Vigogo watano wa CCM kugombea ubunge NCCR
l
Mbatia kumpisha Mrema agombee urais?Na Josephs Sabinus
CHAMA cha NCCR_MAGEUZI, kimeelezwa kuwa kinajiandaa kupokea watu watano maarufu kutoka CCM ambao wanatarajiwa kujiengua ili kugombea ubunge katika chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao na kwamba huenda Bw. James Mbatia, akampisha Uenmyekiti Bw. Augustine Mrema, ili agombee Urais kwa chama hicho.
Habari zilizopatikana jijini zinasema mpango wa viongozi hao kujiunga na NCCR, unalenga katika kutoa changamoto ya kipekee inayoweza kukipa ushindi chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Mwenyekiti wa chama cha TLP, Bw. Augustine Mrema, alipowania urais katika chama cha NCCR_MAGEUZI katika Uchaguzi Mkuu uliopita akitokea CCM, alitoa changamoto kubwa na kwa mujibu wa habari hiyo, ni moja ya sababu za mpango wa Mwenyekiti mpya wa NCCR Bw.James Mbatia, na Makamu Mwenyekiti wake, Bi. Edith Lucina, kuchakarika ili kuwashawishi Bw. Mrema na viongozi wengine kutoka CCM kujiunga na chama hicho.
KIONGOZI lilipofika Makao Makuu ya NCCR, wiki hii halikufanikiwa kumuona Bw. Mbatia kwa kuwa alikuwa nje kikazi lakini Katibu Mwenezi wa chama hicho Bw. Joseph Selasini, alisema, "Ni kweli tumekwishapata watu watano mashuhuri hapa nchini walio tayari kujiunga nasi kutoka vyama na taasisi mbalimbali. Lakini sitaweza kukuambia ni akina nani, au wanatoka chama au taasisi gani."
"Sisi tukifanikiwa kumshawishi mtu kujiunga akakubali, tunafurahi maana ndiyo mafanikio ya chama," alisema Bw. Selasini.
Aliongeza, "NCCR haina mpango wowote wa kumfanya Mbatia ampishe Mrema uenyekiti kwa sababu wanachama kwa hiari yao wameridhika na sifa na uongozi wa Mbatia ndio maana wakamchagua yeye. Kwa hiyo, nasisitiza kuwa mpango wa Mbatia kumpisha Mrema uenyekiti, haupo kabisa NCCR."
Alisema, "Mrema kama mwanachama aliyefukuzwa, ili arudi katika chama, lazima aombe upya uanachama kuanzia ngazi ya chini kabisa pamoja na wale wenzake 13." Hata hivyo Mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya chama hicho alilinong'oneza gazeti hili kuwa upo uwezekano wa Bw. Mrema kurejea NCCR na kuwania urais hasa katika kipindi hiki ambacho Msajili wa Vyama Vya Siasa Bw. George Liundi ametangaza kutoutambua uenyekiti wake TLP.
Bw. Selasini, pamoja na hayo, alitoa wito kwa wanachama wote waliokerwa na migogoro ndani ya chama kurudi na kujiunga pamoja kukiunda hasa baada ya kuzaliwa upya kisiasa.
Awali habari hizo zilisema kuwa washauri wa Mwenyekiti (Mbatia) wakiwemo Dk. Sengondo Mvungi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamemshauri atenge nafasi tano kati ya saba ambazo katiba inampa kufanya uteuzi ili ziwasubiri vigogo watakaojiunga kutoka CCM.
Kwa mujibu wa Katiba ya NCCR_MAGEUZI, Mwenyekiti anayo haki ya kuwateua wajumbe watano wa Halmashauri Kuu ya chama na wawili wa Kamati Kuu bila kuingiliwa na mtu yeyote na kuna habari kwamba huenda Bw. Mbatia akatumia nafasi yake kuwapa watu hao.
