Matumla kutwaa ubingwa leo?

Na Mwandishi Wetu

 KWA mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, leo bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Rashid 'Snake Boy' Matumla, atawania ubi ngwa wa dunia uzito wa Light Middle wa Chama cha Ngumi cha Dunia (WBU), kwa kuvaana na Andras Galfi wa Hungary.

Katika pambano hilo linalotazamiwa kuiingiza Tanzania katika moja ya rekodi za juu za mchezo huo duniani, mabondia hao watachapana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee uliopo jijini, pambano hilo linatazamiwa kuwa la raundi 12 kama hakuna bondia mmojawapo kati yao atakayeshindwa kumudu makonde ya mwenzake katika raundi za kati.

Tayari mabondia hao kila mmoja amshatamba kumpiga mwenzake na kuibuka mshindi wa mkanda huo ambao kwa sasa uko wazi baada ya bondia aliyekuwa akiushikilia, Vernon Philiphs, wa Marekani kuvuliwa ubingwa huo kufuatia kushindwa kwake kuja nchini kuutetea kama alivyotakiwa na WBU inayomiliki mkanda huo.

Ni mara ya kwanza katika hatua ya ubingwa wa dunia kwa vile Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikipiga kwata kwenye ngumi za ridhaa ingawa baadhi ya mabondia wake kwa kiwango fulani wamefanikiwa kuchukua ubingiwa wa Afrika au Kanda za Afrika katika michezo mbalimbali.

Ushindi kwa Matumla leo kwa maana nyingine utakuwa umesafisha zaidi njia kwa mabondia wengine wa ngumi za kulipwa wa nchini ambao wameshapata ari ya kuendeleza bidii zao kwenye mchezo huo hasa baada ya kuona mafanikio aliyoyapata Matumla tangu ajiunge na ngumi hizo takribani miaka mitano iliyopita.

"Naomba Watanzania wajitokeze kwa wingi siku ya mchezo...nimepata mazoezi ya kutosha toka kwa kocha wangu na ninamatumaini makubwa ya kufanya kama nilivyofanya katika michezo ya nyuma,"hivi ndivyo Matumla alivyowaambia waandishi wa habari wakati wa mkutano wa mabondia hao uliofanyika katikati ya wiki kwenye hoteli ya Embassy ya jijini.

Haikuwa kazi rahisi kwa Matumla kufikia hatua ya leo kuwania mkanda wa dunia, bondia huyo kipenzi cha watanzania hivi sasa katika ngumi hizo za kulipwa, tayari ameshawashinda mabondia wengine wanne na kufanikiwa kupata tiketi hiyo ya kucheza na Philips ambaye hata hivyo baadaye 'alichomoa' na sasa ndio leo anapambana na Galfi.

Katika mchezo wa kwanza Matumla alimshinda, David Potsane, wa Afrika Kusini kwa pointi kabla ya Matumla kumpiga kwa Knock Out, Patrice Mbehbenli wa Cameroun katika raundi ya tano, mapambano hayo yalifanyika kwenye ukumbi PTA mjini Dar es Salaam.

Matumla pia aliwashinda kwa Knock Out mabondia Laurent Szabo wa Hungary na Orphan Ojvazoski wa Ujerumani ambao wote kwa pamoja walishindwa kabisa kuhimili masumbwi ya Matumla hali inayoleta matumaini kuwa katika pambano la leo, huenda kweli Matumla akaendeleza rekodi yake ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia.

Kikubwa kinachoweza kumpatia Matumla leo ni kutokana na ukweli kwamba anacheza 'kwenye uwanja wa nyumbani', hivyo anatazamiwa kupata msaada mkubwa wa ushangiliaji na uhamasishaji toka wa wapenzi wake mambo yatakayompa moyo wa kuongeza bidii kwa muda wote atakapokuwa juu ya ulingo kumdhibiti Mhungary huyo.

Hata hivyo Matumla asipokuwa makini leo, anaweza kujikuta anaukosa ubingwa huo mbele ya wapenzi wake kwa vile Galfi ameshasema tangu alipowasili nchini mwanzoni mwa wiki kuwa kilichomtoa kwao si kitu kingine zaidi ya kufuata mkanda huo wa dunia.

