Daraja la tatu Dar kuanza Novemba 21

Na Mussa Mahiki

PATASHIKA na nguo kuchanika ya mashindano ya ligi soka daraja la tatu kanda ya Dar es Salaam inatarajiwa kuanza Novemba 21 wakati timu 15 kutoka mikoa mitatu ya Ilala, Temeke na Kinodnoni zitaonyeshana kazi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki, katibu wa kamati ya kusimamia ligi hiyo Hamisi Ambari alisema kuwa ligi hiyo itafanyika kwenye viwanja sita vya Tandika Mabatini na Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Anthony Mbagala.

Viwanja vingine alivitaja kuwa ni Makurumla (Kinesi), Msasani, Karume na Airwing ambapo ligi hiyo itafanyika katika makundi mawili ambapo kundi 'A' litakuwa na timu nane na kundu jingine litakuwa na timu saba hata hivyo hakutaja timu katika kila kundi.

Alisema ratiba kamili ya mashndano hayo inatarajiwa kutolewa ijumaa ijayo mara baada ya watendaji wa kamati hiyo watkapokutana na viongozi wa timu shiriki katika mkutano wa kujadili kanuni na taratibu zitakazotumika kwenye ligi hiyo.

Katibu huyo alisema kuwa kila timu shiriki inatakiwa kulipa ada ya ushiriki ya shs. 25,000 ambapo tarehe ya mwisho kwa timu hizo kutoa ada hiyo Novemba 18 alizitaja timu zilizopata tiketi ya kushiriki ligi ya kanda kutoka Temeke; Tessema, Transit Camp, Jamaica, Intermilla na Evaret.

Kinondoni Abajalo, Tambaza, New Twiga Cement, Villa Squad na Huduma, Ilala had sasa timu tatu ndizo zilizovuka kigingi hicho, timu hizo msimbazi rovers, Mkunguni, na Vatican na timu zingine mbili zitapatikana mara baada ya kumalizika ligi ndogo iliyoanza mwishoni mwa wiki iliyopita, katika ligi hiyo timu tatu za Msikate tamaa, Black Pool na Ashanti zinashirik, wilaya za Dar es Salaam zimepewa hadhi za mikoa.

Katibu huyo wa kamati ya ligi alisema kuwa timu ambazo zitakuwa zimeshindwa kulipa ada ya ushirika zitakuwa zimejitoa zenyewe katika mashindano hayo ambayo yatatoa timu mbili zitakazocheza ligi hiyo ngazi ya taifa mwakani.

Small Simba kukumbana na kombainia ya Temeke

Na Musaa Mahiki

TIMU ya soka ya Small Simba ya Zanzibar kesho itaumana vikali na timu ya Temeke Kombaini ya jijini katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika kwenye uwanja wa Tandika Mabatini.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi kaimu katibu mkuu wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Temeke (TEFA) Mahd Batash alisema kuwa mchezo huo una lengo la kujenga udugu kati ya timu hiyo ya Zanzibar na wachezaji wanaochezea timu mballi mbali za ligi kuu na madaraja mengine hapa nchini waishio wilayani Temeke.

Aliitaja sababu nyingine ya kuandaa mchezo ho kuwa ni kupanua mfuko wa chama chake ili kiweze kuyaendehsa vizuri mashindano ya ligi daraja la nne ngazi ya wilaya mbayo yanatarajia kuanza mapema mwezi unaofuata.

Small Simba inashiriki ligi kuu ya muungano inatarajia kutoa upinzani mkubwa kwa timu hiyo ya Temeke inayotarajiwa kuundwa na wachezaji Salvatory Edward, Ysufu macho 'Musso', Seif Mtambo, Joseph Mapunda, Joseph Kapinga, Mustafa Hoza, Edward Chumila, Malota Soma, Hussein Bhalo, Prosper Omela, Aman Ali, Omari Kapilima, George Masatu na Rajabu Msoma, Alphonce Modest na Renatus Njohole.

 

HEBU TUJADILI MICHEZO

Simba fanyeni maridhiano mapema uchaguzi ufanyike

Na mwandishi wetu

HABARI za mgogoro katika klabu ya Simba zimesikitisha wapenzi wote wa mchezo huo na wasio wapenzi lakini wanotakia mema michezo nchini.

Tungependa kutanguliza kusema kuwa hatuna nia ya kumlaani aliyepeleka suala hilo mahakamani kwani hiyo ni haki yake ya kikatiba na tunaamini alikuwa na sababu nzuri tu za kufanya hivyo.

Tunasema tumesikitishwa na hali hiyo kwa vile kila mmoja aliamini sasa tatizo katika klabu ya Simba litafikia ukomo kwa kufanyika kwa uchaguzi na wanachama kuchagua viongozi wanaowapenda.

Kuna kitu watu hawakukiangalia kwa makini na ndio maana umetokea utata kama huu uliopo mahakamani sasa. Hili ni fundisho kwa klabu zietu zote kuwa tusipoziba nyufa tutajikua tunalazimika kujenga ukuta.

Juhudi zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika ni njia moja nzuri ya kufikia muafaka lakini kamwe watu wasitake kujipatia umaarufu kwa jambo hili kwani tayari wengine wameumbuka.

Tunadhani suluhu ya jambo hili imo ndani ya wazee wenye heshima na busara ndani ya klabu yenyewe ya Simba na si vinginevyo. tunaamini kuwa busara ikitumika hapana shaka yooyote kuwa Fazal ataridhia kufuta kesi.

Hizi ni pande mbili zinazovutana hata kama upande mmoja ukiwa mdogo namna gani lakini unapaswa kusikilizwa. Tunaamini na kuomba kuwa yawepo maridhiano katika suala hili mapema iwezekanavyo ili uchaguzi ufanyike na amani irejee simba tena.