Habari juu ya kurejeshwa kwa Mrema ndani ya NCCR_Mageuzi, zilikuwa zikisikika hata wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa hivi karibuni wa chama hicho, na baadhi ya wafuasi wa aliyekuwa mpinzani wa Mbatia, Mheshimiwa Mabere Marando, walikuwa wakiwaonya wajumbe wasimpe Mbatia kura kwani atakirudisha chama chao kwa "Mbwa mwitu wa siasa" yaani Bw. Mrema. Mwenyekiti huyo wa TLP bado angali anao wapenzi ndani ya chama chake hicho cha zamnai cha NCCR-Mageuzi.
Kadhalika juu ya suala la vigogo wa CCM kujiunga na NCCR-Mageuzi, iliripotiwa hivi karibuni kuwa viongozi wa chama hicho walikuwa wakiwanyemelea pia Jaji Mkuu Mstaafu Francis Nyalali, na Bi. Getrude Mongela, ambao wote wamekanusha kuwa na nia ya kujiunga na chama hicho.
Chama cha NCCR_Mageuzi ambacho ni cha pili kwa kuwa na idadi ya wabunge miongoni mwa vyama vya upinzani kikitanguliwa na CUF, kilipata umaarufu mkubwa wakati Bw. Mrema alipojiengua kutoka CCM na kujiunga nacho, lakini baadaye kilikumbwa na migogoro, ambayo hatimaye ilipelekea Bw. Mrema kuamua kukikimbia na kujiunga na TLP ambacho nacho kinasuasua.
Mpentekoste aonya: Msibweteke kwa majina ya kidini mkadhani mmeokoka
Na Mwandishi Wetu
WANAJAMII wameaswa kutobweteka kwa majina ya kidini waliyonayo huku wakishiriki uhalifu na badala yake, wakubali kumjua Mungu na hivyo kuyafanya majina yao kuwa kielelezo cha mapenzi yake na kulinda maadili ya jamii.
Ushauri huo ulitolewa Jumapili iliyopita na Mchungaji, Luther Shumba wa Kanisa la Pentekoste Tanzania, Parishi ya Kekomachungwa, Jimbo la Mashariki na Pwani alipozungumza na gazeti hili kanisani kwake jijini.
Alisema anashangaa kuona na kusikia watu wenye majina makubwa ya kidini, wakiwa miongoni mwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwemo mauaji ya makusudi, ubakaji na wizi na kwamba nafsi za watu wa namna hiyo hazina budi kusutwa na majina hayo ya ki-Mungu ili kuepukana na uhalifu na kuyafanya yawe na maana halisi ya mapenzi ya Mungu.
"Mtu ana jina kubwa la kidini lakini ndiye huyo mshiriki wa uasherati, uzinzi,mauaji, uabakaji, ulevi na hata ujambazi,"alisema Mchungaji Shumbi na kuongeza,
"Mtu anaitwa Andrea, Yohana, Athumani, Abdala, utadhani anaendana na matendo ya ki-Mungu kumbe yeye ana jina tu, lakini Mungu hayupo moyoni mwake.Wanadamu wasiridhike kuwa na majina makubwa ya kidini yasiyo kielelezo cha mapenzi ya Mwenyezi."
Awali akihubiri kanisani hapo, mhubiri Elia Ng’onya alisema mara nyingi mipango ya wanadamu imekuwa haifanikiwi kwa kuwa watu wengi wanaomba kibinafsi bila kumshirikisha Roho Mtakatifu.
"Jiulize ni lini mara kwa mara ya mwisho uliomba na kufunga kwa ajili ya Kanisa bila msukumo wa mtu mwingine," alisema Ng’onya.
WAKATI HUO HUO:
Katibu wa Akina Mama Parish hiyo Bi.Grayson na Mama Mlezi Bi.Mambi Shumbe, siku hiyo waliongoza mchango kwa kuuza chupa mbili za chai, glasi dazani moja na nusu, nusu dazani ya vikombe vya chai, trei 3 kwa njia ya mnada na kupata zaidi ya sh.60,000 zitakazotumika kusaidia kutoa huduma za kiroho ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wafiwa, yatima, wagonjwa na wenye shida mbalimbali.Ndoa sio kwa ajili ya tamaa za mwili-tahadhari
Na Getruder Madembwe
WANAJAMII hususan Wakristo wametakiwa kuepuka dhana kwamba kuoa au kuolewa nduio dawa ya kudhibiti tamaa zao za mwili, kwaniingekuwa hivyo wasingekuwapo "wanaokwenda nje" ya ndoa zao halali.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na watoa mada katika semina ya vijana iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kawe, jijini Dar Es Salaam, ambako ilisisitizwa kwamba kinachohitajika ni kuutiisha mwili kwa Roho wa Mungu.