Rekodi za mabondia hao, zinaonyesha Galfi ndiye mwenye uzoefu zaidi katika masumbwi hayo ya kulipwa kwa vile yeye tayari hadi sasa ameshacheza mapambano 33 ambapo kati ya hayo tayari ameshashimda mapambano 29 ambapo 21 kati ya hayo ni ya Knock Out, ameshindwa mapambano manne na hajawahi kutoka sare.

Matumla yeye kwa upande wake ameshacheza mapambano 22 na kushinda 20, kati ya hayo aliyoshinda 16 ni ushindi wa Knock Out, amepoteza pambano moja na ametoka sare pambano moja pia.

Kocha wa Galfi, Zoltan Fuzey, naye kwa upande wake ameshasema kuwa ana matumaini makubwa kuwa bondia wake ataibuka mshindi leo kutokana na alichosema kufahamu mbinu zinazompatia ushindi Matumla kila anapopanda jukwaani.

Leo pia mdogo wake Matumla, Mbwana, atawania mkanda wa kimataifa wa Bantam wa chama hicho atakapokwaana na Mhungary mwingine, Tamas Szakallas.

Aidha Chaurembo Palasa atazipiga na Shabani Mohamed katika pambano la uzito wa Light. Nao Rashid Ally na Rogers Mtagwa watapambana katika uzito wa Bantam wa taifa ambapo Mtagwa atakuwa akitetea ubingwa wa mkanda huo wa taifa.

Adinani akana kujisajili na CDA

Na Said Mmanga, Morogoro

 MLINDA mlango msaidizi wa timu ya taifa ya soka ya vijana, Vijana Stars, Adinani Mohamed, amekanusha taarifa zilizotolewa na viongozi wa CDA ya Dodoma kuwa amejisajili na timu hiyo kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.

Adinani aliiambia Kiongozi katikati ya wiki kuwa anachofahamu yeye kuhusu usajili wake ni kukubali kwake kusaini fomu za Reli ya hapa Morogoro ambayo nayo mwakani itashiriki michuano hiyo baada ya kupanda daraja toka Daraja la Kwanza mwaka huu.

Hata hivyo ushiriki wa Reli kenye ligi hiyo kuu ya bara mwakani, bado uko katika hatihati kwa vile Baraza la Michezo la Taifa (BMT) bado halijatoa uamuzi wake kuhusiana na rufaa iliyokatwa na timu ya Kariakoo ya Lindi kupinga kupandishwa daraja timu za Reli na AFC ya Arusha.

"Nimesaini fomu za Reli hivyo mimi ni mchezaji wa Reli sio CDA...viongozi wa CDA waliwahi kunifuata juu ya suala hilo lakini niliwakatalia," alisema Adinani.

Alisema si jambo la busara kwa CDA kutangaza kumsajili hali katika mazungumzo yao yeye alishaikatalia timu hiyo, "Nadhani wanataka kuniharibia mipango yangu tu".

TRC yatilia ngumu fedha za usajili Reli

Na Mwandishi Wetu

USAJILI wa timu ya soka ya Reli ya Morogoro kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu ya Bara msimu ujao, umesimama kutokana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), linalomiliki timu hiyo kukataa kutoa fedha za kuendeshea zoezi hilo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA), Salum Mwintanga, aliiambia Kiongozi wiki hii kuwa TRC imesitisha utoaji wa fedha za usajili hadi hapo hatma ya rufaa ya timu ya Kariakoo ya Lindi inayopinga kupandishwa daraja kwa timu za AFC Arusha na Reli, itakapofahamika.

Kariakoo ya Lindi iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la kwanza pamoja na Reli mwaka huu, inapinga uamuzi wa Chama cha Soka Nchini (FAT) kuzipandisha daraja timu hizo. Baraza la Michezo la Taifa (BMT) bado limekaa kimya kuhusiana na rufani hiyo iliyowasilishwa kwake zaidi ya miezi miwili sasa.

Mwintanga alisema mapendekezo ya wachezaji gani watasajiliwa na mazungumzo na wachezaji wenyewe tayari yameshafanyika na wengi wao wameshajaza fomu lakini kinachokwamisha sasa ni fedha za kuwapa ili waanze rasmi mazoezi kwa ajili ya ligi hiyo.

