Micharazo ya uzee na ukongwe

Majambazi yanapokuwepo kila mahali hadi vijijini!

SIKU hizi limekuwa karibu jambo la kawaida kusikia habari za ujambazi. Watu wasiokuwa na hatia wanavamiwa na vibaka au majambazi na kuporwa fedha na mali zao nyingine.

Wakati mwingine watu wanaoporwa vitu vyao hujeruhiwa vibaya na pengine kuuawa. Nilifikiri hali hii inatokea katika miji peke yake kumbe sivyo. Katika habari hii tunakula sahani moja na watu wa vijijini.

Hivi majuzi mwenye nyumba mahali ninapopanga hapa jijini Dar es Salaamu maeneo ya Tandika alitembelewa na baba yake. Anafahamika kwa jina la mzee Lugayila.

Bila shaka wengine wanaweza kukusia jina hili. Hawa ni wenyeji wa maeneo ya Bariadi mkoani Shinyanga. Mzee Lugayila, baba wa rafiki yangu, alinieleza kwamba anashangaa hali ya vijijini siku hizi hakuna amani kama zamani. Watu wanaishi maisha duni na karibu kila mtu analalamika maisha yamekuwa magumu. Hata wanapojibidisha kulima, mazao yao hayana soko la hakika. Wale wanaoonekana kufaulu bado hawana amani. Wakati wowote wanaweza kuvamiwa na kuporwa chochote walichonacho.

Kwa sababu ya ukata mzee Lugayila ameonelea aje kumsalimu mwanae akitegemea labda kupata kitu fulani kukwamua maisha yake. Amekuja pia kwa ajili ya kupata matibabu maana vijijini, kama yeye mwenyewe alivyoniambia mambo ya tiba hayana uhakika. Heri yao akina Lugayila wenye watoto wanaowajali na wenye misimamo ya kiungwana. Wana mahali walao pa kukimbilia katika hii patashika ya maisha.

Ujambazi tunaoufahamu wengi wetu ni ule wa kutumia nguvu. Ujambazi wa namna hii huendana na utumiaji wa silaha za hatari zikiwemo bunduki, mapanga, mikuki na visu vikali. Watu wengi wameanza kukerwa sana na hali ya ujambazi wa namna hii. Ndiyo maana mahali pengi siku hizi mtu akikurupushwa na kubainika kuwa ni jambazi basi ndio mwisho wake.

Watu watafanya kila njia kumkamata na kumwadhibu vikali. Baadhi ya watu hawaishii tu katika kuwaadhibu watuhumiwa au kuwapeleka katika vyombo vya usalama na kisheria, lakini hujitwalia mamlaka ya kutoa uhai wao. Watawapiga kwa fimbo, mawe, na hata kuwachoma moto.

Hali ya watu kujitwalia mamlaka kuwaadhibu watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi inajitokeza mijini hali kadhalika vijijini. Hawa wanaoadhibu majambazi hasa kwa kuuwa wakati mwingine hawasubiri kuwa na ushahidi wa kutosha.

Kwa kawaida huja na hasira zao zilizojengeka kwa muda mrefu kutokana na mambo mbalimbali. Ingawa njia wanayotumia pengine haiko sahihi daima na inahitajika kuangaliwa vizuri zaidi, hata hivyo hali hii inaonyesha wazi wazi kwamba kwa ujumla watu wanakerwa sana na tabia ya ujambazi wa kutumia nguvu.

Matokeo ya ujambazi ni kuwafanya wale walio na vitu kutokuwa navyo. Huwafanya watu waishi maisha ya hofu na yasiyo na matumaini. Ujambazi mara nyingi huwafanya wanaohusishwa kuishia kuwa masikini kama siyo kupoteza maisha yao. Ujambazi ni namna ya kuwanyang'anya watu haki yao ya kuwa na vitu au mali au hata maisha.

