Utamaduni katika kupeana zawadi

Nakumbuka sana wakati nilipokuwa bado mdogo, nilipotaka kwenda kumwangalia Mjomba, Mama yangu alikuwa ananiambia kuwa nisingeweza kwenda kwa Mjomba bila zawadi yo yote ile. Kwa maneno mengine Mama yangu alikuwa akinifundisha kwamba daima ninapokwenda kuwatembelea ndugu, na hata marafiki nilitakiwa niwe na zawadi fulani ya kuwapelekea.

Huo ndio utamaduni wetu wa kiafrika. Na kutokana na utamaduni huo kumekuwa na misemo mbalimbali kuhusu jambo hilo kama vile: "Mgeni afike, mwenyeji apone; au pengine "Mgeni ni baraka ya nyumba" na kadhalika.

Maana ya misemo hiyo ni kwamba kila mgeni katika utamaduni wetu alitegemewa kuleta cho chote kwa wenyeji wake. Haikutokea kwamba kulikuwa na mgeni ambaye alifika mikono mitupu na hakuleta cho chote kwa wenyeji wake.

Mambo ndivyo yalivyokuwa pia katika mahusiano ya binadamu na Muumba wake. Tunasoma katika Kitabu kitakatifu kwamba binadamu aliambiwa kwamba hawezi kwenda kwa mtu mkubwa bila kuwa na cho chote mikononi mwake, na hivyo pia hakuweza kuruhusiwa kwenda mbele ya Mungu wake pasipokuwa na zawadi mikononi mwake.

Kwa maneno mengine binadamu alihimizwa kutoa sadaka na vitu mbalimbali kama zawadi kwa Mwenyezi Mungu,Muumba wake. Huo ulikuwa ni utamaduni wa Kiyahudi, na pia ni mapokeo ya kidini halisi.

Ni jambo la kusikitisha kuona siku hizi watu wanaamua kwenda kuwatembelea ndugu zao walio mbali wakiwa mikono mitupu. Tunatambua kuwa hali ya uchumi ni ngumu, lakini papo hapo inatupasa tuushike utamaduni wetu wa kiafrika na pia ule wa kidini.

Tunahimizwa kuwatolea zawadi wale watu ambao wametutendea mema kwa namna moja au nyingine. Pia tunahimizwa kuwapa zawadi wale wote ambao ni marafiki zetu na ndugu zetu kwani kutoka kwao tumefaidika sana.

Sote tunatambua kuwa bila kupata zawadi kutoka kwa marafiki na ndugu zetu hali zetu zisingekuwa nzuri kama zilivyo siku ya leo. Wengi tumekuwa na hali njema katika maisha yetu kutokana na misaada au zawadi tulizojaliwa na wenzetu. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa tuna deni kubwa sana kutoka kwa ndugu, majirani na hata marafiki kwa sababu ya zawadi walizotukirimia.

Kwa hiyo basi mtu anapoamuwa kwenda Kanisani siku ya leo, ni sherti aandae zawadi ya kwenda kumpatia huyo Bwana ambaye anamwendea huko Kanisani. Unapoamua kwenda kwa ndugu na jamaa ambao pengine wanaishi huko mijini ni sharti uandae nawe zawadi ambayo wataipokea pamoja na kukupokea wewe mwenyewe. Tusiende mikono mitupu iwe ni mbele ya Mungu au kwa ndugu zetu.

Mara nyingi zawadi tunazowapelekea wenzetu huwa zinavuta sana huruma na ukarimu wa hao tunaowapatia hizo zawadi. Tukumbuke kuwa kila tunapotoa zawadi ni kama vile tunajiwekea akiba na hivyo kuvuta upendo wenye ukarimu kutoka kwa wenzetu.

Wengi husema kuwa hawana cho chote cha kuweza kuwapelekea wengine. Huo si ukweli, kwani hakuna mtu ambaye hana cho chote kile hata asiweze kutoa kitu fulani kwa mwenzake.

Mara kwa mara katika familia, mwanafamilia moja akiwa amesafiri, wale waliobaki nyumbani humtakia mema huyo msafiri na kumwombea aweze kurudi salama. Daima wanamtakia kila la kheri katika safari yake na pia katika shughuli zake mbalimbali. Hivyo ni wajibu wa huyo aliyesafiri kutoa shukani kwa hao wenzake waliomtakia safari njema, pengine bila yeye mwenyewe kufahamu.Pia tukumbuke kuwa zawadi ni zawadi, hata kama kingekuwa ni kitu kidogo sana. Kwa maana hiyo Waingereza huita ni "token" yaani ni kakitu kadogo, lakini kana maana sana.

Basi tunapenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha kuhusu jambo hilo la kupeana zawadi. Kwa kuwa tunaikaribia ile Sikukuu ya Christmas, tunaona afadhali tukumbushane juu ya kupeana zawadi, kwa Sikukuu ya Krismasi ni Sikukuu wa wanafamilia kupeana zawadi kwa kuwa Mungu Mwenyezi amekuwa tayari kutupatia Mwanae, Yesu Kristu kama zawadi, licha ya kutupatia huu uhai tulio nao. Tunapaswa kupeana zawadi katika maisha yetu, na kwa namna ya pekee hasa katika nafasi ya Sikukuu hii ya Noeli. Bado tuna muda wa kuweza kuwaandalia wenzetu, marafiki, ndugu, jamaa, na majirani zawadi mbalimbali.

Tukumbuke kuwa kama kuna kitu chenye kujenga udugu, au urafiki kati yetu sisi binadamu ni tabia au mazoea ya kupeana zawadi. Urafiki na hata udugu hauwezi kudumu kama hakuna kupena zawadi. Basi, tunakusihi msomaji, tafadhali ujenge tabia na mazoea ya kuwapa wenzako zawadi, nawe hutakosa zawadi na kusaidiwa katika maisha yako.