KIUMBO: Kijana anayeunda vifaa vya umeme

Hakuwahi kusoma hata darasa moja

Na Justine Mwereke

INAAMINIKA kuwa si rahisi mtu kuwa fundi wa umeme au vitu vinavyohusiana na umeme bila ya kuwa na elimu angalau ya msingi au kupitia mafunzo yake lakini Bw, Shaaban Kiumbo(40) ameweza kubuni na kutengeneza vifaa vya kuunganishia umeme (sockets)bila hata ya kupitia elimu ya msingi wala mafunzo ya umeme.

"Si siri, mimi sina darasa hata moja kwa sababu wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunilipia ada," alisema Bw. Kiumbo alipohojiwa na mwandishi wa makala hii..Hata hivyo Bw. Kiumbo, anaweza kusoma na kuandika kutokana na kile alichochokiita ni ujanja wake tu.

Bw. Kiumbo alisema utundu wake ndio uliomwezesha kufahamu shughuli za umeme-mwenendo na tabia ya umeme na tahadhari zake, hata kufikia kumudu kutengeneza vifaa kama hivyo vinavyoonesha kufaa na kufanya kazi vizuri na kwa usalama kama vifaa vilivyotengenezwa viwandani na wataalam wa umeme waliopitia vyuoni.

Alisema alianza utundu huo mwaka 1975 kwa kuunganisha nyaya za umeme kwenye betri za redio na balbu ya tochi na kuweza kutoa mwanga kama tochi.

Baadaye aliweza kuunganisha betri nyingi pamoja na kuweza kuzalisha umeme wa kuenea chumbani mwake. Hali hiyo ilimpa hamasa zaidi kuhusu utundu wake huo.

Lakini kuanzia mwaka 1977 kutokana na kujiingiza katika ngazi za ajira kwa Wahindi na baadaye kwenye kilimo cha mchicha, Bw Kiumbo aliamua kuacha kujishughulisha zaidi na utundu wake kuhusu umeme

Bw. Kiumbo, mkazi wa Kigogo Mbuyuni, jijini Dar es Salaam ni mzaliwa wa kijiji cha Kisanzala. Matombo wilayani Morogoro Vijijini, aliingia jijini mwaka 1972 kutafuta kazi baada ya kuona wazazi wake walishindwa kumlipia ada ya kuanza darasa la kwanza mwaka 1971.

Alifikia kwa mama yake mkubwa Binti Selemani huko Kigogo Mbuyuni na kuamua kufanya kazi za kibarua za kuwasaidia mafundi wa ujenzi na hata zile za nyumbani kwa Wahindi.

Baadaye mwaka 1993 aliamua kujishughulisha na kilimo cha mchicha hadi mwaka 1996 alipoacha kutokana na kushindwa kumudu uzito wa kazi hiyo.

Mwaka uliofuata aliamua kujiingiza katika kazi ya ulinzi kwa mtu binafsi na kurudia tena kujishughulisha na utundu wake wa kubuni na kutengeneza vifaa vya umeme . Aliendelea kutengeneza na kuunganisha umeme kwenye vyombo vya ndani kwa lengo la kuviuza ili kujipatia fedha za kumsaidia kuishi.

Kwa bahati mbaya mafanikio ya lengo lake hilo bado hayajazaa matunda.

Ingawa ameweza kutengeneza viunganishi vya umeme vya njia moja, mbili, tatu hadi njia nne ambavyo vinaweza kuunganisha umeme kwenye vifaa mbalimbali vikiwemo friji,feni, redio, pasi, televisheni na kadhalika, lakini hajapata kuuza hata kimoja.

"Soko sijapata, ila nimewahi kuwapa jamaa zangu baadhi ya vifaa hivyo bure; na kati ya ndugu zangu wote niliopata kuwapa, hakuna aliyewahi kusema kuwa vifaa hivyo vina madhara yoyote. Havijaleta hitilafu ya aina yoyote kwa vifaa vyao,"alisema Bwana Kiumbo.

Alisema sababu kubwa ya kutopata soko ni kutokana kutovitangaza vifaa hivyo kwa umma kwa njia yo yote ile.na akaongeza kuwa hajawahi kuvipeleka kwenye maonesho yoyote ya sanaa ili watu wakaviona.

Bw. Kiumbo alisema katika jitihada za kutaka kuthibitisha kufaa kwa vifaa vyake, aliwahi kuvipeleka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ambako vilijaribiwa na kuonekana vinafaa kutumika.

"Waliniambia tu vinafaa na kunitaka nikaendelee na utengenezaji wake"alisema Bwana Kiumbo alipoulizwa maoni aliyopewa na watalamu wa Taasisi hiyo ya taifa.inayojihusisha na juhudi kubwa za kuiingiza nchi katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia

Alisema katika kutengeneza vifaa hivyo, hutumia vitu mbalimbali vinavyopatikana katika mazingira yake kama vile soli za viatu aina ya kandambili, vipande vidogo vya mbao, misumari ya inchi moja na nusu na vifuniko au vifaa vya plastiki vinavyotumika kuwekea vipodozi au dawa za kuua wadudu kama mbu vyenye umbo la mviringo.vingine ni nyaya za umeme, swichi na vikombe ambavyo huuzwa madukani.

Bw. Kiumbo alisema ana nia kubwa ya kuendeleza kipaji chake hicho kwa kutengeneza vifaa vilivyo bora zaidi kitaalamu, lakini anakwamshwa na hali halisi ya kukosa fedha za kumweza kununulia vifaa anavyohitaji hasa vile vinavyopatikana madukani.

Mbali na vifaa hivyo kutumika kama viunganishi pia vinaweza kutumika kwa kuwekea taa ndefu za umeme (tube light) bablu za kawaida (Lamp Holders) kutokana kuwepo kwa vishikio kama hivyo.