Msimbazi: Parokia yenye utaratibu wa 'ndoa poa'

Imefuta gharama za kufungia ndoa

Inacho chuo cha Ufundi; wanaohitimu hupewa cherehani bure

MIONGONI mwa parokia za Jimbo Kuu la Dar Es Salaam zilizo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Wakristo wote wanapata huduma bora katika kulelewa vema kiroho na kimaadili, ili kuifanya vizuri kazi ya Mungu, ni Parokia ya Msimbazi ambayo licha ya kutoa huduma nyingine nyingi, pia imeanzisha mfumo wa utoaji wa huduma bora zenye msharti nafuu ya Sakramenti ya ndoa unaojulikana kama "Ndoa poa".Paroko wa parokia hiyo Padre Sergi Tarimo, na Msaidizi wake Padre Mansuetus Brinkhof wanaelezea shughuli kadhaa zinazofanyika kanisani hapo kama walivyohojiwa na Mwandishi Wetu Josephs Sabinus:

SWALI:Parokia yako imekuwa ikisifiwa na wakazi wengi wa hapa jijini kwa uamuzi wake wa kuanzisha utaratibu wa "ndoa poa"; unaweza kuwaambia wasomaji maana ya "Ndoa poa kama mnavyoita"?

JIBU:Baada ya kugundua kuwa waamini wengi wanakosa sakramenti mbalimbali kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokushiriki Ekaristi Takatifu na hata watoto wao kushindwa kupata ubatizo kwa kuwa wazazi wao hawajafunga ndoa hususani kutokana na kushindwa kumudu gharama zilizokuwapo awali, parokia ililiomba jimbo na kuruhusiwa kuondoa ada nyingine zote zilizokuwa zikilipwa ili kufunga ndoa. Tuliacha ile ya shahada ya ndoa peke yake ambayo ni shilingi 5,500/=.na ndiyo maana waumini wameamua kuiita hali hiyo kuwa ni "Ndoa poa" kwa maana kuwa ndoa yenye masharti nafuu.

SWALI: Ada nyingine zilizokuwa zikitozwa na sasa zimeondolewa ni zipi?

JIBU:Awali kulikuwa na gharama ya shilingi 5000/= kwa ajili ya kwaya inayohudumia siku ya ndoa; lakini sasa imefutwa na huduma hiyo inatolewa bure, semina kabla ya kufunga ndoa ilikuwa ikiwagharimu waamini (Maharusi) kiasi cha shilingi 4000/=?,; hiyo nayo ; imeondolewa; ni bure nyingine ni maombi ya misa kwa ajili ya ndoa ambayo yalikuwa yanalipiwa shilingi 1000/=; tumeondoa; ni bure.

SWALI: Nini hasa lengo la kuanzisha utaratibu huu wa ndoa poa?

JIBU: Nia hasa ya kufanya hivyo ni kuwapa waamini unafuu wa kupata Sakramenti ya Ndoa na hivyo kuwasaidia wasio na uwezo wa kumudu malipo hayo ili ifikapo mwaka 2000 Wakatoliki wawe wamesimama imara katika sakramenti zao kwa kuondolewa vizuizi ambavyo pia huwakwaza watoto ambao wazazi wao hawajapata sakramenti hii. Oktoba 9,mwaka huu tutafunga ndoa nyingi za pamoja hapa kanisani. Idadi kamili hatujaipata toka vigangoni lakini zitakuwa nyingi sana.

SWALI:Uongozi wa sasa hapa parokiani ukoje?

JIBU:Sisi unatufahamu kama unavyotuona ; lakini wapo wasaidizi wengine Padre Benedict Hema na Bro. Andreas Mwanga, wote ni wa Shirika la Capuchin. Baraza la Walei linaongozwa na Sales Kingumwile (Mwenyekiti), Makamu Mwenyekiti ni Judith Mkoba, Katibu ni Theresia Dimoso, Katibu Msaidizi ni Albano Kachenje na Mweka Hazina ni Alfred Kritikos.

SWALI:Parokia yako baba Paroko ina vyama vya kitume?

JIBU: Tunavyo vigango 10, jumuiya 80 na vyama vya kitume 12 ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo ya parokia na kuona kuwa Neno la Mungu linawafikia Wakristo katika mtindo na maadili yanayokubalika na jamii ya Kikatoliki.

Jumuiya tulizo nazo ni Moyo Mtakatifu wa Yesu, Wanaume Wakatoliki, Waministranti, CPT, WAWATA, VIWAWA, Waterisiari, Uamsho, Visenti wa Paulo, Legio Maria, Virafra na Utoto Mtakatifu wa Yesu.

Vigango vyetu ni Buguruni, Bungoni, Mivinjeni, Sharif Shamba, Kariakoo, IlalaUtete, Kigogo A, Kigogo B, Michikichi na Vinguga.

