Ijue Parokia ya Tabata

KILA parokia ina mipango na shughuli zake za kimaendeleo pamoja na huduma za jamii. Parokia ya Tabata inayopatikana katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam inatoa huduma ya kutunza wazee, watoto yatima pamoja na watoto wa mitaani. Katika Makala haya mwandishi wetu Dalphina Rubyema aliongea hivi karibuni na Makamu Mwenyekiti wa parokia hiyo Bw. Joseph Ibreck .

Swali: Ndugu Makamu Mwenyekiti unaweza ukatoa historia fupi ya parokia yako ?

Jibu:Kanisa Katoliki la Tabata lilianza kama kigango kilichokuwa chini ya Parokia ya Msimbazi na wakati huo tulikuwa hatuna kanisa, ila tulikuwa tunasali katika madarasa ya shule ya Msingi Tabata.

Wazo la kuwa na parokia lilikuja wakati wa misa ya kwanza ya majilio mwaka 1981 ambayo ilifanyika kwenye darasa mojawapo la shule hiyo, ambapo watu wasiopungua thelathini walihudhiria. Misa hiyo iliongonzwa na padri Constance.

Juhudi za kutafuta kiwanja kwa ajili ya kujenga kanisa zilianzisha kwa nguvu na padri Constance akishirikiana na wazee wawili Bw. Francis na January Mkono ambaye hivi sasa ni marehemu.

Juhudi hizo ziliweza kuleta matunda kidogo ambapo viwanja viwili visivyofikia ekari moja vilipatikana.Mwaka 1983/84 mfadhili kutoka Uholanzi aliweza kujenga ukumbi mdogo wa kuweza kukaa watu 300 na ukaanza kutumika Agosti 1985.

Mwaka mmoja baada ya ukumbi huo, ilijengwa nyumba ya masista na Kigango.

Baada ya ujenzi huo kigango kilipata wahudumu wakazi wa kwanza masista saba wa Mama wa Huruma kutoka Kilimanjaro na huo ulikuwa ni mwaka 1987.

Baada ya juhudi hizo ilipatikana nguvu mpya kutoka wa Walei wakishirikiana Padri Constance ambapo kamati ya watu sita iliundwa ikiwa na malengo ya kuiomba serikali viwanja vya kufikia hekta 10 ili kujenga kituo cha Kikatoliki cha kutoa huduma za kiroho na kijamii.

Serikali ilikubali kutoa kiwanja ambapo kanisa limejengwa kwa hivi sasa na Agosti 8 mwaka 1993, Tabata ilizinduliwa rasmi kuwa parokia na Mwadhama Polycarp KardinaliPengo pamoja na padri Albinus Tesha kasimikwa rasmi kuwa paroko wa kwanza wa parokia hii.

Padri Albinus ambaye hadi hivi sasa ameshika wadhifa huo anatoka kwenye Shirika la Watawa wa Mitume wa Yesu, lenye makao makuu mjini Nairobi-Kenya.

Swali: Parokia yako imejiwekea sifa ya kuwa na eneo la kutunza wazee na watoto yatima pamoja na watoto wa mitaani. Hebu eleza ni huduma gani mnazotoa kwa watu hao?

Jibu:Kwanza kabisa, ni kweli parokia inalo eneo la kutosha kwa ajili ya kuwatunza wazee na watoto yatima na huduma tunazowapatia ni pamoja na zile za kiroho pamoja na kijamii ambapo tunawapa elimu ya afya na ufundi bila ubaguzi.

Swali:Je parokia inavyo vigango ? kama ndiyo ni vingapi?

Jibu:Parokia ina Kigango kimoja tu cha Kimanga kinachotoa huduma za misa mbili kila Jumapili.Kigango hiki pia kina jumuiya ndogondogo 15 ambapo Parokia yenyewe ina jumuiya 13.

Mwenyekiti , makatibu na watunza fedha wa jumuiya hizo kwa pamoja huunda Halmashauri ya parokia na kuchagua Kamati ya Utendaji ya watu watano chini ya Mwenyekiti wa parokia.

Swali: Parokia hii inasemekana kuwa haina kwaya Kuu na iliyokuwepo ilivujwa. Je ni kweli?kama ni kweli ni sababu zipi zilizopelekea kuvunjwa kwa Kwaya hiyo?

Jibu:Ni kweli kwaya Kuu ilivunjwa na sababu ya kuvunjwa kwa kwaya hiyo ni mfarakano uliojitokeza katika kipindi cha nyuma baina ya uongozi wa parokia na kwaya hiyo, lakini pamoja na hayo parokia ina mpango wa kuunda kwaya mpya.

Swali:Umekiri kuwa kulikuwepo na mfarakano baina ya Uongozi wa parokia na kwaya Kuu; ni mtafaruku gani huo?