Walisema bado wapo wanawake na wanaume wenye ndoa za Kikristo lakini bado ndoa zao hazifanani kuwa za Kikristo kwa kuwa hurubuniwa na watu wengine wa nje na akawataka wanandoa kuwa na Yesu katika maisha yao vingine hawatavishinda vishawishi vinavyowa songa toka nje kwani bila Yesu hataweza kuyashinda majaribu wa nje
"Hatuolewi au kuoa kwa nia ya kutimiza tamaa za miili yetu kwani kuna watu wana ndoa za Kikristo lakini bado wana nyumba ndogo," alisema Matrida Dondo, na kuongeza, "Tunatakiwa tuwe na Yesu kwani tukiwa naye tutaweza kushinda tamaa za miili yetu."
Naye Naomi Mhamba, alisema kuna mila potofu za Kiafrika kuwa mwanamke anafananishwa na shamba kwani shamba kama halitoi mazao huuzwa au huachwa na kununua shamba jingine ambalo hutoa mazao na hivyo kama mwanamke akiwa hazai lazima aolewe mwanamke mwingine na akasema kuwa kufanya hivyo ni makosa kwani walipooana walikwisha kuwa mwili mmoja na waliamua kuoana kama watazaa au hawatazaa.
"Watu wanapoamua kuoana hawategemei kupata watoto kwani watoto huja kwa baraka za Mungu na Mungu mweyewe anatambua ndoa ambayo haina watoto au yenye watoto, na kamwe watoto si msingi wa ndoa basi si vyema kumuacha mke wako au mume wako kama hana uwezo wa kuzaa"alisema Mhamba
Yaredi Dondo ambao wote kwa pamoja ni waamini wa Tanzania Assembles of God Upanga, alisema kuwa watu wakitaka ndoa zao zidumu waache ubinafsi wa vitu.Akifafanua kauli yake hiyo alisema mwanamke na mwanaume wanapooana vitu ambavyo alikuwa navyo mtu mmojawao sasa vinakuwa nivya wote na wala sivya mtu mmoja.
Waseminari wa zamani waanzisha jumuiya
Na Dalphina Rubyema
VIJANA waliosoma katika Shule ya Seminari Katoliki ya Makoko Jimboni Musoma, wanaoishi jijijini wameanzisha jumuiya inayojulikana kama Makoko Almuni.
Uzinduzi wa Jumuiya hiyo iliyoundwa na vijana wapatao 30 waliosoma seminarini hapo tangu mwaka 1975 -1985, ulifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Hill Top uliopo Ukonga jijini na kubarikiwa na Maaskofu wa Majimbo ya Musoma, Shinyanga na Jimbo Kuu la Mwanza.
Akisoma risala kwa niaba ya vijana hao, Bw.Paulo Basondore alisema wameamua kuwaalika Maaskofu hao kwa vile enzi hizo za 1975 -1985 Askofu Justine Samba wa Jimbo la Musoma na Askofu Balina wa Jimbo la Shinyanga walikuwa ni magombera wa seminari hiyo ambapo Askofu Anthony Mayala wa Jimbo Kuu la Mwanza alikuwa ni Askofu wa Jimbo la Musoma.
Bwana Basondore alisema kuwa madhumuni ya kuundwa kwa jumuiya hiyo ni kupanua wigo wao wa kukutana na kubadilishana uzoefu katika maisha ya kiroho na ya kimwili.
Askofu Justine Samba ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC aliwashukuru vijana hao ambapo alisema kuwa wamefanya kitu ambacho kilikuwa hakitarajiwi.