SWALI: Mbona sijasikia ukitaja kwaya?

JIBU: (Paroko anacheka na kusema) Kwaya si chama cha kitume; hata hivyo tunazo kwaya 8 chini ya Shirikisho la Kwaya Katoliki Msimbazi (SHIKKAM) ambalo huongozwa na Mwenyekiti J.Mkoba, Makamu Mwenyekiti Happiness Nyakulimba, Katibu -Jeremia Msuli, Katibu Msaidizi Gaspar Mbonda na Mweka Hazina F. Gutapaka.

Kwaya tulizonazo na viongozi wake tukianzia na Mwenyekiti, Makamu, Katibu, Katibu Msaidizi na Mweka Hazina ni; Kwaya A; Simon Kala, Resipr Swai, Amina F. Ngowi, G.F. Gutapaka na Restis Swai. Kwaya B ni Ladislaus Ukani, Agapt Komba, Theones Mkoba, Gasper Mponda na S. Riwa.

Kwaya C; Simon Ndekulesa, Sistin Andrew, John Mloka, Imelda Luanda na Stela Ndaki.

Nyingine ni Kwaya D; Leonard Idd, Julianus Impandu, Rosemary Ligugo, Cecilia Clemence na Rosada Masawe.

Kwaya A ya Kariakoo ni Happiness Nyakulimba na Serlijor George. Kwaya B ya Kariakoo ni Anthony Kiami, Amoni Kashaija, C. Kalinda na Donatila Protasi

Nyingine ni kwaya za Moyo Mtakatifu wa Yesu ya Vingunguti; Jeremiah Msuli, Respicius Komzora, Tecla Limbumba, Anthony Limota na Elizabeth Kisesa; pamoja na kwaya ya Mtakatifu Theresia ya Vingunguti ambayo viongozi wake ni Thomas Kisoka, Steven Mwankenja, Yolanda Lutengo, Emmanuel Matonya na Neema Ngandu.

SWALI:Parokia hii ina mradi wowote?

JIBU:Kutokana na hali ya ukata , hatujafungua mradi ; huu wa chuo ni wa wanafunzi wenyewe ambapo nusu ya wanaohitimu waliofanya vizuri baada ya miaka miwili hufanya uzalishaji hapa kwa miezi 6 na kisha kila mmoja huondoka na cherehani yake. Wao hulipia Sh. 35,000/= kwa mwaka. Hujifunza mitindo mbalimbali ya ushonaji na wanazalisha sana hata makanisa mengine huleta oda zao hapa. Pia ndani ya parokia tunacho chuo cha kufundishia walimu wa chekechea (Montessori Training Center) na Kituo cha Kulelea Watoto Yatima kinachohudumiwa na jimbo, pamoja na shule za chekechea.

SWALI: Nini malengo yenu ?

JIBU:Sisi tulijiwekea malengo ya kukarabati ukumbi wa parokia ili hata wenye sherehe wautumie kwa gharama nafuu, kununua "stand by generator" ili kuondoa tatizo la umeme unapokatika ghafla hata wakati wa ibada, kujenga kihekalu cha Bikira Maria kinachogharimu Milioni 7; kazi hii imekwisha anza; uzinduzi wake utakuwa Agosti 15 na malengo yote hayo ya mwaka tutayatimiza hatua kwa hatua.

SWALI: Ni matatizo gani mnakumbana nayo katika shughuli zenu za kila siku?

JIBU: Tatizo kubwa ni msongamano mkubwa katika makaburi kwani watu kutoka parokia nyingine hata wale wasio shiriki shughuli za kikanisa wanapofiwa hutaka ndugu zao wazikwe katika makaburi yetu; pamoja na watu kuwa wagumu kutoa zaka; na sidhani kama hawajui umuhimu na faida ya kutoa zaka; mpaka wanapolazimika na hufanya hivyo kwa kiasi cha chini kabisa.

Hata hivyo hayo tunayashughulikia na kuyatatua kibinadamu na wito wetu ni kwamba Wakatoliki wajiunge na jumuiaya katika maeneo yao ili iwe rahisi kuwasiliana na kuifanya vyama kazi ya Mungu kwa upendo na ujasiri.

SWALI:Mnaweza kuwapa wasomaji wa gazeti hili historia ya pariokia hii kwa ufupi?

JIBU:Ujenzi wa Kanisa la Msimbazi ulianza Septemba,1953 baada ya parokia kuzaliwa Januari 13, 19952 na lilibarikiwa Juni 12,1959. Lilianza na Waamini 7000 na sasa ni zaidi ya 150,000. Paroko wa kwanza alikuwa PadreKlemens Hug akisaidiwa na Padre Lucius Eisenring. Paroko wa Kwanza mzalendo ni huyu Padre Tarimo tangu 1996 (anajibu Paroko Msimbazi).