Ujambazi unaweza kufanywa na mtu mmoja. Lakini ujambazi unaweza pia kufanywa na kikundi cha watu au hata jamii moja ya watu kwa jamii nyingine. Ukiangalia vizuri utaona kwamba ujambazi unaohusisha watu wengi ndio hasa unashamiri siku hizi na unachukua sura na mitindo mbalimbali. Upo mtandao wa ushirikiano wa majambazi. Majambazi yanashirikiana siyo katika eneo moja lakini hata kutoka sehemu hii hadi nyingine na pengine nchi moja hadi nyingine.

Siku hizi licha ya kutumia silaha majambazi pia hutumia udanganyifu. Mara nyingi hutumia nguvu ya ujanja na hata ya kisaikolojia. Mtu anaweza kudanganywa kwa njia ujanja akajikuta anaingizwa mjini na kuachwa hana kitu. Watu wengi wamedanganywa na watu wanojiita maprofesa kwa kutumaishiwa kupata vitu zaidi na kuishia kuporwa hata kile kidogo walichokuwa nacho. Hii ni aina ya ujambazi.

Watu wengine wamedanganywa katika hali ya kutaka kusaidiwa. Pengine kwa kudanganywa kuwa marafiki. Aidha wengine wameishia kuibiwa fedha na vitu vingine vya thamani kwa kupewa madawa ya kulevya. Mambo haya yote ni vielelezo vya ujambazi kwa kuwa vinawaacha watu bila vitu.

Kama kweli watu wamekerwa na ujambazi ni lazima pia kuyangalia mambo haya yote na kuyavalia njuga sambamba na ule ujambazi wa kutumia silaha. Ujambazi ni ujambazi tu. Hata wanawake wanapoendelea kufanya kazi zaidi kuliko wanaume wengi katika familia na kuishia kupokonywa matunda ya kazi yao na baadhi ya wanaume, huu nao ni aina ya ujambazi.

Aidha, vijana wa kiume wanofanya kazi kutwa nzima. Pengine wanafanya kazi ngumu kwa ujira mdogo. Fedha na mali zao zinapochukuliwa kirahisi na akina dada huu nao ni ujambazi. Wengine watauita ni wa kisaikolojia. Hata hivyo ni ujambazi tu. Akina dada wanapopata nafasi ya kulichuna buzi kwa kweli wanafanya ujambazi. Tunapashwa kushirikiana kukomesha matendo haya yote kama kweli tunataka kumaliza ujambazi.

Mtu mwenye kipato cha chini anapoendelea kuhangaika kupata mahitaji yake halafu anatakiwa kulipa kodi. Hana hakika ya matibabu. Hana hakika kama watoto wake watapata elimu ya kutosha. Wala hana hakika ya chakula, malazi na burudani ya haki. Huyo ndiye hatimaye anabeba mzigo wa kulipa VAT kwa kuwa ndiye mlaji na hafanyi biashara yenye kipato cha kutosha. Huu kama si ujambazi pia basi ni kitu gani. Kama mfumo unamwacha mtu, mlala hoi, mama nitilie, na mtu wa kijijini katika hali ya kutojiweza, hali duni, je huu si ujambazi kweli?

Watu wanaojitahidi kuleta maendeleo hasa kwa watu wa kawaida kwa njia ya kujenga shule, vituo vya maendeleo, na sehemu za tiba halafu vitu hivyo vinataifishwa, je hii nayo si aina ya ujambazi? Na zile nchi tajiri, ambazo kwa kweli historia inaonyesha kwamba utajiri wao umetegemea sana mchango wa nchi zinazoonekana masikini na hazijaendelea, zinapoendelea kutawala njia kuu za uchumi bila kujali mahitaji ya nchi masikini, huu nao si ujambazi wa aina yake?

Kama kweli wananchi wamechoshwa na kukerwa na hali na ujambazi basi inafaa sana kuyavalia njunga mambo haya yote. Tunapashwa kuyashambulia yote kwa ushirikiano na nguvu ileile tunayokuwa nayo kwa yale majambazi yanayotumia nguvu au silaha.