"Kwa kweli ninawapongeza sana kuwa wazo lenu la kuanzisha jumuiya ya Makoko Almuni ni kitu ambacho hatukukitarajia kwenu" alisema Askofu Samba.
Naye Askofu Balina akitoa baraka zake, alisema kuundwa kwa Makoko Almuni, ni mfano mzuri wa kuigwa na wengine waliopitia seminari badala ya kukata tamaa wakidhania mtu anapojiunga na Seminari ni lazima awe padre na inaposhindikana ndiyo mwisho wa yote .
"Nia ya Seminari si kutoa tu mapadre bali ni kutoa malezi bora ya kiroho na ya kimwili hata kama nyie hamkuwa mapadre watoto wenu ama wajukuu wanaweza kuwa mapadre hivyo hata vijana wengine waliopitia Seminari mbalimbali nchini hawana budi kuiga mfano wenu mzuri," alisema Mhashamu Balina ambaye pia ni Msimamizi wa Jimbo la Geita. Aliongeza kuwa hata maaskofu hao watatu wameunda umoja wa majimbo ya Musoma, Shinyanga, Mwanza na Geita.
Katika risala hiyo, vijana hao pia walitaka siku ya Mtakatifu Pius wa Kumi iwe pia ni Siku ya Makoko (Makoko Day) na kuwaomba Maaskofu hao wawe walezi wa jumuiya hiyo vitu ambavyo vilikubaliwa na Askofu Mkuu Anthony Mayala.
"Kuhusu siku ya Mtakatifu Pius wa Kumi kuwa Siku ya Makoko, hilo limepita na hilo la sisi kuwa walezi wote jumuiya yenu nalo pia limepita lakini kama watu mnaoishi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, mlezi wa kwanza atakuwa ni Askofu wetu nasi tutafuatia" alisema Mhashamu Mayala.
Ameshauri kuwa umoja huo usiishie vijana waliosoma katika Seminari hiyo katika miaka ya 1975-85 tu bali hata miaka mingine chini ya 1974 na zaidi ya 1986.
Baada ya kushindwa katika wito wa upadre, vijana hao waliosoma katika seminari ya Makoko, wanafanya kazi katika sekta na idara mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, watafiti, wahandisi ,wakufunzi, wahasibu, wasimamizi wa hoteli, wanasheria, Wataalam wa Benki na waandishi wa habari.
Mbunge ashangazwa na utendaji wa maafisa wa afya
Na Peter Dominic
MBUNGE wa Temeke Bw. John Kibaso ameshangazwa na utendaji wa maafisa wa afya katika baadhi ya kata za Wilaya hiyo kwa kukithiri kwa uchafu uliopelekea kuziba kwa mifereji, hali aliyosema inaweza kuwa chanzo cha mlipuko wa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Bw,Kibaso aligundua kukithiri kwa uchafu huo ,baada ya kufanya ziara ya kuzuru maeneo ya mfereji wa maji machafu wa Mji Mpya ambapo wanachi wa eneo hilo walikuwa wakifanya kazi ya kujitolea kuusafisha mtaro baada ya kufurika takataka na maji machafu kufuatia mvua zilizonyesha hivi karibuni.
"Bwana Afya ni kweli huwa unatembeela huku, unaona hali ilivyo!" alimkaripia kwa mshangao huku akimuonesha choo cha mkazi wa eneo hilo ambacho kilifurika na kuruhusu maji yenye kinyesi yatiririrke kuelekea katika mfereji huo.
Sambamba na hali hiyo,Mbunge huyo alimuamuru afisa huyo wa Afya Bw,Kilave Gregory akifungie mara moja choo cha mkazi huyo ili kisiendelee kutumika kwa ajili ya usalama wa wakazi wa eneo hilo.
Mkazi mmoja wa eneo hilo Bw, Hamis Said alisema sababu zinazopelekea kukithiri kwa uchafu na kuziba kwa mifereji,ni wakazi wa eneo hilo kushindwa kushiriki kikamilifu katika kusafisha mazingira.
"Watu wengi hawataki kushiriki katika swala la usafi kwa kuwa wansema eti hiyo ni kazi ya watu wa CCM", alisema Bw,Said.
