Ijue Parokia ya Makuburi

PAROKIA ya Makuburi ni Parokia changa iliyopo katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Pamoja na uchanga wake imeweza kupiga hatua kubwa katika shughuli za kiroho na kimaendeleo. Mwandishi DALPHINA RUBYEMA alihojiana na Mwenyekiti wa Parokia hiyo Bw. GISLAS ZULU.

Swali: Mwenyekiti unaweza kuwaeleza wasomaji wetu historia ya Parokia yako kwa ufupi?

Jibu: Parokia ya Makuburi ilianzishwa kama kigango cha parokia ya Manzese chini ya uongozi wa padri Geraldo Chebanon. Waumini wa Kanisa Katoliki eneo la Kibangu, External, Tabata, Sahara na Ubungo Kisiwani, walianza kushiriki ibada katika kijikanisa kidogo kilichojengwa mithili ya ghala.

Uongozi wa Kigango katika harakati zake za kuendeleza kigango hiki uliunda kamati ambayo mwaka 1995 ilifanikiwa kupata na kununua nyumba iliyopakana na eneo la kanisa. Nyumba hiyo baadaye ilifanyiwa ukarabati wa kina hadi kufikia kiwango cha ubora wa kuwa na hadhi ya kuwa nyumba ya kuishi mapadri.

Mnamo Agosti 2 mwaka huo huo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alifika kigango cha Makuburi kutoa Sakramenti ya Kipaimara. Uongozi wa Kigango ulimwomba afanye kigango hicho kuwa Parokia. Yeye alitaka kuhakikishiwa kwamba kigango hicho kina uwezo wa kifedha wa kulisha mapadri na kujiendesha kama parokia kabla ya kupandishwa hadhi. Uongozi ulimhakikishia kwamba uwezo huo upo.

Shughuli za ujenzi zilianza rasmi mwaka 1996 na mnamo Mei, mwaka jana jiwe la msingi liliwekwa na aliyekuwa Balozi wa Papa nchini Tanzania Mhashamu Askofu Mkuu Francisco Javier Lozano.Ujenzi wa kanisa hilo la Mwenyeheri Anuarite, ulikamilika Novemba mwaka jana ambapo Desemba mwaka huo huo kanisa lilibarikiwa na kuwekwa wakfu na Mwadhama Kardinali Pengo.

Swali:Katika maelezo yako sijasikia unataja waliogharamia ujenzi huo; unaweza ukawataja?

Jibu:Kamati ilibuni mikakati mbalimbali ya kupata pesa za kugharamia ujenzi wa kanisa hilo. Kutokana na uhamasishaji uliofanywa na uongozi wa parokia teule, waumini wa Makuburi walijitolea kwa hali na mali kuchangia ujenzi wa kanisa lao. Juhudi hizo pamoja na misaada mbalimbali iliyotolewa na vikundi, makanisa mengine, wafadhili kutoka nchi za nje, waumini wa maparokia mengine na Makao Makuu ya Baba Mtakatifu Vatican zilifanikisha ujenzi wa kanisa hilo.

Swali: Parokia yako inasifika kwa kuwa na ibada za kuwaombea marehemu kanisani kabla ya kwenda makaburini kwa mazishi. Kwanini utaratibu huo uliwekwa?

Jibu:Uongozi wa parokia uliweka utaratibu kwa vile tuliona unatoa nafasi kubwa zaidi kwa wakristu wengi kushiriki misa hiyo. Hapo awali kulikuwa na utaratibu wa marehemu kuombewa majumbani kwao lakini ilikuja kubainika kuwa waumini wengi walikuwa hawashiriki ibada hiyo. Parokia pia imewafundisha walezi na viongozi jinsi ya kuongoza ibada za mazishi pale ambapo padri hapatikani.

Swali: Je muundo wa utawala wa parokia yako ukoje?

