Korti yavunja uchaguzi Simba

lHatima yake kujulikana Jumatatu

Na Mwandishi wetu

Ndoto za wanachama wa timu ya soka ya Simba kumaliza

mgogoro wa uongozi uliodumu klabuni kwa kipindi kirefu,

zimeyeyuka baada ya Mahakama ya Rufaa nchini

kuusimamisha uchaguzi mkuu wa timu hiyo uliopangwa kufanyika kesho .

Uchaguzi huo ulisimamishwa na Jaji Agusta Bubeshi ambaye amesema ataijadili rufani ya Fazal inayopinga hukumu ya mahakama ya kisutu juu ya shauri la kupinga kuondolewa madarakani na kuwekwa kwa kamati ya muda ya Simba Jumatatu.

Hatua ya Fazal anayetetewa na mawakili kutoka kwa makampuni ya mawakili ya Julius Cahmbers imekuja ikiwa ni siku ya 87 toka mahakama ya Kisutu chini ya hakimu Feroz Sameja kuihalalisha kamati ya Muda kuiongoza timu hiyo.

Mlalamikaji huyo ambaye amebaki pekee katika kesi hiyo kufuatia wenzake Abdalah Manga na Humphrey Laban kujiondoa na kuwania tena uongozi wa Simba.

Viongozi wa Simba chini ya mwenyekiti wake marehemu ismail Kaminambeo na Priva Mtema aliyekuwa Katibu, waliondolewa katika mkutano wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika Januari 13, 1997.

Baadaye timu hiyo ya uongozi ilifungua kesi kupinga hatua hiyo ya wanachama.

Kusimamishwa kwa uchaguzi huo kunaendeleza kampeni za kichinichini ambazo zilijaa kukashifiana na 'vijembe'

Uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Starlight ya mjini Dar es Salaam,..

Kampeni za Simba zilizodumu kwa karibu mwezi mmoja sasa, zilikuwa zikitawaliwa na vijembe toka kwa baadhi ya wagombea, huku wengine wakifanya kampeni zao hadi usiku katika matawi ya klabu hiyo.

Ni uchaguzi ulikuwa ukisubiriwa na wanachama wengi wenye kupenda maendeleo ya kweli ya klabu hiyo hasa kwa kutilia maanani matokeo mabaya kimichezo ambayo Simba imeyapata kwa kipindi cha miaka miwili ya migogoro.

Yanga kutupa karata 'butu'

Na Mwandishi wetu

PAMOJA na kupoteza matumaini ya kuingia fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, Yanga kesho itakuwa na kazi kubwa ya kutetea heshima yake na ya taifa, itakapocheza na Asec Mimosas.

Katika mchezo huo wa marudiano na wa mwisho wa robo fainali ya michuano hiyo utakaofanyika uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Yanga pia itahitaji kulipiza kisasi cha kufungwa mabao 2-1 na Asec ya Ivory Coast.

Yanga ilipata kipigo hicho katika mechi ya kwanza ambayo ilifanyika mjini Abidjan ambacho kilikuwa kama 'kifungua kinywa' tu kwani baada ya mchezo huo Yanga ilianza kumeza mabao katika michuano hiyo yakiwemo 6-0 toka kwa Raja Casablanca ya Morroco.

Kama kweli Yanga inahitaji kulipa kisasi na kulinda heshima yake, mchezo wa kesho ni wa kufa na kupona kwa vile Asec haitataka kupoteza pointi tatu kwa vile inahitaji ushindi ili iweze kujipatia nafasi ya kuingia fainali.

Katika kujipatia pointi hizo, Asec pia itahitaji ushindi wa mabao mengi iwezekanavyo ili yaweze kuwa msaada kwao kwa vile michuano hiyo inachezwa katika mtindo wa ligi na magoli huweza kuwa msaada mubwa.

Asec inachuana na Manning Rangers ya Afrika Kusini katika kubwabania nafasi hiyo ya kuingia fainali, timu itakayopata nafasi hiyo itavaana na mchindi wa kundi a kucheza fainali.

Hata hivyo ushindi kwa Yanga kesho unaweza kuwa ndoto hasa kwa ile matayarisho yake kwa ajili ya mchezo huo yamekuwa yakikatisha tamaa na hayaonyeshi matumaini yeyote.

Tangu irudi toka Afrika Kusini ilikochapwa mabao 4-0, Yanga imeshindwa kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo na badala yake imekuwa ikifanya mazoezi ya kusuasua wachezaji wake wakiwa wametawanyika majumbani.

Kocha wake, Raoul Shungu, pia amekaririwa akidai kupoteza matumaini ya kushinda kesho kwa alichosema kuwepo mgawanyiko wa wachezaji huku wengine wakiunga mkono uongozi wa Kamati ya Muda na wengine wakitaka kurudi kwa uongozi wa Ngozoma Matunda, uliosimamishwa na mahakama.

Kutokana na hali hiyo, mchezo wa kesho kwa kiasi kikubwa unaonyesha kutowatia hamasa wana-Yangu wenyewe na watanzania kwa jumla ambapo wengi hawana tumaini na Yanga.

250 kuchuana Marathoni Zanzibar

Na Mwandishi wetu

JUMLA ya wanariadha 250 wanatazamiwa kushiriki mbio za marathoni zilizopangwa kufanyika kesho mjini Zanzibar kwa kushirikisha nchi sita.

Mratibu wa mbio hizo, John Manyama, alisema hivi karibuni kuwa katika mbio hizo, mshindi wa kwanza atazawadiwa gari dogo toka Japan aina ya Toyota lenye thamani ya sh.. millioni 3.

Kwa mujibu wa Manyama, mshindi wa pili atapata zawadi ya pikipiki aina ya Vespa yenye thamani ya sh. milioni 1.2 mbali na zawadi hizo zitakuwepo zawadi nyingine kadhaa ambazo Manyama hata hivyo hakuzitaja.

Alizitaja nchi hizo kuwa ni Zimbabwe itakayowakilishwa na wanariadha wawili, Kenya itakayokuwa na wanariadha wanne na Afrika Kusini itakayoleta wanariadha watatu.

Nchi zingine ni Ethiopia itakayokuwa na wanariadha watatu, Uganda itakayowakilishwa na mwanariadha mmoja pamoja na wenyeji Tanzania inayotazamia kuwa na wanariadha 237.

Mbio za marathoni za Zanzibar hufanyika kila mwaka kwa kushirikisha nchi mbali mbali.