Kwa kupoteza matumaini ligi ya Mabingwa:

Wanachama wa Yanga ndio wa kubeba lawama zote - Bomba

Na Mwandishi Wetu

WANACHAMA wa Yanga wenyewe ndiyo wanaostahili lawama zote kwa kusbabisha timu hiyo ' kuvurunda' katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na kubakia wasindikizaji, Amesema Abaas Bomba.

Bomba - Katimu Mwenezi wa klabu hiy ambaye uongozi wake kwa sasa umesimamishwa na mahakama, aliliambia gazeti hili katikati ya wiki kuwa hiyo inatokana na kitendo cha baadhi yao (wanachama) kuleta chokochoko na kusababisha mahakama kuamua kusimamisha uongozi huo.

"tulikuwa na mikakati mizuri ya kuhakikisha Yanga inatwaa ubingwa wa Afrika, Lakini sasa zimebari ndoto tu, "alisema Bomba alipozungumza na gazeti hili".

Yana baada ya hivi karibuni kushindwa kulipiza kisasi kwa Raja Casablanca ya Morocco, ilijikuta katika nafasi ambayo timu hiyo imepoteza matumaini ya kuingia fainali ya michuano hiyo. Katika mchezo huo, ilitoka sare ya mabao 3-3 wakati katika mchezo wa kwanza wa timu hizo uliofanyika nchini Morocco, Raja iliisambaratisha Yanga kwa mabao 6-0. Hicho hakikuwa kipigo cha kwanza, siku chache kabla ya Yanga kuchapwa mabao hayo, ilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Asec Abdjan ya Ivory Coast katika mchezo wake wa pili wa robo fainali hiyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Manning Rangers ya Afrika Kusini katika mchezo wa kwanza.

Kwa mwenendo huo Yangi ilijikuta ikiendelea kuburuza mkia wa kundi B la fainali hizo ambapo sasa hata kama itashinda michezo yake iliyobakia haitafika popote. Hata hivyo Bomba katika maelezo yake hakuweza kufafanua kwa kina mikakati hiyo. Kauli yake kwa upande mmoja inafanana na ile ya aliyekuwa kocha wa Yang, tito Mwaluvanda, ambaye alisema kwa kutimuliwa Yanga ameondoka na ubingwa wa Afrika.

Mwaluvanda alitimuliwa baada ya sare ya Manning akidaiwa kufanya mabadiliko 'kizembe' na kusababisha Manning kusawazisha bao dakika ya 89, Raoul Shungu, aliteuliwa kuinoa Yanga kuziba nafasi yake

 

...Kamati ya muda haina madaraka?

Na Dalphina Rubyema

KAMATI ya muda ya Yanga imedaiwa kuwa haina baraka za wanachama na kutokana na hali hiyo timu hiyo itaendelea kuwa kichwa mwendawazimu katika michuano mbalimbali ikiwa ni pamoja na michuano ya klabu Bingwa Afrika.

Mwenyekiti wa Tawi la Yanga Mbagala said Mtapali ambaye ana kadi namba 0611 alisema Yanga watake wasitake lazima waruhusu viongozi waliochaguliwa kihalali na wanachama kuzidi kuendelea na shughuli zao hata kama kesi bado ipo mahakamani.

"Waondoe pingamizi kama wanataka mambo yao yaende shwari "Alisema Mtopali.Alisema inashangaa kamati ya muda kuongozwa na mtu asiye na uzoefu wowote na vibaya zaidi hajawahi kuudhulia mkutano wowote wa Wanayanga.

"Huyu George katoka wapi sijui ?Alihoji na kuongeza kuwa hali hiyo ndiyo iliyopelekea kiongozi huyo kudaiwa kuwa alikuwa nyumbani wakati Yanga inacheza na ppolisi katika ligi ya muungano na kubandikwa bao 1-0.

Kiongozi huyo ameamsha tuhuma kuwa Ngozoma anaihujumu klabu hiyo na kudai kinachotokea ni kwa viongozi wa kamati ya muda kukosa kushirikiana na viongozi wa wanachama wengine wa klabu hiyo.

Alisema habari zilizozndikwa karibuni na baadhi ya vyombo vya habari kuwa matunda anaihujumu klabu hiyo hazina ukweli wala msingi wowote.