Jibu:Muundo wa parokia hii unafuata mfumo wa utawala wa maparokia mengine katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Muundo huo umegawanywa kwenye vikundi vitatu ambavyo ni Radio, Jeshini na Radio Maji.

Kanda ya Relini vikundi vyake ni External, Sahara na Relini viwandani ambapo vikundi vya Darajani, Corner, Gereji, Maziwa na TANESCO vinapatikana kweye kanda ya Ubungo Kisiwani.

Swali: Je, parokia inazo jumuiya ndogo ndogo?

Jibu:Ndiyo parokia inazo jumuiya ndogo ndogo zipatazo 45. Madhumuni yake ni kuelewana kwa ukaribu, kusali kwa pamoja, kuelimishana kuhusu maisha yaUkristu na juu ya yote haya kusaidiana kama ndugu katika Kristu. Jumuiya hizi zimejiwekea siku ya kushirikiana kwa sala , nyimbo na tafrija na kuweka akiba ya pamoja ya kusaidiana katika shida na raha.

Swali: Vipi upande wa vyama vya kitume na vigango vya parokia?

Jibu:Parokia ya Makuburi ina vyama vya kitume vipatavyo sita ambavyo ni Moyo Mtakatifu wa Yesu, Legio Maria, WAWATA, VIWAWA, Karismatiki na Wanaume Wakatoliki.

Kwa upande wa vigango tunavyo vigango vya Makuburi Kibangu , Nzasa,Makoka,Bonyokwa na Kihungule.

Swali: Ili kuwasisimua waumini katika ibada i kunahitajika kwaya. Je parokia ya Makuburi inazo kwaya ngapi?

Jibu:Ndiyo Parokia inazo kwaya tatu zinazoongoza kati misa tatu za Jumapili. Hizo ni Kwaya ya Mtakatifu Cecilia,Kwaya ya Sayuni na Kwaya ya Mtakatifu Kizito. Kila kwaya ina uongozi wake na zimefanikiwa kurekodi kanda mbalimbali ambazo zinauzwa kwenye makanisa mbalimbali Jimboni Dar es Salaam na kwingine.

Swali:Nini maendeleo na Mafanikio ya Parokia?

Jibu:Parokia hii pamoja na uchanga wake imepiga hatua nzuri za maendeleo ambazo kwa kweli zinatia moyo.

Kwa kipindi kifupi tumefanikiwa kujenga ofisi ya mapadri na kumbi mbili za mikutano ambapo kutokana na juhudi za uongozi wa parokia, maeneo kadhaa yameweza kupatikana kwa ajili ya kuanzishia vigango.

Parokia pia imeanzisha madarasa ya kiinjili kwa watoto wadogo ambao hufundishwa elimu ya dini na masomo ya Sunday School hutolewa kila jumapili katika vigango vya Makuburi na Kibangu.

Swali:Kuna ongezeko la waumini kiasi gan?

Jibu:Wakati kigango cha Makuburi kinaanzishwa kulikuwa na waumini wapatao 1,500 tu. Wingi wa waumini uliendelea kuongezeka hadi kufikia jumla ya waumini 9,000 tulio nao sasa.

Swali: Parokia yako ina utaratibu wa Jumapili ya mavuno kila mwaka. Je ni nini malengo ya utaratibu huu?

Jibu:Kwanza kabisa napenda kuwatangazia wasomaji wa gazeti hili na wale wenye mapenzi mema kwamba utaratibu tulio nao ni wa misa ya shukrani na wala siyo Siku ya mavuno kama wengi wanavyodhania. Hapa kila Mkristu anawajibika kutoa kiasi cha mavuno yake ya mwaka husika kwa Muumba wake kama shukrani.

Swali: Parokia inakabiliwa na matatizo gani?

Jibu: Kwa ujumla matatizo tuliyonayo siyo mengi na yanapotokea tunajitahidi kuyamaliza kwa kushirikiana na waumini wa parokia hii.