LIGI YA MUUNGANO

Yanga, Majimaji zaendeleza mchuano mkali kileleni

lZapambana jijini leo

Na Mwandishi Wetu

 WAKATI leo zitakutana kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Yanga na timu ya Songea, Majimaji, ndio zinaoonekana kufukuzana kwa karibu katika kuwania ubingwa wa michuano ya Ligi ya soka ya Muungano mwaka huu, Yanga ni bingwa mtetezi.

Mechi ya leo inazikutanisha timu hizo baada ya mechi yao ya awali iliyofanyika mjini Songea ambayo ilikuwa ya fungua dimba ya michuano hiyo na timu hizo kutoka sare ya 2-2. Timu zote hizo zimeonyesha kwa kiwangio kikubwa ari yao ya kutwaa taji hilo kutokana na jinsi zinavyofukuzana kileleni.

Yanga iliyorudi kwenye michuano hiyo baada ya kumaliza mechi zake za Ligi ya Mabingwa Afrika bila kuambulia lolote la maana, imefufua matumaini ya kutetea tena taji lake baada ya Jumatano kuilaza Polisi ya Zanzibar mabao 2-0 katika mechi ya marudiano.

Lakini wakati Yanga inapata ushindi huo, Majimaji nayo iliyokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, iliilaza KMKM ya Zanzibar kwa mabao 2-1 na hivyo kufikisha pointi 15 na kuendelea kuwa nyuma ya Yanga kwa pointi moja.

Yanga sasa ina pointi 16 baada ya kushinda mechi tano kati ya saba ilizocheza, timu hiyo imetoka sare mara moja na kupoteza mechi moja, hadi sasa Yanga ina mabao 13 ya kufunga huku ikiwa imefungwa mabao matatu tu.

Majimaji yenyewe ina pointi hizo 15 baada ya kucheza mechi saba lakini timu hiyo imeshinda mechi nne kutoka sare tatu, hadi sasa haijapoteza mchezo. Majimaji ina mabao nane ya kufunga na manne ya kufungwa.

Wakati timu hizo mbili zikiendelea kufukuzana kileleni, hali inaonekana kutokuwa nzuri kwa KMKM ambayo hadi sasa inaendelea kuburuza mkia wa ligi hiyo ikiwa na pojnti nne tu ilizopata katika mechi saba.

KMKM imeshinda mechi moja tu na kutoka sare moja ambapo imejikuta ikipoteza michezo mitano. Timu hiyo ndiyo inayoongoza kwa mabao mengi ya kufungwa ambapo hadi sasa imeshafungwa mabao 15 huku yenyewe ikiwa na mabao manne tu ya kufunga.

Prisons, Polisi na Small Simba nazo zinaonekana 'kuzoea' nafasi za katikati za msimamo wa ligi hiyo huku Prisons ikiwa juu yao kwa pointi 9, mabao nane ya kufunga na saba ya kufungwa.

Polisi ndiyo iko katikati yao ikiwa na pointi saba, mabao saba ya kufunga na tisa ya kufungwa, timu hiyo inafuatiwa na Small Simba yenye pointi tano ikiwa na mabao nane ya kufunga na nane ya kufungwa.

 

Fike kutetea taji lake leo

Na Mussa Mahiki

BINGWA, wa kutunisha misuli nchini kwa miaka miwili mfululizo, Fike Wilson, leo atawania tena taji la Mr. Guinnes Tanzania 1998, katika mashindano yatakayofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya New Silent Inn uliopo Mwenge jijini kwa kushirikisha watunisha misuli 20.

Mwenyekiti wa Chama cha Watunisha Misuli na Kunyanyua Vyuma nchini (TWLBA), Edward Mwakasyupa, alisema kuwa washiriki hao ni wale walioshinda mashindano ya kanda mbalimbali yaliyomalizika hivi karibuni.

Alisema kuwa kati ya washiriki hao , watano wanaingia moja kwa moja kwenye mashindano hayo kutokana na kunyakua nafasi tano za kwanza katika mashindano ya mwaka jana ambapo Fike aliweza kulitetea taji lake alilotwaa mwaka 1996.

Mwakasyupa aliwataja walioingia moja kwa moja kutokana na matokeo ya mwaka jana mbali na Fike kuwa ni George Adole, Augustine Joseph, Robi Robinson na Ali Ahmed.

Wengine ambao wataingia kutokana na matokeo ya kanda ni Abasi Mmbaga , Julias Kajole, Deved Mwasonya wote toka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na kutoka Kanda ya Kati ni Khalid Living, Emanuel Ignas na devid Mfum.

Wengine ni Ndeyanla Abeid, Runisha Msanga na Emanuel Kani toka Kanda ya Kaskazini wakati Kanda ya Dar es salaam itawakilishwa na Shomari Nasuma ,Hamis Mpila na Abdallah Mpila. Tonny Simon, Costa Siboki na Mustafa Salumu wataiwakilisha Kanda ya Ziwa.

Mwakasyupa alisema shindi katika kinyang'anyiro hicho atajinyakulia donge la sh. 500,000 pamoja na tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo huo yatakayofanyika Malaysia.

Mshindi wa pili atanyakua sh. 300,000 na watatu atapata sh. 200,000 pamoja na baiskeli wakati washiriki wengine watapata sh. 30,000 ikiwa ninzawadi ya kifuta jasho.

 Mikoa sita kuchuana

Na Said Mmanga, Morogoro

 WACHEZA tennis na gofu wa mikoa sita, mwezi ujao wanatarajia kuchuana katika mashindano ya kila mwaka ya Morogoro Doubles na Coast Opener iliyopangwa kufanyika kwenye viwanja vya Gymkhana vya mkoani hapa.

