HEBU TUJADILI MICHEZO

Kapuya umejifunza nini katika kashfa ya IOC?

Na Mwandishi Wetu

ULIMWENGU wa michezo duniani kote umetikiswa na habari za rushwa ndani ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) ambapo tayari mjumbe mmoja amejiuzulu akisi-ngiza sababu tofauti za kujiuzulu kwake, bado tunaamini ni kutokana na kashfa hiyo.

Tunaambiwa kuwa kumekuwepo na utoaji na upokeaji rushwa mkubwa sana baina ya wapiga kura katika kamati hiyo na pia kamati ya michezo ya Jumuiya ya Madola.

Kashfa hii ambayo ingali inaendelea kwa maafisa kadhaa kutakiwa kujieleza kufuatia kuibuliwa na kiongozi mmoja wa IOC kuwa mji wa Salt Lake huko Marekani (na miji mingine huko nyuma) umepewa nafasi ya kuandaa michuano ya olimpiki ya majira ya baridi baada ya kutoa rushwa kubwa kwa wajumbe wa kamati hiyo. Huo ndio ukweli wa mambo kwenye ngazi ya juu kabisa ya michezo dunaini je katika ngazi za kitaifa, hilo jambo likoje?

Hapa Tanzania bado tunakumbuka jinsi uchaguzi mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) uliofanyika wa Zanzibar mwaka 1996, ulivyoleta utata mkubwa wa matumizi ya bajeti na pia utoaji rushwa wa wazi kabisa wa wagombea hasa wale waliotaka kutetea nafasi zao.

Tukasikia Waziri wa Elimu na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya, ameliingilia kati na tuseme alitilia maanani jambo hilo, lakini kama kawaida ya mambo ya Tanzania limekufa kwa kutolewa kwa taarifa nyepesi na watu wakaendelea kula nchini.

Bila kupoteza muda, tunamuuliza mheshimiwa Kapuya kwa manufaa ya kina Tomaso; `Unaweza kutuwekea bayana kilichopelekea mambo kwenda yalivyo kuhusiana na tuhuma hizo za Zanzibar baada ya kusikia kashfa za IOC?'

Hivi karibuni katika kusisitiza kwake umakini wake katika kupiga vita rushwa, Rais Mkapa alisema na kwa hakika ametimiza - kuwa-chukulia hatua wale watakao-dhihirika kuhusika na rushwa lakini hawana ushahidi wa kuwapeleka mahakamani.

Au Kapuya msemo huo haukuhusu wewe? nani asiyejua kuwa TOC kuna uvundo? lakini kila uchaguzi watapita hao hao, mpaka lini hali hii? Je hata hisia za uhakika hazipo mezani kwa Kapuya au ndio.......

 

Uchaguzi mkuu Simba waendelea kuwa 'ndoto ya alinacha'

lMahakama yatupilia mbali ombi la kupitia upya hukumu yake

Na Mwandishi Wetu

 WAZO la wanachama wa klabu ya Simba kutaka kufanya uchaguzi mkuu, jana lilikumbwa na wingu jeusi baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi la kutaka kupitiwa upya hukumu ya mahakama hiyo ya Desemba 24 mwaka jana, iliyom-rudisha madarakani Mweka Hazania, Fazal Kassam, ambaye wao hawamtaki.

Katika maombi hayo, wanachama hao kupitia ofisi ya wakili, Moses Magesa, walitaka kujua kama upo uwezekano wa wao kufanya uchaguzi huo badala ya uchaguzi mdogo kama ilivyoamriwa katika hukumu hiyo kwa maelezo kwamba licha ya Fazal kushinda kesi yake, muda wake wa uongozi kwa mujibu wa katiba ya klabu yao umeshamalizika.

Jaji wa mahakama hiyo, Josephat Mackanja, alitupilia mbali ombi hilo la kutaka ufafanuzi kwa maelezo kuwa waomba ufafanuzi hawakufuata maelekezo ya kanuni namba 39 (1) ya uombaji wa uffanuzi wa kisheria juu ya hukumu zitolewazo na mahakama.

Jaji Mackanja alisema kwa mujibu wa kanuni hiyo, waomba ufafanuzi wanatakiwa kufuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuwasilisha mahakamani nakala ya hukumu wanayotaka ipitiwe na nakala ya kikaza hukumu ambayo hutolewa baada ya hukumu kutolewa.

