USAJILI WA SIMBA

Fazal aupinga usajili uliowasilishwa FAT na baraza la wazee

lAtaka isajili 22 badala ya 30 ...makipa wawe wawili tu

Na Mwandishi Wetu

 MWEKA Hazina wa klabu ya Simba aliyerudishwa madarakani hivi karibuni na Mahakama Kuu, Fazal Kassam, ameupinga usajili wa klabu hiyo uliowasilishwa FAT na mdhamini wa klabu hiyo, Ramesh Patel, ambapo ametaka kupunguzwa kwa idadi ya wachezaji.

Fazal alisema jana katika mahojiano na Kiongozi kuwa, usajili huo ni mbovu kwa vile haukuangalia utaalam wa soka la sasa lililoingia mfumo mpya wenye ushindani zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma .

"Wao wamesajili makipa wanne, haiwezekani tukawa na makipa wengine kiasi hicho, tunahitaji kupunguza na kuongeza washambuliaji na mabeki," alisema Fazal na kufafanua atawasiliana na FAT-chama cha soka nchini ili aweze kurekebisha usajili huo.

Kwa mujibu wa Fazal, Simba inatakiwa kusajili makipa wawili na kupunguza idadi ya usajili wake kutoka wachezaji 29 iliowasajili sasa na kubakisha 22 tu. Katika usajili huo uliowasilishwa FAT, makipa hao wanne waliosajiliwa ni Miraji Juma, Spear Mbwembwe, Bahatisha Ndulute na Mohamed Mwameja.

Ingawa hakutaka kueleza wazi anataka kuchuja makipa gani, alisema katika mipango hiyo tayari ameshakamilisha mipango ya kumsajili pia kipa mwingine wa zamani wa timu hiyo, Stephen Nemes, kama alivyofanya kwa Mohamed Mwameja ambaye amesajiliwa tena na Simba.

Usajili wa Simba uliowasilishwa FAT uliendeshwa na Baraza la Wazee wa klabu hiyo liliongozwa na Abubakar Mwilima. Hata hivyo baraza hilo kwa kipindi kirefu limekuwa katika mikwaruzano na Fazal juu ya usajili ambapo alishawahi kusema kuwa baraza hilo linamgeuka kila mara wanapokutana na kuzungumza.

Katika kurekebisha usajili huo alisema anatazamia pia kumrudisha beki wa zamani wa Simba, Deo Mkuki, ili kuziba pengo la Alphonce Modest aliyekwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika timu ya Mamelodi Sundowns ya huko.

Mbali na Deo Mkuki, Fazal alisema pia amezungumza na wachezaji wengine wa zamani, George Lucas na William Fahbulleh, ili waweze kusajiliwa tena. Hata hivyo alisema wachezaji hao wamemuonyesha wasiwasi kwa vile wamesajiliwa na timu ya Tanzania Stars kwa ajili ya michezo ya Kombe la Washindi barani Afrika.

Kutokana na suala hilo alisema atawasiliana na uongozi wa Tanzania Stars ili uweze kuwaruhusu wachezaji hao kusajiliwa na Simba kwa ajili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ya Safari Lager. "Ni kwa sababu Tanzania Stars haichezi ligi ya bara".

Fazal alirudishwa madarakani baada ya kushinda rufaa aliyokata kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu ya jijini iliyohalalisha maamuzi ya wanachama katika mkutano wao uliofanyika mapema mwaka 1997 uliouondoa madarakani uongozi wa marehemu Ismail Kaminambeho unaomjumuisha pia Fazal.

Kufuatia kuondolewa kwa uongozi huo, wanachama hao waliteua kamati ya muda iliyokuwa inaongozwa na Salehe Ghullum. Kamati hiyo ilivunjwa siku chache kabla ya Mahakama Kuu kumrudisha madarakani Fazal hali iliyosababisha baraza la wazee kushika hatamu ya uongozi wa klabu hiyo.

Baada ya kushinda rufaa hiyo, Fazal na msaidizi wake, Humphrey Laban, ndiyo waliorudishwa madarakani kufuatia viongozi wengine waliokuwa katika uongozi huo uliochaguliwa Desemba 1995 kujiuzulu na wengine kufariki.

