Kanisa Katoliki lawalilia wafungwa

lLasema magereza si mabwana kwa wakati wa wafungwa

lLataka mfumo wa Magereza utazamwe Upya

lWafungwa Dar wapata mgao wa faraja

Na Josephs Sabinus

"LAZIMA pia kuwe na utazamaji mpya wa taratibu za magereza ambao huwaangalia vya kutosha wale ambao wanaumwa sana; au walio kifoni; kadhalika taasisi zinazotoa ulinzi wa kisheria kwa maskini, lazima ziendelezwe".

Amesema Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Yohane Paulo II katika ujumbe wake uliosomwa makanisani jumapili iliyopita katika maadhimisho ya Jubilei ya Wafungwa.

Pamoja na sala maalum na ujumbe huo kama ishara ya tendo la huruma kwa wafungwa siku hiyo waamini wa Jimbo Kuu Kataliki la Dar Es Salaam, walichanga sabuni za kufulia zenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 2 ambazo Mwadhama Kardinali Pengo alizigawa kwa wafungwa wa magereza ya Wazo Hill, Segerea, Ukonga na Keko jijini Dar es Salaam, Jumatano iliyopita.

Kwa mujibu wa Katibu wa Askofu wa Jimbo hilo Padre Stephano Kaombe uamuzi wa kuwapelekea wafungwa sabuni umefuatia kuonekana kuwa moja ya mahitaji muhimu kwa wafungwa kama ilivyobainika wakati jimbo lilipotoa misaada mbalimbali kwa wafungwa wa magereza ya Keko na Ukonga hivi karibuni.

"Walisema haja yao kubwa ni sabuni ili wafue na kuepukana hata na magonjwa ya ngozi kwa kuwa vitu vingine wanapata walau" alisema Padre Kaombe na kuongeza.

"Pia Kikanisa, Usafi ni ishara ya uongofu katika kiroho na kimwili katika kuondokana na uchafu wa kimwili na kiroho".

Alisema Kardinali Pengo na wajumbe wake kumi utawawezesha kila mfungwa katika magereza hayo kupata mche mmoja wa sabuni.

Katika ujumbe wake papa Yohane wa II, amezitaka serikali mbalimbali duniani kufanya marekebisho yanayofaa katika mfumo wa magereza katika baadhi ya mambo ukiwamo utazamaji mpya wa sheria ya adhabu.

"Taratibu zilizo kinyume na haki za msingi za mwanadamu lazima zikomeshwe kabisa katika sheria za nchi kama vile sheria zinazomnyima mfungwa uhuru wa dini" inasema sehemu ya ujumbe huo wa Papa.

Papa alisema ingawa katika baadhi ya magereza sheria inaridhisha bado wafungwa wanapata mateso mengi kutoka vyanzo vingine.

"Ninasema hasa kuhusu hali duni ya baadhi ya sehemu za mahabusu ambamo wafungwa wanalazimishwa kuishi na usumbufu wanaofanyiwa kwa sababu ya ubaguzi wa kikabila, kijamii, kiuchumi, kijinsia, kisiasa na kidini".

Wakati mwingine magereza yanaweza kuwa sehemu za vurugu yakifanana na mazingira ambayo wafungwa wanatoka ni dhahiri hili linabatilisha jaribio lolote la kuelimisha kwa njia ya magereza.

Alisema inawawia vigumu walio magerezani kudumisha mahusiano ya kawaida na familia zao na wanaowapenda kwa kuwa hata mifumo inayolenga kuwasaidia wanaotoka magerezani kurudi katika jamii mara kwa mara hutiwa hitilafu.

Papa ameshauri Dola na Serikali zinazopanga kuanza kupitia upya mifumo ya magereza zao kwa lengo la kuifanya ilingane na mahitaji ya mwanadamu zitiwe moyo ili zifanikiwe.

"Hii inahusisha kutoa shauri zaidi kwa adhabu nyingine kuliko kifungo.

Alisema kuyafanya magereza kuwa ya kibinadamu zaidi ni muhimu zaidi ili kuwawezesha wafungwa kushiriki kazi zinazowalinda dhidi ya athari za kuvunjiwa heshima.

Papa alishauri wafungwa wapewe mafunzo yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika nguvukazi wamalizapo vifungo vyao na hivyo kuyamudu maisha ndani ya familia zao.

"Msaada wa kisaikolojia ambao waweza kuwasaidia kutatua matatizo ya nafsi usidharauliwe. Magereza yasitoe uzoefu wa uhalifu, sehemu ya uvivu na hata maovu lakini pawe sehemu ya ukombozi," alisema Papa.

"...Nageukia mamlaka za dola nikiwaomba wafanye tendo la huruma kwa wale wote walioko magerezani kupunguza hata kwa wastani wa kipindi cha kifungo itakuwa ni ishara ya unyeti wa hali yao; na kwa hakika itaamsha mwanga chanya katika mioyo yao na kuwatia shime kujutia maovu waliyoyatenda na kuwaongoza katika malipizi binafsi".

