Simba kuwa klabu ya kulipwa

lLengo ni kuipa nguvu zaidi kitaifa na Kimataifa

KLABU Kongwe ya Soka Nchini Simba ya Jijini inaandaliwa kuwa kama klabu ya kulipwa ili kuweza kuipa uwezo wa kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya ligi na ile ya kimataifa.

Habari zilizopatikana mapema wiki hii kutoka ndani ya klabu hiyo zilisema kuwa moja ya mkakati huo wa kuigeuza Simba kuwa kama timu ya kulipwa ni mkataba wa miaka mitatu baina ya klabu hiyo na kampuni ya Mohamedi Enterprisses ya jijini.

Mjumbe mmoja wa Simba ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alidai kwa madai kuwa si msemaji wa klabu hiyo, alisema kuwa Kamati ya Utendaji ya Simba itakuwa na kikao hivi karibuni ambacho kitazungumzia na kujadili mikakakti ya kuifanya klabu hiyo kuwa na nguvu kama zilivyo timu za kulipwa barani Ulaya .

Mjumbe huyo alisema kuwa licha ya kuwepo kwa kanuni nchini, bado hazijaruhusu soka la kulipwa , lakini klabu yao inaona wakati umefika wa kuigeuza timu yao katika mfumo huo ili kuwafanya wachezaji kuwa na Morali na ushindani wanapoichezea timu yao.

Alisema kuwa malipo watakayolipwa wachezaji katika kipindi wanapoichezea timu hiyo yatawafanya kuwa na moyo wa kujituma wakati wote wanapokuwa uwanjani na hivyo kupatia klabu yao mafanikio.

Katibu Mkuu wa Simba Hassan Matumla alipoulizwa kuhusu suala hilo alikataa kusema kwa kirefu, lakini akadai kuwa ni mapema mno kuzungumzia mipango hiyo kwani bado haijakamilika.

Habari zaidi zilizopatikana zimedai kuwa mkataba wa sasa baina ya Simba na Mohamed Enterprisses ni kama majaribio ya kuelekea kuifanya klabu hiyo kuwa ya kulipwa na kuweza kujitegemea.

Katika mkataba huo wa miaka mitatu kampuni hiyo ya Mohamed Enterprises itakuwa inaipatia Simba shilingi milioni 20 kila mwaka kwa ajili ya gharama za kuiendesha katika ligi kuu Tanzania Bara.

Kulingana na mkataba huo Shilingi milioni 1.8 zitatumika kwa ajili ya mishahara ya makocha na wachezaji.

Kila mwezi kocha mkuu atalipwa sh, 120,000 kocha msaidizi sh,100,000ambapo kila mchezaji atalipwa sh, 50,000 daktari wa timu atalipwa shilingi 100,000 katika mkataba huo uliotiwa saini machi 22 mwaka huu unasema kuwa shilingi milioni kumi zitatumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya michezo ikiwemo mipira, jezi na viatu.

Aidha katika hatua nyingine inayoonyesha kufunguliwa kwa njia hiyo ya kuelekea kuwa klabu ya kulipwa ni uataratibu wa kumlipa shilingi milioni tano mchezaji atakayeuimia akiwa katika mechi au mazoezi .

 Monja ,Mtwa wazuiwa kwenda Botswana

PASI za kusafiria nje ya nchi za wachezaji wawili Monja Liseki na Mtwa Kihwelo wa timu ya soka ya Mtibwa ya Morogoro zimekamatwa na Idara ya Uhamiaji na hivyo kuwazuia wachezaji hao kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.

Wachezaji hao wawili ambao pia walikuwa wakiichezea timu ya Tanzania Stars katika michuano ya Kombe la Washindi, walikuwa na mipango ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nchini Botswana pamoja na mshirika wao Wiliamu Fahnbuleh ambaye tayari amekwisha ondoka mapema wiki iliyopita.

Habari zilizo patikana jijini toka kwa marafiki wa karibu wa wachezaji hao zimesema kuwa kuzuiwa kwa pasi za wachezaji hao kulitokana na "ngumu" waliyowekewa na uongozi wa timu ya Mtibwa.

Mchezaji mmoja wa Tanzania Stars ambaye pia alikuwa katika mkumbo wa kuondoka na wachezaji hao, Habibu Kondo alithibitisha jijini kukamatwa kwa pasi za wachezaji hao katika kituo cha idara ya uhamiaji kilichoko Tunduma.

Mchezaji huyo alisema kwamba kuzuiwa kwa wachezaji hao kuondoka nchini kunafuatia kiongozi mmoja wa juu wa Tanzania Stars na Simba ( jina linahifadhiwa) kupiga simu kuwafahamisha viongozi wa Mtibwa kuwepo kwa njama hizo za wachezaji hao wawili kuondoka nchini.

Alisema kuwa baada ya kiongozi huyo wa Tanzania Stars ambaye alikuwa akifahamu mpango huo kuwaarifu Mtibwa, viongozi wa timu hiyo nao walichangamka na kuwasiliana na idara ya uhamiaji kule mpakani Tunduma kuwazuia wachezaji hao.

Katika safari hiyo inaelezwa kwamba pasi za Monja na Mtwa zilikuwa tayari zimetangulia kwa ajili ya uhakiki katika idara ya uhamiaji katika kituo cha Tunduma huku wenyewe wakijiandaa na safari ya gari kupitia njia hiyo.

Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja katika safari hiyo ya kwenda Botswana wachezaji hao walikuwa wakienda kucheza timu gani lakini imethibitika kwamba waliitwa huko na wakala mmoja wa soka Mtanzania ambaye angewapatia timu ya kuchezea.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, kiongozi mmoja wa kampuni ya Super Doll ambayo inamiliki timu ya Mtibwa alikiri kuwepo kwake lakini alikataa kulizungumzia zaidi kwa madai kwamba siyo msemaji wa kampuni hiyo wala timu yake

Aidha juhudi za gazeti hili kumpata msemaji wa Idara ya Uhamiaji Makao Makuu Hubert Chilambo zilikwama jana baada ya kuelezwa kwamba alikuwa nje kikazi.