 

...Mahakama yakubali ombi lake, uchaguzi mdogo sasa kesho

Na Mwandishi Wetu

 UCHAGUZI mdogo wa kujaza nafasi zilizo wazi katika uongozi wa klabu ya Simba uliokuwa ufanyike leo, sasa umesogezwa mbele kwa siku moja hadi kesho.

Jaji wa Mahakama Kuu, Josephat Mackanja, jana alikubali ombi la Mweka Hazina wa klabu hiyo, Fazal Kassam, kutaka kusogezwa mbele kwa uchaguzi huo ili kutoa nafasi kwa wanachama wengi wa klabu hiyo kuweza kushiriki zoezi la upigaji kura.

"Wakili wangu aliwasilisha ombi hilo mapema leo (jana) na mahakama imetukubalia...hivyo usajili ni Jumapili na utafanyika kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo ya Utamaduni la Msimabazi," alisema Fazal alipozungumza na Kiongozi.

Katika kuomba hivyo, Fazal alisema kwa vile jana wagombea walikuwa wanafanyiwa mahojiano na Baraza la Michezo Wilaya ya Ilala (BMWI), isingekuwa vizuri uchaguzi ufanyike leo kutoa nafasi kwa wagombea pamoja na kutoa nafasi kwa wanachama wengi kushiriki kwa vile siku za Jumamosi wengi hukabiliwa na shughuli za kikazi.

Uchaguzi huo unafuatia hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa na jaji huyo Desemba 24 mwaka jana katika rufaa iliyowasilishwa na Fazal kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu ambayo ilihalalisha uamuzi wa kuwaondoa madarakani viongozi waliochaguliwa Desemba 1995.

Uongozi huo unaomjumuisha na Fazal, ulikuwa chini ya uenyekitim wa marehemu, Ismail Kaminambeho, na uliondolewa katika mkutano wa wanachama uliofanyika kwenye ukumbi wa Starlight jijini Januari 3, 1997 ulioitishwa na Waziri wa Elimu na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya, kufuatia mgogoro uliozuka ndani ya klabu hiyo.

Katika maamuzi yake, mahakama hiyo ilisema mkutano huo haukuwa halali kwa mujibu wa katiba ya Simba kwa vile kikataiba mwenye mamlaka ya kuitisha mikutano ya Simba ni Mwenyekiti tu na kwamba katiba hiyo pia haisemi kama waziri wa michezo anaweza kuingilia mamlaka ya Mwenyekiti.

Hivyo mahakama hiyo ilimrudisha Fazal na msaidizi wake, Humphrey Laban, kwenye madaraka na kuamuru kufanyika uchaguzi huo mdogo ili kujaza nafasi zilizo wazi baada ya viongozi wengine mbali na marehemu Kaminambeho kufariki na baadhi kujiuzulu.

Mwingine aliyefariki ni aliyekuwa Katibu Mkuu, Priva Mtema. Waliojiuzulu ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Hamis Kilomoni, Katibu Mkuu Msaidizi, Abdalah Manga na aliyekuwa Katibu Mwenezi, Idd Mchatta.

Mahakama hiyo iliamuru uchaguzi huo ufanyika kabla ya Januari 30 (leo) lakini maandalizi yalichelewa kuanza kutokana na baadhi ya wanachama kuiomba mahakama hiyo kupitia upya hukumu yake na kutoa ufafanuzi kwa kile walichodai kuwa muda wa kufanya uchaguzi mkuu kwa mujibu wa katiba ya Simba tayari umeshafika.

Wanachama hao walitaka kufanya uchaguzi mkuu badala ya uchaguzi mdogo. Hata hivyo mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo kwa kusema hayakuwasilishwa kwa kufuata sheria zinahusika zinavyoelekeza.

Mwaluvanda kutorudishwa tena Yanga

Na Mwandishi Wetu

 ALIYEKUWA kocha wa Yanga, Tito Mwaluvanda, ambaye alitimuliwa na uongozi wa Kamati ya Muda ya klabu hiyo, hatarudishwa tena kuinoa timu hiyo baada ya uongozi wa kuchaguliwa kurudishwa madarakani kama ilivyokuwa ikitazamiwa.

Kaimu Katimu Mkuu wa Yanga, Gaspar Namfua, alisema katikati ya wiki kuwa, uamuzi wa kutomrudisha Mwaluvanda, unatokana na kiango cha kuridhisha kilichoonyeshwa na kocha wa timu hiyo wa sasa, Raoul Shungu anayesaidiana na aliyekuwa msaidizi wa Mwaluvanda, Felix Minziro.