KUSHINDWA KUDHIBITI RUSHWA:

Mkapa asema madaktari, wanasheria 'wanalindana'

Na Peter Dominic

RAIS Benjamin Mkapa amewapiga madongo wanataaluma mbalimbali wakiwamo madaktari na wahandisi kuwa wanalindana na hivyo kukwamisha juhudi za serikali yake katika kupambana na rushwa.

Amewataka Watanzania kuwanyima kura wagombea wa uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 29, mwaka huu, ambao watatafuta kura kwa njia ya utapeli na ulaghai wakiwashawishi kwa rushwa badala ya sifa sahihi za uongozi.

Mkapa aliyasema hayo mjini Dodoma wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mara ya mwisho kabla ya kulivunja Jumanne ijayo.

Katika hotuba yake hiyo mwishoni mwa juma, Mkapa aliyetumia muda mwingi kulieleza Bunge mafanikio ya serikali katika kipindi cha uongozi wake, hotuba iliyorushwa moja kwa moja na Redio Tanzania kutoka Dodoma, alieleza mapungufu kadhaa yaliyojitokeza katika sekta mbalimbali katika mapambano dhidi ya rushwa vikiwamo vyombo vya sheria.

"Iwapo wanasheria na vyombo vya mahakama watakuwa ndicho kichaka cha rushwa, wananchi wakimbilie wapi? Maana hata serikali inapowatuhumu wala rushwa, huwafikisha mahakamani," alisema na kuongeza kuwa ingawa serikali inalifahamu hilo, inashindwa kuingilia uhuru wa mahakama.

"Hata sisi tunasoteshwa mahakamani na wakati mwingine, tunaambiwa hatuna uthibitisho wa kutosha kumtia mtu hatiani,"

Aliwataka Watanzania kuachana na dhana potofu kuwa ili serikali ionekane inapambana na rushwa, lazima iwakamate vigogo na kuwashitaki, bila kujali kuwa, upo umuhimu wa kupata uthibitisho wa kutosha kwanza.

Alionya kuwa kamatakamata ya ovyo ovyo, inaweza kuwafurahisha watazamaji lakini, isisaidie kuondoa tatizo na pia akasema hiyo ni kinyume na utawala wa kisheria.

"Taaluma nyingine zinalalamikiwa kwa rushwa hatuoni hatua zozote zinazochukuliwa juu yao utafikiri wanakula yamini ya kulindana na kufichiana aibu."

Rais Mkapa alisema, "Madaktari na wauguzi wana vyama na wanajuana kabisa ni nani mla rushwa, ni nani mnyanyasaji wa wagonjwa, lakini sijasikia ni mara ngapi, kwa uwazi na ukweli wameonyana na kuchukuliana hatua za kinidhamu kwa misingi ya kanuni na kiutendaji kwa kazi yao ya taaluma," Alizidi kusisitiza kuwa licha ya baadhi ya barabara hukusudiwa kutumika kwa miaka 20,lakini baadhi yake hapa nchini zinaweza kutumika kwa mwaka mmoja tu, bado haijawahi kusikika kuwa taaluma ya uhandisi na ujenzi, wamemfukuza mwanchama mwenzao kwa kazi mbovu itokanayo na rushwa na kwamba wanataaluma hiyo hawastahili kukwepa lawama.

"...Maana wao si lazima wathibitishe kwa kiwango cha kimahakama, ubovu wa kazi unatosha kuchukua hatua za nidhamu," alisema.

Kanisa la AICT ladaiwa milioni 3/=

Na Mwndishi Wetu, Mwanza

DHEHEBU la African Inland Church Tanzania(AICT), linadaiwa jumla ya shilingi milioni tatu na Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT)na huenda likafutiwa uanachama endapo litazidi kuchelewesha deni hilo.

Deni hilo ni malimbikizo ya ada ya michango mbalimbali ya kipindi cha miaka mitatu ya uanachama wa kanisa hilo kwa CCT.

Askofu Mkuu wa AICT nchini, John Nkolla amesema jijini hapa(Mwanza) kuwa kutokana na deni hilo, uanachama wao kwa CCT uko mashakani.

Kulingana na katiba CCT, iwapo mwanachama atashindwa kuwasilisha michango na ada yake kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, uanachama wake utafutwa.

Nkolla ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Shinyanga ya Kanisa hilo, alisema tayari kanisa lao limeanza kuchukua hatua thabiti ili kuwezesha deni hilo kulipwa na hivyo kuendelea na uanachama wake kama kawaida.

Alisema katika kuchukua hatua hiyo, tayari Katibu Mkuu wa AICT nchini, Bw. J.M Mapessa, amewaarifu maaskofu na wachungaji wa dayosisi zote tano za Kanisa hilo juu ya kuwepo kwa deni hilo.

Dayosisi tano za Kanisa hilo zilizoko nchini ni Mwanza yaliyoko makao makuu ya AICT, Pwani, Geita, Shinyanga, Mara na Ukerewe zinazounda dayosisi moja.

Hivi karibuni wakati Maaskofu na Wachungaji wa AICT wa Dayosisi zote walipokutana hapa Mwanza, Katibu Mkuu wa kanisa hilo aliwaagiza kuwasilisha michango yao makao Makao makuu ili kanisa lao liweze kulipa ada yao kwa Baraza la Makanisa kabla ya Desemba mwaka huu.