 

Koffi Olomide kutumbuiza Oktoba 23

Na Dalphina Rubyema

KOFFI Olomide akiwa na kundi zima la Quartier Latin likiwa na wanamuziki 17 (wapigaji vyombo) litawasili nchini siku ya Jumanne ya tarehe 20 Oktoba, 1998 na ndege ya shirika la Alliance tayari kwa kuwaburudisha watanzania.

Katika taarifa yake Mratibu wa safari hiyo Othman Njaidi ,meneja wake katika ziara ya Tanzania, Kayembe Kalodji wa Musongo (Chezi Ntemba), ameshawasili nchini na tayari ameanza taratibu za kufanikisha ziara hii.

Koffi Olomide pamoja na wanaminenguo wake watano watawasili nchini siku ya Alhamisi ya tarehe 22 na ndege ya shirika la Uswisi ambayo itawasili saa 12.00 alfajiri. Kuwasili kwa siku tofauti kunatokana na kuwa mwanamuziki huyo anamalizia kukarabati albamu yake mpya kabisa ambayo inatarajiwa kusambazwa mwanzoni mwa mwezi Novemba.

Katika jiji la Dar es Salaam, Koffi atafanya onyesho moja tu ambalo lifafanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Hall siku ya Ijumaa ya Oktoba 23 .

Katika ziara hii, wapenzi wa muziki wa Dansi watapata fursa ya kushuhudia mtindo mpya wa kucheza ambao unajulikana kama MWANA. Pia wapenzi watapata fursa ya kusikia baadhi ya vibao vyake vipya vinavyo patikana katika album yake mpya iitwayo DROIT DE VOTE. Katika kuonyesha mitindo hiyo mpya Koffi anakuja na wasichana watano wakiwemo na wasichana wapya kabisa.

 

Wagombea wa Simba waendelea kumwaga sera

lMmoja asema ataleta umoja

Na Said Mmanga

WAKATI kesho ikiwa ndiyo siku ya mahojiano kwa wagombea uongozi katika timu ya Simba baada ya kushindikana wiki iliyopita,wagombea mbalimbali wameendelea kumwaga sera zao ili waweze kujipatia nafasi za uongozi wa timu hiyo kongwe hapa nchini.

Mgombea wa nafasi ya uweka hazina msaidizi Mahdi Batashi amesema kwamba endapo atachaguliwa kushika wadhifa huo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba atahakikisha anarudisha umoja katika timu hiyo na kuifanya iondokane na hali tegemezi.

Alisema akichaguliwa atahakikisha Simba inarudisha hadhi yake kama ilivyokuwa miaka ya nyuma katika michezo mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa na kuboresha hali ya wachezaji.

Mahdi alisema atatumia uzoefu wake katika masuala ya uongozi na mahusiano yake na makampuni mbalimbali ya nje ya nchi katika kuifanya Simba iwe inajitegemea na wakati huo huo kurudisha hadhi katika kutandaza soka.

Naye mgombea wa nafasi ya umakamu mwenyekiti katika timu hiyo Abdalah Kipukuswa amesema kuwa endapo atachaguliwa kuongoza timu hiyo mbali na kurudisha umoja katika timu hiyo ambao alisema kwa muda mrefu sasa haupo pia atahakikisha jengo linakarabatiwa na kuwa katika hali nzuri ili kambi ya timu iwe katika makao ya klabu.

Alisema ataanzisha vitega uchumi mbalimbali kwa kutumia jengo la klabu ambapo pia wachezaji watakuwa wakilipwa posho au mishahara mizuri bila ya kutegemea msaada wa wafadhili ambapo alisema hilo litafanikiwa kama klabu itakuwa na umoja ambapo pia alsema amepania kubuni miradi mbalimbali ya uchumi kwa ajili ya timu.

Aidha, Kipukuswa alisema endapo atachaguliwa atayashirikisha matawi yote ya timu hiyo hapa nchini ili yaweze kutoa mchango wao wa hali na mali katika kuiletea Simnba maendeleo na kuifanya ijitegemee na kuondokana na hali yakila kitu kutegemea wafadhili.