Mwaluvanda alitimuliwa siku chache baada ya uongozi wa Namfua unaoongozwa naMwenyekiti, Ngozoma Matunda, kusimamishwa na mahakama ya Kisutu kutokana na kesi ya uongozi wa klabu hiyo inayoendelea kufunguliwa.

Baada ya kutimuliwa, Yanga ilianza kufanya vibaya kwenye michuano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kupata vipigo mfululizo kikiwemo kile cha mabao 6-0 toka kwa Raja Casablancaya Morocco na kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Kufuatia vipigo hivyo, Matunda, aliwahi kukaririwa akisema kama uongozi wake utarudishwa madarakani basi pia utamrudisha Mwaluvanda ili kunusuru timu hiyo.

"Ilikuwa asaidiane na Shungu kwani ni sisi ndiyo tuliofanya mipango ya awali ya kumleta Shungu, lakini sasa hatuoni haja ya kumrudisha tena," alisema Namfua. Shungu ni kocha mwenye sifa nyingi katika ukanda wa Afrika Mashariki ambayeni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aidha Namfua alisema kwa sasa uongozi wake unaandaa mikakati ya kuiwezesha Yanga kushiriki vizuri michuano ya Kombe la CAF inayotarajia kuanza mwezi Machi ambapo uongozi huo umemtaka Shungu kuwasilisha kwao programu ya mazoezi ili kuona nini kinahitajika kufanyika kufanikisha programu hiyo.

Shugu alijiunga na Yanga katikati mwaka jana na ndiye aliyeiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati katika michuano iliyomalizika hivi karibuni mjini Kampala, Uganda baada ya Yanga kuwalaza wenyeji mabao 5-3 katika fainali iliyomalizika kwa kupigiana penati.

Mwishoni mwa mwaka juzi Shungu aliiwezesha Rayon Sport ya Rwanda kutwaa ubingwa huo wakati mashindano hayo yalipofanyika kwenye uwanja wa Aman wa mjini Zanzibar ambapo katika mechi ya nusu fainali ya wakati huo, Rayon iliichapa Yanga mabao 3-0. Kwa wakati huo Yanga ilikuwa chini ya kocha, Sunday Kayuni ambaye alijiuzulu kutokana na kipigo hicho kwa maelezo ya kuchoshwa na ubabaishaji wa viongozi wa Yanga.

Wakati huohuo, Namfua ameutaka uongozi huo wa kamati ya muda kukabidhi mara moja kombe la ubingwa huo wa Afrika Mashariki nas Kati ili mipango ya kulitembeza katika mikoa ya Tanzania Bara na visiwani Zanzibar iweze kufanyika mapema.

Mkongwe Mustapha Hadji ndiye kinara wa Afrika

Na Mwandishi Wetu

MSHAMBULIAJI mkongwe wa timu ya taifa ya Morocco, Mustapha Hadji, ametangazwa kuwa ndiye mchezaji bora wa bara la Afrika kwa mwaka jana, taarifa ya Shirikisho la Sola la Afrika (CAF) imesema hivi karibuni.

Hadji mwenye umri wa miaka 27, ndiye aliyefunga bao la kihistoria katika fainali za mwaka jana za michuano ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Burkina Faso.

Bao hilo alilofunga wakati timu yake ikicheza na mabingwa wa michuano hiyo, Pharaos, ya Misri, ndilo lililoifanya timu yake ya Morocco, Atlas Lions, kuwa timu pekee iliyowalaza mabingwa hao katika fainali hizo.

Hadji ametwaa hadhi hiyo ya uchezaji bora wa Afrika mbele ya wachezaji wengine waliotamba katika fainali hizo akiwemo chipukizi wa Afrika Kusini, Benni McCarthy.

Ifuatayo ndiyo orodha kamili ya wachezaji 10 bora wa Afrika kwa mwaka jana.

1. Mustapha Hadji (Morocco).

2. Austin Okocha (Nigeria).

3. Sunday Oliseh (Nigeria).

4. Hossam Hassan (Misri).

5. Benni McCarthy (Afrika Kusini).

6. Tchiressoa Guel (Ivory Coast).

7. Charles Akunoor (Ghana).

8. Marc Vivien Foe (Cameroon).

9. Finidi George (Nigeria).

10. Rigobert Song (Cameroon).