Maaskofu na Wachungaji hao waliambiwa kuchelewesha kuwasilisha michango hiyo kutahatarisha uanachama wa kanisa lao katika jumuiya hiyo na wakahimizwa kuwasilisha michango yao kabla ya Agosti.

CCT ni Umoja wa Mshikamano wa Makanisa ya madhehebu mbalimbali ya kikristo ambapo mmoja wa viongozi wa juu wa Baraza hilo ni Askofu kutoka Kanisa hilo la AICT

... Pengo aonana uso kwa uso na wafungwa Dar

l"Asema msililie msongamano gerezani, lilieni amani"

lAwakuta watoto wachanga na kuwabeba gerezani

Na Dalphina Dalphina

KAMA walivyo binadamu wengine, wafungwa na mahabusu wanapaswa kulindwa na kupewa haki zote za msingi bila kujali aina wala ukubwa wa makosa waliyotenda; amesema Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Amesema jamii wakiwamo wafungwa kuililia serikali iongeze wingi na ukubwa wa magereza kuepuka ni kujidanganya bali njia muafaka kukabili msongamano katika magereza, ni kuepuka matendo maovu.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini mwishoni mwa juma, Kardinali Pengo, alitoa kauli hiyo alipotembelea magereza za mkoa wa Dar-Es-Salaam, ambazo ni Wazo Hill, Segerea, Ukonga na Keko.

Katika ziara yake iliyowashirikisha mapadre, watawa na walei, Mwadhama Pengo alisema jamii haipaswi kuwachukulia wafungwa na mahabusu kama kundi la watu lililo tofauti na binadamu wengine, bali ijue kuwa wao ni binadamu walivyo wengine na kwamba makosa waliyotenda na kuwafikisha huko, ni ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika cha habari, Kardinali Pengo aliitaka jamii wakiwamo wafungwa kuacha kuililia serikali ili iongeze wingi na ukubwa wa magereza kutokana na msongamano uliopo katika magereza nchini, bali iepuke kufanya matendo yanayo mchukiza Mungu na yaliyo kinyume na sheria za nchi.

"Kuhusu suala la ‘overcrowd’ ambalo ni kilio cha muda mrefu, hili kwa kweli linasababishwa na sisi wenyewe, hivyo tujihadhali kutenda maovu na siyo kuipigia serikali kelele ya kuongeza magereza," alisema.

Aliongeza kuwa mtu anayefanya kwa makusudi matendo hayo yaliyo kinyume cha mapenzi ya Mungu na sheria za nchi, hana budi kwenda chuoni ambako ni magereza ili akajifunze umuhimu wa kufanya hivyo.

Aliwahimiza wafungwa na mahabusu hao kubadili maisha yao na kumgeukia Mungu ili pindi warudipo katika makazi yao ya uraiani, waishi maisha ya kumpendeza Mungu na jamii ya wanadamu inayowazunguka.

Hata hivyo Kardinali alisema kitu cha msingi kwa binadamu walio uraiani, ni kuwaombea hao ndugu zao wafungwa ili wakubali kutubu makosa yao hasa mbele za Mungu na kuwa tayari kubadilika pindi watakaporudi katika familia zao uraiani.

Kwa mujibu wa habari hizo zilizopatikana, Kardinali Pengo alisema, "Unapokataa kubadilika, unapoteza hadhi ya ubinadamu na kuwa na sifa ya kiibilisi na matokeo yake, unapata laana ya milele."

Habari zinasema kuwa katika matembezi hayo yaliyomshirikisha Afisa mmoja wa Magereza mkoani Dar-Es-Salaam kama mwenyeji wa msafara huo, Mwadhama Pengo kwa niaba ya Jimbo lake aligawa sabuni kwa wafungwa na mahabusu hao ambao kila mmoja alikusudiwa kupata mche mmoja wa sabuni ya kufulia.

Kwa mujibu wa habari, katika ziara hiyo Kardinali Pengo alipata fursa ya kuzungumza na mahabusu na wafungwa katika magereza hayo na kuwafariji wafungwa kwa kushikana mkono na baadhi yao.

Habari zimesema katika gereza la Keko, alipata fursa ya kuwabeba watoto wachanga wawili ambao wapo gerezani hapo na mama zao ambao ni watuhumiwa.

Juni 20 na Juni 22 mwaka huu, Tume ya Haki na Amani Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, ilitoa msaada wa viatu, kandambili, nguo na sabuni katika magereza ya Keko na Ukonga na msaada kama huo unatarajiwa kutolewa katika magereza ya Segerea na Wazo.

LICHA YA MAKUBALIANO YA KUWA NA MGOMBEA URAIS MMOJA:

CHADEMA yasema haipendezwi na Sera za CUF

lDk. Kabourou asema zinatishia amani

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Amani Walid Kabourou, amesema mtindo wa CCM na CUF kuunda vikundi vya vijana vyenye sura ya kijeshi ni hatari kwa amani ya Tanzania.