Aidha alisema MRFA imesitisha jihudi ilizokuwa ikizifanya za kutaka kuihamisha timu ya Mtibwa kutoka Turiani inakotumia uwanja wa Manungu na kwenda Morogoro mjini ili itumie uwanja wa Jamhuri pamoja na Reli. "Tumeiagiza Mtibwa ianze mazoezi mara moja kwa vile yenyewe haina tatizo kama la wenzao wa Reli...nia yetu mwakani ubingwa lazima uje Morogoro," alisema Mwintanga.

Miezi michache iliyopita MRFA ilikuwa ikijaribu kuishawishi FAT kukubali kuhamisha nusu ya mechi za Mtibwa kutoka uwanja wa Manungu na kupeleka uwanja wa Jamhuri ili kutoa nafasi kwa wapenzi wa timu hiyo walioko Morogoro mjini kuweza kuiona kwa ukaribu timu hiyo ikicheza.

Wazo hilo lilionekana kupokewa kwa furaha na baadhi ya timu zinazoshiriki ligi hiyo hasa kwa vile katika ligi ya mwaka huu, timu nyingi zililalamikia uwanja huo kutokana na umbali wake toka Morogoro mjini na hali mbaya ya barabara hasa nyakati za mvua.

Pia timu hizo zililalamikia chokaa inayotumika kwenye uwanja huo kuwa ina kemikali zinazodhuru ngozi ya wachezaji, hasa baada ya wachezaji Mathias Mulumba wa Simba na Edibily Lunyamila wa Yanga kupata madhara kwenye miili yao baada ya kuunguzwa na chokaa hiyo ambayo inadaiwa huwa inatumika kuulia wadudu kwenye mashamba ya miwa ya Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa.

HEBUTUJADILI MICHEZO

FAT timizeni ahadi zenu

Na Mwandishi Wetu

 Tunaanza sasa kushuhdia timu kutangaza wachezaji waliowasajili kwa ajili ya mashidano ya nyumbani na kwa baadhi ya timu kwa ajili ya mashindani mbalimbali ya Afrika ya mwakani.

Kitu kimoja ambacho tayari kimeanza kujitokeza ni kile cha majina ya baadhi ya wachezaji kutangaza katika orodha ya timu zaidi ya moja kinyume na taratibu za usajili wa mchezo huu wa soka ambao ndiyo unaoongoza kwa kupendwa na maelfu kwa maelfu ya Watanzania.

Kitendo hiki kwa hakika kinasikitisha na kuhuzunisha kwani hii tuliyosikia kwa timu hizi chache zilizotangaza ni pati ya gazeti, habari kamili ni pale timu zote zitakapomaliza kutangaza wachezaji wao waliowasajili.

Chama cha Soka Nchini (FAT), mapema mwaka huu wakati wa kupitia majina ya wachezaji wa timu zilizoshiriki Ligi Kuu ya Bara, kiliahidi wapenzi wa soka kuwa katika msimu ujao hakutakuwa tena na mambo ya wachezaji kujisajili mara mbili mbili.

Katibu Mkuu wa FAT, Ismail Aden Rage, alisema kwa uhakika kuwa wanatarajia kuanzisha mfumo mpya wa usajili ambao kwao hakutakuwa tena na suala la mchezaji kujisajili katika timu zaidi ya moja.

Tunawauliza FAT kuwa ahadi hiyo iko wapi sasa?, au mlikuwa mnataka kuwanua ngoma juani tu halafu muendelee na usingizi wenu?, kwa hakika hapo tuna hitaji maelezo ya kina toka kwa chama hicho kinachoongoza soka Tanzania.

Tutaendelea hadi lini kusikia jambo hili la wachezaji kujisajili katika klabu zaidi ya moja. Kama ni uongozi wa soka basi ndio huu na sio kusafiri na kula posho pekee.

Kama suala la usajili litaendelea kutuhenyesha miaka nenda rudi hayo maendeleo ya soka kweli tutayaweza?.

Wakati umefika FAT kutupatia jibu makini na sio kusubiri kufungia mchezaji au kuuliza mchezaji mchezaji anataka kuchezea timu ipi kati ya hizo alizoangukia wino.

Usingizi huo wa FAT mpaka lini?, mnatukarahisha, jireke-bisheni, tunataka vitendo siyo ahadi zisizotimilika.