Make your own free website on Tripod.com

SIANG’A: Ni bahati  Express kupangwa na Simba

Na Mwandishi Wetu

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Simba, James Sing’a amesema sasa imekuwa bahati kwake, kwa timu yake ya sasa ya Express kukutana na timu ya Simba  katika kundi moja katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati inayoanza mjini Kigali Rwanda wiki hii.

Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam, zilimkariri Siang’a akiupongeza Ukuu wa Mungu ambaye amewezesha timu yake ya Express kukutana na timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, ambayo aliifundisha kwa miaka mitatu kabla ya kuhamia Express ya Uganda.

Siang’a aliondoka katika Klabu ya Simba baada ya kuibuka mgogoro anaodai kuwa, chanzo chake kilikuwa ni Katibu Mkuu wa Simba Kassim Dewji.

Siang’a na Dewji walifikia uhasama hadi kutumia vyombo mbalimbali vya habari katika malumbano.

Viongozi hao wawili mahasimu Dewji na Sing’a wote wamekwishaondoka kwenda Kigali Rwanda na timu zao za Express na Simba, zinamenyana Jumatano hii.

Siang’a amesema mchezo baina ya timu yake na Simba, ndio utakaodhihirisha wazi kuwa nani bora katika ulimwengu wa soka.

Simba iliyowahi kutwaa kombe hilo mara sita, imepangwa Kundi B pamoja na Timu za Express ya Uganda na Jamhuri ya Zanzibar.

Kikosi cha wachezaji 20 wa Timu ya Simba, kiliondoka Ijumaa iliyopita kuelekea Kigali kwa basi ili kushiriki michuano hiyo.

Kwa mujibu wa habari zaidi zilizopatikana jijini, Simba ilitakiwa kuondoka na makocha wawili, Patrick Phiri na msaidizi wake, Patrick Chamangwana.

Kabla ya kukwaana na Express Jumatano hii, Simba inarusha kete yake ya kwanza kwa kumenyana na Jamhuri ya Zanzibar Jumatatu hii.

Hadi sasa mashabiki wa soka nchini bado wana shauku ya kujua kama Simba itaendelea kuchomoa makucha yake kama ilivyofanya Machi 3, 2002 katika Uwanja wa Amani wa Zanzibar, ilipoichapa Prince Louis ya Burundi kwa bao 1-0 na hivyo, kutwaa kombe la mwaka huo.

Wakati huo huo: Mgogoro wa madai ya fedha za James Siang’a dhidi ya Simba, umeingia katika sura mpya baada ya suala hilo kufikishwa katika Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Siang’a amechukua hatua hiyo baada ya uongozi wa Simba kukataa madai yake ikisema kuwa, haikuwa imemwajiri Kocha huyo.

Klabu hiyo imesema kuwa, Mkenya huyo aliajiriwa na kampuni ya Mohamed Enterprises ambayo ni wafadhili wa timu hiyo na siyo klabu ya Simba.

 

 

 

SIMBA: Yanga wasirukie wasichokijua

Na Joachim Mushi

Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, imewashambulia vikali mahasimu wao, Yanga kwa kuingilia madai ya mchezaji Ramadhan Wasso anayetaka ashirikishwe katika mgawo wa fedha za CAF, kama walivyopewa wachezaji wengine wa timu hiyo.

Meneja wa Simba, Innocent Njovu, amesema hatua ya Yanga kuwashinikiza wamlipe mchezaji Wasso kile alichokiita “madai hewa”

ni kuingilia mambo ya ndani ya klabu nyingine yasiyowahusu.

Njovu alisema, Yanga haijui lolote juu ya madai ya Wasso na kamwe haiwapasi kuzungumzia suala hilo wasilolijiua.

“Sisi kama Simba hatudaiwi pesa zozote na Wasso ama hata Kocha Siang’a kama inavyosikika huko mitaani na kwenye magazeti. Na ndio maana Wasso hasemi anadai shilingi ngapi na ni za mshahara upi ama posho gani ambazo alikuwa hajalipwa,” alisema Meneja huyo.

“Wasso sio mchezaji wa Simba kwa sasa. Sisi tumewapa motisha wachezaji wa Simba, sasa kelele zinatoka wapi tena? “ aliuliza Meneja Njovu kwa mshangao.

Akizungumzia suala la madai ya Kocha Siang’a ya kudhulumiwa pesa zake na klabu hiyo, Njovu alisema Simba, haidaiwi chochote na kocha huyo kwa sababu haikuwa na mkataba nae.

Alifafanua kuwa, Siang’a alikuwa na mkataba baina yake na mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Mohamed Enterprises, na wala klabu haikuhusika na masuala yoyote yahusuyo pesa na kocha huyo raia wa Kenya.

“Kama kuna fedha anadai, aende kwa yule aliyewekeana nae mkataba. Huyo ndiye alikuwa mwajiri wake na angeweza kumpangia kufanya jambo lolote, kama alivyompangia kuja kuifundisha Simba” alisema meneja huyo.

Hivi karibuni, Kocha Siang’a alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akidai kudhulumiwa fedha zake na klabu ya Simba, baada ya kumalizika kwa mkataba wa kuifundisha kabla ya kuondoka kwenda kufanya kazi hiyo nje ya nchi.

Yanga Asili yaiunga mkono FAT

Machumu Manyama  na Libert Lukaya

KUNDI la Yanga Asili, limekiunga mkono Chama Cha Soka chini (FAT ), kwa hatua yake ya kuvitaka vilabu viwe na vitega uchumi badala ya kutegemea mapato ya mlangoni.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kundi hilo, Yusufu Mzimba alisema kuwa, umefika wakati kwa vilabu vinavyoshiriki ligi mbalimbali hapa nchini, kuwa na vitega uchumi vyao na siyo kutegemea fedha za mlangoni ambazo hazikidhi mahitaji kwa mwaka.

Mzimba alisema kuwa, iwapo mbinu hiyo mpya ya kubuni na kuanzisha vitega uchumi itafanikiwa basi, itakuwa njia nzuri ya kuleta maendeleo ndani ya vilabu na taifa kwa ujumla na tabia ya vilabu kuwa tegemezi itakwisha.

Akifafanua zaidi Mzimba alisema mpango huo wa FAT, unapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote na wadau wa sekta hiyo, hususan wapenda michezo, ili waendane na mabadiliko ya wakati na kuepusha tabia ya vilabu kuwa ombaomba.

Kundi hilo ambalo limekuwa likilumbana na kundi jingine la “Yanga kampuni”  limesema kuwa, vilabu vingi hapa nchini vinakabiliwa na uhaba wa fedha kutokana na kutokuwa na vyanzo vya mapato vya kuaminika na visivyo tegemezi.

Hivi karibuni Chama Cha Soka nchini, FAT kilivitaka vilabu vinavyo shiriki Ligi Kuu Bara, kuanzisha mpango mpya  wa kujiletea mapato kutoka katika vitega uchumi vingine badala ya kutegemea mapato ya mlangoni tu.

Kauli hiyo ya FAT, ilikuja kufuatia vilabu vinavyoshiriki ligi kuu bara, kutaka kugawana mapato ya mlangoni, badala ya timu mwenyeji kuchukua mapato yote kama ilivyoamriwa na chama hicho cha soka.