Dk. Kabourou, alikuwa Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kinondoni, jijini wiki iliyopita, juu ya hali ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Alisema, kikundi cha "Blue Guard" cha CUF na vile vya Maskani na Mashina ya Wakareketwa ambavyo viongozi wake wanaitwa Makamanda kama ilivyo jeshini, ni mbegu ya machafuko ambayo vyama hivyo vinaipada bila kujua.

CCM ina kamanda wa vijana katika kila Jimbo la Uchaguzi nchini.

alitoa mfano wa vikundi vya namna hiyo kuwa ni kama kile cha "Interahamwe" (tupigane pamoja) cha Burundi ambacho nacho kilitokana tu, na vijana wa mtaani waliotumiwa na wanasiasa hadi kiliposhiriki katika mauaji ya maelfu ya watu.

Alikilaumu Chama cha Mapinduzi kuwa ndicho chanzo ch hali ya sasa inayoilekeza nchi katika maafa na kuwatetea CUF kuwa wao wamelazimika kuunda Blue Guard kwa vile wananyanyaswa sana na watawala na vyombo vya dola.

Juu ya sera za "jino kwa jino" za CUF na zile za "shavu kwa mashavu" zilizotangazwa hivi karibuni na Makamu Mwenyekiti wa CCM -Taifa Bw. John Malecela, Kabourou alisema nazo ni ishara kuwa tuendako si salama.

Mwanasiasa huyo alisema hali hiyo pamoja na ile ya polisi kutumika kuwapiga au kuwadhibiti wapinzani kimabavu inawajenga na kuwazoeza wananchi roho ya machafuko ambayo ikishakomaa haitawezekana tena kuidhibiti.

"Watu wanazoezwa ‘violence’, wakishazoea hawatawezekana tena," alisema.Akiongelea Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alisema haina maafisa katika mikoa kwa hivyo, unapofika uchaguzi, maafisa utawala wa mikoa na watendaji wengine na Serikali hugeuka kuwa maafisa wake(wasimamizi wa Uchaguzi) na baada ya hapo, uhusiano huisha.

"Ina maana Mwenyekiti wa Tume hana Mamlaka yeyote juu ya watu hawa wanaomfanyia kazi. Hawezi kuwafanya lolote hata wakicheza rafu," alisema.

Kabourou, alisema wapinzani wataendelea kushiriki Uchaguzi licha ya Tume kutokuwa huru kwani ipo siku ulaghai wanaodhani wanafanyiwa, utakoma.

Alisema demokrasia Tanzania bado changa, na akatoa mfano wa mtindo wa kuwapa wanachama kadi na kupeperusha bendera kila mahali, huku wanachama hao wakiwa hawajui vizuri sera za vyama na hata masuala muhimu ya nchi.

"Nchi kama Marekani, watu hawabebi tena kadi za vyama na ni nadra kukutan ana bendera zikipepea. Watu wanaelewa nini wanachotaka si kadi wala bendera", alisema.

Hatua ya Dk. Kabourou kukosoa vikundi vya Blue Guard, Maskani na vikosi vya wakereketwa wa CCM, imekuja siku tatu tu, baada ya chama chake (CHADEMA) na CUF kukubaliana kumsimamisha Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya vyama hivyo viwili.

Askofu ngonyani kuongoza mahujaji Israel

Na Leocardia Moswery

MWENYEKITI wa Tume ya Ekumene na Mahusianao na Dini Nyingine, Askofu Bruno Ngonyani,Jumapili hii anaongoza msafara wa mahujaji 16 wa Tanzania kuelekea Israel.

Kwa Mujibu wa Mratibu wa Msafara huo ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Kichungaji ya Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania (TEC), Padre Theobald Kyambo,safari hiyo ya mahujaji itaanza Julai 16 hadi 27, mwaka huu.

Alisema safari hiyo itakayoongozwa na Mhashamu Ngonyani ambaye ni Askofu wa Jilbo Katoliki la Lindi,itawahusisha waamini kwenda mahali palipowekwa wakfu kwa matukio fulani ya ki-Mungu ili kutolea sadaka zao katika mazingira yanayokubalika.

Akihimiza umuhimu wa Wakatoliki kushiriki hija, Padre Kyambo alisema, "Hija huwakumbusha mahujaji kuwa wako safarini kumuendea Bwana Yesu Kristo, chini ya uongozi wake."

Alisema mahujaji hao wataondoka nchini na ndege ya Shirika la Ndege la Uswis,(Swiss Air) na kuitumia hiyo hiyo wakati wa kurudi.

Alisema katika safari yao wawapo Islael, watashirikiana na Padre Adam Civu wa Notre Dame, Yerusalemu. Mratibu huyo wa Hija aliyataja maeneo watakayotembelea wawapo katika nchi Takatifu kuwa ni kanisa la Mtakatifu Anna, Stephen’s Basilica.

Mengine ni sehemu ya Yerusalemu ya Magharibi, Mashariki, Kusini na Kaskazini na kisha kumalizia katika maeneo ya Pwani ya Mediterania.

