Padre P. Haule

na Nguvu ya Hoja

Je ni lazima Tukielewe Kile tunachoimba?

LICHA ya mazungumzo ya kawaida, binadamu huwasilisha ujumbe alio nao moyoni mwake kwa njia ya nyimbo.

Wakati binadamu akiwa katika furaha hucheza na kuimba. Wakati huyo binadamu akiwa katika msikitiko huimba nyimbo za masikitiko.

Jambo la msingi ni kwamba kila wimbo huwa una lengo na maana yake. Binadamu anapoimba huwa na maana ya kuwapasha wengine habari, lakini pia huimba kwa ajili ya kujifurahisha au kujiliwaza yeye mwenyewe binafsi.

Kuna nyimbo zenye maneno ya kueleweka na pia kuna nyimbo ambazo maneno yake hayaeleweki kwa yule anayeimba na kucheza.

Mara kwa mara tunashuhudia watu wanavyoweza kucheza wakifuatisha melodia au sauti za zana zinazotumika katika muziki huo. Jambo hilo sio geni sana hasa siku hizi zetu. Tunashuhudia jinsi wale wanaopenda muziki wanavyocheza na kurukaruka wanaposikia nyimbo za kizungu au za kikongo.

Ingawaje maana ya maeneo ya nyimbo hizo hayajulikani kwa wachezaji lakini watu wanafurahia sana zile melodia za nyimbo hizo hata kama hawaelewi maana ya maneno yake.

Tumesema kuwa nyimbo zina maana ya kuwakilisha ujumbe kwa wale wanaosikia na pia kwa wachezaji.

Tumekuwa na watunzi wetu wengi wa nyimbo za kiswahili na hata kiingereza. Nyimbo hizo zimekuwa na mafundisho mazuri sana. Wasikilizaji na pia wachezaji ( na siku hizi katika TV tunao watazamaji) hufaidika kwa vikubwa kutokana na ujumbe wanaoupata katika nyimbo hizo.

Tunapenda tueleweke vizuri katika Hoja Yetu hii kuhusu huo muziki unaowafurahisha wengi bila maneno yake kufahamika kwa wengi. Tungetamani kuona kuwa wapenda muziki katika nchi yetu wanaelewa kile wanachokifurahia na hata pengine kuimba.

Tunatumaini kuwa wakati umefika wa Wizara ya Utamaduni kujiuliza kwa nini wananchi wengi wa Tanzania wanapenda sana muziki wa Kikongo kuliko muziki mwingine?

Watanzania kwanza hatuna budi kukiri kuwa tumewapoteza wale wanamuziki waliokuwa wakigusa mioyo yetu kama vile akina marehemu Mbaraka Mwishehe, akina Marijani na wengine. Zile bendi zetu zilizokuwa zikipiga na kusisimua mioyo ya watu hazipo tena na wala hakuna zilizofika badala yake.

Lililobakia sasa hivi ni kupiga kanda za Kikongo au za Kizungu na zile za ndugu zeti Wamarekani weusi.

Hatusemi kuwa hakuna jitihada kutoka kwa wanamuziki wetu. Wako akina TOT akina F.M. na wengineo. Lakini kwa bahati mbaya hao wote wanshindwa kuzima kiu ya wapenzi wa muziki.

Tunauliza hao wanamuziki wetu wanaofanya jitihada mbali mbali ni misaada mingapi wanapewa kutoka kwa wahusika. Tukitaka wapenzi wetu wa muziki wasiuhusudu muziki wa kigeni tunapaswa kuuenzi muziki wetu kwa hali na mali.

Tunakumbuka sana kwa miaka mingi katika Kanisa Katoliki ibada takatifu kwa vikubwa zilikuwa katika lugha ya Kilatini. Waumini waliokuwa wakielewa lugha hiyo walikuwa wachache sana. Lakini muda ukafika ambapo mambo yalilazimika kubadilika na hivyo ikaruhusiwa kutumika kwa lugha ya mahali, ya kueleweka.

Tokea hapo kumekuwa na mabadiliko katika kanisa ili waumini waweze kuelewa kile wanachokisali au kukiimba.

Wataalamu wanatuambia kuwa yule anayeimba katika ibada huwa amesali mara mbili. Lakini atakuwa amesali mara mbili ikiwa anaelewa ni nini anachokiimba. Katika muziki mwingi kuna maneno hasa yale ya mapenzi, na pia ya kujenga maadili. Tunatazamia kuwa yule anayesikiliza muziki hufarijika na kuliwazwa na melodia nzuri ya sauti ya mwimbaji na ya vyombo.

Vitu hivyo vyote viwili huhitajika sauti ya vyombo na ya mwimbaji pamoja na ujumbe ulio katika maneno.

Kwa hiyo wapenzi wetu wengi wa muziki wanakosa ule ujumbe ulio katika maneno. Je, wataupataje ujumbe huo?.

