Ijue Kwaya Kuu ya Mtakatifu Yosefu

lAwali ilikuwa inaimba kwa lugha ya Kilatini

Na Neema Dawson

NENO la Mungu linaweza kuenezwa au kuhubiriwa kwa njia mbalimbali kwa lengo la kuwafikia na kuweza kuwaokoa wanadamu.Uimbaji ni njia mojawapo.

Lakini uinjilisti kwa njia ya uimbaji huweza kuzaa matunda yake pale tu ambapo msikilizaji atafungua moyo wake kuupokea ujumbe uliokusudiwa kwake, ndivyo anavyoeleza Mwalimu wa Kwaya Kuu ya Mtakatifu Yosefu iliyopo katika kanisa la Mtakatifu Yosefu jijini Bw. Peter Kamugisha baada ya kutembelewa na gazeti hili hivi karibuni.

Mwalimu huyu wa kwaya anatoa wito kwa watu wenye fikra potofu kwamba Neno la Mungu lina kuwa na nguvu linapohubiriwa mimbarani tu na kueleza kuwa Uimbaji ni njia mojawapo yenye nguvu kubwa ya kueneza ujumbe wa Mungu na kuleta wokovu.

Kwa kuelewa hayo Bw. Kamugisha anasema kwaya yake imesharekodi nyimbo mbali mbali ili kuweza kusambaza zaidi ujumbe wa Injili ya Kristo kwa watu wengi zaidi.

Akielezea historia ya kwaya hiyo ambayo iko katikati ya jiji la Dar es Salaam, Bw. Kamugisha amesema kwaya yake ni kwaya kongwe ambayo imeanzishwa mwaka 1945 ikiwa na umri wa miaka 54 hivi sasa. Anasema katika miaka hiyo ya "45" kwaya ilipoanzishwa ilikuwa ikiimba kwa lugha ya Kilatini tu tofauti na sasa ambapo huimba pia kwa Kiswahili.

Ikiwa na wastani wa waimbaji 60 hivi sasa, kwaya hiyo imefanikiwa kujipatia umaarufu mkubwa na hivi karibuni inakusudia kutembelea jiji la Nairobi kwa ajili ya mwaliko maalum wa kuhubiri Neno la Mungu kwa njia ya nyimbo.

Sambamba na hayo pia alitaja matatizo ambayo yanayoipata kwaya hiyo katika uimbaji kuwa ni pamoja na wanakwaya kutohudhuria mazoezi mara kwa mara kutokana na kutingwa au kuwa na kazi nyingi za maofisini, hali ambayo inapelekea usumbufu mkubwa wakati wa mazoezi.

Bwana Peter Kamugisha aliwataja baadhi ya viongozi wa kwaya hiyo ambao wanaifanya iweze kuimba na kusali katika Misa Kuu za Kiaskofu katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu ni Mwenyekiti Bw.Simoni Byanyuma, Katibu wake Mrs Oliver Malya na bila kumsahau mpiga kinanda wa kwaya hiyo Bw.Dismas Malya.