Kwaya ya Mt. Sesilia iliyopania kuimarisha amani

Na Getruder Madembwe

Kwaya ya Mtakatifu Sesilia ni mojawapo ya vyama vya kitume vilivyopo Parokia ya Mtakatifu Maxmillian Maria Kolbe, Mwenge jijini. Shughuli yake ni kutangaza Neno la Mungu kwa njia ya nyimbo.

Mwenyekiti wa kwaya hiyo Merida Mulumba amesema hivi karibuni kwamba kwaya hiyo ilitokana na Wakristu wachache ambao wengi wao walikuwa ni viongozi wa kigango walioanza kuimba kwa sauti moja hapo mwaka 1973.Mnamo mwaka 1979 kwaya ilianzishwa rasmi na Mwenyekiti wakati huo alikuwa Mchaeli Luziga (kwa sasa marehemu)na Katibu John Nkwazi na Mwalimu wa kwaya wakati huo alikuwa Barnabas Byabato ambaye hadi sasa ni mwalimu wa kwaya hiyo. Katika kipindi hicho kwaya ilikuwa na wanakwaya 17 na hadi wakati huu ina jumla ya wanakwaya 40.

Alisema kimuundo kwaya inaongozwa na Kamati ya Nidhamu,ya Fedha mipango na maendeleo pamoja na Kamati ya ibada na nyimbo.

Mwenyekiti alisema kwamba katika uongozi huo Makamu Mwenyekiti ni Peter Msaiya, Katibu Renock Kibassa akisaidiwa na Christian Mtweve na msaidizi wa Mwalimu wa kwaya Fidelis Kashumba.

Mweka Hazina ni Michael Sipemba, msaidizi wake ni Severa Mmasy na Mwenyekiti wa Nidhamu ni Alexander na Katibu wa Nidhamu ni Edgar Mtey.

Kwaya ya Mt. Sesilia katika kipindi cha miaka 20 tangu ilipoanzishwa rasmi imefanikiwa kurekodi kanda 18 za nyimbo na kwaya hiyo inamiliki kanda 8 na kanda 6 zinamilikiwa na Masista wa St.Paulo Communication, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Alizitaja kanda ambazo zinamilikiwa na kwaya kuwa ni Tumpokee kwa Shangwe iliyohusu Ujio wa Papa mwaka 1990, Tunamshukuru Papa (Shukrani kwa ujio), Hodie ambao umeimbwa kwa lugha ya Kilitini, Nishike mkono, Tangazani Uweza na Ua la upendo ulioimbwa kwa ajili ya Kumbukumbu ya miaka 100 ya Theresia wa Mtoto Yesu toka atangazwe kuwa Mwalimu wa Kanisa. Nyimbo nyingine ni Mwanga wa milele uwaangazie (nyimbo za marehemu),Utukufu wa Bwana utaonekana(nyimbo za ufufuko).

Na kanda ambazo zinamilikiwa na Masista ni Nakupenda Maria, Tunakushukuru Mama Maria, Ahsante Mama wa Yesu, Mwokozi kazaliwa, Neno lako taa yangu na Nyumbani kwa Bwana.

Kwaya ya Mt. Sesilia ina uhusiano na kwaya za ndani na nje ya jimbo kwani mpaka sasa ni mwanachama hai wa Shirikisho la Kwaya Katoliki Jimboni (SHIKWAKA) na hutembeleana, kubadilishana utalaamu na pia kushirikiana katika matukio mbalimbali.

Katika maandalizi ya kuelekea Jubilei ya miaka 2000 tangu kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristu kwaya hiyo imemejiandaa kudumisha Amani na Upendo na pia ushirikiano kati ya kwaya na kwaya na kati ya vyama vya kitume popote pale vilipo na pia kutoa kipaumbele kwa suala la Elimu ya Muziki kwa wanakwaya. Hii ni pamoja na kutumia wataalamu tulionao kuhakikisha kila mwanakwaya anatumia kipaji alichonacho kwa ufanisi zaidi katika kulitangaza Neno la Mungu na Kanisa Katoliki kwa uhakika zaidi. "Kwa vile kwaya ni chama cha kitume tutaendelea kushirikiana na Baba Paroko pamoja na Baraza la Walei kwa ukaribu zaidi na tutaendelea kutii na kuheshimu uongozi wa Kanisa Katoliki kwa ajili ya ustawi wa amani na upendo" alisema Mwenyekiti huyo.

Aliongeza kwa kusema kuwa kwaya yake inamuomba Mwenyezi Mungu awasaidie waweze kuyatimiza malengo yao hayo kwa ajili ya utukufu wake.