Ijue Parokia ya Bagamoyo

PAMOJA na kwamba Ukristo katika Afrika ya Mashariki ulianzia katika eneo la Bagamoyo lakini kwa hivi sasa eneo hilo linaonekana kupoteza idadi kubwa ya Wakristo. Paroko wa Parokia hiyo ambayo ni moja ya parokia za jimbo la Morogoro Padri Valentino Bayo pamoja na hali hiyo anajitahidi kufufua juhudi za Wamisionari wa kwanza. Mwandishi Dalphina Rubyema alihojiana na paroko huyo.

Swali: Baba wasomaji wetu wangependa kujua historia ya parokia hii; sijui unaweza kutoa maelezo kwa ufupi?

Jibu: Parokia ya Bagamoyo ni parokia mama katika Afrika ya Mashariki.

Nasema hivyo kwa vile Kanisa la kwanza kujengwa Afrika ya Mashariki lilijengwa hapa mnamo Juni 17 mwaka 1868.

Enzi hizo kulikuwa na biashara ya utumwa. Wakati wa biashara hiyo iliyokuwa imeshamiri barani Afrika, Shirika la Holy Fathers lilituma watu wake Afrika ya Mashariki. Walizunguka maeneo mbalimbali na walipofika kwenye visiwa vya Reunion waliona namba kubwa ya watumwa inatoka visiwa vya Madagasca; na hapo ilikuwa ni katika miaka ya 1860 -1863.

Wamisionari hawa wa Holy Fathers kutoka nchini Ufaransa walikuja moja kwa moja hadi kwenye eneo la Zanzibar ambapo walianza kazi ya kuwakomboa vijana ambao waliletwa kama Watumwa .

Baada ya kukusanya idadi kubwa waliona wajenge sehemu ya kuhifadhia vijana hao ambapo eneo la Bagamoyo lilipata tunu hiyo.

Mwaka 1968 Wamisionari walianza rasmi kazi ya kueneza dini ambapo waliendelea kukusanya watumwa wengi na kuwaweka eneo hili la Bagamoyo na mwaka huo huo ndipo lilijengwa Kanisa.

Mwaka 1876 Wamisionari hao wa kwanza walijenga nyumba ya Maria (Hekalu la Bikira Maria) na lengo kubwa la ujenzi wa nyumba hii lilikuwa kutoa shukrani kwa watu hao walionusurika kifo wakati wa biashara ya Utumwa kwani watu wengi walipoteza maisha yao na hao waliookolewa na Wamisionari ilikuwa ni bahati yao.

Baada ya hapo ilijengwa nyumba ambayo ilitumika kwa ajili ya mafunzo ya ufundi kwa vijana na hapo ndipo wakazaliwa wataalamu wa kwanza katika masuala ya upishi, Makatekista, Makenika, wajenzi wa nyumba na wataalamu wa fani nyingine.

Swali: Parokia yako ina historia nzuri sana lakini cha kushangaza ni kwamba pamoja na kwamba wataalamu wa kwanza walipatikana hapa lakini wenyeji wa hapa wanaonekana kuwa mbali na dini ya Ukristo. Je ni sababu zipi zilizopelekea hali hii?

Jibu:Kwanza kabisa ni kweli kwamba wenyeji wa Bagamoyo wengi wamepoteza dini ya Ukristo. Hali hii ilianza kwenye miaka ya 1930 ambapo wenyeji wa huku wengi walianza kukimbilia Bara.Wale waliobaki wengi wakawa ni wafuasi wa dini ya Kiislamu ambayo iliingia huku baadaye.

Wenyeji pia wamejenga imani kwamba dini ya Ukristo ni dini ya watumwa kwa vile wamisionari wa kwanza walipokuja kueneza dini hii katika Afrika ya Mashariki walikuja wakati wa biashara ya Utumwa .

Kitu kingine kilichochangia kuporomoka kwa dini ya Ukristo ni kuhamishwa kwa Seminari ya kwanza Afrika ya Mashariki ya Mtakatifu Petro iliyojengwa hapa kwenye miaka ya 1930.

Baada ya kuhamishwa kwa Seminari hii iliyohamia Morogoro mwaka 1969 hapa Bagamoyo alibaki Padre mmoja tu na padre huyo alikaa hapa hadi mwaka 1989 alipoondoka ambapo parokia ilibaki bila padri kwani kila padre aliyetaka kuletwa huko alikataa hadi mwaka 1991 nilipokuja mimi.

Swali: Kitendo cha parokia kukaa zaidi ya mwaka mmoja bila ya padri bila shaka kilisababisha hali ya parokia kukosa maendeleo. Je hali ya parokia yako uliikutaje?

Jibu: Kwa kweli hali ilikuwa inatisha sana. Eneo hili la kanisa lilikuwa limeishageuka pori...yaani yalikuwa ni maficho ya vibaka na wanyang’anyi. Sehemu hii ilikuwa inaogopwa kabisa kwa sababu ya waporaji.

Niliona njia ya kujenga amani katika eneo hili ni kuwa na darasa la watoto wadogo (Chekechea) hivyo niligeuza ukumbi wa parokia kuwa darasa la watoto hao na hapo ilikuwa ni mwaka 1992.

