Make your own free website on Tripod.com

Bendi ya muziki wa mapipa yaundwa Dar

Na Christopher Udoba

BENDI pekee inayopiga muziki wa dini kwa kutumia mapipa matupu inayoitwa Mapipa ya Mbingunii meanzishwa katika Kanisa Katoliki Kurasini jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa bendi hiyo ambayo pia inajulikana kwa kimombo kama "The drums of Heaven" ni kwa ajili ya kuwasaidia vijana kuwa na maadili mema, Paroko wa kanisa hilo Padre. Mieczyslaw Kijaczek amesema.

Pia paroko huyo amesema katika mahojiano na KIONGOZI ofisini kwake wiki iliyopita kuwa bendi hiyo hutumika kuwatumbuiza wakristo katika kila ibada ya Jumapili jioni.

Mwenyekiti wa bendi hiyo yenye wasanii 36, Fred Mhagama amefafanua sifa zinazotakiwa kwa wapiga muziki wanaotaka kujiunga nayo kuwa sharti wajue kusoma noti za muziki.

Aidha, wanamuziki waliopo katika bendi yake, ameongeza kuwa wote wamejifunza alama za muziki (noti)

Katika upigaji wa vyombo vya muziki wa mapipa villivyoundwa kwa ustadi mkubwa, mwenyekiti huyo amesema kuwa vimepangwa kulingana na milio ya sauti mbalimbali au noti.

Ndiyo maana mwanamuziki sharti awe anajua kusoma alama za muziki.

Hata hivyo matumizi ya muziki wa mapipa matupu yalilianza hapa nchini mnamo 1985, mtindo huo ukiwa umetokea nchi ya Guyana barani Amerika ya Kusini, Sospiter Masima ambaye ni fundi wa kuunda na kutumia ala za mapipa amesema, na akaongeza kuwa yeye alijifunza fani hiyo akiwa Jeshi la Kujenga Taifa kabla ya kuacha.

Viongozi katika bendi hiyo ni Rejina Motto ambaye ni Makamu wa Mwenyekiti, Katibu ni Nathalia L. Anney na Mtunza Hazina, Catherine Msafiri, kwa mujibu wa Mwenyekiti ambaye pia mwalimu.