Ukarabati wa uwanja kugharimu milioni 4 Kisarawe

Shughuli za ukarabati wa uwanja wa michezo wa wilaya hii zinatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi milioni nne pamoja na nguvu za wanachi katika kufanyakazi mbali ili kukamilika.

Afisa Utamaduni, Vijana na Michezo wilayani hapa Bw. Julius Kisamba aliliambia gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni kuwa katika ukarabati huo ulioanza mapema mwezi Octoba mwaka jana, bado zaidi ya nusu ya urefu wa mita 500 (mita 300) za uwanja huo zinazohitaji matengenezo, hazijafanyiwa ukarabati.

Akifafanua juu ya kiasi hicho cha pesa, Kisamba alisema ni kwa ajili ya kununulia vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwemo mifuko 200 ya saruji.

Afisa Utamaduni huyo alitoa mwito kwa vijana, wapenzi wa michezo pamoja na wafadhili mbalimbali kujitokeza na kuiga mfano wa TANESCO wilayani hapa, Benki, jeshi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hii Bi. Maimuna Tarishi pamoja na Mkuu wa Wilaya Kapteni James Yamungu ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa misaada mbalimbali ya kuendeshea ukarabati huo ikiwemo ya usafiri na upatikanaji wa mchanga.

Aidha, alikipongeza kikundi kimoja cha vijana mafundi wanaojishughulisha na ujenzi katika ukarabati wa uwanja huo kwa moyo wa kujituma bila kulipwa chochote na akawataka wapenzi wa michezo na watu wengine kuiga mfano huo ili kuinua kiwango cha michezo wilayani hapa.

Sehemu kubwa ya uwanja wa michezo wa wilaya hii licha ya kuwepo sababu nyingine, umebomoka kutokana na mvua za el-Nino na hivi sasa umezungushiwa makaratasi ya mifuko ya saruji, makaratasi ya nailoni pamoja na viloba.

 Mandela kuagwa na wanasoka maarufu duniani

TIMU ya wanasoka maarufu duniani inatarajiwa kushuka dimbani nchini Afrika kusini kucheza mchezo maalum kwa ajili ya kumuaga Rais Nelson Mandela wa nchi hiyo ambaye anastaafu.

Timu hiyo inatarajiwa kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo Bafana Bafana ,mchezo huo ambao utafanyika Agosti utakuwa wa aina yake kutokana na kuwa utakuwa umewaleta kwa pamoja wachezaji wote maarufu duniani katika ardhi ya Afrika.

Wachezaji wa timu hiyo maarufu ya dunia wanategemewa kuongozwa na mchezaji bora duniani Zinedine Zidane( Ufaransa) ,Ronaldo di Lima ,Rivaldo na Denilson (Brazil),Jay Jay Okocha na Nwanko kanu( Nigeria ),Mustapha Hadji (Morocco), Michael Owen(Uingereza), Peter Schmeiche (denmark).

Wengine ni Iran Zamorano (Chile), Roberto Baggio( Italia) , Edgar Darisna Clarence Sedolf (Uholanzi), Oliver Biholf (Ujerumani) na GeorgeWeah (Liberia).

Viongozi wa soka wa Afrika Kusini na wale wa serikali wanaiona nafasi hiyo kama njia moja ya kufanyia kampeni yao ya kutaka kupewa nafasi ya kuandaa fainali za kombe la dunia mwaka 2006 nafasi ambayo inagombewa pia na nchi za Ujerumani na Uingereza.

 Ushirikina unaathiri soka la Tanzania - Mtaalam

IMANI za kishirikina kwa baadhi ya wachezaji na viongozi wa soka nchini inadaiwa kuwa ndio chanzo kikubwa cha kutokupanda kiwango cha soka kwa ngazi za vilabu hadi ile ya Taifa.

Hayo yalisemwa na mtaalam wa mchezo wa mpira wa miguu kutoka nchini Sweden; Lenhadt Nilsen ambaye alikuwepo nchini kwa likizo binafsi ya miezi miwili na kufutilia soka la nchi hii.

Mtaalam huyo wa soka toka Sweden ambaye amedai kuwa amekuwa akifuatilia soka la Afrika kwa muda mrefu na kutembelea nchi nyingi za Afrika alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa utaratibu wa kutumia "juju" katika soka ni wa kawaida katika nchi za Afrika lakini kwa Tanzania ameona juju inahusudiwa sana.

''Viongozi wa vilabu wanachojua ni uchawi tu na fedha , wachezaji mlionao wanahusudu sana ushirikina na hawaamini kuwa bila uchawi wanaweza kucheza na kushinda."alisema Nelsen Aidha alisema kuwa hata katika timu za watoto wadogo wa mitaani alikutana na imani hizo na kusema kuwa watoto wale wanapokuwa huendelea kuamini kuwa uchawi ndio unaocheza mpira na hivyo kupoteza vipaji vyao.

Mtaalamu huyo alisema kuwa ameona vilabu vingi nchini vinapoteza fedha nyingi kwenye suala la uchawi bila kujali mambo ya kitaalamu kama vile mazoezi vifaa na matunzo mazuri kwa wachezaji.

Nilsen ambaye ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Stochlomy aliishauri serikali ya Tanzania iwaelimishe viongozi wa soka na imani potofu ya ushirikina ili waweze kuijenga upya hali ya soka nchini la sivyo Tanzania itabaki kuwa msindikizaji siku zote.