Kwa kawaida, kabla ya kuondoka kwenda hija, mahujaji hupewa semina juu ya mambo kadhaa muhimu ya kuzingatia wawapo safarini.

Watakaoshiriki safari hiyo na majina ya majimbo wanayotoka kwenye mabano ni, Padre Fortunato Amadori (Dodoma), sista Oktavya Y. Gomano(Iringa),Askofu Bruno Ngonyani (Lindi), Monsinyori Calitus Mdai (Mahenge) na Padre Emil L. Mpeka (Morogoro).

Wengine ni Bw. Theobald I. Mkongwa (Morogoro), Bw. Abiud Jeremia Silaa (Moshi), Bi. Irene A.J. Silaa(Moshi),Sista Galgani Shirima (Shinyanga), Sista Ludwina katabi (Sumbawanga),Padre Paul Chiwangu Kongocha(Songea), na Bw. Ernest E. haule (Songea)

Wengine katika msafara huo ni, Padre Denis Ndomba (Sumbawanga) Sista Cyrilla C. Kessy (Tanga), Bi. Mary B. Hokororo na Padre Theobald Kyambo wote wa TEC

KUBORONGA KWA UVIKIUTA:

BET yasema haihusiki

Na Waandishi Wetu

KAIMU Mkurugenzi wa Uwanja wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara jijini, Bw. Emanuel Buriki, amesema Uongozi wake hauna uhusiano na Kikundi cha UVIKIUTA, mbali na zabuni waliyoshinda ya kusimamia shughuli za maonesho mwaka huu.

Kauli hiyo imekuja baada ya gazeti hili kutaka kupata ufafanuzi kutokana na malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya vijana waliofanyiwa usaili na kikundi hicho kuwa majina yao yalifutwa kwa kuwa uongozi wa BET, uliwashinikiza UVIKIUTA

kuajiri watu wao kushiriki usimamizi huo badala ya walioshinda usaili.

"Hatuna habari na kikundi hicho na hatujui ni lini walifanya usaili wala walihitaji watu wangapi.

Haiwezekani BET ikashirikiana nao kuajiri. Wao walipewa ‘contract’ baada ya kishinda kusimamia maonesho. Suala la kuajiri liko juu yao, na wala sisi hatuhusiki," alisema Kaimu Mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa, BET haiwajibiki kwa suala hilo.

Vijana kadhaa waliofanyiwa usaili huo siku chache kabla ya kuanza kwa Maonesho ya 24 ya Biashara ya Kimataifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Sabasaba jijini,

Walilalamika kuwa katika usaili huo kulikuwa na upendeleo na usumbufu ulioashiria kutaka rushwa.

Pia, baadhi ya vijana hao walisema baadhi ya majina yaliyochaguliwa katika usaili huo, yalifutwa katika orodha ya mwanzo na kupandikiza mengine hali inayodaiwa kuwa ilifanyika baada ya wahusika kushindwa kuwapa chochote wasimamizi.

Gazeti lilipofuatilia ukweli wa tuhuma hizo katika ofisi ya muda ya (UVIKIUTA) iliyopo ndani ya ofisi za BET chumba namba 6 kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Idara ya Uzalishaji Bw. Joel Lushinga, na Mkuu wa Idara ya Biashara na Utawala wa UVIKIUTA, Bw. Ben Mongi, walikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa wao si wasemaji na kwamba anayepaswa kulizungumzia ni Mwenyekiti wao Bw. Jordan Lugimbana, ambaye yuko katika mbio za mwenge.

Baada ya kushinda zabuni ya kusimamia maonesho, UVIKIUTA walitangaza nafasi za kazi kwa vijana bila kufafanua sifa zinazotakiwa.

Taarifa za awali zilizotolewa na kikundi hicho zilimtaka muombaji kuandika barua na kufika siku ya Ijumaa katika ofisi zao saa 2:00 kwa ajili ya usahili .

Siku hiyo umati wa vijana ulizingira eneo hilo wakisubiri usaili hadi saa nne mabasi yalikuwa yakiendelea kuwamwaga vijana kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar-Es-Salaam.

Vijana zaidi ya 400, barua zao zilisomwa hadharani kwa kutaja jina na kisha kuingia chumba cha usaili, walielezwa kuwa waliotakiwa ni 90.

Kwa mujibu wa walalamikaji hao, walikuta majina yao katika orodha ya washindi lakini yalipigwa mstari na walipohoji wakaelezwa kuwa majina yao yalipitishwa kimakosa na wengine kupewa majibu yaliyoashiria kudaiwa rushwa.

"Nilielezwa kuwa nisingeweza kupitishwa bila kwenda na mkono mrefu" alisema mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Watu wazima Mwanza watishia kwa ukimwi

Na Steven Mchongi

IDADI kubwa ya watu wazima wanajitolea damu katika hospitali ya Rufaa ya Bugando ya mjini hapa, wameathirika na Ugonjwa hatari wa ukimwi.