"Waomba ufafanuzi wameleta nakala ya hukumu tu, wanadai nakala ya kikaza hukumu hawajaipata na kwa kuwa shauri bado liko kwa Jaji yule yule aliyetoa hukumu wamedhani kwamba si makosa kuwasilisha nakala ya hukumu tu...mahakama yangu haikubaliani na hilo," alisema Jaji Mackanja ambaye ndiye aliyetoa hukumu hiyo.

Jaji alisema katika hoja zao, wataka ufafanuzi walisema hawajawasilisha nakala hiyo ya kikaza hukumu kwa maelezo bado hawajaipata.

Kwa uamuzi huo, mahakama imewataka waomba ufafanuzi ambao ni Salehe Ghullum na wenzake (waliokuwa Kamati ya Muda ) kulipa gharama za shauri hilo.

Desemba 24, mwaka jana Jaji huyo alitengua hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu ambayo ilikubaliana na uamuzi wa mkutano wa wanachama wa Januari 13, 1997 ambao uliwaondoa madarakani viongozi waliochaguliwa Desemba 1995 (akiwemo Fazal), uongozi huo ulikuwa chini ya marehemu, Ismail Kaminambeho.

Katika kutengua uamuzi huo, Jaji Mackanja aliyekuwa akisikiliza rufaa iliyowasilishwa mahakama kuu na Fazal kupinga kuenguliwa madarakani, Mackanja, alisema mkutano huo ulikuwa si halali. Kutokana na vifo na kujiuzulu kwa viongozi wengine waliokuwa kwenye uongozi huo, mahakama hiyo ilimrudisha madarakani Fazal na kuagiza kufanyika uchaguzi mdogo kujaza nafasi zilizo wazi kabla ya Januari 30 mwaka huu.

Wakili wa waomba ufafanuzi aliyemuwasilisha Magesa jana, Mwita Wisaka, alisema nje ya mahakama kuwa atawasiliana na wateja wao kujua kama watataka kuchukua hatua nyingine baada ya maombi yao ya kuomba kupitiwa upya hukumu kutupwa na mahakama hiyo jana.

Hatua hiyo sasa inaonekana kuvuruga kabisa zoezi la usajili ambalo liliendeshwa na Baraza la Wazee wa klabu hiyo usajili ambao tayari Fazal ameshasema yeye kama kiongozi anayetambuliwa na mahakama hautambui usajili huo.

Fazal tayari ameshasema atatangaza usajili wake hivi karibuni ingawa muda wa kuwasalisha usajili kwa Chama cha Soka nchini (FAT) umeshamalizika tangu Januari

 

....watani zao nao wadai kucheleweshewa kesi

Na Dalphina Rubyema

WAKILI wa walalamikiwa katika kesi ya kutaka kuondolewa madarakani viongozi wa Yanga, Mkongwe & Company, amemwandikia barua Msajili wa Mahakama kupinga uendeshaji wa kesi hiyo iliyo chini ya hakimu, Stella Majanjala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Barua hiyo yenye kumbukumbu namba FE/CV.219/98/YASC/1 ya Januari 15 mwaka huu, inafuatia agizo la msajili wa Mahakama nchini lilomtaka wakili huyo kutoa maoni yake kufuatia malalamiko ya viongozi wanne waliosimamishwa na mahakama hiyo kudai kuwa kesi hiyo inacheleweshwa kwa makusudi na hakimu huyo kwa sababu zake binafsi.

Barua hiyo ya Wakili Mkongwe imeeleza kuwa yeye na wateja wake wana haki ya kuwa na wasiwasi na mwenendo mzima wa kesi hiyo, kutokana na ucheleweshwaji wa makusudi kwa kuzingatia maelezo ya upande mwingine bila kuzingatia kuwa kesi hiyo ina pande mbili.

Pamoja na mambo mengine wakili huyo alisema katika barua hiyo kuwa Majanjala alitoa siku za kusikilizwa kesi hiyo kuwa Desemba 31 mwaka jana siku ambayo alifahamu fika kuwa hatakuwepo kazini.

"Siku hiyo tulipofika tuliambiwa yupo likizo" ilisema sehemu ya barua hiyo na kuongeza kuwa waliambiwa hivyo na karani wake ambaye aliwafahamisha kuwa kesi yao ilipangwa kusikilizwa Januari 26 mwaka huu.

Katika baru hiyo, wakili huyo ameendelea kusema kuwa hali hiyo imemfanya hata yeye kuwa na wasiwasi kuwa kuna ucheleweshwaji wa makusudi hata ukizingatia kuwa hakimu huyo aliwahi kuandika hati ya kusimamisha uongozi baada ya kusikiliza malalamiko ya upande mmoja katika siku hiyo hiyo aliyoletewa malalamiko.

