Make your own free website on Tripod.com

El-Nino yawaneemesha Wamasasi

Na Dalphina Rubyema

PAMOJA na Mvua za El-Nino zilizonyesha mwaka juzi na kuleta madhara makubwa katika maeneo kadhaa ya Tanzania zimedhihirisha ule msemo usemao " kufa kufaana" kwani wakti ilikuwa kilio kwa wananchi wengi, hali ilikuwa tofauti kwa wasanii wakazi wa wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara.

Bibi Stella Livinga ambaye ni mkazi wa Masasi mjini anaeleza kuwa mvua kubwa za El-nino zilisababisha kuporomoka kwa mawe makubwa kutoka sehemu za milimani na kurundikana sehemu ambazo ni tambarare,. hali ambayo licha ya kuleta kero kwa wananchi, pia ilikuwa imebeba baraka kwani mawe hayo ambayo ni mazuri sana kwa uchongaji wa vinyago huwa hayapatikani kirahisi.

Anasema kutokana na kero hizo ambazo ziliambatana na ukosefu wa eneo la kulima kutokana na mawe hayo kufunika eneo kubwa wakazi walibuni mbinu ya kuyapuguza mawe hayo kwa kuyatumia kuchonga sanamu.

Anasema kujazana kwa mawe hayo katika maeneo ya tambarare kulichochea kasi ya uchongaji vinyago vitokanavyo na mawe na hayakuchukua muda mrefu kwisha.Hivi sasa wananchi wameingia katika kazi kubwa ya kuyasaka mawe hayo sehemu za milimani ambapo yalikuwa yakitoka kipindi cha mvua na bahati nzuri wamefanikiwa kuyapata eneo la Ndanda ingawa yanapatikana kwa taabu chini ya miamba .

"Ni kazi ngumu sana kuyapata mawe haya kwani yanapatikana chini kabisa hususan katika eneo laNdanda"anasema Bibi Liviga .

Bibi Liviga ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi kiitwacho Wanaume na Wanawake wachonga Mawe (WAWAMA) kinachojishughulisha na uchongaji wa sanamu hizo kilichoanzishwa mwaka jana, anasema kuwa mawe haya yanatengeneza pia mapambo mbalimbali.

Akieleza njia zinazotumika hadi kupata sanamu, bibi Liviga anasema kuwa kwanza akina baba wenye nguvu huchimba shimo kubwa hadi kwenye mwamba ambapo yanapatikana mawe hayo, na baada ya hapo inafuatia kazi ya upasuaji wa miamba hiyo ambayo inafanywa na akina baba hao hao.

Anasema baada ya hapo inafuatia kazi ya kubeba miamba hiyo iliyopasuliwa vipande hadi juu ya ardhi na baada ya hapo zoezi la kulipa jiwe hilo sura ya kinyago kinachotakiwa inafuata.Kazi hiyo ngumu pia hufanywa na akina baba.

Anaongeza kuwa baada ya kazi zote hizo kukamilika inakuwa imebaki kazi ya kurembesha sanamu hizo, kazi ambayo sasa hufanywa na akina mama.

"Sisi akina mama kazi yetu ni kurembesha tu"alisema bibi Liviga.

Anaongeza kuwa kutokana na uzito wa mawe hayo kuwa mkubwa, kazi za utengenezaji wa sanamu hufanyika huko porini (milimani) na baada ya zoezi lote kukamilika ndipo sanamu hubebwa hadi nyumbani tayari kwa kuuzwa

Anasema kutokana na hatua zinazopitiwa hadi kupata sanamu kuwa nyingi kikundi chake chenye wanachama 15, wanawake saba na wanaume 8, huweza kuchonga kati ya sanamu mbili hadi 3 kwa siku kazi ambayo inategemea na ukubwa wa sanamu yenyewe.

"Kama inatakiwa sanamu kubwa basi tunatengeneza tatu"anasema na kueleza kuwa bei ya sanamu hizo ni kati ya sh. 5,000 hadi 800,000/= wateja wakuu wakiwa ni makanisa na watalii.

Akieleza kwa nini makanisa wanakuwa wateja wakuu, alisema kwa vile sanamu zinazotengenezwa zaidi na kikundi chake zile za Bikira Maria, Yosefu na mtoto Yesu.

Anasema watalii hupenda sanaa nyingine zinazotengenezwa kwa mawe haya ambazo amezitaja kuwa ni viti , meza, picha ya mtu na samani za aina zote zinazotengenezwa kwa mbao amabazo pia hutengenezwa na kikundi chake.

Anasema kikundi chake kimefanikiwa kufungua akaunti pamoja na kuunda katiba na hivi sasa kipo katika hatua za mwisho za usajili. . Pia kikundi kilifanikiwa kushiriki Maonyesho ya 21ya Biashara ya Kimataifa yaliyomalizika hivi karibuni. Kikundi hicho pia kinajishughulisha na kazi za ususi wa vikapu , mikeka pamoja na ufinyanzi.

Tatizo kubwa linalokikabili kikundi hicho ni ukosefu wa masoko yanayolingana na kiwango cha uwezo wao wa uzalishaji.

Alisema njia wanazotumia kupunguza tatizo hilo ni kuandika mabango yanyoonyesha aina za sanamu wanazotengeneza na hivi sasa wanatafuta wafadhili watakaowatafutia wateja zaidi ndani na nje ya nchi.