Hatuwezi kuwalazimisha wale wanamuziki wa kikongo watutungie nyimbo hizo za "Ikibinda Nkoi, Ndombolo" katika lugha ya kiswahili. Lakini lingekuwa ni jambo zuri kwa wahusika wa muziki kutoa ushauri au ombi la kuwa na tafsiri ya nyimbo hizo za kikongo.

Kwa kuwa mashabiki wengi wa nyimbo za kikongo ni kutoka Tanzania kwa nini isiandikwe tafsiri ya nyimbo hizo katika hizo majarida yake 'cover' za kanda za Video au za Kaseti.. Tunapenda kuona wapenzi wa muziki wanafaidika kikamilifu katika kuusikiliza na kuucheza huo muziki wa kikongo.

Tunatumaini kazi hiyo isingekuwa ngumu kwani tunao Waswahili siku hizi katika sehemu mbali mbali za ulimwengu. Wako huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na pia wako kule Ufaransa na sehemu nyinginezo za Ulaya. Tunaamini kuwa wangeweza tu wakafanya kazi hiyo.

Lakini la kuzingatia hapa, Je, sisi watanzania hatuna wanamuziki wabunifu. Kwa hakika tunao siyo tu akina Kapteni John Komba peke yao, bali wako na wengine wengi. Tunao watu wenye karama ya muziki katika taifa letu lakini wamezikwa kwa sababu labda ya umaskini au unyonge.

Taifa haliwezi kunufaika vilivyo ikiwa jamii haiko tayari kugundua na kutumia karama za raia wake. Wako watanzania wengi wenye karama ya utunzi katika muziki. Wako wengi wenye karama ya ubunifu wa kuweza kuunganisha mambo yetu ya utamaduni na yale ya kisasa.

Hao wote lakini wanahitaj sana kupewa jeki ya kusaidiwa. Ni lazima tukiri kuwa mahali pale ambapo watu wengi hukusanyika na kufurahi ni mahali pazuri. Kwa hiyo huko kwenye maholi ya madisco na madansi ambako watu wengi hukusanyika na kufurahi sharti pawe ni mahali pazuri tena pa faraja.

Hapo tunapaswa kukumbuka pia ni kwa jinsi gani wazee wetu katika jamii yetu walivyotumia nyimbo kama shule ya kuwafunza maadili vijana na hata watu wazima.

Kulikuwa na nyimbo za kuonya wale watu wasiotaka kushirikiana na wenzao au kujitenga; kulikuwa na nyimbo za kuwafundisha na kuwahimiza vijana kuhusu bidii katika kazi, kulikuwa na nyimbo za kuwakanya vijana na hata watu wazima kama kulikuwa na ukiukwaji wa maadili, kulikuwa na nyimbo za kuwasifu watu hodari, na kinyume chake kulikuwa pia na zile nyimbo za kuwalaumu wale ambao walikuwa waoga na watepetevu.

Kwa kifupi tunasema kuwa nyimbo kama nyimbo zilikuwa zina maana kubwa sana katika jamii. Hata sisi katika jamii yetu ya leo tunahitaji sana kuwa na nyimbo za kuwaonya, kuwashauri, kuwahimiza na hata kuwakanya vijana, na watoto wetu. Wazee wetu walifundishana na hata kushauriana katika ngoma kwa njia ya nyimbo. Nasi siku ya leo tunahimizwa kutumia ngoma zetu, madisco na madansi yetu tukiwa na nyimbo za kueleweka zinazotufunza maadili na mbinu bora za kuishi kwa furaha zaidi.

Tunatumaini hakuna mtu asiyetambua faida ya muziki na hasa ile ya nyimbo. Tunazidi kutoa rai kwa wote kupenda kusikiliza muziki kwani hiyo ni zawadi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Angalia ni kwa jinsi gani kile kitabu cha Zaburi kinavyopendwa na waamini. Ni kwa sababu humo kwa njia ya Nyimbo na Tenzi Mungu na mtunga Zaburi ametufunza mambo mengi. Licha ya kuburudisha moyo, nyimbo hutuletea mafundisho makubwa yawe ya maisha au ya kiimani.

Napenda kutoa rai kwanza kwa wanamuziki wetu walete muziki wenye nyimbo zinazowafunza watu, hasa vijana, zinazowafurahisha watu kwa maneno na lugha nzuri. Tunawahimiza wanamuziki wetu kutuletea zile nyimbo zenye maadili safi, zenye utamaduni wa kikweli. Tunahitaji muziki wenye melodia nzuri pamoja na maeneo yanayoeleweka. Tufurahie kile ambacho tunakielewa maana ikiwa kinaeleweka kitazidi kutujenga. Hali na tabia tuliyo nayo ya kufurahia tu melodia bado haitoshi katika malezi na maadili yetu.