumzika Baba.

Huzuni hiyo ya kuondoka kwa Padre Kija si kwamba imewagusa tu Waandishi wa Kiongozi bali umewagusa watu mbalimbali wakiwemo Maaskofu, Mapadre, Watawa na Walei.

Kiongozi ilipata nafasi ya kuzungumza na watu mbali ambao walitoa masikitiko yao;

Mojawapo wa watu hao ni Mkurugenzi wa utume wa Walei Jimbo la Mbulu, Bw.Peter Massay ambaye alisema kuwa marehemu Kija alikuwa ni mtu anayetoa ushirikiano mzuri na alikuwa ni mtu wa watu.

"Nakumbuka tulishafanya wote semina ya kichungaji ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya maandalazi ya Jubilei Kuu Kanda ya Mashariki, kwakweli alioneka dhahiri alivyo mtu wa watu"alisema Bw.Massay.

Katibu Mhutasi wa Padre Kija, Bibi.Mariam Gama alipohojiwa juu ya kifo cha padre Kija, alisema kuwa alikuwa ni mtu wa kujituma na alikuwa tayari kumsaidia kila mtu ambaye alihitaji msaada kutoka kwake.

"Yoyote aliyehitaji msaada kutoka kwa Padre Kija, alisaidiwa, hata siku moja hakukataa kutoa kitu cha msaada labda kama hicho kitu alichoombwa hana".

Aliongeza kusema kuwa Marehemu Padre Kija alipenda sana michezo na alikuwa ni shabiki mzuri wa timu ya Yanga na alishawahi kuipatia timu hiyo fulana.

"Nakumbuka siku moja alikuja Shungu pamoja na familia yake, alinitambulisha kwa familia hiyo, hii inaonyesha ni jinsi gani alivyokuwa na mapenzi mema na timu hiyo ya Yanga"alisema Bibi Gama.

Aliongeza kusema kuwa kifo cha Padre Kija kimetokea mapema mno kwani hakuna aliyetarajia kuwa atakufa kwani hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.