Hospitali hiyo sasa inategemea zaidi kupata damu salama kutoka kwa vijana na wanafunzi wa shule za sekondari ambao imeonekana bado hawajaathirika sana na ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa Benki ya Damu hospitalini hapo Dk. Abdul Mohamed alisema kati ya watu wazima 425 waliojitolea damu mwaka jana, zaidi ya 34, sawa na asilimia 8.3 walionekana wameambukizwa ukimwi, wakati asilimia 1.8 ya wanafunzi 110 waliojitolea damu, walionekana wana virusi.

Alisema mwaka 1998, kati ya watu wazima 1546 waliojitolea damu, 177 sawa na asilimia 11.4, walipatikana na virusi vya ukimwi, wakati kati ya wanafunzi 404 waliojitolea damu, ni 14 tu, sawa na asilimia 3.4 waliokutwa na virusi.

Kulingana na takwimu hizo, mwaka 1997, kati ya watu wazima 1956 waliojitolea, 205 sawa na asilimia 11, waliokutwa na virusi.

Takwimu hizo zimetolewa katika kipindi hiki ambapo Rais Benjamin Mkapa amewataka Watanzania kupambana waziwazi na ugonjwa wa Ukimwi bila kuona haya.

TANGO yataka wanawake kupigiana debe katika uchaguzi

Na Neema Dawson

TATIZO la wanawake kutopata nafasi za uongozi litaendelea kuwepo endapo wanawake hawatasaidiana katika kuhamasisha kuwapigia kura wenzao wakati wa uchaguzi mkuu kwa kuhofia kuambiwa kuwa wanavipigia debe vyama vingine.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini(TANGO),Bi. Marie Shaba, alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini kuhusu nafasi maalumu ya kugombea viti maalum vya wanawake katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Madiwani na Wabunge unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

"Wanawake tumekuwa tukilalamika kuwa wanaume wanatugandamiza wakati wanaume wako mstari wa mbele katika kupigania kampeini wakati wa kugombea nafasi muhimu za uongozi. Haya sasa, tumeishapewa nafasi maalum kwa wanawake na zinaweza kutushinda endapo tutaweka ubinafsi na kutopendana sisi kwa sisi," alisema.Alisema pamoja na UWT kupewa viti maalum, bado kuna wanawake wenye uwezo wa kuongoza.Alitolea mfano Bi. Edith Lucina aliyemsema kama mwanamke pekee kutoka chama cha NCCR-Mageuzi, aliyejitokeza kugombea nafasi ya urais hivyo kuwataka wanawake wengine kujitokeza kumuunga mkono bila kuhofia kufikiria kuwa watasemwa kwamba wanavipigia debe vyama fulani.

Mwenyekiti huyo aliongeza kusema kuwa, katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO) wapo wanawake wengi wenye uwezo wa kuongoza na kwamba hata wao hawana budi kujitokeza.

Bibi.Shaba alisema kufanya hivyo kutawasaidia wanawake wengi kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Diwani akataa matokeo ya kura za maoni

Na Gerald Kamia, DSJ

WAKATI Kura za maoni za kuchagua wagombea wa kiti cha Udiwani watakaowakilisha Chama cha Mapinduzi(CCM) katika Uchaguzi Mkuu ujao zikiendelea mkoani Morogoro, mmoja wa vigogo kadhaa walioangushwa katika kinyang’anyiro hicho. Bw.Yusuph Thabiti, amedai hakubaliani na matokeo kwa madai kuwa uchaguzi haukufuata haki.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jijini dar-Es-Salaam, wiki iliyopita, Bw. Thabiti amesema, "Sikubaliani na matokeo haya kwa kuwa haki haikutendeka katika tawi la Forest badala yake, rushwa ilitawala katika tawi hilo kwani katika matawi ya Kibwe na Madizini, nilimshinda Nyambulizi baada ya kuona hivyo ilibidi atumie rushwa ili kuweza kuwarubuni wananchi wa tawi la forest mimi ushindi ninao na nitakata rufani kupinga matokeo hayo," alisema.

Katika kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni, inaonesha kuwa madiwani wengi wamekuwa wakiangushwa katika kata zao kwa kile kilicho lalamikiwa na wananchi kuwa walikuwa wakijali zaidi manufaa yao kuliko ya wananchi.

Wakati huo huo: wakazi wa manispaa ya Morogoro wamekitahadharisha chama cha mapinduzi kuwa makini zaidi katika kupendekeza jina la mgombea wa Ubunge wa Manispaa hiyo.

Kuna habari kuwa Mkurugenzi wa Makampuni ya Abood, Aziz Abood kuwa ni miongoni mwa watu watakao waniia Ubunge katika manispaa hiyo.Wakizunguma na Mwandishi wa gazeti hili Bw. Musa Abasi na Nestor Mgaya kutoka Kata ya Kichangani na Hamisi Dikwe, kutoka kata ya Kilakala, wamesema kama CCM watalipendekeza jina la Abood basi wajue watashindwa vibaya ni bora tuvipe kura vyama vya upinzani kuliko kumpa Abood walisema.