 

 

Padre P. Haule na Nguvu ya Hoja

Tunadaiwa tuishi katika Haki na Wajibu

WATAALAMU wa maisha ya binadamu hutufundisha kuwa binadamu ni kiumbe kinachodaiwa kuishi maisha ya "kijamii".

Maisha ya kijamii ni maisha ya mtu panoja na binadamu mwezake. Binadamu hukamilika kimaisha anapoishi na binadamu mwenzake.

Hivyo tunaambiwa kuwa binadamu ana macho mawili aweze kumwona binadamu mwenzak vizuri na amsaidie, amepewa masikio mawili aweze kumsikiliza binadamu mwenzake vizuri. Anayo mikono miwili ili aweze kumsaidia mwenzake kwa kutenda kitu fulani.

Pia binadamu anayo miguu miwili ili aweze kutembea na kukutana na wenzake.

Isitoshe binadamu amepewa mdomo aweze kuzungumza na kuwasiliana na binadamu wenzake. Kwa kifupi binadamu ni kiumbe chenye mahusiano na binadamu mwenzake kimaumbile.

Katika mahusiano hayo, kun haki ambazo anapaswa kuzipata kutoka kwa binadamu mwenzake. Pia kuna wajibu anaodaiwa na binadamu wenzake. Kuna mambo anayodaiwa kutendewa na binadamu mwenzake, lakini pia kuna mambo ambayo anayodaiwa kuwatendea binadamu wenzake.

Kila binadamu ana haki ya kuishi na kupewa kila hifadhi ya uhai wake. Hakuna binadamu aliye na haki ya kuondoa maisha ya binadamu mwenzake.

Wataalamu wa mwili wa binadamu na walimu wa kanisa hutufundisha kuwa uhai wa binadamu huanzia pale tu mimba inapotungwa ndani ya tumbo la mama. Kwa hiyo hicho kiumbe kina haki ya kuishi na binadamu wengine wano wajibu wa kukitunza, kuanzia na huyo mama na majirani wote wanaomzunguka.

Baada ya kuzaliwa mtoto anayo haki ya kupata malezi kutoka kwa wazazi wake, kutoka kwa majirani na pia kutoka kwa wanajamii wote.

Naye mtoto kwa kadiri anavyozidi kukua akipata nguvu na akili, hupasika kuwa na heshima na pia utendaji kwa wazazi na binadamu wote wanaomzunguka.

Mtoto akishapata akili hupasika kupelekwa shuleni akapate elimu na maarifa mbali mbali. Ni haki ya kila mtoto kupata elimu na maarifa huko shuleni na mahala pengine pa mafunzo.

Kuna baadhi ya wazazi ambao hawataki kutambua wajibu wao wa kuwapeleka watoto wao shuleni ili wakapate elimu na maarifa kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Kuna wazazi ambao hawaoni umuhimu wa kuwasomesha watoto wao kwa kadiri ya uwezo wao.

Mtoto kama binadamu siyo mali ya wazazi tu, bali ni mali ya jamii nzima. Kwa hiyo jamii inadaiwa kumsaidia kila mzazi katika kumpa mtoto elimu ya maisha, iwe ni huko nyumbani au kule shuleni.

Jamii ya kwanza huhusika katika kuwaelimisha watoto ni "serikali". Tukianzia na serikali ya mahali au serikali ya kijiji hadi serikali kuu tunaona kuwa ni wajibu wake kuwasomesha watoto zikisaidiwa na wazazi.

Kila binadamu anayetokea hapa ulimwenguni anao mchango wake na pia wapekee katika ujenzi wa taifa na jamii kwa ujumla.

Tunaweza kusema kwa lugha rahisi kuwa kila binadamu ni sehemu katika jamii na hivyo ana wajibu na kazi maalum, mahali pake na pia wakati wake. Hakuna binadamu asiyo na mchango wa namna moja au nyingine katika jamii.