Jibu:Kwa kweli mfarakano huu si vizuri kuutaja ama kuuelezea gazetini, lakini ninachoweza kusema ni kwamba tatizo linatatuliwa na viongozi wa Parokia wenyewe.

Swali: Parokia ina utaratibu gani katika masuala ya kutoa huduma za kiroho kwa waumini wake?

Jibu:Parokia imeonelea njia ya kuwasaidia waumini wake katika masuala ya kiroho ni kuandaa misa na ibada, ambapo katika siku za juma kila siku kunakuwepo na misa ya asubuhi isipokuwa siku ya Jumatano misa huwepo jioni.

Kanisa pia lina masista na katekista wanoendesha mafundisho ya dini katika shule za msingi zilizopo katika Kata ya Tabata na kwa vijana watarajiwa kupokea Sakramenti ya Komunio ya kwanza, Ubatizo na Kipaimara.

Mapadri nao hawako nyuma, mara kwa mara huendesha ibada ya mazishi na isipowezekana viongozi Walei huomba kuongoza ibada hizo.

Swali:Parokia yako ina miaka sita sasa tangu izinduliwe rasmi, lakini kwa kuangalia haraka haraka inaonekana maendeleo sio ya kasi ya kuridhisha. Je, nitakuwa kinyume nikisema Parokia ya Tabata inalala?

Jibu:Swali lako naweza kusema kuwa kwa namna moja au nyingine linajaribu kuwa karibu na ukweli, kwani parokia yetu ikilinganishwa na parokia ya Makuburi ambayo ina muda wa mwaka mmoja tangu ianzishwe na ina maendeleo kupita parokia yetu. Lakini pamoja na hayo hatuko nyuma sana, kwani tumeweza kuwa na Shule ya Chekechea na Sista Mkuu akisaidiwa na Kamati ya Elimu hivi sasa wanaandaa mpango wa kuanzisha shule ya msingi mwaka ujao.

Kwa hivi sasa parokia kwa kutumia nguvu na michango ya waumini wake inajenga kanisa jipya chini ya uongozi wa paroko akisaidiwa na Kamati ya Ujenzi na jopo la wahandishi watano, hivyo sio kweli kwamba tumelala.

Swali:Parokia inavyo vyama vya kitume?

Jibu: Ndiyo parokia yetu inavyo vyama vya kitume ambavyo ni Moyo Mtakatifu wa Yesu, Legio Maria, VIWAWA, na WAWATA.

Swali:Nini mipango yenu ya baadaye?

Jibu: Mipango ya parokia tuliyonayo ni kuendelea kujenga kanisa na kulikabidhi kwa Baba Kardinali katika Jubilei ya mwaka 2000.

Kanisa pia lina mpango wa kujenga shule ya msingi na kuanzisha mafunzo mwaka 2000.

Pia tuna mpango wa kuwaelimisha Wakristo kuhusu kulitengeneza kanisa parokiani na jimboni kwa zaka na sadaka na kubuni mbinu ya kujenga majengo muhimu ya kuwezesha kuendesha masomo ya sekondari na ufundi kwa watoto wetu wanaoongezeka haraka ni miongoni mwa mipango tuliyonayo.

Parokia pia ina mpango wa kubuni miradi ya vijana kujiariri na kujiendeleza wenyewe.

Kuna mpango mwingine wa kuanzisha majenzi (formation) kwa ngazi zote kwa Wakatoliki wa rika zote na kuamsha ari yao kushiriki katika vyombo vya utawala na uongozi wa ngazi zote za mtaa na taifa kwa ujenzi wa haki na amani nchini Tanzania.

Swali: Parokia ina matatizo yoyote? Na Kama yapo ni yapi na Mnayatatua vipi?

Jibu: Kama makanisa mengine, hata Tabata inayo matatizo yake.

Lakini makubwa ni ya ukosefu wa wahudumu , ukosefu wa maeneo ya kuendeshea miradi ya kusaidia vijana katika jamii na kadhalika.

Ukosefu wa ajira kwa vijana wetu wengi wa wahamiaji na wastaafu pamoja na kuwepo kwa wanamaombi na wenye mwamsho potofu ni miongoni mwa matatizo yanayoikabaili Parokia.

Parokia yetu pia inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa fedha za kuendeshea miradi pamoja na ukosefu wa fedha za kujengea shule na hospitali

Kuhusu njia tunazozitumia kutatua matatizo hayo ni kwamba tunaendelea kuelimishana kutoka kila ngazi ya jumuiya ndogo ndogo kuyatambua magumu ya maisha na vyanzo vya maovu yanayojionyesha wakati huu na kuendelea kubuni mbinu za kuyakabili.