Hata hivyo katika utaratibu wa awali waliojiwekea wakazi wa eneo hilo ilikuwa ni kwamba, yule atakayeshindwa kuhudhuria katika siku ya kusafisha mazingira basi atatakiwa kutoa kiasi cha shilingi elfu moja.
HPI yaombwa kuboresha zaidi mazingira ya mkulima
Na Getruda Madembwe
ILI kuyafanya mazingira ya mkulima na mfugaji wa Tanzania yaweze kuonekana ya kisasa, Mradi wa Kimataifa unaojulikana kama HEIFER PROJECT INTERNATIONAL ( HPI) umeombwa kushirikiana na Kanda Katoliki ya Kaskazini Magharibi kukifufua Chuo cha Kilimo Mwadui.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini hivi karibuni kuoka mkoani Shinyanga, ombi hilo lilitolewa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga Mhashamu Aloysius Balina kwenye sherehe ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa vikundi vya akinamama katika kanda hiyo.
Mhashamu Balina ambaye ni mdhamini wa HPI, alisema kuwa chuo hicho ambacho kimekabidhiwa kwenye Jimbo la Shinyanga kitasaidia kuwaelimisha wakulima na wafugaji mbinu bora za kilimo na ufugaji katika mkoa huo na mikoa ya jirani.
Habari zinasema askofu huyo ameishukuru Serikali kwa kuipatia mazingira mazuri kanda hiyo yaliyowaondolea usumbufu katika juhudi za kuwafikia walengwa wao ambao ni akinamama.
Mhashamu Balina aliwataka pia akinamama kuutumia vema ufadhili huu katika kuinua na kubadili maisha yao kimwili na kiroho kwani kufanya hivyo kutaonesha ni jinsi gani wanavyomheshimu Mwenyezi Mungu aliyeweza kutumia viumbe vyake kuwapa ufadhili huu.
Awali wakisoma risala yao akimama hao walisema kuwa katika kuinua hali za wakulima vijijini, mwaka 1995 jimbo lilihamasisha uundwaji wa vikundi ambapo kikundi cha kwanza kilijulikana kama "Nyota Njema" kilichoanzishwa Lubaga ambapo mwaka mmoja baadaye Jimbo lilipokea ng’ombe 16 kutoka HPI Arusha.
Katika risala hiyo ambayo KIONGOZI ina nakala yake, ilielezwa kuwa hadi sasa kuna vikundi zaidi ya 5 vyenye wastani wa wanachama 15 kila kimoja na mradi una ng’ombe 79 ambao tayari wameisha gawiwa katika vijiji vya Lubaga, Mwalugoye Bugaya mbele, Kitangili na kwenye kambi ya walioathirika na Ukoma ya Kolandoto.
Taarifa hiyo ilizidi kueleza kuwa mbali na ngo’mbe hao, mradi huo pia umepokea ufadhili wa mbuzi 48 wa maziwa. Tayari wameisha gawiwa katika vijiji vya Lubanga,Mwalugoye, Mwasele, Bugayambele na kambi ya wenye ukoma Kolandoto.
Serikali yatakiwa irekebishe sheria ya ubaharia
Na Dalphina Rubyema
CHAMA cha Wafanyakazi wa Usafiri Baharini kimesema serikali kushindwa kutekeleza tamko la Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, la kufanya marekebisho ya Sheria ya Ubaharia ya mwaka 1967, inaonesha namna isivyojali ajali zinazotokea majini.
Katibu wa chama hicho cha TASU, Bw.Said El-Mazrui, alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini.
Alisema baada ya kuzama kwa meli ya MV.Bukoba Mei 21, 1996 , Waziri Mkuu BW. Fredrick Sumaye, aliitaka Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kufanya marekebisho ya Sheria ya Ubaharia ya mwaka 1967 iliyosainiwa na Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere , lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea na bado ni fumbo lisilofumbuliwa.
