‘Serikali kuwashughulikia waliofanya mkutano Yanga’

WANACHAMA 223 wa Klabu ya Yanga walioendesha mkutano wa mapinduzi ili kuung’o uongozi wa Mwenyekiti,Ngozoma Matunda na wenzake wanakabiliwa na hatari ya kuangukiwa na mkono wa sheria kwa kuvunja amri ya hivi karibuni ya Serikali ya kutofanya mikutano siku za sikukuu za kitaifa za serikali.

Katika siku za karibuni Serikali ilitangaza kuwa ni marufuku kwa kikundi au taasisi yoyote nchini kutumia siku za mapumziko ya sikukuu za kitaifa kuendesha mikutano yao kwani siku hizo zimetengwa ili wananchi wote washerekee kwa mapumziko.

Habari zilizopatikana jijini mapema toka kwa Mjumbe mmoja wa Klabu ya Yanga ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa klabu hiyo zimesma hatua hiyo inatarajiwa kuchukuliwa na Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambalo ni chombo cha serikali kinachosimamia shughuli za michezo nchini.

Mjumbe huyo alisema wanachama hao chini ya Abbas Tarimba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya muda ya mapinduzi na Makamu wake George Mpondela walivunja agizo hilo kwa kuendesha mkutano siku ya Sikukuu ya Muungano iliyoadhimishwa Aprili 26 mwaka huu.

Alisema kuwa tayari viongozi halali wa Yanga ambao wamedaiwa kung’olewa madarakani wameshatoa taarifa hiyo kwa vyombo vinavyohusika kuhusu ubatili wa kikao hicho.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo Mweka Hazina aliyeondolewa wa klabu hiyo, John Gingi alisema ni kweli mkutano huo siyo tu kwamba ulikiuka katiba ya Yanga, bali pia hata agizo la serikali la kuzuia mikusanyiko katika siku za sikukuu za kiserikali.

Akizungumza ofisini kwake Chuo Kikuu sehemu ya Mlimani jijini katikati ya wiki, Gingi alisema kuwa tayari vyombo vyote vinavyohusika na usimamiaji wa soka mkoani Dar es Salaam vimeshafahamishwa juu ya suala hilo na kinachosubiriwa ni utekelezaji kwa waliohusika.

Alisema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba ambaye ni kiongozi wa serikali pia anajua suala hilo wazi kwamba wanachama waliokutana walikuwa wamekiuka amri ya serikali iliyopiga marufuku mikutano siku ile.

Hata hivyo haikuweza kufahamika wazi ni hatua gani ambayo labda serikali inaweza kuwachukulia wanachama hao ambao walivunja amri hiyo ya kukusanyika katika siku ya sikukuu ya kiserikali na kuendesha mkutano wa klabu yao

CHANETA kuendesha semina ya wakufunzi

lMikoa mitano yathibitisha kushiriki

CHAMA cha mchezo wa Netiboli nchini kinatarajia kufanya semina maalum itakayofanyika Mei 17 jijini.

Katibu Mtendaji wa CHANETA, aliitaja mikoa iliyothibitisha kushiriki katika semina hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Lindi na Mtwara.

Alisema semina hiyo itatoa mada mbalimbali kwa wakufunzi watakaohudhuria yakiwemo mafunzo ya sheria, kanuni, na taratibu mbalimbali za mchezo wa netiboli.

Aliongeza kuwa mikoa ambayo haijathibitisha kushiriki inayo nafasi ya kuwasilisha taarifa zao za uthibitisho ili kushiriki semina hiyo.

Mwaka jana CHANETA iliandaa semina kama hiyo, lakini haikufanyika kutokana na mikoa kutojitokeza kushiriki.