Padre P. Haule

na Nguvu ya Hoja

Tunapaswa kupiga vita udanganyifu

MARA nyingi nimewasikia watu wakisema kuwa 'mzungu hadanganyi, daima ni mkweli'.

Maneno hayo yanaweza yakawa sahihi kwa kiasi fulani. Tumezoea kumhusianisha mzungu na ile hali ya ustaarabu. Sifa mojawapo ya mtu mstaarabu ni kuwa mkweli.

Kwa hiyo tungeweza kusema kuwa kila mstaarabu ni mtu aliye mnyoofu, aliye mwadilifu na pia mkweli.

Kinyume chake lakini hali ya kutokuwa mkweli, yaani kuwa mdanganyifu ni hali ya kutokuwa mstaarabu.

Mtu mkweli ni pia mtu aliyemcha na kumwogopa Mungu.

Na ndiyo maana Bwana Yesu aliwaagiza wafuasi wake wawe wa kweli. Anasema hivi katika ile Injili ya Matayo: 'Ukisema Ndiyo; basi, iwe 'Ndiyo', ukisema 'siyo, basi iwe kweli 'siyo. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu (Mt. 5:37).

Yule mwovu ni shetani ambaye kwa asili ni mwongo yaani si mstaarabu. Lakini tunasema kuwa Mungu ni ukweli wenyewe.

Wakati Rais Benjamini Mkapa alipoanza kushika madaraka ya kuiongoza nchi yetu alitangaza sera zake. Licha ya vita dhidi ya rushwa alitangaza kuwa uongozi wake utakuwa ni wa ukweli na uwazi. Natumaini sote tunakubaliana na sera hiyo.

Watu wale ambao wamekusudia kusafiri pamoja kuelekea mahali fulani imewapasa waambiane ukweli. haifai kabisa kama watadanganyana. Wakidiriki kudanganyana watapotezana na itakuwa vigumu kufika kule wanakokusudia.

Kati ya mambo ambayo yametukwamisha kimaendeleo moja wapo ni ile tabia ya kutokuwa wakweli. Kumekuwa na tabia ya kudanganyana sana.

Hali hiyo ya kudanganyana imekuwa toka pande zote toka upande wa viongozi na pia toka upande wa raia.

Kuna neno la kiingereza lisemalo vizuri zaidi. Neno hilo ni 'transparency'. Hiyo ni hali au tabia ya kuwa mwazi kabisa bial wingu au giza giza katika usemi na hata katika utendaji.

Ni jambo baya sana kumdanganya binadamu mwenzako Udanganyifu hutokea siyo tu katika maneno bali pia katika matendo.

Wakati inapotokea kuwa kiongozi anasema kinyume kabisa cha matendo na hata maisha yake hapo tunasema huo ni udanganyifu. Pia wakati inapotokea kuwa raia wanakubali kwa maneno kuhusu jambo fulani kisha hawaendi kutekeleza kwa vitendo au kufanya kinyume chake.

Hali hiyo huwa ni ya kudanganyana na haiwezi kuwapeleka popote pale. Kwa hiyo tunapaswa kuwa wakweli na pia kuwa wa wazi.

Waalimu shuleni sherti wawe wa kweli, wasidanganye . Lakini tunapaswa kuanzia na wazazi kule majumbani. kwa kuwa wazazi ni walezi wa awali kabisa, basi imewapasa wawe wa kweli. Watoto hasa wa siku hizi wanapenda uwazi na ukweli. Ule udangnyifu wa kale katika makabila mengi, wakati wazazi (akina mama) wakiulizwa na watoto : Je, mtoto umempata toka wapi, na kujibiwa kuwa nimekwenda kumchukua kutoka mtoni. Jibu hilo si sahihi kabisa. Huo ni udanganyifu. Siku ya leo tunaambiwa kuwa mtoto aambiwe ukweli na kueleweshwa sawasawa kuhusu masuala kama hayo.

Tumechelewa kuendelea kutokana na udanganyifu. Kumekuwa na wanasiasa wengi ambao wamekuwa wadanganyifu. Kumekuwa na viongozi ambao mbele yao wakubwa wao wameonyesha kuwa na nia ya kuwatumikia wananchi, kumbe matendo yao yakawa kinyume kabisa.

Nchi yetu ya Tanzania ni kati ya nchi zile zinazoendelea zilizobahatika sana kupata misaada toka kwa wafadhili na wahisani. Lakini kumekuwa na udanganyifu mkubwa sana hapo katikati. Pengine hiyo misaada haikuwafikia walengwa, na pengine imetumika kinyume kabisa cha lengo. Umetokea udanganyaifu pamoja na wizi

Mapato yake hali ya walengwa wengi imebakia kuwa duni. tunavyofahamu udanganyifu huenda pamoja na wizi. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa watu wametumia udanganyifu katika kuliibia taifa letu.

Watalaamu hutuambia kuwa 'ukweli unauma'. Watu wengi huogopa kusema ukweli kwa sababu eti watawaumiza wahusika. Lakini ikiwa hatuambiani ukweli hatuwezi kupata maendeleo tunayotarajia.

Mtu mkweli ni yule aliye jasiri. Lakini yule anayeficha ukweli au kusema uwongo ni mwoga. Na mtu aliye mwoga hafai kabisa kuwa kiongozi wa kweli.

Katika utamaduni wetu wa kiafrika, mtu mdanganyifu au mwongo alichukiwa sana na hata kutengwa na jamii. Pengine ilisemwa kuwa afadhali ubaya wa mtu mwongo au mdanganyifu. Sisi Watanzania hatuwezi kuingia katika karne ya sayansi na tekinolojia ikiwa tunasema uwongo au kudanganywa. Sote tunapaswa uwa wakweli.

Tunapenda kukazia katika Hoja yetu hii na kutoa rai kwa kila mwananchi kuwa mkweli. Waganga wanapaswa kuwa wakweli kwa wagonjwa wao. Nao wagonjwa wasiwadanganye waganga wao.\Wataalamu wa kilimo inawapasa kutoa maelekezo yanayowasaidia wakulima katika ukweli bila kuwadanganya.

Hao wafanyao kazi za ukandarasi imewapasa wawe wa kweli wanapochukua tenda yoyote ile hasa zile za ujenzi na ufundi mbali mbali. Kuna wengi wao ambao hudanganya na kutokuifanya kazi kwa uaminifu, ukweli na uadilifu.

Mambo ni pia hivyo hivyo hata waandishi.

Waandishi wakiandika mambo yasiyo ya kweli huweza kusababisha hasara kubwa sana kwanza kwa wao wenyewe, na pia kwa mashirika yao. Iko ile kanuni ya uandishi inayodai kuhakikisha mambo zaidi ya mara moja. Hakuna nafasi ya kuficha ukweli wala ya ktunga mambo. Linalotakiwa ni kusema yale yaliyo ya kweli na ambayo yatajenga zaidi jamii kuliko kubomoa.

Hivyo pia hata kwa wale wahubirio Neno la Mungu. Hao kwa vikubwa zaidi hudaiwa kuwa wakweli, wanyoofu na wala wasiwadanganye watu kwa maneno yao matatu.

Maendeleo ya kweli yawe ya kimmwili (kidunia) au ya kiroho (kimbingu) yatapatikana kwa kusema ukweli - Uwongo haujengi.