Mawaziri wa Z'bar wavutiwa na maonesho ya akinamama Sabasaba

Christina Mbezi na Debora Kasomwa (DSJ)

BAADHI ya mawaziri kutoka Tanzania Visiwani, wamevutiwa na Maonesho ya akinamama yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar-Es-Salaam, wakati wa Maonesho ya 24 ya Kimataifa ya Biashara Wakielezea kuridhishwa kwao kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania Bara, Shamim Khan siku ya mwisho ya maonesho hayo wiki iliyopita, mawaziri hao wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wa Viwanda na Masoko, Hamis A. Musa na Waziri wa Kilimo Brigedia Adam Mwakanjuki, walisema nje ya jengo la Bodi ya Biashara ya Nje (BET), kuwa wamevutiwa kutokana na ushirikiano uliooneshwa baina ya washiriki toka Tanzania Bara na Visiwani.

Hata hivyo, akifananisha maonesho hayo na yale yaliyofanyika Visiwani Zanzibar kwa mara ya kwanza, Novemba mwaka jana, Brigedia Mwakanjuki, alisema idadi ya Watanzania Bara, walioshiriki maonesho hayo, ilikuwa ndogo ikilinganishwa na Wanzanzibar walioshiriki maonesho ya mwaka huu jijini Dar-Es-salaam.

Mwakanjuki alishauri mamlaka husika kuona uwezekano wa kupunguza nauli za boti zifanyazo safari kati ya Tanzania Bara na Visiwani, wakati wa maonesho ili kutoa unafuu kwa wananchi wa pande zote kushiriki.

"Pengine ungetafutwa utaratibu ili bei za boti wakati wa maonesho zipungue ili watu wavuke kwa unafuu," alisema.

Akisifia maonesho hayo ya akinamama mbele ya wageni wake, Naibu Waziri Shamim Khan, alisema, "Watu wengi wanaofika katika maonesho ya viwanja hivi, wasipofika katika mabanda haya ya akina mama, wanajisikia kama kwamba hawajafika kwenye maonesho."

Milioni 5.6 zachangwa kwa ajili ya wanawake

Na Dalphina Rubyema

CHUO Kikuu Huria nchini ‘Open University of Tanzania’ kimepokea zaidi ya shilingi milioni 5.6/= kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchangia mfuko wa wanawake.

Taarifa kutoka chuoni hapo zinasema kuwa pesa hiyo sh. 5,614,819, imechangwa wakati chuo hicho kikifanya uzinduzi wa vituo vyake katika mikoa ya Lindi, Kagera, Shinyanga, Arusha na Tanga.

Taarifa zilithibitishwa na Makamu Mkuu Msaidizi wa Chuo, Profesa Msungu, zimesema uzinduzi wa vituo hivyo ulifanyika kati ya Mei 2 na Juni 27, mwaka huu.

Jumla ya sh. 410,000/=, zilichangwa Mei 2 wakati wa uzinduzi wa kituo cha Mkoa wa Lindi, wakati mkoa wa Kagera katika uzinduzi wake Mei 6, ulichanga sh. 1,289,819/=.

Zimesema chuo hicho huria katika uzinduzi wa kituo cha Shinyanga, Mei 9 mwaka huu, zilichangwa sh 2,000,000/= ambapo uzinduzi wa kituo cha mkoa wa Arusha hapo Juni 24, uliingiza sh 415,000/=

Katika uzinduzi wa kituo cha mkoani Tanga Juni 27, jumla ya sh. 1,300,000/= zilichangwa na jumla ya pesa yote kwa mikoa hiyo mitano ni sh. 5,614,819.

Wakati huo huo: Chuo Kikuu hicho huria kimepokea vitu mbalimbali vyenye thamani ya dola za kimarekani 45,000 ambayo sawa na sh. 36,000,000 pesa ya Kitanzania.

Waislamu wasio ona kushindana kusoma Quran

Na Jenifer Aloyce, DSJ

TAASISI moja ya Kiislamu nchini, World Muslim Congress, inatarajia kufanya mashindano ya kusoma Quran kwa wasioona mkoani Dar-Es-Salaam, ambayo kwa mara ya kwanza yatafanyika nchini katika Hotel ya Star Light , jijini Julai 30, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkurugenzi wa World Muslim Congress, Sheikh Mohamed Rukara, aliyezungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa juma ofisini kwake eneo la Kariako jijini, lengo la mashindano hayo ni kuwawezesha Waislamu wasioona kujifunza zaidi namna ya kusoma kitabu hicho licha ya hali yao ya ulemavu wa macho.

Kwa kawaida walemavu wamacho hutumia maandishi maalunu wanayoyasoma kwa kupapasa na vidole.

Pia alisema taasisi yake ina mpango wa kufungua duka la akina mama la mshikamano katika eneo la Kawe jiji hapa ili akina mama wajisaidie katika kuyakabili maisha kwa kufungua miradi mbalimbali ya uzalishaji.

Aliwataka pia viongozi wa taasisi hiyo kuwa tayari kutenda mema yanayoamriwa na pia kuwa tayari kukosoana kwa kuwa mkosaji mwema ni yule anayekubali kukosolewa.

Taasisi hiyo iliyofunguliwa Desemba 28, 1998,pia hutoa mafunzo mbalimbali kwa watu mbalimbali wasiojiweza ukiwemo ushonaji na ufumaji wa vitambaa.