Mwaka huo huo niligeuza sehemu ya mabafu ya kufulia nguo kuwa karakana ambapo niliwakusanya vijana wote waliokuwa wakijishirikisha katika vitendo vya uporaji na unyang’anyi na kuwafungulia shule ya ufundi.

Nikageuza banda la mbwa kuwa ofisi ya walimu na vijana wote niliowakusanya niliwapa jukumu la kilinda mali zote za chuo chao pamoja na waliokuwa vibaka , mali zote zilibaki katika hali ya usalama.

Mwaka uliofuata nilijenga shule ya ufundi kwa ajili ya watoto wa kike. Kwa vile mabinti hao walionekana kuwa na majukumu mengi nyumbani kwao hali ulizuka utoro katika masomo yao na ndipo niliona ukumbi wa parokia waliokuwa wakisomea watoto wadogo niugeuze kuwa bweni la wasichana na shule ya chekechea ikahamishiwa pwani.Hata hivyo malezi ya wasichana hao yalitushinda.

Swali: Umesema mlishindwa kuwalea wasichana; Je ni sababu zipi zilizowafanya mshindwe kazi hiyo?

Jibu:Kulea wasichana ni kazi kubwa kwani wengi wao walionyesha hali ya kukatisha tamaa kwa kubeba mimba hovyo. Mbali na mimba vijana wengi wa kutoka vijijini walikuwa wanaingia hovyo kuwafuata wasichana hao, hali iliyoleta kero kubwa na matokeo yake yalikuwa hayaridhishi.

Swali:Mbali na Parokia yako kufungua shule za ufundi na chekechea kwa ajili ya vijana na watoto, kuna shughuli nyingine za maendeleo zilizokwishafanywa chini yako?

Jibu: Kwa kweli shughuli za maendeleo zilizokwishafanywa chini yangu ni nyingi mno kwani mwaka 1994 niligeuza sehemu ya ghala na jiko kuwa zahanati kwa ajili ya kutoa huduma ya afya kwa watu.

Mwaka huu tunataka kuigeuza zahanati hii yenye wafanyakazi 12 kuwa kituo kamili cha afya.

Mwaka 1996-1997 Parokia pia imefungua shule ya Bweni inayoitwa St. Mirian kwa ajili ya watoto wa kike waliomaliza elimu ya msingi.

Lengo la shule hii ni kujitahidi kuibadilisha Bagamoyo ambayo ina kiwango cha chini kielimu na pia ni kuwafanya wazazi wapate kuelewa kwamba msichana kama alivyo mvulana anahitaji elimu.

Mwaka 1993 wakati tulipoadhimisha Jubilei ya miaka 125, parokia pia ilipanda msalaba wa chuma wa historia kwa kuondoa ule wa kwanza uliopandwa mwaka 1868 uliokuwa wa mbao.

Msalaba huu wa chuma tuliutengeneza kiutalaam ambapo tuliujenga baharini na una njia 14.

Swali: Je, parokia yako ina vigango vingapi?

Jibu: Parokia ina vigango sita lakini kinachojulikana zaidi ni kigango cha Matibwa ambapo jirani yake kuna gereza la Kigangoni. .Kigango hiki siku za kawaida hutumika kama shule ya chekechea ambapo siku ya Jumapili hutumiwa kwa ajili ya misa takatifu na wanaosalia humo wengi ni wafanyakazi wa gereza hilo.

Watoto wanotumia kigango hicho wote ni Waislamu tu; hali hii inaweza kuonyesha jinsi gani Bagamoyo ilivyojaa Waislamu.

Swali: Vipi Upande wa Kwaya?

Jibu:Kutokana na uchache wa waumini; parokia yetu inayo kwaya moja tu ya Moyo Safi wa Maria.

Swali:Unajisikieaje unapoona parokia yako imepata mabadiliko makubwa kwa kipindi hiki uliposhika nafasi ya kuwa Paroko wa Parokia hii?

Jibu:Kwa kweli bado sijaridhika na kazi yangu najitahidi kufanya maendeleo zaidi ndio maana kila siku ratiba ya kuamka kwangu ni saa 11:30 alfajiri ambapo naanza kazi kwa kuendesha misa ya asubuhi na baada ya hapo saa 1.00 asubuhi hadi saa 2:00 usiku nakuwa nikifanya kazi ndani na nje ya kanisa .

Swali:Kazi zako ni nyingi sana, je, una watu wengine wa kukusaidia?

Jibu:Ndio kwa hivi sasa ninao mapadre wengine watatu wa shirika la Roho Mtakatifu wanaonisaidia, hivyo najisikia kupungukiwa mzigo tofauti na nilipokuwa peke yangu.

Swali: Parokia yako inakabiliwa na matatizo gani?

Jibu:Kwa kweli parokia hii zaidi inakabiliwa na tatizo la kukosa mwamko mkubwa kwa wakristo wa Bagamoyo ambao kwa kweli ni kama ardhi iliyokwishalimwa na kuchoka ambayo ili upate mavuno ya kutosha ni lazima uweke mbolea ya kutosha.

Hapa nina maana kwamba Wakristo wa hapa tayari walishahubiriwa juu ya Ukristo tofauti pengine na maeneo mengine ambayo Ukristo haujafika kabisa... Wakristo wa Bagamoyo ni wale ambao hawahitaji kuelezwa nini maana ya Ukristo na ili kuwaamsha kutoka usingizini ni kazi inayohitaji kujituma zaidi.