Akina Mama wanaojivunia zao la Mwanzi Mbeya

Na Dalphina Rubyema

WATU na vikundi mbalimbali katika jamii wamekuwa wakitumia njia mbalimbali katika kujipatia mahitaji ya kila siku ili mradi njia hizo haziendi kinyume na sheria za nchi.

Viongozi wa Serikali wamekuwa wakisisitiza makundi mbalimbali kujishirikisha kikamilifu katika kazi za kujiajiri wenyewe na sababu tosha ni kwamba serikali haina nafasi za kuiajiri jamii nzima hususani vijana na akinamama.

Kutokana na hilo makundi mbalimbali yamekuwa yakitumia rasilimali ziliopo kujiajiri wenyewe.

Kikundi cha akinamama kinachojulikana kwa jina la "Jamii" kilichopo Wilaya ya Mbeya mjini, mkoani Mbeya ni kikundi kilichojiinua kimaisha ambapo hutengeneza sanaa mbalimbali kutokana na rasilimali ya miti aina ya mianzi.

Mwenyekiti wa kikundi hiki Bi. Amina Kasenga anasema kuwa kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka juzi kina jumla ya wanachama 12 na makao yake makuu yapo wilayani Mbeya mjini.

Anasema kikundi kinajishirikisha katika kutengeneza mapambo kutokana na miti ya mianzi ambapo pambo mojawapo ni tungi la taa ambalo linawekwa juu ya kioo cha taa ili kupunguza mwanga.

Anaeleza kuwa utengenezaji wa tungi hupitia hatua kadhaa baada ya muanzi uliokomaa kukatwa na kukaushwa. Hatua ya kwanza mwazi huchanwachanwa katika kiwango kinachotakiwa.

Anasema hatua inayofuata ni ushonaji ambapo chombo chochote kama ndoo ama kopo kinawekwa chini na ile miti iliyochanwachanwa inasukwa juu ya kifaa hicho ambapo ikifikia mwisho kifaa kinatolewa na kinachobaki ni tungi ambalo huwa na umbo la kifaa kilichotumika.

Bibi Kasenga anasema kuwa kusuka tungi haichukui muda mrefu sana kwani kwa siku matungi kama 10 ama zaidi huweza kutengenezwa na mtu mmoja kutegemeana na ukubwa wa kifaa kilichotumika.

Anasema kama unasuka umbo la kopo lenye ujazo wa kilo tatu ama nne unaweza ukasuka matungi 10 kwa siku ili mradi vifaa vyote vipo.

Kazi kubwa ipo mwanzoni unapoanza kusuka kwa sababu hatua ya upangaji wa chane chini ya kifaa unachotumia kusuka (ndoo,ama kopo) husumbua lakini baada ya kufanikiwa kupanga chane hizo, kazi inayokuwa imebaki ni kuinua juu hizi chane ambazo zinakupa mwelekeo kadri unavyokuwa umezipanga.

"Bei ya tungi moja ni kati ya sh.1,200-5000 ambapo tungi lenye uwazi sehemu ya juu tu pamoja urembo mwingine huuzwa kati ya sh 3,000-5,000/=," anasema na kuongeza kuwa wateja wakuu ni mikoa ya jirani ikiwa ni mkoa wa Iringa, Ruvuma na mkoa wa Dar es salaam pamoja wa wenyeji wa mkoa huo.

Tofauti na matungi, kikundi hicho pia kinatumia miti hiyo kutengenezea vikombe, nyundo, jagi, ‘matrei’ pamoja na kujengea nyumba.

Kikundi kimefanikiwa kufungua ofisi iliyopo Ileje, mkoani Mbeya pamoja na kufanikiwa kushiriki maonyesho ya 21 ya Biashara ya kimataifa mwaka huu ambapo kilipata oda nyingi.

Anasema baadhi ya wanakikundi hawajapata mwamko wa kuona umuhimu wa kikundi hicho kwani hukataa kutoa michango pindi inapohitajika. Hata hivyo Bi Kasenga, anasema kuwa uongozi wa kikundi hicho kinachojishughulisha pia na ususi na kilimo unajaribu kadri iwezekanavyo kuwaendeleza wanakikundi kwa kukutana na mtu mmoja mmoja.