Ngano za Padri Haule

Kwanini watu wanakosa tunu adimu ya uadilifu?

Hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ambayo yamedhihirisha kwamba kuna baadhi ya Watanzania ambao si waadilifu.

Tunapozungumzia kuhusu uadilifu tuelewe kuwa ni ile tabia au hali aliyo nayo binadamu ambaye ni mstaaarabu.

Binadamu mwadilifu ni yule ambaye ni mwaminifu, ni mwenye haki, ni mwenye tabia bora, ni mnyofu, aliye mwema na mwenye maadili mazuri.

Uadilifu huenda sambamba na uaminifu kaatika utendaji na pia katika kuishi katika jamii yo yote ile, iwe ni ya watu wachache au watu wengi.

Tunaweza kusema kuwa tabia ya mtu kuwa mwadilifu ni ya lazima kabisa katika maisha ya binadamu popote pale alipo, ilimradi anahusiana na watu wengine.

Tukio la watu kuiba mitihani na kuanza kuiuza ni kitendo cha kukosa uaminifu, kukosa haki , ni tabia mbaya na pia ni ukosefu wa maadili mema katika jamii zetu.

Tunapenda kuwauliza wahusika wa vitendo kama hivyo, ikiwa kweli kwa njia hiyo tutaweza kulijenga taifa hili ama sivyo.

Lakini kitu cha kujiuliza zaidi ni kwamba wenzetu kutoka nje wanatuonaje kuhusu kiwango chetu cha elimu?

Ukweli ni kwamba elimu inayotolewa hapa Tanzania itakuwa haina hadhi au itaonekana kuwa ni ya kiwango cha chini kabisa kwa vile wanafunzi wetu wanafaulu mitihani kwa njia ya wizi na kununua mitihani.

Mapato yake huonekana siku kwa siku katika fani mbalimbali, kwani uwezo wa hao vijana na utendaji wao ni duni sana.

Taifa letu limeshapata hasara na aibu nyingi sana kutokana na ukosefu wa uadilifu na pia uaminifu katika utendaji.

Kuna kazi mbovu sana kutoka maofisini, kuna utendaji mbaya katika maofisi mengi kwa sababu kubwa hasa ya kukosa uadilifu.

Tunaweza kusema ule mtindo wa zamani wa "ndugunaizesheni" au "jamaanaizesheni" uko bado. Ni wazi kuwa kabla ya wizi huo wa mitihani kusambaa karibu nchi nzima ulianzia kwa kuwasaidia watu au wanafunzi wa karibu au ndugu.

Tunapohubiri kuhusu "rushwa" katika taifa letu tukumbuke kuwa imetupasa kwanza kuwa na tabia ya uadilifu na uaminifu.

Hatuwezi kusema kuwa ukosefu wa uadilifu uko tu katika sekta ya Elimu, lakini uko karibu katika kila sekta ya huduma katika taifa letu.

Pengine tukio hilo la wizi wa mitihani linaonekana kuwa zito sana kwa vile limejulikana waziwazi, na kumbe kuna matendo mengi ya aina hiyo ambayo yamefichika lakini ya athari kubwa sana katika taifa letu.

Hapo awali sisi Watanzania tulikuwa na sifa kubwa sana huko nje, na tukajulikana kama watu wenye uadilifu.

Lakini baada ya kusoma na kusikia jinsi tulivyo na tabia ya udanganyifu na kukosa uadilifu, situmaini kuwa hao ndugu zetu waliokuwa na imani nasi wataendelea na imani ile ile.

Natumaini wakati umefika kwetu sisi Watanzania kubadilisha mtindo wetu wa tabia.

Wachunguzi wa mambo wanatuambia kuwa ukosefu wa uadilifu umechangiwa na umaskini au ukata tulio nao katika taifa letu.

Lakini hata hivyo haatuwezi tukachukua njia za mkato ili kuhalalisha vitendo vyetu vilivyo viovu kwa sababu hiyo.

Tunapenda kuungana na yule kiongozi ambaye alitamka hivi karibuni kuwa ukosefu wa uadilifu katika taifa letu umechangiwa na kima kidogo cha mishahara.

Jambo hilo ni la kweli kwa namna fulani, lakini hiyo mishahara mikubwa itapatikana vipi ikiwa wafanya kazi hawafanyi kazi zao kwa uaminifu na uadilifu?

Hapo tunaona kuwa ni kama vile mzunguko unaorudia pale pale, kwani bila kufanya kazi kwa uaminifu na kwa uadilifu hatuwezi kabisa kuwa na mishahara mizuri.

Kwa hiyo jambo linalotakiwa ni kuzingatia kwanza uadilifu katika kazi pamoja na bidii katika utendaji wetu wa kila siku.

Tunahitaji kuwa na moyo wa kujituma katika kazi zetu na hivyo kuwa na fahari katika utendaji wetu wa kila siku.

Napenda tena kurudia yale ambayo tulikuwa tumeyaandika katika Hoja zetu za hapo awali kuwa tunapaswa kuwalea na kuwafunza watoto na vijana wetu katika hali na tabia ya uadilifu na uaminifu.

Maadili mema ndiyo msingi hasa wa taifa lo lote lile ambalo linataka kujiendeleza na katika hali ya ustaaarabu wa kweli.