Katibu huyo aliendelea kuwa baada ya tamko hilo Wizara hiyo ilionesha juhudi za mwanzo ambapo iliunda Tume na TASU yenyewe ilishirikishwa na mapendekezo mbalimbali yalipelekwa kwenye Wizara hiyo lakini hadi hivi sasa ni zaidi ya miaka mitatu wizara bado haijatoa tamko lolote.
"Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi haitaki kutujulisha imefikia wapi kuhusu tamko hilo la Waziri Mkuu licha ya Chama chetu cha TASU kupeleka mapendekezo mbalimbali juu ya urekebishwaji wa sheria hiyo. Suala hili sisi linatugusa moja kwa moja kwani katika meli ya MV.Bukoba mabaharia wetu wapatao 16 walipoteza maisha yao," alisema.
Alisema, "Wizara kukahidi tamko hilo la Waziri Mkuu inaashiria jinsi gani Waziri wa wizara hiyo walivyo wazito, kama siyo hivyo mbona sheria hii haibadilishwi?" alihoji kwa mshangao.
Alisema kuwa ukimya huu pia unaonyesha jinsi gani serikali isivyoitilia maanani sekta ya ubaharia kitu kinachowanyima moyo wahusika "Ndio maana hata Mkurugenzi wa Umoja wa Vyuo vya Kimaifa vya Ubaharia (IDMO) ,anasema kuwa hakuna ajali yoyote mbaya ya baharini inayotokea kwa bahati mbaya bali ni ki-uzembe," alisema.
Masista wa Moyo Safi wa Maria Morogoro wapata marubani wapya
Na Sr.Gaspara Shirima,Morogoro
Kishindo kilichojaa vifijo,nderemo, na kengele za hapo kwa hapo viliwashitua Majirani na Wakazi wa Mgolole; kwa ujumla wakati Mhashamu Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro alipomtangaza rasmi Sista Maria Pudensiana Kibena kuwa Mama Mkuu mpya atakayeliongoza Shirika la Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Morogoro (CICM) kwa kipindi cha miaka sita ijayo.
Sista Kibena (45) aliyechaguliwa kwa kura nyingi za wajumbe wa Mkutano Mkuu uliofanyika Machi 22, mwaka huu huko Mgolole, anashika nafasi ya Sista Veronika Maria Petro, aliyekuwa Mama Mkuu wa Shirika hilo kwa kipindi cha miaka kumi na tatu iliyopita.
Masista wajumbe pia walimchagua Makamu wa Mama Mkuu Sista Maria Mamertha (41). Pamoja na hao, walichaguliwa pia wajumbe wa Halmashauri ya Shirika watakaoliongoza shirika hilo pamoja na Sista Kibena
Waliochaguliwa ni: Masista M. Restituta (51), Mshauri wa Kwanza, Sista Maria Celestina Olympya Masaule (48), Mshauri wa Pili na Sista Maria Hermenegilda (47) ambaye ni Mshauri wa Tatu.
Kabla ya Mkutano wa uchaguzi huo, wajumbe wa Mkutano Mkuu walikaa huko Mgolole kwenye nyumba ya Asili ya Shirika hilo la Watawa ili kutathimini na kuona hali ya maendeleo ya shirika kwa kipindi cha miaka sita iliyopita, kufanya marekebisho ya Katiba na kupokea taarifa za Kamati mbalimbali ikiwemo ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa kipindi cha miaka mitatu.
Katika ripoti hizo wajumbe waligundua hitaji kubwa la Elimu kwa wanashirika litakalowasaidia kutoa huduma zao za uenezaji Injili kwa ufanisi zaidi.
Ripoti ya Mama Mkuu ilionesha idadi ya Masista wa shirika hilo tangu lianzishwe 1937 hadi 2000 kuwa ni 422. Huduma zao zimesambazwa katika majimbo ya Morogoro, Dar es Salaam, Same na Zanzibar.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu waliazimia kuteua uongozi unaoingia madarakani ujenge shule ya Sekondari ili kuwawezesha wanashirika kuinua kiwango cha Elimu.