Mahenge wapata 'wali' wanane kwa mkupuo

Na Pd. Chrysantus Ndaga, Mahenge

JIMBO katoliki la Mahenge limetunukiwa baraka za Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 kwa kuwapata kwa mara ya kwanza, mapadre wanane kwa pamoja, kati yao, wawili wakiwa ni Watawa.

Katika sherehe zilizoanzia parokiani Mlimba Julai Mosi mwaka huu, shemasi Godfrey Gingo alipewa Daraja ya Upadre, na kufuatiwa na shemasi Wolfram Ngwambala aliyepewa Daraja hiyo parokiani Mchombe siku iliyofuatia.

Parokiani Ifakara, mashemasi, Deogratias Kisweka, Ignas Kilolero na Revocatus Ngukuyaweni, walipewa Daraja hiyo Julai 3, mwaka huu na shemasi Norbert Kalimang’asi akaipata Daraja siku iliyofuataa parokiani Malinyi.

mwingine aliyebahatika kupata Daraja Takatifu ni shemasi Pius Nagawantu wa Shirika la Mitume wa Yesu aliyepewa Daraja hiyo Julai 5, katika parokia yaIsongo na hivyo kuwa padre wa kwanza wa Shirika hilo jimboni Mahenge na Parokia ya Isongo iliyozinduliwa mwaka 1996 wakati wa sherehe za miaka 75 za Uinjilishaji wa Jimbo la Mahenge na wamisionari wa Shirika la Ndugu Wafransiskani Wakapuchini na Masista wa Balgegg kutoka Uswisi.

Sherehe zilifikia kilele Julai 7, mwaka huu, siku ya Jubilei ya Wakleri (mapadre) ambapo Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo alitoa Daraja ya Upadre kwa Shemasi Victor Lijaji wa Shirika la Wamisionari wa Afrika katika kanisa Kuu la Kristu Mfalme Kwiro Mahenge, Padre Lijaji anakuwa Padre wa kwanza wa Shirika la Wamisionari wa Afrika Jimboni Mahenge.

Kwa idadi hiyo ya mapadre wanane kwa mwaka mmoja, Jimbo la Mahenge limeweka rekodi mpya tangu lianzishwe Julai Mosi, 1964.

Rekodi ya juu ya zamani iliyofikiwa ni mapadre sita kwa mwaka mmoja ambapo walipatikana mwaka 1972 na mwaka 1992.

Akizungumza katika kilele cha sherehe hizo zilizofanyika katika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme Kwiro, Askofu Ndorobo aliwataka waamini wote kumshukuru Mungu kwa neema kubwa ambazo Mungu amelijalia jimbo la Mahenge na hivyo kuwataka waumini wote wafanye hija, kila parokia na mpango wake ikiwa ni ishara ya shukrani hizo kwa Mungu.

"Kiutaratibu Daraja ya Upadre hutolewa katika Kanisa Kuu, lakini kwa kuwa mwaka huu ni Jubilei, tumeona ni vema baraka hizo zifike pia Maparokiani. Ninaomba tufanye hija. Parokia ile ambayo inataka kufanya hija naomba iniarifu ili nami nipate kushiriki," alisema.

Wakati huo huo: Mapadre Jakob Danda, paroko wa parokia ya Mofu na Padre Yonas Mayombo paroko Msaidizi Parokia ya Kwiro wamemshukuru Mungu katika misa ya Jubilei ya Wakleri kwa kudumu katika utumishi wa Shamba la Bwana kwa miaka 25.

Naye Steveni Mchongi anaripoti kutoka Mwanza kuwa: Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza limefanya mabadiliko ya uhamisho wa mapadre watatu katika parokia tatu za hapa Mwanza.

Taarifa iliyotolewa Julai 2 na Mhashamu Askofu Anthony Mayala kwa parokia zote hapa Mwanza imesema kuwa mabadiliko hayo yanaanza mara moja.

Mapadre waliohusika katika uhamisho huo ni Mathayo Bujiku na Doni Andresson wa parokia ya Kirumba, Valentne Kabati wa parokia ya Nyabiti na Pius Chiza wa Parokia ya Kawekamo.

Kulingana na mabadiliko hayo Padre Mathayo Bujiku wa Parokia ya Kirumba iliyoko katika jiji la Mwanza (Zamani manispaa) anahamia Parokia ya Magu iliyoko nje kidogo ya mji, wakati Padre Doni Andresson anahamia Arusha.

Padre Valentine Kabati aliyekuwa parokia ya Nyambiti anakwenda parokia ya Kirumba ambapo atasaidiana na Padre Pius Chiza aliyetoka parokia ya Kawekamo yaliyoko makao makuu ya Askofu.

Taarifa hiyo ya Kanisa imewataka waamini wote katika parokia hizo zilizohusika kuwapokea na kushirikiana na mapadre hao.

Kufuatia mabadiliko hayo tayari waamini wa parokia zilizohusika wameanza kuandaa sherehe za kuwaaga na kuwapokea mapadre hao.