Kocha mkuu wa Tennis mkoani hapa, Sebastian Mtupili, alisema katikati ya wiki kuwa mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Zanzibar pamoja na wenyeji Morogoro ambapo washindi wa kwanza na wa pili watazawadiwa sh. 200,000. Michezo hiyo itafanyika kwa siku tatu kuanzia Desemba 4.

Wakati huohuo, timu za mpira wa kikapu za maveteran wa mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro leo zitachuana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa katika pambano la kirafiki.

Katibu Mkuu wa chama cha mchezo huo mkoani hapa, Moses Loga, alisema hivi karibuni kuwa awali mchezo huo ulikuwa ufanyike wiki iliyopita lakini ukasogezwa mbele hadi leo kufuatia maombi ya maveteran wa Dar es Salaam.

 

Kina dada wa Sauti ya Umma, Mji Mpya kuwania Mbuzi leo

Na Gaudence Massati, MSJ, Morogoro

 

TIMU za netiboli za Sauti ya Umma na Mji Mpya, leo zitaumana kwenye Uwanja wa Mji Mkuu mjini hapa katika fainali ya kuwania Kombe la Mbuzi lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mji Mkuu.

Sauti ya Umma ilifanikiwa kuingia fainali hiyo baada ya Mapinduzi kwa mabao 31-30 katika nusu fainali wakati Mji Mpya iliitoa Chipukizi kwa taabu baada ya kuicharaza mabao 23-21 katika uliojaa upinzani mkali.

Mashindano hayo yalianza Oktoba 26 kwa kushirikisha timu 12 zilizogawanywa katika makundi mawili ya timu sita kila kundi. Mashindano hayo yameandaliwa kwa lengo la kufufua hadhi ya mchezo huo mkoani hapa ambao kwa muda mrefu ulikuwa umedorora.

Mshindi katika mchezo wa leo atajinyakulia mbuzi wawili wakati timu itakayofungwa itazawadiwa mbuzi mmoja. Zawadi kwa mshindi wa tatu itakuwa sh. 5,000 wakati timu yenye nidhamu itakabidhiwa saa ya ukutani.

 

HARAKATI ZA USAJILI TANZANIA BARA

SAMI kukutana na Reli, Mtibwa

Na Said Mmanga, Morogoro

SIKU tisa kabla ya tarehe ya mwisho ya kumalizika kwa zoezi la usajili kwa ajili ya msimu ujao wa soka, Kamati ya Saidia Morogoro Ishinde (SAMI), inatarajiwa kukutana na timu za Reli na Mtibwa za mjini hapa kupanga mikakati ya usajili wa timu hizo.

Timu hizo zote zinatazamiwa kushiriki michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ya Safari Lager ya mwakani, tarehe ya mwisho ya usajili kwa ajili ya msimu huo ni Novemba 30.

Katibu Mkuu wa SAMI, Edward Hiza, ameieleza kiongozi kuwa mbali na usajili, lengo lingine la kikao hicho ni kupanga mikakati ya kuziwezesha timu hizo kushika moja ya nafasi za juu katika ligi ya mwakani.

Hiza alisema kuwa katika kikao hicho, SAMI na viongozi wa timu hizo watajadili pamoja na mambo mengine taarifa ya makocha na mapendekezo yahusuyo masuala ya uchaguzi.

 

HEBU TUJADILI MICHEZO

CHAMUDATA 'mmechemsha' na MASHIBBOTA yenu

Na Mwandishi Wetu

 

MASHINDANO ya Bendi Bora Tanzania (MASHIBBOTA) yalisubiriwa 'ingawa sio kwa hamu' na sasa yamepita na kuacha mfadhaiko miongoni mwa washiriki na wapenzi wa muziki kwa ujumla wao.

Tunasema mashindano haya yameacha mfadhaiko mkubwa kwa sababu hayakufanyika kama ilivyotarajiwa kuwa yangefanyika katika mtazamo wa karne ijayo japo hata kwa mnuso wake tu.

Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) kinapaswa kubeba lawama zote kwa kuwapotezea muda watanzania na wanamuziki wenyewe kwa kuandaa kichekesho katika wakati huu wa kuelekea karne ya ishirini na moja.

CHAMUDATA imetupotezea muda kwa vile ilifikia hatua hadi ya kuzuia ziara ya mwanamuziki Koffi Olomide toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na pia kushinikiza kuhamishia kwa mashindano ya disko kwenda mkoani Morogoro. Kama huu si ukiritimba wa muziki ni kitu gani?, tunatumaini ukitiritimba huu hautarudiwa.

Moja ya nguzo kuu ya maendeleao ni kujifuna kila wakati ili kila unachokifanya sasa kesho kiwe na ubora zaidi, lakini inaelekea CHAMUDATA hilo hawana kabisa. Walivyofanya miaka kumi iliyopita wanataka kufanya hata kesho.

CHAMUDATA wamechemsha katika kuandaa mashindano pia wamechemsha katika upande wa majaji ambapo walidhani majina makubwa ndio ufumbuzi kumbe hawakujua kuwa wanaingia mkenge mkubwa ambao wengi tu wamekuwa wakiukwaa mkenge huo na siku haijafika bado ya kustukia mkenge huo

Safari nyingine tumieni wataalam waliosomea kazi hiyo, tunao watu wana digrii za hadi falsafa ya muziki, tuna watu wanaofundisha muziki wote hawa ndio wanaofaa kuwa majaji na sio kutuletea majina. Wakati huo umepita hatutaki urudi. Kila la kheri mkinifanikiwa kuandaa tena MASHIBBOTA.