Mvua yafanya mambo katika ibada ya Uaskofu
Na Josephs Sabinus
MVUA iliyonyesha wakati wa ibada ya Uaskofu kwa Mhashamu Methodius Kilaini, imeushangaza umma baada ya kuanza sambamba na maaskofu kumuwekea mikono kichwani na kuisha walipomaliza kisha kuanza na kuisha baada ya Kilaini kuwakomunisha Rais Mkapa na Spika wa Bunge Pius Msekwa.
Katika tukio hilo lililotokea katika viwanja vya Kanisa Katoliki la Msimbazi jijini Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Pengo, aliongoza ibada ya kutoa Daraja la Uaskofu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini.
Ibada hiyo iliyohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamini Mkapa, Spika wa Bunge la Tanzania Bw. Pius Msekwa, Mama Anna Mkapa, Mwenyekiti wa Chama cha siasa cha UDP Bw. John Cheyo na wageni wengine toka ndani na nje ya nchi.
Ulipofika wakati wa maaskofu kumwekea askofu mikono kichwani kumuombea Paji la Roho Mtakatifu, mvua ilianza kunyesha na kuisha sambamba na zoezi hilo lililofanywa na maaskofu wote.
Wakati wa kukomunika, mvua ilianza tena na kumfanya Askofu Kilaini kwenda kukominisha katika jukwaa alilokaa Rais Mkapa na Bw. Msekwa kwa kusindikizwa kwa mwavuli huku maofisa walioandamana na viongozi wao wakitumia miti kusukuma maji yaliyotuama juu ya hema walilokuwa.
Kilichoshangaza ni kukatika ghafla kwa mvua hiyo kubwa baada ya Askofu Mpya Kilaini kukomunisha upande uliokuwepo ujumbe wa Rais akiwemo Rais Mkapa mwenyewe na Bw. Msekwa hali iliyozua hisia mbalimbali.
Akizungumzia hali hiyo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Mhashamu Norbet Mtega, alisema kwa Kiitaliano "Sposa bagnata, Sposa amata" yaani "Mchumba aliyelowa maji ndiye mchumba anayependwa sana."
Akifafanua kauli yake Mhashamu Mtega alisema,
"Kwa tukio hilo ambalo maaskofu wote walikuwapo, Rais wa nchi na waamini, ni ishara ya wazi kwamba Mwenyezi Mungu ametubariki kwa namna ya pekee, Kanisa, Serikali ya Tanzania na watu wake na amembariki askofu mpya kwa namna yake hivyo Watanzania wote tunapendwa na Mungu"
alipoulizwa kama labda ni ishara ya maafa kama mafuriko kwa Tanzania, Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo la Moshi alisema "Hiyo ni tafsiri yako. Mimi ninachojua mahali popote mvua kiasi ni baraka na ile ni baraka watu walilowa tu, kwa kuwa ni maji huwezi kufananisha na mafuriko ya Msumbiji. Kwanza imetokea katika tukio la neema."
Alipoulizwa na gazeti hili jijini, Spika wa Bunge Bw. Pius Msekwa, aliangua kicheko na kukataa kabisa kutoa hisia zake.
"Kwa kuwa ni hiari ya Mungu kufanya lolote kwa namna na wakati wowote, nadhani huenda katika tukio hili ameamua kutuonesha papo hapo kuwa amekubali sala zetu" alisema Askofu wa Jimbo la Rulenge, Mhashamu Severine Niwemugizi.
Askofu Kilaini mwenyewe alisema "Hii naona ni baraka za Mungu kwani haikumdhuru mtu. Na hii mvua si ya kwanza katika sherehe zangu. Hata niliposheherekea Jubilei ya miaka 25 kule nyumbani Bukoba ilianza mvua na tulipomaliza tu, ikaisha"
Januari 8 Baba Mtakatifu alimteua Method Kilaini aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kwa miaka 9 kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na alipewa daraja hilo Machi 18 mwaka huu.
Askofu azawadiwa gari
Na Dalphina Rubyema
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kikatoliki Dar- es -Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amemzawadia gari Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo Mhashamu Method Kilaini akimpongeza kwa kupata daraja la Uaskofu.