Serikali kama jumuiya kuu ya kuwalea raia haina budi kuwalea raia wake wote kwa usawa. Ile hali ya kuwa na upendeleo kwa baadhi ya raia wa mahali fulani na wa hali fulani ni kuwakosea haki wengine.

Tumesema kuwa wanaodaiwa kwanza jukumu la kuwalea na kuwaelimisha watoto ni wazazi na wanajamii wanaowazunguka. Kuna wazazi wengine hadi hivi leo ambao hawajatambua kabisa umuhimu wa kuwaelimisha watoto wao. Bado hawaoni kuwa ni wajibu wao kuwasomesha watoto wao.

Ukipita huko vijijini unaweza ukaona ukweli wa jambo hili. Ikiwa kweli wazazi na jumuiya ya mahali inatambua umuhimu wa kuwaelimisha watoto, unaona jinsi majengo na mazingira ya shule yalivyo. Lakini ukiona majengo ya shule ni kama mazizi ya wanyama, na mazingira machafu, hapo ujue kuwa hao wazazi na jamii yote hapo hawajatambua umuhimu wa elimu na jukumu lao la kuwapatia elimu watoto wao.

Inasikitisha kuona wazazi hawashughuliki kabisa kuchangia chochote kuhusu elimu ya watoto wao.

Lakini kwa upande wingine tunaweza kushuhudia jinsi wazazi na wanajamii wanavyojitahidi kuwalea watoto wao kwa hali na mali.

Ninaambiwa kuwa ndugu zetu wa Mkoa wa Kilimanjaro wamefanikiwa kuwa na shule nyingi za msingi na sekondari na hata kuwasomesha vijana wengine kutokana na ile michango ya mauzo ya kahawa. Kila mkulima hata yule asiye na mtoto alichangia elimu katika mkoa wa Kilimanjaro.

Hivi leo kuna wasomi wengi kutoka Mkoa huo wa Kilimanjaro . Na hao wasomi wanatambua wajibu wao wa kuwasaidia wenzao na pia kuujenga Mkoa huo kwa hali na mali.

Mambo kama hayo yanapaswa kutendeka pia katika Mikoa mingine ya hapa nchini.

Kila mwananchi ajisikie kuwa anao wajibu wa kuleta elimu kwa hali na mali kwanza katika mahali pale alipozaliwa na kisha katika taifa.

Nao waliojipatia elimu wanapaswa kutambua wajibu wao wa kuwatumikia hao waliowezesha kujipatia elimu hiyo. Wanapaswa nao kufanya juu chini katika kuwapatia elimu wenzao.

Baada ya kueleimishwa na kupata maarifa hufuata wajibu wa kutoa elimu na maarifa kwa wengine.

Tungeweza kusema kuwa ku elimishana ni kama vile ule mchezo wa kupasiana vijiti. Kila mmoja anacho kijiti (cha elimu) anapaswa kumpasia mwenzake kijiti hicho ili elimu na maarifa vizidi kudumu na kustawi katika jamii yetu.

Hapo tunapenda kuwakumbusha wasomi wote, hata yule aliyefika darasa la I, tu, kwamba kile alichokipata anadaiwa kukitoa kwa wengine kwa faida yakena ya wengine.

Jumuiya ya mahali na serikali kwa ujumla (hata kanisa) vimetusomesha kwa gharama tofauti. Hiyo ni haki tuliyopewa kutoka jamii. Baada ya kutendewa haki hiyo linalofuata ni wajibu wetu kuihudumia hiyo jamii kwa hali na mali.

Tunapofanya kazi ya kuajiriwa au ya kujiajiri tunatumia elimu na maarifa ambayo tumepewa na jamii. Hatuna budi kutoa shukrani kwa jamii kwa kufanya kazi tulizo nazo kwa adilifu, uaminifu na kwa juhudi na maarifa.

Wajibu na haki huenda pamoja.