"Msajili wa mahakama hiyo hakuweza kupatikana ofisini kwake kuelezea kuhusiana na barua hiyo lakini karani wake alikiri kupokelewa barua ya namna hiyo.

Wanachama watano wa timu hiyo wakiongozwa na Ali Kibaun walifungua kesi namba 219/98 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakitakata viongozi waliopo madarakani waondolewe kwa kushindwa kuongoza timu hiyo. Uongozi uliosimamishwa ni ule wa Mwenyekiti, Ngozoma Matunda.

 

Warembo Miss Tanzania 'wang'ara' Tanga kwa mitindo ya mavazi

Na Mwandishi Wetu, Tanga

 MREMBO wa Tanzania, Basila Mwanukuzi, pamoja na warembo wengine saba walioshiriki mashindano ya Miss Tanzania mwaka jana, siku ya Idd Mosi 'waliuteka' mji wa Tanga wakati walipofanya onyesho maalum la mitindo ya mavazi.

Katika onyesho hilo lililofanyika kenye ukumbi wa bwawa la kuogelea la hoteli ya Mkonge iliyopo mjini hapa, warembo hao walionyesha mitindo kadhaa ikiwemo ile ya mavazi ya nguo za kutokea jioni, nguo za kuvaa ofisini, nguo za ufukweni pamoja na mitindo mingine.

Onyesho hilo lilifanyika kwa masaa matatu kuanzia saa 4:00 usiku, lilihudhuriwa na wapenzi wengi wa mitindo yamavazi wa mjini hapa na liliandaliwa maalumkwa ajili ya kuonyesha vipaji vya warembo wa kitanzania ambao kwa mujibu wa waandaaji wake Kamati ya Maandalizi ya Miss Tanzania, warembo wa hapa nchini bado vipaji vyao havijapewa nafasi ya kutangazwa.

Warembo wengine walioshiriki onyesho hilo ni pamoja na Tally Kassim, Dyana Muhere, Zaina Daudi, Salama Muhidin, Rehema Mtawe, Susan John na Kisa Geodfrey. Mavazi yaliyotumiwa na warembo hao yamebuniwa na kampuni ya mavazi ya Tausi Fashions ya jijini.

Akizungumza kabla ya kuanza onyesho lenyewe, mratibu wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, alisema wakati sasa umefika kwa makampuni ya hapa nyumbani kujitokeza kutumia warembo wa kitanzania katika matangazo yao ya biashara badala ya kutumia warembo wa nje ya nchi.

Alisema njia hiyo itasaidia kutoa ajira kwa wasichana wanaoshiriki fani hiyo na hivyo kuikuza hali itakayoweza kufikia kiwango cha juu kama kilichofikiwa na baadhi ya nchi zilizopiga hatua katika fani hiyo ya urembo duniani.

 

'Ruhusuni watoto kushiriki Urembo'

Na Saidi Mmanga - Morogoro

 MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, John Gille, amewataka wazazi wilayani kwake, kuwaruhusu watoto wao wa kike kushiriki mashindano ya urembo.

Akifungua mashindano ya kumtafuta mrembo wa hoteli ya Oasis, Miss Oasis Hotel 1999, yaliyofanyika mjini hapa hivi karibuni, alisema mashindano hayo ni sawa na sanaa zingine zinazohitaji vijana chipukizi ili kuziendeleza kwa faida ya taifa. Katika mashindano hayoi, Leila Rajabu, aliibuka mshindi.

Gille alisema kwa vile mashindano ya urembo yanafanyika ulimwenguni kote na Tanzania hushiriki mashindano ya kumtafuta mrembo wa Dunia, hivyo wazazi wa kitanzania hawana budi kuondokana na kasumba kwamba mashindano hayo ni uhuni.

Mashindano ya kumtafuta mrembo wa hoteli hiyo yalifanyika siku ya sikukuu ya Idd el Fitr ambapo jumla ya wasichana 13 walishiriki.

Wakati huohuo, baadhi ya washiriki wa mashindano hayo, wamemlalamikia muandaaji wa mashindano hayo, Augustine Nduda, wa Salama Promotions kwa madai ya kuwatapeli.

Washiriki hao kuanzia mshindi wa nne hadi wa mwisho wamelalamikia kitendo cha muandaaji huyo kushindwa kuwapa kifuta jasho cha shilingi 20,000 kila mmoja kama alivyoahidi awali.

Walisema badala ya kupewa kitita hicho, muandaaji huyo aliwapa sh. 5,000 tu kila mmoja. Washiriki wa mashindano hayo walichuana katika mavazi ya asili, khanga na vazi la jioni.