Akikabidhi funguo za gari hilo wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa katika Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) siku Mhashamu Kilaini alipopewa Daraja la Uaskofu, Mwadhama Pengo alisema hakuona zawadi nzuri ya kumpa Askofu huyo Msaidizi zaidi ya gari hilo aina ya Toyota Rava alilosema analipenda sana.
Alisema gari hilo ( namba tunadhihifadhi kwa usalama ), ni zawadi ya kibinafsi aliyopewa Pengo na waamini wa jimbo lake la Dar Es Salaam wakati akiadhimisha Jubilei ya miaka 25 katika uaskofu mwaka 1996.
"Mimi nimeangalia zawadi nzuri inayofaa kumpa Askofu Kilaini sikuaona zaidi ya hili gari nililopewa mwaka 1996 katika jubilei yangu.," alisema Mwadhama.
Aliendelea kuwa, pamoja na gari hilo kuwa ni la siku nyingi kidogo, ana imani kuwa bado ni jipya kwani amekuwa akilitumia mara chache na kwa utaratibu mzuri.
Alisisitiza kuwa endapo watafanikiwa kukishirikiana na kufanya kazi zenye kuleta matunda bora na manufaa katika Kanisa, hana shaka kuwa Mhashamu Kilaini atapata gari jingine jipya.
"Najua wewe bado ni kijana zaidi yangu lakini gari hili litakufaa maana tangu nipewe nimekuwa nikilitumia kwa taratibu sana, ingawa najua kuwa ni la siku nyingi kidogo tofauti na magari ya kisasa, lakini utapata jipya na zaidi tukishirikiana na kufanya kazi pamoja zenye kuleta matunda bila shaka hautakosa kununua gari," alisema Mwadhama.
Akidhihirisha kuifurahia zawadi hiyo, mara tu baada ya kukabidhiwa gari hilo, Kilaini aliamua kuliendesha gari hilo kwa kuzunguka maeneo kadhaa ya Baraza la Maaskofu huku akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria hafla hiyo wakiwemo maaskofu wa majimbo mbalimbali na wazazi wake.
Mhashamu Kilaini ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) , Januari 8 mwaka huu aliteuliwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo ll Pili kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na alipewa Daraja la Uaskofu na Kardinali Pengo katika ibada iliyofanyika kwenye viwanja vya Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Askofu Kilaini ni tunda la malezi ya TEC
Na Waandishi Wetu
IMEELEZWA kuwa kazi nzuri iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Mhashamu Method Kilaini hadi kuteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam imetokana na malezi bora na ushirikiano alioupata kutoka kwa Sekretarietiya TEC.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam,Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati wa hafla ya kumpongeza na kumuaga Askofu Kilaini iliyoandaliwa na wafanyakazi wa TEC na kufanyika katika ukumbi wa Baraza hilo.
Mwadhama Pengo alisema kuwa kama wafanyakazi wa TEC wasingeonyesha ushirikiano mzuri kwa kipindi hiki cha miaka tisa ambacho Mhashamu Kilaini amekaa hapo bila shaka matunda mazuriya kutoa Askofu yasingeweza kuonekana.
"Ushirikiano wenu mzuri ndio uliowezesha kupatikana kwa Askofu wa kwanza aliyetoka ngazi ya ukatibu Mkuu ,hivyo ahsantei sana kwa kutulelea Askofu Wetu"alisema Mwadhama Pengo.
Mwadhama Pengoaliendelea kusema kuwa kama wafanyakazi wa TEC wangetenda mambo mabaya dhidi Askofu Kilaini bila shaka angekata tamaa hivyo kushindwa kutenda mambo mazuri aliyoyafanya.
"Siyo kwamba wote wanaokata tamaa na kufanya maamzi mabaya yanatokana yanatokana tu na mawazo binafsi bali hata mazingira ya kazi yanachangia hali hiyo"alisema Mwadhama.
Hadi anateuliwa kuwa Ashofu,Mhashamu Kilaini alikuwa ni Katibu Mkuu wa baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)kazi aliyoifanya kwa kipindi cha miaka tisa kwa hawamu tatu tofauti.